Je, Fisadi RA na kampuni yake ya kifisadi Richmond/Dowans kupata mkataba mpya toka serikalini?
Mgawo wa umeme waanza upya
na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
ZIKIWA zimepita wiki mbili tangu Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO), lisitishe mgawo wa umeme, shirika hilo jana limetangaza kuanza tena kutoa umeme wa mgawo kwa nchi nzima.
Katika mgawo huo, Mkoa wa Dar es Salaam, utapata mgawo mara nne kuanzia Jumatatu.
Ofisa Mawasiliano wa Shirika hilo, Badra Masoud, alisema hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema Tanesco imelazimika kuurejesha tena mgawo wa umeme baada ya transfoma moja kubwa ya kuzalisha umeme katika kituo chake cha gesi cha Ubungo kuharibika, sambamba na kuharibika kwa jenereta kubwa la kuzalisha umeme katika kituo cha Aggreko.
Alisema kuharibika kwa transfoma hiyo ya mtambo wa gesi wa Ubungo, kuna sababisha upungufu wa megawati 40 katika mtambo huo, unaozalisha megawati 100.
Alisema pia kuharibika kwa jenereta ya Aggreko, kuna sababisha kuwepo kwa upungufu wa megawati 20 ambapo kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 40.
"Kutokana na sababu hizo mbili, kumekuwapo na upungufu wa megawati 60 na hivyo kulilazimu shirika hilo kugawa kiasi kidogo cha megawati zinazobaki katika gridi ya taifa," ilisema taarifa hiyo.
Aidha, alisema mashine mbili za Songas zenye uwezo wa kuzalisha megawati 70, nazo bado ziko katika matengenezo kutokana na wahusika wa Kampuni ya GE ya Marekani kwa kushirikiana na Songas kuagiza injini mbili, moja kutoka Marekani na nyingine Uholanzi.
Kwa mujibu wa ratiba ya mgawo huo iliyotolewa katika taarifa hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Jumatatu utapata umeme wa mgawo kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Mkoa wa Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Arusha, Mbeya, Tanga, Dodoma na Morogoro, itakuwa na mgawo siku ya Jumanne kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Dar es Salaam, tena itakuwa na mgawo siku ya Jumatano kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni wakati mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Arusha, Mbeya, Tanga, Dodoma na Morogoro, itapata mgawo mwingine wa umeme siku ya Alhamisi kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
"Dar es Salaam itapata umeme mwingine wa mgawo Ijumaa, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni na Jumamosi itakuwa zamu ya mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Arusha, Mbeya, Tanga, Dodoma na Morogoro, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni," alisema.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumapili itakuwa tena zamu ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
"Tanesco inawaomba radhi wananchi kwa usumbufu wa mgawo huo uliojitokeza," ilisema taarifa hiyo.
Wiki mbili zilizopita Tanesco ilitangaza kumalizika kwa mgawo wa umeme baada ya mafundi kutoka Marekani kufanikiwa kutengeneza mtambo mmoja wa umeme unaozalisha megawati 40, uliokuwa umeharibika ghafla.
TANESCO iliwahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na mgawo tena wa umeme, labda kwa dharura ndogo ndogo ambazo shirika litatangaza endapo zikitokea.
Juzi, Rais Kikwete akizungumza na wafanyabiashara katika mkutano wa kwanza wa majadiliano kati ya serikali na wafanyabiashara wakubwa, uliofanyika jijini Dar es Salaam, alisema serikali imejipanga kuhakikisha tatizo la kukosekana kwa umeme wa uhakika halitokei tena na litabaki kuwa historia.
Rais aliyasema hayo baada ya baadhi ya washiriki wa mkutano huo kuonyesha wasiwasi juu ya hali ya upatikanaji wa umeme usio wa uhakika nchini na kuitaka serikali kuliangalia vizuri suala hilo, kwani ni moja ya mambo yanayokwamisha shughuli zao.