Pinda acha POROJO, chukua hatua | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Pinda acha POROJO, chukua hatua

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Pdidy, Oct 3, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Oct 3, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,132
  Likes Received: 5,571
  Trophy Points: 280
  Dkt Slaa: Pinda acha kulalamika, chukua hatua
  Thursday, 01 October 2009 16:09
  Na Waandishi Wetu

  KAULI za hivi karibuni za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa Watanzania waache kununua suti kwa sababu zina gharama kubwa na ile ya kutaka viongozi waandamizi kuacha kununua magari ya kifahari zimeibua mjadala na upinzani mkubwa.

  Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na Majira wameonyesha kutokubaliana na kiongozi huyo na wengine kumshambulia kuwa ameanza kulalamika badala ya kuonyesha kuwa mtendaji.

  Mbunge wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa alimtaka Pinda kuwa Waziri Mkuu Mtendaji na siyo mlalamikaji.

  Dkt. Slaa alisema kuwa Waziri Mkuu ni mtendaji na ndiye mwenye maamuzi, anachotakiwa kufanya ni kuwachukulia hatua wale wote wanaokwenda kinyume na maagizo yake.

  "Pinda analalamika kama mimi ninavyolalamika kuhusu mashangingi, kambi ya upinzani tumelisemea sana hilo toka mwaka 1996, tulisema magari yanayotakiwa kutumika yawe Suzuki tukatoa mifano mingi wenzetu wa nchi ya India viongozi walivyo na utaratibu
  mzuri wa kutumia magari.

  "Lakini hatukusikilizwa, kama kauli yetu ingetekelezwa kutoka mwaka huo tulipokuwa
  tunapiga kelele tungekuwa tumejenga zahanati ngapi nchini sasa?" alihoji.

  Alisema kuwa kinachomuudhi ni pale anaposikia Waziri Mkuu analalamika wakati yeye anatakiwa kuchukua hatua na kwamba tatizo kubwa lililopo nchini ni kwamba hakuna watu wanaofikiria na wanaobuni na ndio maana analazimika kusema kuwa serikali imechoka.

  Akizungumzia vazi la suti, Dkt. Slaa alisema kuwa anaunga mkono kauli ya Bw. Pinda kwa sababu anashangazwa na baadhi ya viongozi wanaokwenda kukagua bustani au mashamba wakiwa amevaa suti.

  "Sasa hivi hata bwana maji utamkuta anakwenda kukagua bomba akiwa amevaa suti na ndio maana mimi unikuti hata siku moja nikiwa nimevaa suti ninajivalia mgololi wangu na kama wangekuwa wanaruhusu ningekuwa ninauvaa hata bungeni," alisema.

  Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Anna Abdallah aliunga mkono kauli ya Bw, Pinda akisema kuwa wanaovaa suti sehemu zisizohusika anawaona kama weu na ndio maana kazi nyingi zina mavazi yake rasmi.

  "Kila kazi ina miiko yake, sisemi kuwa watu wasiwe nadhifu, ni vema turudi tulikotoka, ila sijaona mbunge anayekwenda kuwatembelea wananchi wake akiwa amevaa suti labda kwa Dar es Salaam, ila ninachoomba kuwepo vazi la kazi na rasmi," alisema.

  Naye Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Hassan Zungu akizungumzia magari ya kifahari alisema kuwa suala hilo aliwahi kulipigia kelele bungeni na kwamba anashangazwa sana kuona kiongozi akiwa ametinga kwenye gari kubwa la kifahari akienda jimboni huku wananchi wake wakiwa hawana mbele wala nyuma.

  Lakini Bi. Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) alisema umaskini wa Watanzania hauwezi kwisha kwa kutovaa suti kwani wanaovaa vazi hilo ni matajiri na viongozi ambao ni sehemu ndogo.

  Bi. Mdee alisema kuwa vazi hilo hupendelewa kuvaliwa na viongozi wa serikali na watu wenye uwezo kwa sababu wanamudu gharama za manunuzi.

  "Nashangaa kusikia Waziri Mkuu kusema kuwa umaskini unachangiwa na kuvaa suti hii sio kweli kwani wavaaji wa vazi hilo hawajafika watu 2,000, kinachotakiwa aangalie kitu ambacho kinasababisha umaskini na sio hili analolisema," alisema Bi. Mdee.

  Alisema kuwa kama Pinda anataka wananchi wavae mavazi mengine serikali inatakiwa iboreshe viwanda vya kutengeneza nguo ili Watanzania wasiagize nguo kutoka nje, zikiwemo suti ambazo anasema zinauzwa kwa gharama kubwa.chukua hatua

  "Kwa kweli sisi ndio tunazunguka mikoani na tunaona Watanzania mavazi wanayovaa ni ya kawaida ikiwemo mitumba ambayo wanamudu gharama zake," alisema Bi. Mdee.

  Kwa upande wake, Mbunge wa Micheweni kwa chama cha wananchi (CUF) Bw. Shoka Khamis Juma alisema kuwa kuvaa suti au kutokuvaa ni changuo la mtu.

  Alisema kuwa kinachotakiwa Waziri Mkuu asiingilie utamaduni wa mtu kumtaka avae vazi gani na pia vazi hilo halisababishi umaskini wa nchi.

  "Kama Waziri mkuu anataka watu waache kuvaa suti angeanza kuonesha mfano kwa kuwapiga marufuku watumishi wa serikali kama inawanunulia nguo hizo, lakini kama haiwanunulii haina haja ya kuwapangia.

  Naye mkazi wa jiji Bw.Isiaka Mdoe alisema uvaaji wa suti umetokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia na watu wameanza kuiga vitu kutoka nchi za Magharibi vikiwemo na mavazi.

  Jana Pinda alikaririwa akisema kuwa vazi la suti wanalovaa Watanzania ni la gharama kubwa ukilinganisha na kipato chao cha kawaida, na hivyo kushauri wavae mavazi mengine ya kawaida.

  Imeandikwa na Gladness Mboma, Arusha, Rehema Mohamed na Rehema Mwakasese, Dar
   
Loading...