Polisi wahusishwa na mauaji ya raia Ukerewe

M-bongotz

JF-Expert Member
Jan 7, 2010
1,734
405
Frederick Katulanda, Ukerewe

WAKATI Jeshi la Polisi likitangaza kuendelea na msako wa majambazi wanaotuhumiwa kuvamia Kisiwa cha Izinga na kusababisha vifo vya watu 14, imebainika kuwa watuhumiwa wawili kati ya waliohusika na mauaji hayo walikuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi wilayani Ukerewe.


Kwa mujibu wa taarifa za siri kutoka kwa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya na baadhi wa wauguzi wa hospitali hiyo, majina ya maafisa hao yamebainika ambapo pia moja kati ya silaha zilizotumika zilikuwa ni mali ya Jeshi la Polisi.


Taarifa hizo zimebainisha kuwa silaha hiyo ya polisi ndiyo iliyosababisha kuuawa kwa idadi hiyo kubwa ya wananchi kwa kile kilichoelezwa kuwa harakati za polisi hao kujiokoa wasibainike baada ya kuzidiwa nguvu na wananchi.


Wakizungumza kwa siri kwa hofu ya kuhofia kuuawa, baadhi ya majeruhi hao wameeleza kuwa wameshindwa kutoa maelezo hayo kutokana na ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi kuwaonya baadhi ya majeruhi hao wasibainishe jambo hilo na hivyo kushindwa kulielezea.


"Mauaji haya ya wananchi wengi yametokea baada ya wananchi kuwazidi nguvu majambazi hao, lakini baada ya kuona wamezidiwa mmoja wa majambazi hao ambaye sauti yake na hata sura yake imetambulika kuwa ni askari polisi alimwambia mmoja wao aliyekuwa katika mtumbwi amejificha kuwapiga risasi wanannchi ili kuokoa silaha naye kuanza kuachia risasi na kuua watu saba papo hapo," kilieleza chanzo chetu.


Alisema kabla ya kuanza kwa upigaji wa risasi, awali majambazi hao walikuwa wakifyatua risasi za rashasha za aina ya blancoo ambazo ameeleza kuwa mara nyingi zimekuwa zikimilikiwa na Jeshi la Polisi jambo ambalo wananchi waliligundua na mmoja wao kueleza kuwa hawana silaha na wananchi wengi kukimbilia kuukamata mtumbwi huo ili kuwatia mbaroni majambazi.


"Katika tukio hili baadhi ya majambazi waliohusika ni pamoja na maaskari wawili ya Jeshi la Polisi ambao majina yao na wao tumewatambua ambao mmoja wao toka wavamiaji hao walifika kisiwani humo alikuwa na silaha amelala na kujificha katika mtumbwi,"alisema mmoja wa majeruhi hao

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho alisema kuwa maafisa upelelezi wanaendelea kukusanya ushahidi kuhusu tukio hilo na kwamba malalamiko yanayotolewa kuhusu askari wake ni sehemu ya tuhuma walizopokea na kukusanya kama sehemu ya vielelezo vya uchunguzi.


"Katika upelelezi tunakusanya kwanza kila kitu, tunachoambiwa na wananchi au kuona au kupokea. Unaweza kufika mwisho wa uchunguzi ukakutana na matokeo tofauti na vielelzo ulivyokusanya katika uchunguzi, lakini hatutapuuza, kila tunachokipokea tutakifanyia kazi,"alisema

Manumba ambaye alikagua pia nyumba mbili za kulala wageni zilizovamiwa na majambazi hao na kuangalia maeneo yote ya kisiwa kwa ujumla alisema mwelekeo wao wa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea vizuri.


Hata hivyo, kwa nyakati tofauti baadhi ya majeruhi wa tukio hilo walieleza uwezekano wa askari hao kuhusika na tukio hilo ni mkubwa kutokana na kubainika kwa baadhi ya vielelezo vya kipolisi katika mmoja wa maiti za tukio hilo la aina yake.


"Ni kweli kuna baadhi ya vielelezo ambavyo tumevikuta chumba cha maiti kwa maiti mmoja ambaye hajatambuliwa mpaka sasa, vina uhusiano na vifaa vya kipolisi na tumewakabidhi polisi,"alieleza mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ya wilaya.


Ilisemekana mmoja wa watuhumiwa ambaye aliuawa na wananchi ambaye alikuwa akimiliki nyumba ya kulala wageni ndiye aliyekuwa na mawasiliano na askari hao na siku chache kabla ya tukio alionekana mjini Nansio akiwa na askari hao wawili ambao mpaka sasa maelezo yao na jinsi ambavyo wametoweka kazini hayajabaainishwa wazi.


Taarifa hizo zimethibitishwa na ofisa mmoja wa polisi wilayani hapa ambaye amedai kuwa askari hao wawili wametajwa kuhusika na jeshi hilo limeanzisha upelelezi wa siri dhidi yao .

"Ni kweli kuna wenzetu wametajwa na mwenendo wao na jinsi ambavyo walitoweka kazini unatia mashaka, lakini tumesikia ofisi ya Afande IGP (Said Mwema), imeagiza uchunguzi wao,"alieleza.

Source: http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=17425
 
Mmmh haya.,huu ni uozo mwingine ndani ya Jeshi la Polisi, mimi nadhani jeshi hili linapaswa kuwa overhauled
 
Back
Top Bottom