Pole Zitto, huu ndiyo mrejesho wa wananchi

Molemo

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
14,534
13,225

ban.blank.jpg



MWANAFALSAFA mmoja aliwahi kusema kuwa anao uwezo wa kuihamisha dunia hii na kuipeleka sehemu yoyote ile wanakotakiwa watu, isipokuwa akatoa sharti la kupatiwa eneo la kusimama nje ya hii dunia.
Huyu hataki ukitafsiri kwa mapana dhana yake ni kwamba ana upeo mpana, anajaribu kuwafungua watu akili kuwa huwezi kuwa sehemu ya tatizo kisha ukaondoa tatizo. Ana hamu na uwezo wa kuihamisha dunia lakini naye amekaa humo, anataka atoke kwanza ndipo aweze kuihamisha.
Wiki iliyopita niliandika makala nikijaribu kuelezea vituko vya kisiasa anavyovifanya mwanasiasa kijana na rafiki yangu mkubwa Kabwe Zitto ambaye vile vile ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na aliyekuwa Naibu Kiongozi wa upinzani bungeni.
Katika makala hayo niliyoyapa kichwa cha habari kilichosomeka “Zitto Anaifahamu Thamani ya Umaarufu?” nilieleza umaarufu wa mwansiasa huyo, jinsi ulivyomjenga na kuaminika kwa wananchi yeye na chama chake.
Lakini kati ya mengi niliyoandika, pia niligusia kuwa katika siasa, hakuna aliye maarufu kuliko chama chake, ila kwa Zitto, lazima tukiri kuwa umaarufu wake umeipaisha CHADEMA na amefanikiwa kujizolea imani zaidi kwa vijana.
Kwamba amekuwa gumzo kitaifa kwa kupiga vita ufisadi. Nikakumbusha alivyosulubiwa na Bunge mwama 2007 kwa kukaa nje miezi minne, alipohoji uhalali wa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Nazir Karamagi, kusaini mkataba wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi.
Ila kwenye hoja nikasema bila kutafuna maneno kuwa Zitto wa enzi zile si huyu tunayemuona sasa. Leo amegeuka ana sura mbili, hajulikani yuko upande upi. Huyu mbali na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, bado anakwenda kinyume na itikadi zao.
Huyu amekuwa kigeugeu yaani ndumilakuwili. Anataka kumfurahisha kila mtu ili asionekane mbaya, jambo ambalo ni hatari na gumu kutekelezeka.
Zitto ni mpinzani, lakini siku hizi amegeuza siasa zake kujenga urafiki ili kukidhi haja ya maswahiba zake kwenye vyama hasimu vinavyokazana kuibomoa CHADEMA.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi ndani ya chama hicho, Zitto amekuwa akitoa kauli zenye utata dhidi ya hali ya mambo ndani ya CHADEMA, zikionyesha anatofautiana na viongozi wenzake na hata wanachama.
Nikafafanua wazi kabisa kuwa mipango ya Zitto ya kuuporomosha umaarufu wake haikuanza sasa, bali ni ya muda mrefu na si ajabu kusikia kuna watu nyuma yake.
Nalisema hilo nikikumbushia hatua yake ya kuibuka kwenye vyombo vya habari mwaka jana, akiishauri serikali inunue ama itaifishe mitambo ya Dowans iliyonunuliwa kifisadi.
Itakumbukwa ni CHADEMA akiwemo na Zitto, ndiyo walikuwa wa kwanza bungeni kupinga mkataba wa kampuni hewa ya kufufua umeme ya Richmond LLC ambayo baada ya kushindwa kazi ikatoa zabuni kwa Dowans.
Nisema kuwa ni jambo la kawaida kutofautiana kimtazamo na hivyo sipingi kabisa hatua ya Zitto kutofautiana na chama chake wakati mwingine, lakini kama kiongozi, maamuzi ya chama hana budi kuyazingatia, kama hataki, anatoka.
Nikamhakikishia yeye na wengine wenye siasa za kizamani kuwa CHADEMA haitadumu milele kwa kumtegemea Zitto, Mbowe, Dk. Willbrod Slaa, John Mnyika, Tundu Lissu pekee. Na ndivyo hivyo haiwezi kufa siku wao wakijitoa ndani ya chama.
Zitto anapaswa kutambua kuwa siasa zake kwa sasa zina walakini, haaminiki tena bali anatatanisha wafuasi wake na wanachama wengine kwa ujumla. Heri kama anaitaka CCM au NCCR bora aende huko. Pamoja na mengi niliyoandika nikahitimisha na, “Tafakari na niachie ujumbe.”
Nashukuru sana, wasomaji wote waliosoma makala hiyo, wakatafakari kisha wakanipa ujumbe wa simu, nimepokea maoni mengi sana dhidi ya msimamo wa Zitto. Pengine huu nitauita mrejesho. Nasema hivyo kwa vile hapo juu nilimejaribu kuonyesha fikra ya mwanafalsa aliyekuwa akitaka kuihamisha dunia, lakini akaomba apewe mahali pa kusimama nje ya dunia. Na Zitto ni sawa na mwanafalsafa yule, atambue kuwa hawezi kuipinga CHADEMA akiwa sehemu ya uongozi.

