Rai ya mzee Aboud Jumbe

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,246
02f6d4580da21fcc47efc19173275eb8.jpg
RAI YA MZEE ABOUD JUMBE
Ukiachilia mbali kitabu chake cha THE PARTNERSHIP, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, aliyewahi kuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Wa Kwanza wa Rais wa Tanzania kabla ya kushinikizwa kujiuzulu na chama mwaka 1984 kutokana na msimamo wake wa serikali tatu, ameandika pia kitabu kingine kinachoitwa TUISHI BILA KUBAGUANA.
Kwenye kitabu hicho kilichochapishwa mwaka 2003 Mzee Jumbe anaeleza mengi kuhusu kuvuliwa kwake nyazifa za uongozi kwenye chama na serikali.
Hizi ni baadhi ya nukuu kwenye kitabu hicho.
KIKAONI DODOMA
"…Siku tatu za kwanza za mkutano, Jumanne hadi Alhamis, ni wajumbe wachache tu, wote wakiwa kutoka Zanzibar, ndio waliosimama mmoja baada ya mmoja kulalamika na kushambulia kule walikokuita 'kupenda kwangu na kunyima madaraka, kutosikiliza shauri wala maoni, kujifanyia nitakavyo, kutoipenda CCM na Azimio la Arusha na madai mengine kama hayo'…"
KUJIUZULU
"….Siku ya Jumamosi, baada ya kumuachia Ramadhani Haji (aliyekuwa Waziri Kiongozi) kutoa maelezo yake, ndipo mimi nilipochambua tuhuma zilizotolewa. Nilipomaliza nikashauri niruhusiwe kuacha shughuli zote za chama na serikali"
BAADA YA KIKAO
"….Nilipowasili nilikofikia, si muda walifika Mabwana Kawawa na Sokoine wakifuatiwa muda mfupi na Mwalimu Nyerere. Niliambiwa kwa vile niliacha madaraka kwa mdomo hakuna ushahidi, bora kufanya uthibitisho kwa maandishi.
Kwa kutotaka 'kuchafua hali ya hewa' niliandika kuacha madaraka ya Makamu Mwenyekiti wa chama na Makamu wa wa Rais wa Muungano, nikampa aliyekuwa mpiga taipu wangu achape. Mwalimu aliponiuliza kuhusu Zanzibar nilimwahidi nitafanya hivyo nikifika Zanzibar"
HAIFAI KWENDA ZANZIBAR!
"...Hapo ndipo aliponiambia ingekuwa bora kwa 'sasa' kutokwenda Pemba (Nilikotaka kumpeleka kwao mke wangu niliyekuwa nimefuatana naye) wala kwenda Unguja na kwa hiyo niandike na kuacha kwangu shughuli za Zanzibar. Kwa kuona wazi wasiwasi uliojidhihirisha, nilikubali yote."
ULINZI MKALI
"...Tulipofika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukuta ulinzi mkali wa Jeshi na Polisi, wakiwepo mkuu wa jeshi na mkuu wa jeshi la polisi, nilishindwa kabisa kuelewa sababu na maana ya yote hayo yalikuwa ni ya nini au kwa nini? Mpaka leo hakuna aliyenielimisha na bado niko ujingani"
SIMU IMEKATWA!
"....Nilipwerewa nilipofika nyumbani Mjimwema na kutaka kupiga simu Unguja. Niliona, kabla ya kutangazwa yaliyotokea, niwatulize wake zangu na wanangu Unguja angalau wajue tu nilikuwa salama Mjimwema. Niligundua simu hazifanyi kazi! Hapo nilimshukuru Mwenyezi Mungu nikamwachia yeye na kukaa kusubiri maajabu mengine huku nikiwaza 'Tunakwenda wapi'?"
SERIKALI TATU
"....Mfumo wa serikali tatu ndio umekuwa msimamo wangu na ndio mtizamo wangu uliopingwa vikali na chama..."
MAHUBIRI YA KUUVUNJA MUUNGANO!
"....Wenye kuhubiri kuuvunja muungano, watambue kuwa hawawezi kufanya hivyo kienyeji… Huu ni muungano wa Watanzania, si wa chama hiki au kile. Wote wenye umri wa miaka ishirini na tisa (akimaanisha mwaka 2003 Muungano ulipotimiza miaka 29) na chini ya hapo ambao naamini ndio wengi, hawajawahi kuwa chochote isipokuwa Watanzania.
Kabla ya kuwanyang’anya au kuwafutia utanzania wao, wana haki ya kushirikishwa kuamua nasaba yao. Hii inamaana itapaswa kufanyika kura ya maoni ili Watanzania wenyewe ndio waamue kuvunja au kubadili mfumo wa Muungano.
RAI YAKE
"....Katika zoezi hili (kuhusu Muungano), wanasiasa na Watanzania kwa ujumla wanapaswa wawe wakweli, wenye busara na zaidi kuliko yote ni uaminifu. Miaka 100 ijayo hapatakuwa, sio tu katika hili bali kote duniani, hata mmoja miongoni mwa walio duniani leo na hata akiwepo hatakuwa na lake. Bali, vizazi vyetu vitakuwepo. Mazao ya mbegu tunazoatika au kupanda leo itabidi kuvunwa na vizazi vyetu kesho".
Mungu akulaze mahali pema peponi.

Sauti Ya Wazanzibar
 
Back
Top Bottom