Rutashubanyuma
JF-Expert Member
- Sep 24, 2010
- 219,468
- 911,174
Profesa Msolla aipa somo CCM kura za maoni
Imeandikwa na Frank Leonard, Kilolo; Tarehe: 26th December 2010 @ 23:44
MBUNGE wa Kilolo mkoani Iringa, Profesa Peter Msolla ameomba mfumo wa kura za maoni unaotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata wagombea wake katika nafasi za ubunge na udiwani kuangaliwa upya kwa sababu unachochea makundi ndani ya CCM yanayozidisha hatari ya kushindwa katika chaguzi.
Profesa Msolla ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema kama mfumo huo hautafanyiwa marekebisho upo uwezekano kwa chama hicho kuendelea kupoteza ushindi katika maeneo yatakayokuwa na wagombea wengi kwenye kura hizo.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Ruaha Mbuyuni juzi, Profesa Msolla aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wa awamu ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete, alipendekeza kamati maalumu ya Kitaifa katika chama hicho iundwe ili kushughulikia suala hilo.
Akikumbushia maagizo ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Profesa Msolla alikita chama katika ngazi zote kufanya tathimini ya Uchaguzi Mkuu uliopita ili kubaini mambo yaliyosababisha chama kifanye vibaya kwenye baadhi ya maeneo.
"Pamoja na kufanya vibaya katika maeneo fulani fulani, ni vizuri pia tukajiuliza kwa nini wananchi hawakupiga kura kama ilivyotarajiwa na tuzitumie changamoto tutakazozibaini kuimarisha chama vinginevyo vyama vya upinzani vinaweza kuutumia mwanya huo kujiimarisha zaidi," alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM katika jimbo hilo, Profesa Msolla alisema vipaumbele vyake vikubwa vitakuwa katika maeneo makubwa manne ambayo ni pamoja na elimu, afya, miundombinu na shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, alisema katika kutekeleza Ilani ya CCM miaka mitano iliyopita, alikumbana na ushirikiano mdogo kutoka kwa madiwani na akawataka madiwani wapya wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilolo, kutimiza wajibu wao kwa wananchi kama walivyoahidi wakati wa kampeni. Miaka mitano iliyopita kwangu mimi ilikuwa ni miaka ya mpito kwa sababu hata zile kazi zilizopaswa kufanywa na madiwani katika kata zao, bado zilionekana zinatakiwa kufanywa na mbunge na kwa kweli nilijitahidi nikazifanya, lakini sasa muda umefika kwa madiwani wapya kutekeleza wajibu wao, alisema.
Kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Joseph Muhumba alisema wanaendelea kujipanga kikamilifu ili kumpa ushirikiano wa kutosha mbunge huyo katika kutekeleza ahadi mbalimbali alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Muhumba anayekuwa mwanaCCM wa pili kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, aliikwaa nafasi hiyo hivi karibuni baada ya kumuangusha dada wa Profesa Msolla, aliyekuwa mwenyekiti katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya za Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).