Patashika

Patashika

PATASHIKA - 15


Walitembea hadi walipofika barabara kuu.
“Twende tukasimame kwenye kile kichaka, tusubiri basi, tukifanikiwa kupata basi itakuwa vema zaidi. Maana nimeona si salama kuendelea kusafiri kwa lile gari lako. Kutumia gari lako itawapa urahisi wa kutupata haraka.” Alisema yule dereva huku akimuonesha Vivian kichaka alichotaka waende. Yule dereva alikimbia hadi kwenye kile kichaka, kuona hivyo Vivian na yeye alikimbia kizembe huku akiwa anakunywa juisi yake kuelekea pale alipoenda yule dereva. Vivian hakuelewa kwa nini alikuwa akitii kila alichoambiwa na yule dereva, lakini pia, hakuona sababu ya kutotii mradi awe na uhakika wa usalama wake.
“Wakati tukiwa hapa, nitajaribu kukuelezea kwa kifupi kuhusu mimi na wewe. Maana sina hakika nini kitafuata dakika chache kutoka sasa. Nimekaa miaka mingi nikiwa nasubiri muda kama huu ili niweze kufanya hiki nikifanyacho sasa kwa faida yenu na Taifa hili…” Alisema yule dereva huku akiwa anavua sura ya bandia aliyokuwa amevaa. Vivian aliweka chini boksi la juisi aliyokuwa anakunywa.
“Naitwa Mwasumbi, Luteni Mwasumbi.”
“Ooooh my God!, kwa hiyo muda wote ule tulikuwa tukiongea na wewe kule kijijini tukidhani kuwa u Askofu Alphonso kumbe haikuwa kweli! Kwa nini umeamua kufanya hivi?” Vivian alisema kwa mshangao mkubwa. Huku sasa akitazamana na sura ya mtu mwingine tofauti na ile ya Askofu Alphonso. Kabla Mwasumbi hajajibu walisikia mlio wa gari ukija kwa kasi. Vivian alitaka kukimbilia barabarani ili kulisimamisha.
“Stop!, usifanye hivyo Vivian, nimekwambia tutapanda basi, huo mlio wa gari si wa basi ni wa gari ndogo tu tena wanaweza kuwa wenyewe!” Mwasumbi alisema huku akimshika mkono Vivian na kuukandamiza chini, Vivian akaanguka chini kutokana na ule mkandamizo.
“Wewe vipi sasa tusipopata hilo basi tutalala hapa? Si bora tukaomba msaada kwenye magari madogo yanayoelekea Kamanga.” Vivian aling’aka kwa hasira na mshangao. “Sikiliza we mtoto, si muda mrefu utajua uko kwenye kisa gani na kwa nini unatafutwa san…” Kauli ya Mwasumbi ilikatishwa na mlio wa gari lilokuwa likija kwa kasi. Mlio ulionyesha kuwa lilikuwa karibu sana na pale walipokuwa wamejificha na lilikuwa kwenye mwendo wa kasi. Mwasumbi alisogea na kuchungulia barabarani kupitia matawi ya kile kichaka walichokuwepo. Macho yake yaliweza kuliona gari aina ya Land Rover 110 rangi ya kijani likiwa na alama kubwa nyeupe, alama hiyo ilikuwa herufi T ubavuni.
“Oooh yeah!, unaona sasa ndiyo wenyewe, wanatutafuta!” Mwasumbi alisema kwa kunong’ona. Vivian alibaki ametoa macho wala hakuwa anajua kinachoendela.
“Vivian, naomba nikueleze kwa kirefu kuhusu kisa hiki. Mwaka 1967 kulikuwa na harakati kubwa sana hapa nchini. Ilikuwa ni wakati ambao Mwalimu Nyerere alikuwa katika harakati kubwa za kutaka kuonyesha kuwa nchi ilikuwa huru kutoka katika mikono ya wakoloni. Mambo mengi yalifanyika, nuruni na gizani, ya kusemeka na ambayo hatuwezi hata kuyatamka. Mengi yalitokea, machache yaliandikwa na ambayo mnaweza kuyasoma leo. Harakati ziliendelea sana hadi mwaka 1976 ambapo wazungu wengi walikuwa wameshaondoka nchini na Nyerere akaikoleza zaidi ile sera ya Ujamaa na misingi ya Kujitegemea. Kama nilivyosema, kulikuwa na harakati nyingi sana ila ukweli ulikuwa wazi sana kuwa, wazungu waliokuwa hapa nchini walikuwa wakiijua nchi yetu kuliko tulivyokuwa tukiijua wenyewe. Walijua nini kiko wapi na kina faida gani. Wazungu wengi walibaki kulinda maslahi yao kwa kutumia dini. Kanisa Katoliki kwa upande wake walianza ujenzi wa Hospitali ya Bugando mnamo mwaka 1968. Ujenzi huo ulifanywa na kampuni ya Kiyahudi iliyoitwa COSATA. Wayahudi hao walijenga Bugando kwa ustadi mkubwa kama ambavyo walifanya kwa majengo mengine muhimu hapa nchini kama vile KCMC, jengo la Usalama wa Taifa, UDSM na Hospital ya Taifa ya Muhimbili. Lakini hata kabla hawajamaliza ujenzi wake sawasawa, Mwl. Nyerere aliwafukuza Wayahudi hao.
