Polisi wamtelekeza mtoto waliyempiga risasi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Polisi wamtelekeza mtoto waliyempiga risasi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MAMMAMIA, Jan 16, 2011.

 1. MAMMAMIA

  MAMMAMIA JF-Expert Member

  #1
  Jan 16, 2011
  Joined: Feb 26, 2008
  Messages: 3,822
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 0
  Hivi ndivyo walinzi wa "Usalama wa Raia" wanavyotufanyia Watanzania kila uchao. Mpaka lini?

  Polisi wamtelekeza mtoto waliyempiga risasi Saturday, 15 January 2011 08:58

  Source: Mwananchi na Editha Majura
  POLISI wanatuhumiwa kumtelekeza mtoto Juma Hamza (12) waliyempiga risasi na hivi sasa hali ya mtoto huyo ni mbaya kiasi cha kumlazimu kutolea haja kubwa katika kidonda kilichotokana na jeraha la risasi hiyo.Baada ya kupigwa risasi, utumbo ulitoka nje na sasa sehemu ya utumbo uliokatika ndio unaotumika kutoa haja kubwa nje.
  Tuhuma hizo zimekuja wakati polisi wakigubikwa na tuhuma nyingine za kufanya mauaji kwa kutumia risasi za moto dhidi ya raia katika mikoa ya Arusha na Mbeya.Januari 5, mwaka huu polisi waliwaua kwa risasi watu watatu wakati wakizuia maandamano ya wafuasi wa Chadema mkoani Arusha na juzi walimuua mkazi wa kata ya Ubaruku, Mbarali mkoani Mbeya baada ya kutokea mabishano baina yao na wananchi.

  Lakini Mwananchi limebaini kuwa Juma ambaye ni mwananfunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Makole mkoani Dodoma, alipigwa risasi usiku wa kuamkia Oktoba 24, mwaka jana katika tukio ambalo hadi sasa limezua utata kutokana na polisi kutoa maelezo yanayokanganya.
  Tukio hilo lilitokea eneo la Keko Molemo katika wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam katika tukio ambalo polisi wanadai kwamba walikuwa wakisaka watuhumiwa wa unyanganyi, karibu na ukumbi unaojulikana kama Jumba la Dhahabu.
  Wakati polisi wakitoa madai hayo, wananchi wanapinga nao wakidai kwamba eneo hilo hakuna ukumbi wenye jina hilo lililotajwa na polisi na kwamba waliokamatwa katika msako huo walivamiwa kisha kumatwa na wakiwa wamelala kwenye nyumba zao.

  Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa tangu Oktoba mwaka jana hadi sasa mtoto Juma hajapata matibabu ya kuridhisha yanayoweza kufanya kupona jeraha lililotokana na kupigwa risasi, zaidi ya kuwekewa mpira kwenye kidonda ambao anautumia kutolea haja kubwa.

  Mpira huo ambao gharama yake ni Sh 5,000 hubadilishwa kila siku, na gharama hizo ni mbali na gharama nyingine za tiba ambazo familia ya mtoto huyo inalazimika kuzibeba ili kumwezesha kuendelea kuishi.
  Babu wa mtoto huyo, Khamis Lulange alisema mjukuu wake alilazwa kwenye wodi ya Kibasila namba 11 baada ya kufanyiwa upasuaji kufuatia utumbo wake kutolewa nje kwa risasi na kwamba aliporejewa na fahamu, akamudu kuzungumza hivyo aliruhusiwa ili awe anapelekwa kuchunguzwa kadri anavyoendela.
  Lulange alisema muda mfupi baadaye afya yake ilianza kuzorota hivyo kulazwa katika kituo cha afya cha polisi kilichopo Mgulani, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kwa ahadi kwamba polisi wangempa huduma za tiba na mahitaji mengine.Kwa mujibu wa Lulange, mtoto huyo alilazimika kurejeshwa nyumbani ambako anaugulia hadi sasa kutokana na kukosekana kwa chakula katika kituo hicho cha afya cha Polisi.

