Paul Scholes: Dhahabu iliyonyimwa thamani

Matanga

JF-Expert Member
Nov 13, 2019
2,281
3,973
Wakati macho na akili za wapenda soka wote wa Tanzania zikiwa kule Maseru, Lesotho; sehemu pekee ambayo pengine Taifa Stars inaweza ikaandika historia nyingine katika soka kwa kufuzu kwa mara pili Michuano ya Mataifa ya Africa, fikra zangu zimenituma kutumia fursa hii kufikisha salam zangu za heri ya siku ya kuzaliwa kwa mwanadamu mwenye jina halali la PAUL.

Achana na Paul Makonda, wala si Paul Pogba mwenye vituko kila leo, achana ni Paul Gazza aliyefunga pingu za maisha na cocaine, wala usimfikirie mtoto wa Kiargentina mjukuu wa bibi pale Turin Paul Dyabala. Huyu ni Paul Scholes. Ni Paul mwenye umiliki halali wa miguu yenye dhahabu.

Ni siku tatu zimepita toka Paul asherekee siku yake ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 44. Kama ilivyo desturi ya kiungwana katika soka tunapenda kumtakia heri na fanaka katika maisha mwandamu huyu wa kipekee.

Anaitwa Paul Scholes mzaliwa wa pale Salford akakulia Langley Middleton katika ardhi ya malkia Elizabeth pale United Kingdom, akikua katika makuzi ya kucheza cricket na soka akiwa shuleni.

Paul Scholes mwanadamu mwenye sura nyekundu iliyoshabihiana vilivyo na walemavu wa ngozi maarufu kama albino, akiwa na nyele nyekundu, aliweka alama zisizosahaulika katika ulimwengu wa soka.

Ni Paul aliyejimilikisha dimba la kati la uwanja licha ya kukulia katika nafasi ya ushambuliaji katika makuzi yake ya soka.

Akiwa na miguu ya dhahabu, ubongo wenye ufanisi wa hali wa juu, macho angavu yenye uwezo wa kuona angle zote za uwanja, viliufanya ule mwili imara uliokamilika kisawasawa kuwa na tija katika uwekaji wa alama zisizofutika uwanjani. Uwezo mkubwa wa kupora mipira toka kwa maadui, kupiga passi kutoka eneo lolote la uwanja, bila kusahau uwezo mkubwa wa kufunga magoli yakipekee nje ya box.

Kutokana na uwezo mkubwa alionao Paul huyu, ulimfanya kucheza maeneo mengi zaidi katika uwanja kulingana na majukumu ya mechi husika, alicheza kama kiungo mkabaji wa chini (defensive), kiungo mshambuliaji (offensive), kiungo wa pembeni, na wakati mwingi alitumika kama kiungo mchezeshaji toka chini (deep-lying playmaker) kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi za mbali katika ufanisi wa juu zaidi. Huyu kitaalam alijulikana kama versatile midfielder, kiungo mwenye uwezo wa kucheza zaidi ya nafasi moja.

Wala haikushangaza kuona Paul anafanya yale ambayo watangazaji wa soka waliyatunuku kwa majina mbalimbali ya kuvutia, watu kama Jim Beglin, John Champion, Peter Drury walitunuku sifa zilizosadifu uwezo wa Paul kila weekend pale EPL. Paul alikuwa ni maaana halisi ya shetani mwekundu (Red Devil).

Jezi yake ilikuwa halali ni vazi la shetani iliyojaaa jasho la damu. Na huyu ndie aliyehalalisha bahadhi ya matokeo muhimu katika ile Manchester ya sir Alex Furgerson na kuufanya Old Trafford kuwa kweli ni theatre of dreams.

Paul aliifanya Manchester kuwa hatare zaidi nyakati zote za mechi kwani haikushangaza kuona wakati wao wakiwa wanashambuliwa ile kupepesa macho ukashuhudia ronaldo au Giggs anashangilia kwenye kibendera cha kona cha team pinzani, ni kazi ya Paul hiyoo. Kupiga pasi za magoli kutoka kwenye hatua 6 ya box lao mpaka kumkuta mchezaji wao katika eneo hatare la wapinzani. Manchester yenye Paul haikuhitaji passi zaidi ya mbili kufika golini.

Wakati Fulani pale St James Park Manchester Utd ilikuwa ikicheza na Newcastle wakati wanashambuliwa wao; ghafla Paul aliunasa mpira wakati huo Ronaldo akaanza kukimbia kwa speed kulekea goli la wapinzani huku akionesha kidole kwa Paul kuashiria amweke mpira ule. Cha kushangaza wakati Paul anaupiga ule mpira kabla haujafika kwa CR7, tayari Ronaldo alinyanyua dole gumba juu kumwonesha Paul nimekubali kaka. Kwa ufanisi wa hali ya juu, mpira ule ulimkuta Ronaldo palepale alipo. Huyu ndio Paul.

