Na Askofu Kalikawe Bagonza:
UJINGA WANGU SASA UMEKOMAA
Niliamini UHAINI ni kosa kubwa. Neno lenyewe tu, linaogopesha kulisoma, kuliandika na kulitamka. Ni kitendo cha kutaka au kupindua serikali yoyote (halali au haramu).
Sasa kuna mtu mmoja katuhumiwa kutaka kutufanyia hayo. Huyu atakuwa ni mtu mbaya sana. Kwa nini atuhumiwe yeye kwa kosa hili baya? Nikawaza;
1. Kesi yake ingesikilizwa wazi (uwanja wa Taifa maana Kisutu hapatoshi).
2. Pale uwanjani wangeweka vipaza sauti na televisheni zote zirushe mubashara ili watu wote waone.
3. Makarandinga ya polisi yangesomba wote wasio na nauli kwenda kusikiliza kesi.
4. Asasi za kiraia na kianaharakati wangetoa maji ya kunywa bure kwa waliofika kusikiliza.
5. Posho za watumishi wa mahakama zingeongezwa ili kuwatia moyo wakati wa usikilizaji.
6. Siku ya hukumu ingekuwa siku ya mapumziko ili nchi itulie na kusikiliza hukumu hiyo.
Kwa nini nafikiri hivi?
a) Ingetoa fundisho la wazi kwa watu wote wanaopenda kuchezea amani ya nchi yetu.
b) Elimu ya uraia na utii wa sheria bila shuruti ingetolewa kwa vitendo kupitia kesi hii.
c) Hatua hii ingehamasisha watu wengi zaidi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu bila kuhofia Polisi kuvuruga uchaguzi huo.
d) Wale wenye “mdomomdomo” kama mimi, wanaopenda kutumia neno HAKI kuliko amani, wangekuwa wamefungwa goli la kisigino na timu AMANI isiyopenda kutamka neno haki.
e) Hatua hii, ingeua kabisa kampeini za za NO REFORMS, NO ELECTION kwa sababu utawala wa sheria ungeonekana wazi.
f) Chama kingepata fursa nzuri ya kuonyesha ushahidi jinsi mabeberu wanapandikiza wahaini katika siasa zetu.
SASA, nimegundua ujinga wangu umekomaa. Kumbe kesi hii ni muhimu na nyeti. Haiwezi kuwa wazi. Ni kwa ajili ya wanasheria na wateule wachache wenye vifurushi kwenye simu.
Nilidhani nchi hii ni yetu wote kumbe ya wana sheria tu na polisi. Hata serikali iliyotaka “kupinduliwa” ni yetu au ya wana sheria na polisi?
Kama ni yetu wananchi, kwa nini hairuhusiwi watu kwenda mahakamani kusikiliza?
Aisee ujinga wangu una gharama. Akili zimeisha kichwani. Nimebakiza za kunipeleka msalani.
Wajinga wengine kama mimi wameenda wakaishia kuvunjwa viuno, mikono, na migongo.
Hili giza la kuona haki ikitendeka haliwezi kutuacha salama.
Nawaombea uponyaji walioumizwa.
Nawaombea waliowaumiza ili wao wasiumizwe maishani maana inauma.
Vitendo hivi vimelaaniwa vya kutosha. Nafasi za kulaani zimejas. Nitalaani kesho.