  Alisema tangu wakati huo afya yake imeendelea kudhoofu kutokana na kunyimwa huduma za afya na kwamba hata walipokweda Muhimbili wamekosa huduma hizo kwa madai kwamba faili lake halionekani. “Novemba 23, mwaka jana jina lake liliitwa wakatuelekeza chumba cha kumpeleka, walihudumiwa wagonjwa wote isipokuwa sisi tukaambiwa faili halijapelekwa pale, mmoja wao akasema, “mwandikieni tarehe nyingine huyo.”
  Tukaambiwa turudi Disemba 31,” alieleza Lulange.Lulange alisema hata walipompeleka tena Desemba 31, alikosa tiba kwa maelezo kwamba faili lake halionekani hivyo kupangiwa kwenda tena Februali 2 mwaka huu.
  “Hofu yetu kubwa ni kwamba hatufahamu hatma ya afya ya mtoto wetu, kwa sababu mpaka sasa anatumia mfuko kutolea uchafu (haja kubwa) tumboni,” alisema Lulange.Alisema kinachowashangaza ni ukimya wa polisi wa kutotekeleza ahadi yao ya kumuhudumia, hivyo kuiacha familia ikibeba mzigo wa tatizo hilo peke yao.
  Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alipohojiwa na Mwananchi kuhusu lilipo faili la mtoto huyo alisema, hawezi kuzungumzia suala hilo ila atafuatilia kumbukumbu zinazohusu mgonjwa huyo na kutoa ufafanuzi mapema iwezekanavyo.
  Maelezo ya mtoto JumaNaye mtoto Juma akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao Keko, alielezea kusikitishwa kweke na kubadilishiwa mfumo wa maisha kwa kupewa ulemavu na kumfanya ahisi kwamba atashindwa kutekeleza ndoto zake za kuwa rais au mrusha ndege (Rubani).
  Juma katika shule yake ya Makole anadaiwa kwamba alikuwa akifanya vizuri darasani kwa kushika nafasi ya kwanza mpaka ya tatu, lakini tangu akumbwe na mkasa huo hajawahi kurejea darasani.Alisema askari aliyempiga risasi, akimuona anaweza kumtambua na kwamba hajamsamehe kwa sababu hajawahi kumuomba radhi.

  “Natamani sana kusoma kwani naamini ndiyo njia pekee ya kunikomboa kimaisha lakini sifahamu kama naweza kutokana na maumivu makali ninayoyapata kwenye kidonda,” alisema Juma na kuongeza:“Ninaumia sana ninapomuona mdogo wangu akienda shule... naumia lakini nitafanyaje maana sijui kama naweza kukaa muda mrefu kwasababu ya maumivu ni makali.
  .”.Ilikuwaje akapigwa risasi ? Akizungumzia tukio hilo, mjumbe wa nyumba kumi shina Namba 33, Shaban Mashua, alisema Oktoba 23, 2010 kulikuwa na sherehe za uzinduzi wa kikundi cha kusaidiana cha kinamama kiitwacho Wanadafana, zilizopata kibali kutoka kwa ofisi za serikali ya mtaa huo.Alisema kibali hicho kiliruhusu sherehe hizo kuanzia saa 10:00 jioni mpaka saa 2:00 usiku Oktoba 24, 2010. Alisema watu walijumuika nyumbani kwa baba wa mtoto huyo aitwaye Hamza Juma.
  Alisema majira ya saa 9:00 usiku, akiwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, waliyokuwa mbele ya nyumba hiyo wakisherehekea kwa kucheza muziki, alifuatwa na mke wa Hamza akimueleza kuwa mume wake (Hamza Juma) amekamatwa na Polisi kutoka chumbani mwao walimokuwa wamelala na kufungwa pingu.
  Alisema alipofika kwenye ukumbi wa nyumba hiyo, alikuta polisi hao wakiwa wamevunja mlango wa chumba kingine na kumfunga pingu mpangaji mwingine, Mohammed Mpile. Alisema alijitambulisha na kuhoji sababu ya watu hao kukamatwa na kwamba badala ya kujibiwa, askari hao walianza kuwasukuma waliofungwa kuwatoa nje ya nyumba.
  Wanafamilia hizo mbili, ndugu na majirani waliamua kufuata askari wakiongozwa na Mashua pamoja na kibali cha kufanya sherehe hiyo, kwa imani kwamba ndugu zao walikamatwa kutokana na sherehe hiyo.
  Tofauti na matarajio, Mashua alisema walipofika kwenye kituo cha mafuta cha Oil Com, askari waliamuru wananchi hao wasisogelee gari walimowekwa ndugu zao ama wangepigwa risasi.Alisema katika kamatakamata hiyo, polisi waliwatia mbaroni Abdallah Abdullahman Bakari ambaye ni mgonjwa wa akili, Khadija Issa Bakari (mke wa Mpile), Chiku Abdullahman Bakari aliyekuwa mjamzito na Msafiri mtoto Mohammed Idd mwenye mwaka mmoja na miezi tisa.

