chakii
JF-Expert Member
- Sep 15, 2013
- 19,696
- 22,729
Mwenyezi Mungu msaidie apone mapema.
=======
Kwa ufupi
Loyani amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili ikiwa ni pamoja na kunyofolewa sikio na kuvunjwa taya.
Mmiliki wa Kambi ya Utalii ya Maramboi, Wilbard Chambulo amezungumzia mkasa wa mfanyakazi wake Kilopa Loyani (46) kushambuliwa na simba na kujeruhiwa.
Loyani amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili ikiwa ni pamoja na kunyofolewa sikio na kuvunjwa taya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Chambulo alisema Aprili 22 saa tisa usiku, akiwa amelala kwenye hema kambini hapo aliamshwa na sauti ya kelele za kuomba msaada kutoka kwa Loyani ambaye ni mlinzi.
“Nilishtuka nikawasha taa kabla ya kuzima kwa sababu ya usalama, baadaye niliitwa kwa radio call na askari wa Tarangire. Mlinzi huyo alikuwa kwenye korido ya nyumba ya wageni iitwayo Simba, ndipo alipovamiwa na alipiga kelele kuomba msaada,” alisema.
“Kwenye korido alikuwa na mwenzake ambaye alimsaidia kupiga kelele, tulifika kumuokoa tukawaona simba watatu, mmoja dume na majike mawili. Hatukuweza kuwafanya chochote kutokana na sheria, badala yake nilichukua gari na kumpeleka mgonjwa hospitali.”
Alisema mlinzi huyo amejeruhiwa upande mmoja wa uso na sikio la kushoto lilinyofolewa na pia alivunjwa taya.
Chambulo alisema walimfikisha Loyani katika Hospitali ya Karatu alikopatiwa huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na kuongezwa damu na baadaye alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
“Amelazwa KCMC na amefanyiwa upasuaji mara mbili kwenye taya. Nashukuru hali yake inaendelea vyema kwa sababu kuna wakati anazungumza,” alisema mmiliki huyo wa kambi ya utalii.
Chambulo alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea kwenye kambi hiyo na aliziomba mamlaka husika kuchukua hatua ya kuzuia madhara kwa watu kwa kudhibiti wanyama wakali wakiwamo simba.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Minjingu ilipo kambi hiyo, Bariki Kisiri alisema hilo ni tukio la kwanza kijijini hapo lakini ana taarifa kuwa kuna mtu aliuawa na simba mwezi uliopita kwenye Kijiji cha Vilima Vitatu kilichopo jirani.
“Shambulio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji changu, lakini nina taarifa kuwa kijiji cha jirani kuna mtu aliuawa mwezi uliopita, tumetoa taarifa kwenye Idara ya Wanyamapori bado hatua hazijachukuliwa,” alisema.
Chanzo: Mwananchi