Mwaka 2011 kiungo fundi wa Spain xavi Hernandez alinukuliwa akisema kuwa Paul ndio kiungo wake bora zaidi kumwona akicheza katika miaka 15-20. Ndiyooo! Kizuri kisifiwee. Umesahau Thierry Henry alisema mini kuhusu Paul? Alisema Paul ndio mchezaji bora wa muda wote wa EPL kwake yeye kwani ana uwezo wa kufanya kile anachokitaka wakati wowote.

Kiungo mkongwe na kocha mwenye historia ya pekee pale Bernabeu, Zizzou, hakupepesa macho kukiri kuwa ni furaha zaidi kumuona Paul akicheza. Ni mchezaji aliyebarikiwa sana; anajua nini afanye na kwa wakati gani kulingana na uzito wa mechi husika.

Mnamkumbuka yule mbabe wa Kiholanzi mvaa miwani wa Turin Edgar Davids wala hakuwa mbali kuusadifu ufundi alionao Paul katikati mwa kiwanja. Ni kweli, pengine wahuni hukubaliana lakini hii sifa Paul anastahili kwelikweli. Sio wao tu, hata fundi wa Kiitaliano Andre Pirlo alitanua kinywa chake kuusifu uwezo wa Paul huyu.

Wakati Andres Iniesta akisema kipindi bora zaidi Barcelona ni nyakati Pep Guardiola anaichukua Barca alikuwa akitenga muda maalumu na kuwawekea wachezaji wake video za Paul Scholes na kuwaambia mnamwona mwanadamu huyu? Iniesta anakiri walikuwa wakifurahi mno kipindi hicho na walimfanya Paul kuwa role model wao.

Mchezaji mkongwe wa Kibrazil, Socrates aliwahi kusema Paul amebarikiwa sana; pengine ana kila sifa ya kucheza team ya taifa ya Brazil kama angekuwa na uraia wa nchi hiyo. Ana kila kitu miguuni, ana macho yanayona mbali zaidi ya wengine; ni mpigaji mzuri wa mashuti nje ya eneo la hatare. Kwa hakika Paul amekamilika.

Kwa uwezo na uhodari wa Paul haikushangaza hata pale kocha aliwapa Italy kombe la dunia pale Berlin, Marcelo Lippi alipotumia haki yake ya msingi kumwelezea Paul huyu mwenye mwili usiochoka haraka, akili inayofikiria kila second na hisia za Hali ya juu katika kupambania jezi iliyofunika mgongo wake.

Pengine hakuwa anatajwa sana kwenye vinywa vya wapenda soka wengi wa kileo kutokana na hulka zao za kupendana vilivyopikwa ni si wapikaji. Pengine hata Waingereza wenyewe hawamuimbi kama David Beckham au wengineo, huyu ni mnyonge aliyenyimwa haki.

Mkongwe wa Manchester Utd Bobby Charlton aliwahi kusema Paul ni wa kipekee sana, anastahili pongezi pengine ambazo amekuwa hapewi ipasavyo katika ulimwengu juu wa soka. Huyu ni Paul ambae bao lake la dhahabu iliihakikishia utd ticket ya kwenda final UEFA Moscow, Urusi. Pale Old Trafford dhidi ya Barcelona 2008.

Pengine kazi zake ngumu zilizompelekea kupata kadi za njano zakutosha na nyekundu kadhaa, kwa kucheza foul za hatare zaidi, tackling toka nyuma zimeweza kumpunguzia sifa kwa baadhi ya mashabiki wapendao sexy football lakini angefanya nini Paul katika kazi ile? Alikuwa anatimiza anachostahili kuipa team yake kwa wakati huo. Na wala hajali mtamchukuliaje.

Kwa Paul heri lawama kuliko fedheha, sifa halali ya mwanaume halisi. Na ndio kazi iliyomhalalishia makonde 25 ndani ya Utd, huku akiwa na UEFA 2 na EPL 11. Kama kuna tafsiri halali ya mwanaume wa soka au jemedari vitani, basi Paul ndio tafsiri sahihi. Mwanadamu aliyetumwa kufanya kazi sahihi na kwa nyakati sahihi.

Pumzika Paul. Na kila la kheri katika kazi yako mpya ya uchambuzi hapo BT Sport.

Kwanini ni Paul scholes? Majibu yako YouTube. Nenda tafadhali, nenda kashuhudie ladha yake katika ile miguu ya dhahabu iliyonyimwa thamani na wengi kwa kumkatili sifa anazostahili.

Paul Scholes 1.jpg

Paul Scholes

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Jamaa ni wakawaida tu ukimlinganisha na mafundi wa kweli. ILa vilaza vingi vya PL anaviburura.
 
Pongezi ziende kwake
Paul Scholes ...Steven Gerrard,Modric...Iniesta na Xavi na Fabrigas Pirlo ..Pavel Nedved na Edga David nilikubali kuwaona enz zao.
 
Back
Top Bottom