Pirikapirika zangu baada ya Magharibi mitaa ya Kariakoo

FIKRA NASAHA

Member
May 22, 2023
8
8
prkr.png

Baada ya Maghribi, Mitaa ya Kariakoo

Nipo jijini Dar es Salama, vitongoji vya mitaa ya Kariakoo, unyounyo na rafiki yangu, tukitembea sako kwa bako, hamadi kibindoni tukajikuta tupo mtaa ya Msimbazi, kona na mtaa wa Magila.

Kwenye kijiwe hiki cha Kahawa, kumekusanyika wazee kwa vijana wapo himahima kama wapo kwenye Matwana, wakiongelea matokeo ya mpira kati yao na watani zao wa jadi. Aghlabu mazungumzo haya hutokana na ile hali ya kutamaukiwa na tamaa ya kupata ushindi tu.

Nikasimamisha masikio kama Sungura aliyeona mbwa wa Msasi, nipo angeange kusikiliza, sina ngoma sina maulidi, nasikiliza kinachojiri kwenye mpororo wa majaka ya majadiliano yale, wakiongelea makorowezo ya kile kilichojiri kabla...

Nikawasikia wakiongea kwa raghba, huku mzee mmoja wa makamu akitikisa bakora yake ya mkanja, akisema kwa hamaki kabisa; "...hii kamati ya ufundi ni bure kabisa, hivi wameshindwa nini kumtupia Kibuki yule sijui anaitwa nani yule, Mayenu sijui Mayele? Jini mmoja tu toka Komoro, wa kumpindisha kidole gumba cha mguu, ashindwe kupiga mpira. Na bado wanajiita wachawi, mbona..."

Mwingine akadakia; "Wanashangaza sana... yaani ovyoo kabisa!"

Huyu mwingine naye akiwa na miraa kinywani na huku mashavu yake yametuna kama anauguwa Matukwa; Weee! Unafanya mchezo na Wangwana, Mkongo yule, hakuna anae weza kumjaribu..."

Mwingine akaingila kati: Bongo kuna Wachawi!? Wao kazi kusumbua watu tu, usiku kwenye mapaa ya nyumba, harafu kwenye ishu za muhimu hawaonekani!

Mwingine akamuunga mkono kwa kusema; "...umeonaa eeh usiku kwaruuuu kwaruuuu kazi za muhimu hawazioni, yaani yule jamaa kasababisha baba mkwe kalazwa sipitali, kwa presha, yaani waganga wa Bongo ovyo kabisa..."

Na huyu akarukia; Sasa sijui kama ni waongo au wanazidiwa mbinu hapo ndo hatujajua...!

Bwana weee! Bongo kuna wachawi, wachawi wa Tanzania wana uchawi wa kuroga ndugu zao tu...!

Yule mzee aliyekamata bakora yake ya mkanja, akaongeza kwa kusema; "Kwanza huyu Mayele, anapaswa kushtakiwa, we uoni zile nywele zake kama vitunguu saumu, wazee wengi wanateswa na mengi kuhusiana na huyu kijana, sipitali zimejaa wagonjwa wa presha kwa ajili yake, tukimwachia anaweza kutuletea inalilahi hapa nchini, watoto zetu tukawaacha mayatima na wake zetu wakawa wajane..."

Sauti ikasikika toka nyuma; "Akamatwe kwa kweli na vinywele vyake kama dudu washa, kwanza kuweka nywele vile ni kinyume cha haki za binadamu..."

Akadakia mwingine; "Huyu sisi hatuendi kumfungulia mashtaka wala nini, tutamshtakia kwa Mungu tu, matokeo yake atayaona, albadiri moja tu ya mtama mkavu na yai viza vinamtosha, hawezi kutunyima raha..."

Sauti moja ndogo ikasikika; "Wallahi tusipokufa mwaka huu, hatufi milele nakwambia, si kwa mateso haya, kudadeki, hii nchi ngumu sana... Shubaa miti huyu laanakum chura pori huyu, mbinguni aendi huyu..."

Mwingine naye; "Yaani we acha tu, tumekuwa kama mwanamke aliyepaka liwa, iliyofumaniwa na mvua...!"