Kiongozi hapingani na wenzake; wanashauriana na kuelekezana hatimaye wanaweka tofauti zao kando na kuwa kwenye msimamo wa pamoja. Nilipoaandika niliamini ningeeleweka hivyo, lakini Zitto hakunielewa bali alinilaumu kuwa nimeegemea upande mmoja.
Tafakari ya kwanza kabisa kuipata ilikuwa ya Mtanzania aiishie Sweden, akaniambia, “Nimesoma makala yako kuhusu Zitto, hakika huyu kijana anahitaji ushauri nasaha, anakoelekea si kuzuri. Mimi nimekuwa nikishauri ajiondoe CHADEMA, kama ulivyosema kuwa chama hicho hakiwezi kufa yeye akiondoka au viongozi wengine.”
Lakini kadiri muda ulivyokwenda, ndivyo maoni yalitolewa mengi na hatimaye Zitto mwenyewe naye alinitumia ujumbe mfupi. Kwa vile sikuwajulisha wahusika kuwa ningechapisha maoni yao, sitawataja majina wala namba zao za simu, walau uone walisema nini baadhi.
Ujumbe wa Zitto ulisomeka hivi: “Salaam. Nimesoma makala yako. Ni nzuri na umejenga hoja. Tatizo umeegemea hoja za upande mmoja kufikia suluhisho lako. Hata siku moja sijawahi kujidaia umaarufu (huu ndio unaowatesa).
“Mie ni mtu wa kawaida sana, mtoto wa kimaskini na sijioni maarufu. Endelea kumtafuta Zitto umjue. Zitto ni msemaji wa fikra zake huru bila woga. Umesemea Dowans, umesikia matokeo ya kesi ambapo twalipa mabilioni? Maslahi ya taifa yako wapi? Hata kama humpendi Zitto, msikilize.”
Nami katika kumtendea haki Zitto nataka asome walau kwa uchache maoni ya wananchi aone wanamtazamaje kwa sasa. Huyu anasema, “Kwa hali jinsi ilivyotathminika ninyi waandishi mnashughulika zaidi na matukio badala ya kutafiti chanzo.
Kwa namna ulivyoelezea kuhama kwa Kafulila ni wazi kuwa si mfuatiliaji wa mambo yanayofanywa na 'wenye chama'. Punda akichoka hugeuka na kurusha mateke. Zitto kachoshwa na wasiopenda changamoto ndani ya chama chetu.”
Mwingine ulisomeka, “Umeandika ukweli kabisa, Zitto hata nia yake ya kutaka kugombea nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni ilikuwa ni kuvuruga chama, hapendi kufuata taratibu.”
Yuko aliyesema, “Zitto ni zigo kwa CHADEMA, kabla hawajashika dola hawajui dhana ya uwajibikaji wa pamoja, je wakiishika kina Zitto si watayumbisha baraza la mawaziri? CHADEMA ionyeshe kutokuwa na mzaha na kumwengua, kwani wasipoziba ufa watajenga ukuta.”
Msomaji mwingine alisema, “Nilikwisha washauri CHADEMA kuendelea na harakati zao bila Zitto na ikibidi hata bila kuwa na Jimbo la Kigoma Kaskazini. Yaani wamfukuze na uitishwe uchaguzi mdogo na kama wakishindwa sababu Zitto si mgombea wao, basi na iwe hivyo.”
Na huyu akaniandikia, “Makala yako imejaa ukweli mtupu, Zitto ni ndumilakuwili na mpenda madaraka, ni mtu wa hatari.” Na msomaji mwingine akasema: “Zitto akae chini na wazee wa chama wamshauri na kumpa mifano ya waliomtangulia naamini atabadilika.”
Kuna aliyeniambia, “Umeandika na kuhukumu ili kulinda wanasiasa maslahi ndani ya CHADEMA. Tuliokijenga chama kabla yenu na hao kina Zitto tunahuzunika mnavyozamisha jahazi.”
Maoni yakawa mengi, mara nikambiwa, “Mimi naona Zitto ana mpango wa kukisaliti chama maana tangu alipoteuliwa kuingia kamati ya madini, amekuwa ni kinyonga. Natoa ushauri kwa chama wampe masharti na asipotii afukuzwe, aende huko anakotaka.”
