Pinda abaini madudu chuo kikuu Dodoma

Mallaba

JF-Expert Member
Jan 30, 2008
2,554
47
0diggsdigg

dompinda.jpg
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisisitiza jambo katika mkutano wa usuluhishi baina ya wahadhiri wa chuo kikuu cha Dodoma UDOM na utawala. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk James Msekela. Picha na Habel Chidawali.

Habel Chidawali, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekiri kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kina matatizo makubwa likiwemo suala la uongozi kwa baadhi ya vitengo.

Kutokana na kubaini hali hiyo, jana, Pinda alimuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufika mara moja chuoni hapo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kueleza kuwa mkaguzi tayari alikuwa njiani na kwamba kazi hiyo itaanza mara moja leo.

Mbali na hilo pia alijitwika mzigo pale alipoomba wahadhiri wa chuo hicho kumbebesha mzigo wa madeni yote, ambayo yalitokana na mapunjo waliyokuwa wakifanyiwa na kuwaahidi kuwa yote yatalipwa mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Pinda alisema hayo jana alipokuwa akisikiliza matatizo na kero za wahadhiri wa chuo hicho, ambao waliingia katika mgomo tangu mwanzo mwa wiki iliyopita kutokana na madai mbalimbali yakiwemo fedha za kujikimu pamoja na makato ya mishahara yao yasiyo na maelezo.

Akiwa katika Jengo la Chimwaga, Pinda ambaye alipokewa na nyimbo kutoka kwa wahadhiri hao wakisema ni ‘mtoto wa mkulima’ na kwamba wangetegemea ukombozi kutoka mikononi mwake, hakuficha hisia zake na kusema wazi kuwa Udom ina matatizo makubwa likiwemo suala la uongozi.

Alisema kuwa yapo matatizo ndani ya chuo hicho ambayo hayakupaswa kuwepo hadi jana, lakini kutokana na uongozi uliopo kushindwa kuwashirikisha wanachuo pamoja na wahadhiri wao ndiyo maana yamefikia katika hatua hiyo.

Desemba 20 mwaka jana chuo hicho kiliingia katika mgogoro baada ya wanafunzi wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii, kuitisha maandamano makubwa yaliyozimwa kwa mabomu ya polisi jambo lililowalazimu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kufika chuoni hapo kwa ndege ya kukodi.

Hata hivyo moto wa wanachuo hao uliwashwa tena Jumatatu ya Januari 10 mwaka huu, baada ya wale wa Kitivo cha Elimu kuandamana ambapo katika maandamano hayo polisi walishindwa kuzima maandamano licha ya kupiga mabomu ya machozi, lakini walizidiwa mbinu za wanachuo hadi wakafika katika eneo lililokusudiwa.

Juzi pia wanachuo hao Kitivo cha Elimu walifanya kile kilichoonekana kama ni kiini macho baada ya kuteka gari la Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, John Tupa kwa zaidi ya saa nne wakishinikiza kuonana na Waziri Mkuu bila ya mafanikio.

“Hapa nakiri kuwa kuna matatizo makubwa ikiwemo pamoja na uongozi, kwani sioni kwa nini mnashindwa kufanya mambo kwa kutumia ubunifu na mnaacha yanakuwa makubwa kiasi hiki? Hii inaonyesha kuwa mlishindwa kuwashirikisha kwa kila jambo watu mnaowaongoza na mkawa wasiri mno,” alisema Pinda.

Jana katika mazungumzo yao mbele ya Waziri Mkuu, wahadhiri walisema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa kwa kipindi kirefu na Makamu Mkuu wa Chuo katika Idara ya Utawala na Fedha, Profesa Shaaban Mlacha ambaye walimtaka Waziri Mkuu kuondoka naye jana hiyo kwani walisema yeye ndiye chanzo cha kuibiwa fedha zao.

Wahadhiri hao walisema kuwa kumekuwa na wizi mkubwa ambao Udom hawajapata kuuona na umekuwa ni wizi wa hadharani, lakini kila wanapotaka kuhoji wanakutana na majibu ya ukatili kutoka kwa Mlacha.

"Kumekuwa na wizi mkubwa ambao katika maisha yangu sijapata kuuona na ninasema bila woga kuwa huyo Mlacha ndiyo chanzo cha migogoro yote mheshimiwa Waziri Mkuu na pamoja naye, lakini kuna viongozi hapa ambao hawaitakii mema nchi hii pamoja na chuo hiki kwa ujumla kama ni hivyo basi waondoke mara moja ama toa tamko wewe sisi tunalipwa lini,” alisema Mchungaji Dk Diana ambaye ni mmoja wa wahadhiri waliogoma.

Mhadhiri huyo alisema kuwa kila mara wanapofika kwa Mlacha wamekuwa wakikemewa kama mbwa jambo linalowapa woga hata wa kufuatilia madai yao mengine na kuwafanya kukosa ari ya kufanya kazi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhri hao (Udomasa), Iddy Mwerangi aliutaka uongozi wa chuo hicho kuwaomba radhi kutokana na taarifa zilizoripotiwa katika vyombo vya habari zikimnukuu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula kwamba madai ya wahadhiri hao hayakuwa ya msingi.

Kutokana na kauli hiyo ilimlazimu Pinda kumsimamisha Profesa Kikula ambaye aliomba radhi mbele ya mkutano wa wahadhiri hao na wakapokea ombi lake kwa kumpigia makofi ishara ya kuwa wamemsamehe, lakini kila lilipotajwa jina la Mlacha walikuwa wakizomea na kumuita kondoo mweusi.

Pinda aliwataka kukubaliana na wazo lake la kumleta CAG kwa kile alichosema kuwa Kamati ya Makatibu aliyoituma chuoni hapo kabla, ilibaini mapungufu makubwa katika eneo la fedha na kwamba mtu pekee atakayeweza kumaliza hayo yote ni Mkaguzi Mkuu.

“Ninyi mnasema ni bora huyu Mlacha akubali kulipa madeni yenu pamoja na kujiuzulu ama niondoke naye, lakini bado inawezekana kuna na wengine la huyu niachieni nalipeleka kunakohusika, lakini lazima kwanza aje akaguliwe kuanzia kesho (leo) ili kujibu yale atakayotakiwa kufanya hivyo naomba mvumilie kwani mambo yameiva sasa,” alisema Pinda.

Alisema kuwa amempa muda wa wiki mbili mkaguzi huyo kuwa ametoa taarifa kwa usahihi ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki huku akisisitiza kuwa wale ambao wana madai yao basi waandike kwa majina na kumkabidhi yeye Pinda ili naye ayawasilishwe Hazina.

Kwa upande wa wanachuo alisema kuwa alibaini mambo mengi pia ikiwemo suala la upungufu wa vifaa vya kujifunzia pamoja na chuo kuendesha mafunzo ya nadharia bila vitendo jambo alilosema kuwa ameliundia tume kwa ajili ya kulishughulikia.
 
Back
Top Bottom