Nimesikia kuwa Pweza ana mioyo mitatu ambayo inafanya kazi tofauti tofauti, pia ana bongo 9, kuna ukweli hapo Wakuu?
- Tunachokijua
- Pweza ni mnyama wa baharini mwenye mwili wa kipekee ambao hauna mifupa, ana mikono (mikia) minane inayoweza kujikunja na kufanya inachotaka kwa urahisi. Mnyama huyu ni wa jamii ya mollusks.
Aidha Kuna madai kuwa Pweza ana mioyo mitatu na bongo 9.
Ukweli ni upi?
JamiiCheck imefatilia tafiti mbalimbali kuhusu maisha ya Pweza na kubaini kuwa ni kweli Pweza ana nyoyo tatu na kila mmoja una kazi maalum ya kuhakikisha damu inazunguka mwilini vizuri
Moyo mmoja mkuu wa pweza (systemic heart) Huu ni moyo unaosukuma damu kwenye mwili mzima wa pweza, baada ya damu kujaa oksijeni kutoka kwenye mapezi ya kupumua (gills) na kazi yake kuu ni kusambaza damu yenye oksijeni kwa viungo vyote vya mwili.
Mioyo miwili ya pembeni (branchial hearts) kila pembe moyo mmoja, mioyo hii miwili ipo karibu na mapezi ya kupumulia na kazi yake ni kusukuma damu isiyo na oksijeni kwenda kwenye mapezi ya kupumua ili damu ipate oksijeni. Baada ya damu kupata oksijeni kwenye mapezi haya, inarudi kwa moyo mkuu ili kusambazwa mwilini.
Mifumo ya mioyo hizi tatu husaidia kuhakikisha pweza anapata oksijeni ya kutosha, hata katika mazingira yenye kiwango cha chini cha oksijeni kama vile kwenye kina kirefu cha bahari.
Pweza ana damu ya buluu au kuelekea ukijani, Mioyo yao inasukuma damu ambayo ina ubuluu au kuelekea ukijani, damu ya pweza ina madini ya shaba (hymocianin) ndio sababu ya rangi hiyo na siyo nyekundu sababu haina madini ya chuma ambayo hutufanya binadamu tuwe na damu nyekundu.
Ubongo wa Pweza
Ubongo wa pweza (octopus) ni wa kipekee sana, una muundo wa tofauti ikilinganishwa na wanyama wengine wasio na uti wa mgongo, pweza ana mfumo wa neva wa kipekee ambao unamfanya kuwa miongoni mwa wanyama wenye akili nyingi zaidi kwenye kundi la wanyama wasio na uti wa mgongo (invertebrates)
Pweza ana ubongo Mkuu mmoja na bongo ndogo ndogo (neurons) 8 zilizoko kwenye mikono au mikia yake kitu ambacho humfanya pweza kuwa na jumla ya bongo tisa.
Pweza ana Ubongo mkuu ambao uko katikati ya mwili wake, unafunika umbo la mviringo karibu na umio (esophagus). Ubongo wa pweza una vitundu zaidi ya 500 milioni vya neva (neurons), lakini ni asilimia 40 tu ya neva hizi zinazopatikana kwenye ubongo mkuu kwa sababu asilimia 60 ya neva za pweza zipo kwenye mikia wengine huita mikono au miguu yake minane (tentacles) aliyonayo.
Kila mkono wa pweza una kiasi kikubwa cha neva ambazo zina uwezo wa kufanya maamuzi kwa kujitegemea bila kuhitaji amri kutoka kwenye ubongo mkuu. Kila mkono wa pweza unaweza kujitegemea kutafuta chakula, kugundua mazingira, au hata kufanya kazi ya kushika kitu kwa wakati mmoja, bila msaada wa ubongo mkuu.
Kila mkono una neva karibu vitundu milioni 40-50, na hii inawapa uwezo mkubwa wa kuhisi vitu kwa kugusa na kuonja kupitia viungo vyao vya kunyonya (suckers). Mkono unaweza kugundua vitu vya kipekee, na unaweza kufanya kazi ya kuamua iwapo kitu ni chakula au la.
Aidha, ubongo Mkuu una kazi ya kusimamia na uratibu wa jumla wa mwili na kuhakikisha kwamba mikono inafanya kazi kwa ushirikiano wakati inapohitajika, lakini pia inaruhusu uhuru mkubwa kwa kila mkono.
Mbali na hayo, pweza pia anaweza kubadili rangi ya mwili wake au kubadili muuondo wa ngozi yake, pia ana uwezo wa kujifinya na kupenya kwenye upenyo mdogo sana kwa sababu hana mifupa kwenye mwili wake, akishambuliwa hujilinda kwa kujificha au kutema wino unaosababisha giza kwenye maji na hivyo kujilinda na adui.