Mmoja akasema; "Tatizo sio Simba wala Mayele, tatizo Katiba ya nchi yetu, maana sheria ya nchi inaruhusu Simba kufungwa mara kwa mara, tukibadirisha katiba, hatutafungwa tena...."

Mmoja akauliza; "Hivi kweli mashabiki wa Dar mmeshindwa kweli kumtafutia jishangazi hapo Magomeni au kule Tandale kweli, jishangazi la haja, limtulize Mayele, kwani yule Ashura wa Tabata ni shabiki wa timu gani, hivi kweli ameshindwa kumteka nyara ile siku, leo ingekuwa raha mustarehe hapa!"

Na huyu naye; "Kwanza alicho kifanya Mayele jana kweli hakikubariki kabisa kwenye sheria za Fifa, yaani anamsindikiza mwenzie kwa kutetema daaaah!"

Kijana mmoja naye akachangia; "Tatizo huyu mzungu ni wa royo tua, kacheza danadana basi wakaona anaweza, wakamleta... Ila nasikia ni ajenti wa vifaa vya sensa!"

Sauti ikasikika ya jamaa mwingine, kidogo tende ilikuwa ishamkolea kichwani, akiongea kwa kigugumizi; "Hu-hu-huyu jjjamaa Ma-ma-ma-mayele si-si-sisio ji-ji-jina la-la-lake na-na-na ndo ma-ma-maana wa-wa-waki-ki-kiroga ji-ji-jina la Ma-ma-mayele ha-hapatikani na-na-na ji-ji-jina la-la-lake ni-ni-ninge-ninge wa-wa-tajia i-i-ila ta-ta-tati-titi-zo ha-ha-ham-m-mni-ni-nisa-sa-sali-li-limiagi...!"

Mmoja akakumbushia; Mie nawaambia, ile ni laana ya kwenda na mthalaba na jeneza kwenye thimba dei, ndio maana mthimu wote hu tutashindwa tu. tumewakathirisha midhimu ya mababu..."

Ghafla Swahiba wangu akanigusa bega, kaka unasikia adhana hiyoo, isha ishaingia, twende tukawahi hapo Msikiti wa Idrissa... Tukaongozana kuelekea kwenye kufaridhika...



MSAMIATI WA MANENO MAGUMU
  • 1. Angeange: Kuonyesha umakini au utayari wa mtu au kitu
  • 2. Kibuki: Aina ya Majini
  • 3. Kufaridhika: Kulazimika, Ulazima, wajibu
  • 4. Kutamaukiwa, Tamauka: Kutokuwa na tamaa au matarajio ya kupata kitu. Kata tamaa
  • 5. Liwa: Rojo ya mliwa na sandali inayotumika kuwa ni manukato au dawa ya joto la Ngozi.
  • 6. Majaka: Pasipo kufuata utaratibu uliowekwa.
  • 7. Makorowezo: Hali ya kuchanganyikiwa, hususani katika kufanya jambo fulani.
  • 8. Matukwa au Matukwi: Ugonjwa wa kuvimba mashavu.
  • 9. Matwana: Lori au basi la kubeba abiria Pamoja na mizigo... mf: Chai Maharage
  • 10. Miraa: Mirungi
  • 11. Mkanja: Mti unaomea porini na kutoa fimbo ndefu na nyembamba
  • 12. Mpororo: Mfuatano wa vitu au watu.
  • 13. Msasi: Mwindaji wa wanyamapori.
  • 14. Raghba: Hamu inayomfanya mtu atende jambo fulani, muhemko, shauku, haja.
  • 15. Sako kwa bako/Sago kwa Bako: Andamana au tembea pamoja ubavu kwa ubavu
  • 16. Sina ngoma sina maulidi: Kutofurahia jambo
  • 17. Unyounyo, Unyo: Kufuatana Pamoja kwa nyuma, andamana.
  • 18. Wangwana: Waswahili wa Kongo.
 
Shukrani nimepata maana ya neno "unyounyo" niliyokuwa naitafuta na kujikuta naangukia jf kwenye uzi huu.
 
Back
Top Bottom