Ufunguzi wa hospitali hiyo ulifanyika rasmi tarehe 3 Novemba 1971. Na baadaye hospital hiyo ilitaifishwa na Serikali mwaka 1972.
Wengi hawakuelewa kwa nini Nyerere aliwafukuza Wayahudi hao. Kulikuwa na uvumi mwingi, lakini kwa sababu mimi kama mwanajeshi nilikuwa jirani sana na mkuu mmoja wa jeshi ambaye alining’ata sikio. Sababu ya kwanza ni ya kisiasa na msimamo wa Nyerere juu ya uhusiano wa Wayahudi na Wapelestina. Lakini pia, kulikuwa na sababu nyingine ya siri ambayo ndiyo inasumbua hadi leo. Nitakueleza sababu zote mbili zilizo sababisha Nyerere akosane na Wayahudi; ya kisiasa yaani uhusiano wa Wapalestina na Wayahudi na hiyo nyingine. Ila hiyo nyingine ndiyo ambayo inanifanya mimi na wewe tuwe tumejificha hapa hii leo.
Wewe ni msomi najua umesoma historia. Kama ujuavyo kuwa Ujerumani ilikuwa ikiitawala Tanganyika tangu mwaka 1885 mara baada ya Carl Peters kusaini mkataba wa kitapeli na viongozi wa kiafrika. Mtu huyo baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro – Moshi mnamo mwaka 1891. Jamaa alikuwa mkatili kiasi kuwa watu wa maeneo hayo walimwita Mkono wa Damu. Nadhani wajua mengi yaliyofanywa na Carl Peters hadi pale majaji wa Kijerumani walipotuma taarifa Ujerumani juu ya ukatili wa huyo jamaa na mwaka 1897 aliondolewa katika shughuli za kikoloni. Ujerumani ikaendelea kutawala Tanganyika huku wajerumani wakiongezeka kumiminika Tanganyika.
Nadhani unajua yaliyotokea kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambapo baadaye Ujerumani ilishindwa lakini wakati huohuo ikiacha wakimbizi wengi wa Kiyahudi ambao walikuwa wameikimbia Ujerumani. Hapo kabla Waingereza walikuwa wamenunua kama heka 50,000 ndani ya Tanganyika na kuwapangisha Wayahudi. Mara kwa mara Uingereza ilikuwa ikipendekeza kuwa ili kukabiliana na shida ya wakimbizi wa Kiyahudi ni vema Tanganyika, British Guiana, Kenya, Zimbabwe ya wakati huo na Nyasaland zikatengwa na kuwa makazi ya Wayahudi hao. Kwa hivyo baada ya Ujerumani kushindwa vita, nguvu ya chama cha NAZI na shughuli zake zikaathirika sana. Na sasa Tanganyika na Palestina zikawekwa kwenye mchakato wa kuzifanya kuwa makazi ya Wayahudi. Nchi kadhaa za Ulaya na Wamarekani wakawa kwenye kampeni kubwa kuhakikisha hilo linafanikiwa. Mapango huo haukufanikiwa kwa Tanganyika lakini ukafanikiwa kwa Palestina.
Haiko wazi sana kama Nyerere alipata taarifa za ule mpango wa mwaka 1930 wa kuifanya Tanganyika na Palestina kuwa makazi ya Wayahudi. Maana kwa wakati huo Nyerere alikuwa na miaka kumi na tano tu na ni wakati wakati vijana wa NAZI walipofanya maandamano kupinga Wayahudi kupewa Tanganyika. Maandamano hayo yalifanyika Moshi katika Shule ya Kijerumani ya Mweka. Hata hivyo, haina ubishi kuwa Nyerere alikuwa akijua vema historia ya Palestina wakati alipokua akiamua Sera ya Tanzania, kuhusiana na Palestina ule mwaka wa 1977 ambapo alisema anaitambua Palestina na kuwa anaunga mkono Palestine Liberation Organization (PLO). Ngoja nikueleze ili ulewe suala hili kwa upana, japo linaoneka la kisiasa lakini ni muhimu kwako kujua. Tanganyika muda wote ilikuwa mstari wa mbele katika kutaka Palestina ijitawale. Kumekuwa na mivutano mingi sana juu ya suala hili hadi leo. Lakini chanzo chake ni cha kihistoria zaidi. Sasa kuna watu wanaoamini kwa sehemu kubwa kuwa Nyerere hakupenda huduma ya Wayahudi na kuwaondoa kwenye miradi yote kwa sababu ya matashi yake kwa Wapalestina ambayo hayakuja hivi hivi bali yaliletwa na hisia kuwa Palestina na Tanganyika zingekuwa kwenye mkondo mmoja kama mambo yangekwenda kama ilivyopangwa kuwa zote ziwe makazi ya Wayahudi. Japo mpango huo haukufanikiwa kwa Tanganyika…” Kabla hajaendelea na maelezo walisikia mlio mwingine wa gari. Safari hii mlio uliashiria kuwa lilikuwa gari kubwa.
