Yoyo Zhou
Senior Member
- Jun 16, 2020
- 169
- 287
Kufuatia mahitaji ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya haraka ya teknolojia ya nishati mpya duniani, Afrika imeanzisha mapinduzi ya pikipiki ya umeme. Kwa upande wa gharama, bei ya wastani ya pikipiki ya umeme ni sawa na ile ya pikipiki ya kawaida ya mafuta bila betri, lakini gharama ya matumizi ya pikipiki ya umeme ni kama nusu ya gharama ya pikipiki ya mafuta. Hivi sasa, soko la pikipiki ya umeme barani Afrika linapanuka kwa wastani wa asilimia 7.8 kwa mwaka.
Mwaka huu, serikali ya Rwanda imetangaza kutenga dola milioni 300 katika mpango wa kuhimiza maendeleo ya kijani, ikiwa ni pamoja na kukuza mageuzi ya pikipiki ya nishati safi, na kubadilisha pikipiki 100,000 za mafuta kuwa pikipiki za umeme. Licha ya Rwanda, nchi nyingine za Afrika pia zinazingatia sana matumizi ya nishati safi katika uchukuzi na usafiri. Inatabiriwa kuwa soko la usafiri wa nishati safi barani Afrika litaongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 17 mwaka 2025 hadi dola bilioni 28.3 mwaka 2030. Hivi sasa, idadi ya pikipiki za umeme inaongezeka kwa kasi kaitka nchi za Afrika haswa Nigeria, Kenya, Malawi na Afrika Kusini.
Katika mchakato wa mabadiliko haya muhimu barani Afrika, China, ikiwa mshirika mkubwa wa maendeleo wa Afrika, hakika haitakosekana. Kampuni ya Transsion ya China inayojulikana kutokana na utengenezaji wa simu za mkononi barani Afrika, sasa pia imejianza utengenezaji wa pikipiki za umeme barani Afrika. Mwaka 2023, Transsion ilizindua pikipiki yake ya kwanza ya umeme TankVolt nchini Uganda, na kuingia katika soko la pikipiki za umeme barani Afrika. Mwaka huu, Transsion iliongeza masoko mengine manne katika nchi za Nigeria, Kenya, Tanzania na Ethiopia, ikitarajia kustawi zaidi kupitia ushirikiano na serikali na makampuni ya kienyeji. Transsion imechukua uzoefu wa maendeleo ya magari ya umeme nchini China, na kutoa huduma inayoendana na mazingira maalum ya bara la Afrika. Pikipiki zake za umeme zina betri zinazoweza kutolewa na kubadilishwa moja kwa moja, na pia kampuni hiyo inakodisha betri kwa watu wanaotumia pikipiki za umeme.
Makampuni ya Afrika pia yanatafuta ushirikiano na makampuni ya China. Spiro ni kampuni kubwa zaidi ya pikipiki za umeme barani Afrika. Hadi sasa, kampuni hiyo imeuza zaidi ya pikipiki 17,000 za umeme nchini Togo, Benin, Kenya na Rwanda, na kwa kushirikiana na makampuni ya China, imepanga kuuza pikipiki 500,000 za umeme zinazotengenezwa nchini China katika nchi za Afrika ndani ya miaka 5.
Makampuni mengine mawili makubwa barani Afrika, Ampersand na Roam, pia yanashirikiana na makampuni ya China katika teknolojia za betri na mnyororo wa ugavi ili kupunguza gharama na kuboresha ubora wa bidhaa zao. Gigmile ni kampuni nyingine ya usafiri kutoka Afrika Magharibi, miaka miwili iliyopita, iliingiza kundi la kwanza la pikipiki za umeme za China nchini Nigeria, na sasa ina idadi kubwa zaidi ya pikipiki za umeme nchini humo. Mwanzilishi wake, Kayode Adeyink, anatarajia ushirikiano wa kina zaidi na China. Amesema, anaamini kwamba China itachangia zaidi mustakabali wa Afrika, na uzoefu wa China katika maendeleo ya miundombinu na teknolojia unaweza kuwa injini ya maendeleo ya Afrika.