Askari Polisi apigwa risasi na majambazi
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha ya moto, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi kichwani na ubongo kutoka nje, askari Polisi, Konstebo Emmanuel Gama (30), baada ya majambazi hao kutilia shaka kuwa askari huyo na mwenzake walikuwa wanawafuatilia.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana saa 5 asubuhi katikati ya Jiji la Arusha eneo la Majengo, wakati askari akiwa na mwenzake aliyetambulika kwa jina moja la Konstebo Hassani,
wakitafuta vipuri vya magari kwenye moja ya maduka yaliopo eneo hilo la Majengo.
Majeruhi huyo ambaye baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru akiwa hajitambui, amehamishiwa Hospitali ya Serian, baada ya hali yake kuwa mbaya, kwani amepoteza fahamu.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa majambazi hao walikuwa zaidi ya watatu na walikuwa wakitumia gari ndogo ambalo halikujulikana na walikuwa wakifuatana kwa nyuma na gari nyingine aina ya Pick Up, gari ambalo linadaiwa lilikuwa likiwafuatilia kwa kuwafukuzia.
Shuhuda huyo, Leonard Mushi maarufu kwa jina la Nyokaa ambaye ni fundi magari Majengo, alisema majambazi hao baada ya kufika eneo hilo, walishtuka kuona gari la Polisi lenye namba T806 ASD aina ya Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikitumiwa na askari hao ipo mbele yao.
Akizungumzia tukio hilo, askari aliyesalimika, Konstebo Hassan alisema walisimama ghafla kwa lengo la kutafuta vipuri vya magari ambapo yeye baada ya kuteremka kwenye gari, ghafla alimwona jambazi nyuma yake akikoki silaha huku akiwa amemwelekezea mwenzake.
Alisema aliamua kulala chini ndipo jambazi huyo alipofyatua risasi moja iliyompiga Gama kisogoni kwani ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa ni miongoni mwa askari waliofika katika Hospitali ya Mount Meru kumjulia hali majeruhi huyo; na pamoja na mambo mengine ameahidi kufanya uchunguzi na msako juu ya majambazi hao na kuhakikisha watatiwa mbaroni.
HabariLeo | Askari Polisi apigwa risasi na majambazi