Pinda maji shingoni

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,329
33,139
pinda.jpg
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.


KWA UFUPI

  • Wasomi, wananchi wataka naye ang’oke kwa madai ya kushindwa kusimamia Serikali.

Dar/mikoani. Watu wa kada mbalimbali wameupongeza uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne waliotajwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, huku wakimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda naye kufuata nyayo hizo.

Wasomi na wanasiasa hao waliozungumza na gazeti hili mbali na kupongeza hatua hiyo, wamesema tatizo linaloikabili nchi ni kuwa na mfumo mbovu wa utawala hivyo kupendekeza wote waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria na siyo kuhukumiwa mawaziri pekee.

Juzi ripoti ya Kamati ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wake, James Lembeli na kuwang’oa mawaziri hao kutokana na kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Waziri Mkuu Pinda alilitangazia bunge kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao, baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.

Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.

Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Katibu Mkuu wa (Chadema) Dk Willbrod Slaa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwangoye na Bukene wilayani Nzega mkoani Tabora, alisema kuondolewa kwa mawaziri hao haitoshi kwani anayepaswa kujiuzulu ni waziri mkuu kutokana na kuruhusu Polisi na vyombo vingine vya dola kuwapiga watu, kauli ambayo aliitoa bungeni.

“Wala msilindane kama ripoti ya kamati imebainisha unyama huu, basi wasiishie kwa hao mawaziri wanne, waziri mkuu naye anapaswa kupima na kujiuzulu, kwani hii itasaidia pia kuwaondoa mawaziri wengine ambao wamekuwa wakielezwa na CCM kuwa ni mzigo,” alibainisha Dk Slaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema, kung’olewa kwa mawaziri hao hakutoshi bali hata Waziri Mkuu Pinda naye awajibike.

“Hao mawaziri wameng’olewa kutokana na wizara zao kukosea, lakini Waziri Mkuu Pinda ndiye msimamizi wa kazi za Serikali, kama wizara zimekosea na yeye amekosea hivyo awajibike mwenyewe na kama atagoma basi mkuu wake amwajibishe kwani ameshindwa kuwasimamia mawaziri wake,” alisema Dk Bisimba.

Aliongeza: “Pinda angeweza kupona endapo angechukua hatua mapema za kuwawajibisha hao mawaziri pindi taarifa alipozipata za uteswaji, ubakaji, mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia na si kusubiri hadi Bunge lichachamae. Hapa Serikali yake imevurunda, naye aondoke.”

Dk Bisimba alisema; “Mawaziri sawa wameng’olewa lakini watendaji wote waliohusika wachukuliwe hatua, ikiwemo kufunguliwa mashtaka mahakamani kutokana na kusababisha vifo, mateso na majeraha kwa watu na mifugo.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema; “Waziri Mkuu naye anatakiwa kuondoka kwani yeye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali na kilichotokea kilikuwa chini yake.”

Aliongeza; “Ngoja tuone labda alifikiri akijiuzulu wakati Rais hayupo anaweza kuiweka nchi katika matatizo hivyo ngoja tusubiri itakuwaje.”

Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema; “Nadhani Baraza zima la mawaziri linatakiwa kumulikwa maana operesheni hii ilipitishwa na mawaziri wote, sasa iweje wawajibike wanne tu.”

Alisema ni jambo la kushangaza kutokea kwa matukio ya kutisha katika operesheni hiyo bila vyombo vya ulinzi na usalama vya mikoa na wilaya kubaini lolote. “Inaonekana kama waliotekeleza operesheni hii walijipanga na walijua jambo wanalokwenda kulifanya,” aliongeza.

Aliongeza; “Bunge limefanya kazi yake lakini jambo kubwa ambalo linatakiwa kufanyika ni kuhakikisha kuwa wote waliohusika kutekeleza operesheni hiyo wanachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.”

Mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Gulam Obela alimpongeza Waziri Kagasheki kwa kujiuzulu, ila alisikitishwa na Dk Mathayo, Dk Nchimbi na Nahodha waliosubiri kuondolewa na Rais Kikwete.

“Nampongeza Kagasheki kwani amefuata nyayo za Edward Lowassa ambaye yeye alijiuzulu kutokana na makosa ya viongozi wa chini yake, sasa Kagasheki japo hakushiriki unyama wa Operesheni Tokomeza Ujangili lakini amejiuzulu kwa ridhaa yake,” alisema Obela.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Peter Maina alisema; “Ni jambo zuri kuona utaratibu uliokuwepo miaka ya nyuma wa viongozi na watendaji wa Serikali kujiuzuru unarejea.”

Profesa Maina ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema miaka ya 1970, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alijiuzulu kutokana na kukithiri kwa matukio ya kuuawa kwa watu waliokuwa wakidhaniwa kuwa ni wachawi.

“Siyo Mwinyi tu, hata aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Peter Kisumo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Marko Mabara pamoja na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Usalama, Peter Siyovelwa walijiuzulu. Mawaziri hawa wanne wamefanya vyema kuonyesha uwajibikaji kwa makosa yaliyofanywa na waliopo chini yao” alisema Maina.