“Daaah! historia yako inasisimua lakini bado haijanipa picha yote ya hili tunalopitia.” Hatimaye Vivian alisema huku akiwa anasimama. Mzee Mwasumbi alijipenyeza hadi sehemu ambayo aliweza kuona upande lilikokuwa linatokea lile gari.
“Twende, ni Basi linakuja.” Mwasumbi alisema. Wote wakawa wanaelekea barabarani Walisimamisha gari na kuingia ndani. Basi lilikuwa limejaa sana hivyo kulikuwa na nafasi ya kusimama kwa shida. Gari lilitembea kwa dakika kama ishirini kisha, Mzee Mwasumbi akapiga kelele.
“Tushushe hicho Kijiji cha mbele hapo!”
Kweli gari lilipofika hicho Kijiji alichokusudia kushuka, lilisimama, wakashuka.
“Upande huu kuna ufukwe wa Ziwa Victoria, kutakuwa na watu wanatusubiri hapo.” Alisema huku wakiwa wanavuka barabara kwenda upande mwingine wa barabara.
Huko kulikuwa na makazi machache ya watu. Walianza kufuata barabara ndogo ya vumbi iliyokuwa ikitelemka kwenda sehemu ambayo Mwasumbi alisema wangekutana na ufukwe.
“Sasa hayo maelezo yako yanahusiana vipi na haya yanayotokea?” Vivian alihoji wakati wakitembea.
“Huyo mkubwa wangu wa jeshi anasema kuna sababu nyingine ya kiusalama ambayo ilisababisha Nyerere asitake Wayahudi waendelee kuwa hapa nchini. Wakati wa Vita ya Pili ya Dunia, Marekani na washirika wake walikuwa wanaelekea kushindwa, hadi pale Marekani walipofanikiwa kutumia lile bomu la Atomic na kuipiga Hiroshima na Nagasaki, Japan. Ili kulipua mabomu hayo, ilihitajika neno la siri ‘password’. Maneno ya siri ya kufyatulia mabomu hayo yalitengenezwa na kuwekwa na mtengenezaji ambaye ni Myahudi. Myahudi aliyevumbua bomu hilo, Bwana J. Robert Oppenheimer alitengeneza maneno ya siri. Neno la siri la lile bomu lililolipua Hiroshima lilikuwa ni ‘Little Boy’. Wakati lile neno la siri la lile bomu lililolipua Nagasaki ilikuwa ‘Fat Man’.
Baada ya kwisha vita hiyo, huku Marekani na washirika wake wakiwa wameshinda, ilikuja kugundulika kuwa, baada ya Bwana J. Robert Oppenheimer kulazimishwa kutoa kanuni za kutengeneza bomu hilo kwa Serikali ya Marekani, aliona kuna umuhimu wa kutengeneza bomu jingine ambalo likipigwa kwa wakati mmoja na lile la Atomic huondoa madhara yanayoweza kuletwa na bomu hilo la Atomic. Ikiwa na maana kuwa hilo bomu jingine lina uwezo wa kulidhibiti lile la Atomic. Inasemekana wazo hilo alikuwa nalo akiwa katika hatua za mwisho za kutengeneza bomu la Atomic. Hivyo alitengeneza kanuni ya kutengeneza hilo bomu jingine, lakini hadi leo haijulikani mahali ambapo kanuni hiyo imewekwa. Kumekuwa na harakati kubwa za kutafuta mahali ambapo Myahudi huyo alificha karatasi zenye kanuni hiyo. Mashirika ya ujasusi yanaamini kuwa kuna siri kubwa katika maneno ya siri aliyoyatoa Bwana J. Robert Oppenheimer kulipulia yale mabomu mawili ya Atomic. Maneno ‘Little Boy’ and ‘Fat Man’ inasemekana yana siri na ufunguo wa kujua sehemu na mtu ambaye ana kanuni ya kuwezesha kutengeneza hilo bomu jingine la kulidhibiti lile bomu la Atomic. Katika kuchimba na kufuatilia wapi hiyo kanuni inaweza kuwa, ilikuja kugundulika kuwa mjomba wake na Bwana J. Robert Oppenheimer aitwaye Eud Benjamin, ambaye aliingia Tanganyika miaka hiyo kama walivyoingia wakimbizi wengine ndiye Fat Man. Myahudi huyo alikuwa mtaalamu wa mambo ya utabibu wa binadamu. Hivyo akajikuta anaishia kuwa Daktari katika hospitali ya Bugando.
