..jamani hii imekaaje?
..madai ya Prof yana ukweli kiasi gani?
LIPUMBA: UFISADI BADO HAUJASHUGHULIKIWA
Na Muhibu Saidi
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema nchi inakabiliwa na hali mbaya kimaendeleo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo tatizo la ufisadi kushindwa kushughulikiwa, huku kukiwapo tuhuma dhidi ya baadhi ya vigogo kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Profesa Lipumba alitoa madai hayo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema hadi sasa ufisadi haujashughulikiwa, ukiwamo ule uliothibitishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya nchini Uingereza, unaohusisha ununuzi wa rada ya Serikali ya Tanzania kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
Hali ni mbaya nchini. Ufisadi haujashughulikiwa, hata ule wa rada uliothibitishwa na SFO, alisema Profesa Lipumba.
Gazeti la The Guardian la Uingereza mwanzoni mwa mwaka jana, liliandika kuwa katika uchunguzi wa SFO, iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni 1 (sh. bilioni 1.2), iliyopo katika Kisiwa cha Jersey, Uingereza.
Kutokana na hali hiyo, gazeti hilo liliandika kwamba, SFO ingefanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28 (bilioni 70), mwaka 2002. Uchunguzi wa SFO ulishakamilika.
Gazeti hilo lilimkariri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Profesa Lipumba alisema wakati ufisadi ukishindwa kushughulikiwa, kuna tuhuma zilizoibuliwa hivi karibuni kutoka kwa wanaopata habari nyeti, zinazowahusisha baadhi ya vigogo kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini.
Hivyo, CCM si chama cha mafisadi tu, bali kimekuwa chama cha wauza unga, alisema Profesa Lipumba.
Alisema kikao cha Baraza Kuu kinatarajia kujadili ajenda 13, ikiwamo ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inayoituhumu Tanzania na baadhi ya nchi kuhusika katika usambazaji wa silaha haramu kwa kikundi cha waasi cha FDLR cha Kongo kinachopigana dhidi ya raia wa Rwanda, mashariki mwa nchi hiyo ya Maziwa Makuu.
Profesa Lipumba alisema ameisoma ripoti hiyo, lakini hakuona serikali ya Tanzania ikihusishwa moja kwa moja na kashfa hiyo, badala yake kuna watu wakubwa wenye vyeo, ambao wana mawasiliano na wafanyabiashara wa dhahabu wa Kongo.
Kutokana na hali hiyo, alisema katika kikao cha Baraza Kuu wanatarajia kupitisha azimio la kuliomba Bunge kuunda kamati maalum ya kuchunguza suala hilo na kutoa ushauri kwa serikali.