  Alisema hakuna aliyezuia askari kufanya kazi yao bali yeye ndiye aliyeomba maelezo ya kilichojiri, tena baada ya kujitambulisha kwao lakini badala yake askari mmoja alipiga risasi hewani, watu wakaanza kukimbia ovyo kisha askari mwingine akawa anawalenga na kuwashambulia kwa risasi, moja ikampata mtoto Juma.
  Alisema hata baada ya kumuokota mtoto huyo akiwa hajitambui, utumbo ukiwa nje na kumpeleka kwenye gari la askari hao lililokuwa limeegeshwa kwenye kituo cha mafuta cha Oil Com kusudi wamkimbize hospitali, askari hao walikataa kutoa msaada badala yake waliingia kwenye gari kisha kuondoka.
  Alisema walisaidiwa na gari jingine la polisi lililokuwa likifanya doria na kwamba wakati wakiendelea kumuhudumia ili apelekwe hospitali, askari waliyojeruhi walifika kituo cha polisi cha Chang’ombe na askari waliotoa msaada wakawaamuru waendelee kumuhudumia kwa sababu ndio waliyosababisha hayo.
  Mgonjwa walimpeleka moja kwa moja hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alianza kupatiwa matibabu.
  Alisema wote waliokamatwa waliwekwa rumande Chang’ombe bila kuelezwa kosa lao na kwamba kesho yake, mlezi wa familia ya Hamza, Lulanje alitakiwa kuwasilisha kitambulisho chake cha kazi ili awadhamini wote waliyowekwa ndani kwa madai kwamba wanatuhumiwa kwa unyang’anyi.
  Maelezo ya polisi Oktoba 26, 2010 Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Kamishna Msaidiz wa Polisi David Misime, alikaririwa na vyombo vya habari akisema mmoja wa polisi wa kituo cha Chang’ombe alimjeruhi kwa risasi Juma Hamza wakati wakijihami wasipigwe mawe na wananchi.
  Alieleza kuwa awali Polisi walipokea taarifa kuwa mtu mmoja (hakutajwa jina) aliporwa kamera kwenye makutano ya barabara ya Chang’ombe na Mandela, baada ya kutishwa kwa panga na vijana wawili.
  Alisema polisi saba wakiwa ndani ya gari walifanya msako na kuwakamata watuhumiwa wanne akiwemo mwanamke mmoja (hawakutajwa majina).
  Misime alikaririwa akisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa karibu na ukumbi wa Jumba la Dhahabu na kwamba wananchi waliyokuwa ndani ya ukumbi huo walitoka nje na kuwashambulia kwa mawe askari ili wasiwakamate watuhumiwa hao. Alisema hakuna askari aliyekamatwa kwa kwa kumpiga risasi Juma, kwama maelezo kwamba lilikuwa ni tukio la bahati mbaya.
   
Loading...