Daktari huyo alikuwa maarufu sana hadi pale alipouawa katika usiku ambao wewe, Milka na Maganga mlizaliwa. Wakati huo yaani mwaka 1981 alikuwa na umri wa miaka 41 na inaaminika wakati bomu la Atomic lilipotumika kwa mara ya kwanza kule Japan mwaka 1945 yeye alikuwa na miaka 5 tu.
Neno ‘Fat Man’ lilikuja kutambuliwa kuwa ndiyo huyo mjomba wa Bwana J. Robert Oppenheimer. Lakini neno Little Boy halikuwa limegundulika hadi hapo baadaye baada ya kifo cha huyo mjomba wake na mgunduzi wa bomu la Atomic, hapa namaanisha kifo cha Daktari wa Kiyahudi Eud Benjamin katika Hospitali ya Bugando …” Kabla hajaendelea Mwasumbi alikatishwa na swali la Vivian
“Kwa hiyo usiku ule tuliozaliwa una nini sasa?”
“Jambo la kwanza ninalotaka ujue ni kuwa wewe ni Milka na Milka ni wewe. Nikiwa na maana kuwa mama Maganga alienda kujifungulia Mwanza katika Hospitali ya Bugando. Alifanya hivyo kwa vile mama yake mzazi alikuwa akiishi Mwanza hivyo kama wafanyavyo wanawake wengi wa Ki-tanzania, huenda kujifungulia kwa mama zao. Maana hilo huwapa haueni ya kisaikolojia kuwa watapata msaada wa uzoefu toka kwa mama zao na hali ya kujaliwa itakuwa juu. Na kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopatikana wakati wa kuzaliwa wewe na Maganga huduma ilitolewa na yule Daktari wa Kiyahudi. Kwa vile tayari mashirika mengi ya kimataifa ya Kijasusi yalikuwa yameshapata fununu kuhusiana na mahali alipokuwa huyo mjomba wake yule mgunduzi wa bomu la Atomic, walikuwa wameshaweka majajusi kufuatilia nyendo za huyo Myahudi kwa vile walikuwa wakitafuta maana ya neno Litle Boy na wapi zilipokuwa kanuni za kutengeneza bomu la kudhibiti bomu la Atomic…” Kabla Mwasumbi hajaendelea zaidi, mlio wa risasi ulisikika. Wote wakashtuka!
“Pancha au nini?” Vivian alihoji, hakuwa anajua mlio wa risasi. Hakuwahi kusikia wala kuona risasi ikipigwa.
“Hapana ni risasi!”
“Sikiliza, Vivian, sitaki watukamate wote, maana wewe sasa ni wa muhimu kuliko mimi, najihisi kama nimeshamaliza kazi yangu. Ufukweni si mbali toka hapa, ukifika huko, utakuta kuna boti ndogo ya kijani, waambie mimi nimekuelekeza kwenda pale, waambie Luteni Mwasumbi ameniagiza kuja, wao ni wanajeshi, hawajui wewe ni nani ila watakupeleka sehemu salama. Najua utaonana na Hellen, msimulie haya na yeye atakusimulia yote niliyomsimulia yeye na Maganga.
Ukiona mambo yanaharibika na unahitaji msaada wa haraka na uhakika basi utapiga hizi namba +255785975443…” Hata kabla Mwasumbi hajamaliza maelezo yake mara walisikia gari likiunguruma kuja upande waliokuwepo.
“Vivian, I love you so much and I always wanted to see you, nashukuru nimekuona. Jitahidi sana kuificha hiyo alama hapo pajani asiione mtu yeyote. Kama unataka kujua ukweli kuhusu hiyo namba na wakati huohuo uendelee kuwa salama, basi kuna watu wanne tu ambao unaweza kuwauliza. Mtu niliyekupa hiyo namba ya simu, Maganga, mimi au yule Daktari wa Kiyahudi japo na yeye anaweza kukudhuru akigundua kuwa umeshagundulika na unatafutwa….haya nenda…mimi nitajitahidi kuwazuia hapa ili kukupa wewe nafasi ya kufika ufukweni….tafadhali kuwa makini na kinywa chako.” Mwasumbi alisema hayo maneno kwa hisia kali kisha akamvuta Vivian na kumbusu. Wakati huu mlio wa gari ulikuwa jirani zaidi, Mwasumbi alimvuta Vivian hadi pembeni ya barabara, wakabana nyuma ya nyumba moja ya nyasi eneo hilo.