Mitazamo ni mingi, yuko aliyeema, “Ulichoandika kuhusu Zitto ni sahihi lakini mimi nasema pamoja na umaarufu wake wote, hata akiondoka au kufukuzwa bado CHADEMA kitabaki imara, natamani hilo litokee sasa.”
Laiti ningeweza kuyachapisha yote, ila Zitto atakuwa amebaini kuwa nilifanya kazi kama mwandishi nikitazama siasa ndani ya chama chake na si kumwonea yeye wala kiongozi yeyote.
Nanukuu ujumbe wa wasomaji kadhaa zaidi nikianza na huyu akisema, “Niko pamoja na wewe, Zitto amekuwa mwana mapinduzi, yaani imekuwa ndani ya Simba kuna Yanga.”
“Zitto ameshapata asali ndani ya ile kamati ya madini. Wanasiasa wetu ndivyo walivyo.”
Mwingine akasema, “Hivi ni kwa nini wasimuite wakamuulize na kama atabainika wamfukuze kuliko kukiua chama?”
“Nakubaliana na makala yako, kweli tumemchoka Zitto na mambo yake. Tumemsikia wakati wa kampeni jimboni kwake akiwaambia wananchi kuwa 2005 atarudi kama mgombea wa urais. Alijua njama za uporaji wa kura za Dk. Slaa, je chama kitampitisha kugombea? Hatumpendi wala umaarufu wake hautamsaidia.”
“Sisi wananchi wa Kigoma tunasema kuwa kama anaona anataka kwenda CCM ili amfurahishe rafiki yake Kikwete ni vema aende atuachie chama chetu kwani Kigoma tumewazoea. Hakuna kiongozi tuliyempenda Kigoma kama Dk. Amani Kabourou lakini njaa yake naye ilimkimbiza tukazoea, sasa sembuse Zitto.”
“Zitto amepoteza mwelekeo kila mahali. Yaani huku Kigoma hata akiamua kuondoka na uchaguzi kurudiwa, hapati robo ya kura alizopata uchaguzi wa mwaka huu. Ametuvua nguo watu wa Kigoma.”
“Nadhani kama kuna mashabiki wa Zitto, basi hapa Kigoma mimi ni namba moja. Lakini kwa matendo yake hayo watu wa huku tumemkinai mno.”
“Ulichomwambia Zitto ni kweli, mkumbushe habari za wkina Dk. Masumbuko Lamwai na umaarufu walioupata wakiwa kambi ya upinzani lakini walipohamia CCM wakapoteza mwelekeo kabisa.”
“Zitto ni msaliti wa aina yake, kama anafikiri bila yeye CHADEMA haifiki mbali basi atakuwa anajidanganya nafsi yake mwenyewe, sisi wafuasi wengi wa upinzani ni waelewa na shule inatusaidia ila sijui kama yeye shule ilimkomboa na huo uanaharakati wake kumbe ulikuwa lengo lake kubwa ilikuwa madaraka.”
“Mi namshauri Zitto afanye uamuzi wa kweli wa kutubia madhambi yake hayo, ndipo watu tutarudisha imani yetu kwake na atambue kuwa undumilakuwili ni kitu cha hatari. Ajue umaarufu wake umekuja kwa sababu yuko upinzani lakini akiamua kurudi huko CCM ajue amekwisha, hivi karogwa au kawaje jamani?!”
“Zitto kweli kwa sasa hajatulia, kinachonitisha ni nguvu ya mafisadi wanavyoweza kuwanunua hata wale tuliodhani ni watetezi wa wanyonge. Bado tuna kazi nzito ya kupambana na mafisadi.” Nahitimisha na ujumbe huu: “Ni kweli Zitto wa sasa si yule tuliyemfahamu na ubovu wake ulianza pale alipoteuliwa na Rais kuingia kwenye Kamati ya Madini, chama chake kilimkataza yeye akalazimisha. “Tayari ametangaza kugombea urais 2015. Wakati wa kampeni hakuwahi kutoa neno lolote kuhusu CCM, huyu kwa sasa ni mzigo. Amefikia hatua ya kumhujumu John Mnyika akidai eti aliunga mkono kufukuzwa kwa Kafulila na wenzake.”

SOURCE:TANZANIA DAIMA
 
Back
Top Bottom