KWA KUZINGATIA UKWELI KUWA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA TANZANIA NI MTEULE WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AMBAYE NI MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) TAIFA. - KUNA VIASHIRIA KUWA UTEKELEZAJI WA MAJUKU YAKE UNA USHAWISHI WA CCM – SEI SHARIF HAMAD
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linatambua kuwa Chama cha The Civic United Front (CUF) kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014, iliokubalika na kusajiliwa na ofisi yako, ambayo haijapata kuhoji uhalali wake.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa kuanzia tarehe 5/08/2015 ambayo ni siku aliyoandika barua hiyo na aliutangaza uamuzi wake huo mbele ya vyombo vya habari tarehe 6/8/2015.
Katika Barua yake ya kung’atuka wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ilisema ;
”Leo tarehe 5 Agosti 2015 najiuzulu rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF. Naendelea kuwa Mwanachama na kadi yangu nimeilipia mpaka 2020.”
Prof. Lipumba alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya Chama. Prof. Lipumba alikua na mamlaka ya kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu unaitishwa ili kukubali kujiuzulu kwake lakini hakufanya hivyo.
Kama ulivyoeleza katika taarifa yako, Katiba ya CUF inatambua haki ya kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii kutengua uamuzi wa kujiuzulu. Prof Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu kwa sababu alishautekeleza. Na aliacha ofisi na majukumu ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba ya Chama kwa zaidi ya miezi kumi.
Kamati ya Uongozi ya awali iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mhe. Twaha Taslima ambayo hukuhoji uhalali wake na uliitambua na hata kufanya kazi nayo ilipokuwa ikiwasiliana na wewe. Haiwezekani uone na utambue uhalali wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuunda Kamati ya Uongozi kwa kipindi cha Agosti 2015 hadi Agosti 2016 lakini usione uhalali wa kuundwa Kamati ya aina hiyo hiyo iliyoundwa tarehe 28 Agosti, 2016.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limejiridhisha kuwa katika taarifa yako fupi umeweka hitimisho ambalo linatoa hukumu (judgment) mamlaka ambayo huna kisheria badala ya kushauri au kutoa taarifa kama ulivyoitaja.
Mwisho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF haliukubali ushauri wako kwa sababu umevuka mipaka ya mamlaka yako uliyokabidhiwa na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992, imekiuka miongozo ya mhimili wa Mahakama ambayo imekwishatolewa juu ya mamlaka yako na unakiuka misingi ya katiba ambayo inamtaka kila mtu aliyepewa mamlaka katika nchi yetu azingatie sheria za nchi.
Chanzo : Seif Sharif Hamad