“Haya nenda, pita kwenye hayo mashamba hadi ufike ufukweni, ukiwapata nendeni, kama nitatoka hai najua nitakapokupata. Kama sitotoka hai nakutakia kila la heri mwanangu!”
“Mbona sikuelewi, unanitisha, unanihuzunisha, unanichanganya na kuniweka kwenye sintofahamu!” Viviani alimudu kusema huku akiwa anasukumwa na Mwasumbi kama ishara ya kumhimiza aondoke eneo lile.
“Natamani ningekusimulia kisa chote ila nachelea wote tutakuwa maiti hapa au twaweza kuangukia kwenye masahibu mazito na mateso. Chukua hii…” Hatimaye Mwasumbi, aling’oa nywele chache zilizokuwa kichwani kwake akampatia Vivian.
“Ipo siku utazihitaji hizi.” Mwasumbi alisema huku safari hii akichomoa bastola iliyokuwa mgongoni kwake.
“Go, go, go!” Alipiga kelele. Kusikia hivyo, Vivivan alikurupuka kuelekea kwenye vichaka vilivyokuwa kwenye mashamba yaliyokuwa jirani na eneo hilo. Alitembea kwa shida, maana hakuwa mtu aliyezoea taabu. Mawazo mengi yalikuwa kichwani. Kwa mara ya kwanza akajikuta anafanya kitu asichokielewa, ila hakuwa na namna zaidi ya kufanya hivyo. Alimfikiri Mwasumbi, alimfikiria Maganga na Milka kwa wakati mmoja huku akiwa bado anakatiza vichaka kueleke upande kulikokuwa na Pwani ya Ziwa Victoria.
 
PATASHIKA - 16

Aliwafikiria wazazi wake ambao walikuwa mapumzikoni Brazil halafu, akafikiria simulizi ya Mzee Mwasumbi kuwa yeye na Maganga ni mtu na kaka yake. Akakumbuka kauli ya Mwasumbi, “Wewe ni Milka na Milka ni wewe.” Hapo akachanganyikiwa. Akakumbuka kuhusu alama aliyokuwa nayo pajani ambayo kwa mujibu wa Mwasumbi ndiyo chanzo cha yeye kutafutwa. Vivian alihisi kuna ukweli kwenye hayo maelezo kwani aliyalinganisha na tukio aliloliona wakati ameenda Hospitali ya Bugando ili kujua wodi aliyozaliwa, maana yule Daktari alimuuliza ile alama kwanza. Hivyo aliona kuna kitu katika ile alama na mtu pekee ambaye anaonekana kujua hadi sasa ndiyo huyo ameachana naye dakika chache zilizopita, huku sababu iliyotolewa ni usalama wake yeye Vivian. Alishangaa jinsi hayo mambo yalivyotokea kwa kasi. Alishangaa kuona kama ni kweli mtu aliyehangaika naye siku chache zilizopita pale Hospitali ya Sengerema alikuwa ni mama yake mzazi. Hilo lilimuuma zaidi.
Sasa alikuwa amekaribia zaidi Pwani na kwa mbali waliweza kuiona boti ambayo Mwasumbi alikuwa amemwambia. Aliziangalia zile nywele alizopewa na Mwasumbi, akafikiria ujumbe aliopewa kuhusu hizo nywele. Kama kweli siku moja angezihitaji kama Mwasumbi alivyosema basi aliona kuna sababu ya kuzihifadhi vema. Alifikiria sehemu sahihi ambayo angeweza kuzihifadhi hizo nywele. Alifungua saa yake ya mkononi aliyokuwa ameivaa, akafungua sehemu ya kuwekea Betri, akaziweka zile nywele kisha akaifunga na kuivaa tena. Mara akasikia mrindimo wa risasi kule alikokuwa anatokea. Mara hii aliweza kujua ni risasi maana hakukuwa na tofauti na ile aliyoambiwa na Mwasumbi. Japo alikuwa amechoka lakini akajikuta anatumia nguvu zilizobaki kwa kutimua mbio kuelekea upande ule alioiona Boti.
***************************

“HELLEN, inawezekana akawa anaongea ukweli.”
“Sijui Milka, lakini ungemwona wakati anaongea nami na Maganga tulipokuwa kwake, usingemtilia shaka. Anaoneka kujua habari zetu za utotoni vizuri sana. Sasa shida ni kuwa tutawezaje kuthibitisha akisemacho?”