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally alikuwa na mtazamo tofauti kuhusu hatua hiyo kwa maelezo kuwa jambo kubwa linalotakiwa kutazamwa ni mfumo wa utawala.

“Kama utakumbuka sakata la Richmond watu walijiuzulu, sakata la akina Jairo na hata vurugu zilizotokea mkoani Mtwara kupinga gesi kutoka nje ya mkoa huo,” alisema na kuongeza; “Matukio hayo yote bunge liliunda Kamati ambazo zilitoa ripoti, lakini kuna ripoti ambazo hazijawekwa wazi na hata kama zimewekwa wazi mapendekezo yake hayajatekelezwa hadi leo hii,” alisema.
Bashiru alitolea mfano Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kwa kipindi kifupi imekuwa na mawaziri watatu tofauti, lakini wote wameondoka kwa mtindo unaofanana jambo ambalo linaonyesha kuwa tatizo ni mfumo.

“Bunge linatakiwa kutazama jambo hili kwa kina ili kuepuka kutumiwa kisiasa, ndani ya miaka 10 Bunge letu limekuwa na maspika wawili ambao wameunda kamati nyingi za kuchunguza mambo mbalimbali, lakini bado ripoti hatuzioni na hata utekelezaji hakuna,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kitendo hicho ni matokeo ya watendaji wa Serikali, hususani vyombo vya dola kukosa uadilifu.

Alisema operesheni hiyo badala ya kutokomeza ujangili, imefanya kazi ya kutokomeza wananchi kwa kuwatesa na kuwanyanyasa.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete anapaswa kutafakari juu ya utendaji kazi wa mawaziri, kwa kuwa wengi wanaonekana kuwa mzigo.

“Ukweli utabaki kuwa Rais anapaswa kuangalia watendaji wake, mawaziri wengi ni mzigo wakiongozwa na Waziri wa Tamisemi (Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi) na Waziri wa Elimu, ”alisema Lipumba.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege alisema; “Nimewasikiliza baadhi yao wakizungumzia kuhusu hilo sidhani kama kuna tatizo hiyo ni sehemu ya uwajibikiaji unapoona wengi wanakulalamikia unapofanya kazi siyo wote watapongeza tatizo kubwa ni mawasiliano ya utekelezaji wa ile operesheni.”

Katibu wa Chadema Wilaya ya Simanjiro, Frank Oleleshwa alisema huo ni uthibitisho wa wazi kabisa kuwa Rais Kikwete amekuwa akiteua watendaji wabovu na dhaifu kwani haiwezekani kila wakati viongozi wabovu wanapewa nafasi ya kuongoza.

Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei alisema kuwa operesheni hiyo iliacha makovu mengi hususan kwa raia ambao ni wanyonge hapa nchini na kushangaa hatua kutochukuliwa mapema kwa watu kutowajibishwa.

“Kila siku nilikuwa naomba kwa Mungu kuhusu hawa viongozi wabovu nashukuru salamu zangu zimesikika hatimaye yametimia, Crime does not pay(uhalifu haulipi) ipo siku ukweli utajulikana tu,” alisema Mtei.

Imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Fidelis Butahe, Elizabeth Edward, (Dar), Frederick Katulanda (Tabora), Joseph Lyimo (Manyara)na Moses Mashalla (Arusha). Chanzo. Pinda maji shingoni - Kitaifa - mwananchi.co.tz







Mzee Pinda nae Rais ampumzishe amesha zeeka Kisiasa. Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda naye

amekali kuti kavu........

 
Huyu mtoto wa mkulima HAPATI HATA DK YA KUPUMUA..!Afya yake mpaka imekuwa DHAHIFU...!Yule wa kabinti kidogo anapumua sasa kwan mawaziri ndio habari za MJINI.
 
Yeye ndiye aliyeruhusu watu kujichukulia sheria mkononi, "Na wapigwe tu, tumechoka". Ni wakati wake kujiuzulu kwa vile asivyozingatia utawala wa sheria.


pinda.jpg
Wapigwe tu na sasa kesi iko mahakamani na anaanza kupigwa tu mwenyewe kwa kuwa tumemchoka kwa kutuchokesha na kuipindisha serikali.
 
Hata kama ataondoka leo, bado itakuwa amechelewa sana labda adhabu pekee anayostahili sio ku-resign bali kupigiwa kura ya kutokuwa na imani nae kabisa na kisha kura husika ndiyo imuondoe. It's very unfortunately CCM can't do this pamoja na kelele zote.
 
Mpaka 2015 kila mbunge wa ccm atakuwa ameonja uwaziri hata wiki moja.hongera ccm awamu ya nne.lakini pia lembeli ripoti yake inmeshindwa kuchana nyavu kama ile ya mwakyembe huyu pinda hakustaili kubaki hata kidogo huyu ndiye kiranja mzigo hasaaaaaaaaaaaaa!!!!!!!!!!!!!
 
Back
Top Bottom