Polisi wapambana na raia Dar

Polisi wapambana na raia Dar
Wednesday, 25 May 2011 21:56

Felix Mwagara na Ellen Manyangu
VURUGU kubwa zilizuka usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, baada ya maofisa wa Manispaa ya Temeke kuendesha operesheni ya kubomoa vibanda vya wafanyabiashara wadogo kwenye hifadhi ya barabara.

Ilibidi polisi kuingilia kati kuwatawanya wafanyabiashara hao waliokuwa na hasira, wakipinga uharibifu wa mali zao wakidai kuwa mkakati huo umetekelezwa bila wahusika kupewa taarifa.Zaidi ya mabanda 50 ya wafanyabiashara hao yalibololewa katika agizo hilo kwenye eneo lililopo karibu na Feri, ambalo mji wa Kigamboni unakua kwa kasi.

Baadhi ya walioshuhudia vurugu ambazo ziliandamana na vitendo vya uporaji wa mali na fedha, walisema wafanyabiashara wapatao 50, walikamatwa. Hadi jana mchana, kulikuwa na idadi kubwa ya polisi kwenye eneo hilo wakiwazuia wafanyabiashara hao wasifanye fujo huku maofisa wa manispaa wakibeba bidhaa mbalimbali zilizozagaa hapo.

Wafanyabiashara hao walisema kwamba walilazimika kupambana na askari hao ili kunusuru mali zao katika mpango huo uliotekelezwa bila notisi.

"Ilitulazimu kupambana ili kuokoa japo mali kidogo kwani ubomoaji huo umefanyika usiku wa manane pasipo taarifa yoyote. Hatujapewa notisi yoyote ya kuhama katika eneo hili," alisema Rajabu Mohamed.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Omary Mkwesu alisema tukio hilo ni la kusikitisha kwa sababu wamepoteza mali nyingi.

Alihoji kuwa kama ubomoaji huo ulikua wa haki kwa nini wasingewapa notisi ili walau watoe mali zao katika mabanda hayo?

Alidai kwamba hatua hiyo ni njama za diwani wa eneo hilo: "Zoezi hili limesimamiwa na diwani wetu ambaye amekuwa akitutishia kwa muda mrefu kuwa ipo siku atatubomolea na kwa kuthibitisha hilo, tumemuona akisimamia zoezi hili la ibomoaji hovyo saa nane usiku."

Hata hivyo, Diwani wa eneo hilo, Dotto Msama alikanusha kuhusika na tukio hilo akisema Manispaa ya Temeke ilishatoa notisi zaidi ya sita kuwataka wafanyabiashara hao waondoke katika eneo hilo.

"Jambo hili limenisikitisha hata mimi na sasa hivi naelekea manispaa kuongea na uongozi wake juu ya tukio hili. Ni kweli sikuwa na taarifa za zoezi hili kufanywa leo, tena usiku wa manane, ila notisi zilishatolewa na nakala yake iko kwa mtendaji na mwanasheria wa manispaa.

Polisi kwa upande wake, wamekanusha kuwanyanyasa wananchi hao na kusema walikuwepo kwa ajili ya kulinda usalama hasa baada ya wananchi hao kufunga barabara.
 
Back
Top Bottom