“Japokuwa amenilea na kunikuza sijawahi kumpenda Mzee Paul, kwangu hakuwa kama baba kwa kweli. Mtu katili sana. Hivyo nitafurahi sana kujua kuwa yeye siyo baba yangu mzazi. Siku hiyohiyo nitaachana na mambo ya utawa na nitakuwa huru. Halafu hii inamaanisha mimi na Maganga siyo ndugu, usikute hata mama zetu ni tofauti.”
“Ha ha ha ha!, Milka bwana, usiniambie kuwa utafurahi kusikia Maganga si ndugu yako.”
“Heeeh!, we Hellen, nikijua hilo mbona nguvu zote nitaelekeza kwa Maganga. Aisee! nampenda sana Maganga, na namjua vizuri sana, wala hatonisumbua kumpata yule. Sielewi kwa nini Vivian alikuwa anashindwa kumpata?”
“Hii balaa! Ila kwa kweli Maganga hata mimi nilivyomuona siku ile nakutana nanyi pale Kijijini, alinivutia kwa kweli, ila nikahisi ni mtu na mpenzi wake kwa jinsi mlivyokuwa mmekumbatiana. Maganga kifaa kwa kweli, sema ndiyo hivyo mimi yule ni kaka yangu maana kwa namna zote ni ndugu yangu. Kwa maelezo yao wote wawili yanaonyesha kuwa Mzee Paul ni baba yangu. Ila kama ulivyosema, nimekutana na kuongea na baba yangu kwa siku moja tu katika maisha yangu ila katika siku hiyo moja tu baba yangu alikuwa tayari kuniua. Hii inaonyesha ni jinsi gani asivyonihitaji. Kiu ya heshima na ufahari wa kutaka aonekane mwema mbele ya kanisa na jamii ndiyo iliyomfanya awe tayari kuniua mimi. Kweli nikifikiria hilo suala linaniuma sana, kuwa kuna watu ambao huwatoa sadaka za kafara watu wengine ili mradi wao wapate kile wakitakacho. Milka, sijui kama nitamsamehe baba yangu Mzee Paul.”
“Daaah!, Hellen, kweli hiyo habari imenisikitisha sana. Nikifikiria jinsi mtu niliyedhani kuwa ni baba yangu alivyompiga mama yangu na kupelekea kifo chake, halafu na hili unalonisimulia nashindwa kupata nafasi ya huyo Mzee moyoni mwangu. Hali hii yote tuliyomo ndani yake ni kwa sababu yake.”
“Milka, hebu turudi kwenye hiki kisa tulichopo sasa. Hivi nini kilifanya hasa Mzee Paul na wale watu wengine wawili wawe radhi kuangamiza Kijiji kizima namna ile?”
“Hellen, kwa kweli sijui hasa ni nini, ila nakumbuka nilimsikia Mzee Paul akimuuliza mtu mmoja kuwa anataka aonyeshwe Maganga alipo. Hivyo inawezekana mauaji na ukatili wote ule ilikuwa ni katika harakati za kumtafuta Maganga.”
“Daaah!, na wale watu walikuwa ni nani, maana walivyokuwa wakifanya mambo yao ni kama nilikuwa naangalia sinema ya mapigano jinsi wale wababe wa kivita wafanyavyo! Halafu, Milka, hivi si unasema Mzee Paul alikuwa amevunjika mguu?”
“Hilo hata mimi linanishangaza sana Hellen, maana siku kadhaa kabla ya tukio, Mzee Paul ndio alikuwa amerejea toka Hospitali ambako nilikuwa nimempeleke kwa ajili ya matibabu ya mguu. Alikuwa amevunjika mguu, hii ni kwa mujibu wa madaktari wa hospitali zote mbili, ile ya Katunguru misheni na ile ya Wilaya ya Sengerema. Sasa nashangaa jana yalipotokea yale alikuwa mzima haswa wala hakuwa na dalili yoyote ya kuonyesha kuwa alikuwa amevunjika mguu.”
“Na wale watu na lile gari je, Milka?
“Sijui, Hellen!”
“Mhhh!, nahisi kuna kitu hapa Milka.”
“Hata mimi nahisi Mzee Paul ni zaidi ya vile tulivyokuwa tunamfahamu. Japo alikuwa mtu wa Kanisa lakini matendo yake na misimamo yake mara zote haikuwa sawasawa. Halafu alikuwa akimchukulia na kumwongoza Maganga zaidi ya baba awezavyo kufanya kwa mtoto.”
“Unamaanisha nini Milka?”
“Mzee Paul ni mvivu sana wa kufanya kazi, lakini tofauti na wazee wengine pale Kijijini hatukuwa tunapungukiwa chakula wala sikuwahi kumsikia akilalamika juu ya upatikanaji wa mahitaji yetu yote ikiwemo karo za shule.
Kwa vipindi tofauti nilikuwa najiuliza namna ambavyo alikuwa akipata pesa. Hakuwa na rafiki wa kusema huyu ndiye msiri wa baba. Sasa kuwaona wale watu pale Kijijini wakiwa wanachukua amri za kijeshi toka kwa Mzee Paul kunanifanya nifikirie mara mbilimbili. Hellen, unajua lile gari nililoliona limepaki pale nyumbani ni moja ya yale magari ya kifahari?”
“Mmmmh! kwa kweli kilichonitoa Dar sasa nakiona. Ila unajua nini Milka?”
“Mmh, niambie Hellen?”
“Sijutii hata kidogo, nimetii kile ambacho marehemu mama yangu aliniomba nikifanye. Pia, nikifikiria sana, naona kuja kwangu ndiyo kumefanya haya yote yametokea…”
“Kivipi Hellen kuja kwako unakuunganisha na haya yote? Maana kama ni Mzee Paul kumpiga mama lilikuwa limeshatokea sasa mbona unataka kujitwisha lawama mdogo wangu?!”
“Hapana Milka, nimeshasema sijutii kwa lolote lililotokea, ila ninachosema ni kuwa kama nisingekuja Mzee Paul asingeenda kunining’iniza kwenye mti kule shambani. Mwasumbi asingeniona na kuja kuniokoa, na kisha utaona Mwasumbi alipata nafasi ya kuongea na mimi na Maganga kwa sababu ya lile tukio alilolifanya Mzee Paul...”
“Hellen, kwa hiyo unaona sasa, ina maana aliyesababisha haya si wewe bali ni Mzee Paul na tamaa zake…”
“No, Milka, Mzee Paul ana sehemu yake lakini nina sehemu yangu kubwa tu!”
“Eeeeh!, bibie haya vyovyote vile, sasa tuko hapa. Hivi hapa ni wapi na watu hawa wana mpango gani na sisi?
“Milka bwana, sasa unaniuliza mimi wakati wote tumejikuta hapa, ila ninachoweza kusema ni kuwa, Askofu Alphonso anahusika sana na sisi kuwa hapa, maana kabla fahamu hazijanipotea nilipokuwa kwenye ule moto ndani ya nyumba, nilimwona akitokea na kuja pale nilipokuwa. Nahisi kama niliongea maneno japo sikumbuki ni maneno gani. Inaonekana kama tuko sehemu ambayo kuna nyumba za kotazi, maana nikichungulia nje naona kama nyumba zote zinafanana. Halafu naona raia wengi hapa hasa wanaume wamevalia sare za jeshi.”
“Daaah! ngoja tuone.” Kabla Milka hajamalizia ile kauli yake, mlango wa chumba walichokuwemo ulifunguliwa. Aliingia askari Jeshi mmoja wa kike akiwa amebeba mafurushi mawili. Hakuwasalimia, aliwarushia kila mmoja furushi moja la nguo. Kisha akawafanyia ishara wamfuate. Hakuna aliyebisha wala kuuliza, walikuwa wameshaona mengi na sasa walijikuta wako tayari kwa lolote, wakati huu hawakuwa na hakika nani alikuwa mwema au mbaya kwao. Yule askari alitembea kwa mwendo wa kiaskari japo usichana bado ulionekana dhahiri kwa jinsi nyonga zake zilivyokuwa zikinesa wakati akitembea.
“Ingieni kwenye gari.” Alisema yule mwanajeshi wa kike. Kama mwanzo, hawakubisha waliingia. Wakati wameshaingia kwenye gari, gari lingine lililoonekana kuwa la jeshi lilifika eneo lile. Yule askari jeshi aliyekuwa kwenye gari walilopanda Hellen na Milka alipoliona lile gari lingine likiwasili, alishuka na kwenda lilipokuwa limeegeshwa. Baada ya kuongea na mtu aliyekuwa anaendesha lile gari lingine walionyesha kama kukubaliana kitu. Yule askari wa kike alienda upande wa nyuma wa gari akafungua mlango.
“Toka nje!” Alisema. Mara akatokea binti aliyeoneka kuwa amechafuka sana. Alikuwa ni Vivian.
“Nifuate!” Yule askari jeshi wa kike aliongea kama alivyokuwa ameongea na Hellen na Milka, hakuwa mtu wa maneno mengi. Alimwongoza Vivian hadi pale palipokuwa na gari alilokuwa amewaweka Milka na Hellen. Alimfungulia mlango, yeye aliwaona Milka na Hellen kabla wao hawajamwona, hivyo Milka na Hellen walipogeuka upande wa mlangoni walikutana na sura mbili, ya yule askari na ya Vivian. Milka alitaka kupiga kelele lakini alikutana na sura ya Vivian huku akiwa amefanya ile ishara ya kuweka kidole katikati ya mdomo kuashiria kuwa anyamaze. Hivyo Milka akaishia kufanya kama mtu aliyepotewa na kwikwi iliyokuwa imekuja kwa nguvu. Vivian akaingia ndani ya gari mlango wa nyuma wa gari aina ya Land Rover 110 ulifungwa. Dakika chache baadae gari lilitiwa moto. Zaidi ya ule mlango walioingilia, upande huo wa nyuma hakukuwa na mlango mwingine wala dirisha kwa hiyo hawakuweza kujua walikuwa wakielekea wapi. Gari hilo ambalo muungurumo wake ulionyesha kuwa lilikuwa likiendeshwa kwa fujo na kasi kubwa lilikwenda bila kusimama huku likionekana kupiga kona kadhaa. Kule nyuma walikokuwa abiria kulikuwa kimya kabisa, kwani Milka alipojaribu kuongea Vivian alimwashiria kuwa anyamaze.
“Huyu ndiyo Hellen?” Vivian alimuuliza Milka kwa kunong’ona. Milka alitingisha kinywa kwa namna ya kukubali.
“Ameshakusimulia walichoambiwa na Mwasumbi?” Vivian alinong’ona tena. Kama hapo awali, Milka alitingisha tena kichwa kuitikia.
“Usimwambie mtu yeyote aliyokusimulia Mwasumbi, wakijua tu kuwa unajua wanakuua na utasababisha na Maganga auwawe.” Milka alinong’ona huku akionyesha msisitizo kwa macho, mdomo na mikono yake.
“Maganga na Mwasumbi wako wapi?” Hatimaye Milka alihoji kwa kunong’ona.
“Mwasumbi au Askofu Alphonso wa bandia nimemwacha yuko anapambana nao. Maganga sijui yuko wapi.” Vivian alisema huku akionyesha kuwa hakuwa na hamu ya kuongea tena.
“Na…”
“Shiiiiii!, tutaongea tukipata nafasi na tukiendelea kuwa hai.” Vivian alikatisha swali la Hellen. Vivian alijua kuwa walikuwa na mengi ya kuongea lakini haukuwa wakati muafaka kufanya hivyo. Hata hivyo maneno machache aliyoongea Vivian yaliwafanya Milka na Hellen waweze kuunganisha mambo machache juu ya mlolongo mrefu wa maswali waliyokuwa nayo. Kutokana na maelezo hayo mafupi ya Vivia, ikawa dhahiri vichwani mwa Hellen na Milka kuwa Mwasumbi ndiye aliyekuwa amewaokoa, kama Mwasumbi ndiye aliyejifanya kuwa Askofu Alphonso wa bandia. Na sasa imani yao kwa Mwasumbi ikaimarika zaidi na kuanza kutoa nafasi ya kuyaamini yote ambayo walipata kuyasikia toka kwa Mwasumbi.
Ghafla walisikia gari likipiga honi na kisha baada ya dakika chache walisikia kitu kama lango kubwa likiburuzwa. Baada ya ukimya kidogo, gari liliingizwa na baadaye wakasikia lango likiburuzwa tena. Walisikia mlango wa upande wa dereva wa lile gari ukifunguliwa, kisha ukafungwa. Hapo zikasikika hatua za watu wakiwa wanatembea. Baadaye wakasikia kama mlio wa geti likiwa linafunguliwa. Hatimaye mlango wa gari walilokuwemo ulifunguliwa. Yule mwanajeshi wa kike pamoja na wanaume wengine wawili walikuwa wamesimama. Waliangaliana kwa muda na macho ya kina Vivian, Milka na Hellen.
“Shukeni!” Alisema yule mwanajeshi wa kike. Hakuna aliyebisha, alianza Vivian, akafuatia Hellen kisha Milka.
“Mfuateni huyo!” Alisema yule mwanajeshi wa kike huku akionyesha kwa mmoja wa wale wanaume. Wasichana wale watatu wakaingizwa ndani. Ilikuwa nyumba nzuri ya kisasa iliyokuwa na kila kitu ndani. Hawakuweza kuona upande wa nje maana sehemu waliyokuwa wameshukia ilikuwa kwa ndani, sehemu ya kuegeshea gari.
“Haya ndiyo yatakuwa makao yenu ya muda wakati tukisubiri maelekezo mengine kuwahusu. Mtapata huduma zote muhimu, na mtapewa chakula kizuri, msisite kutoa mapendekezo ya chakula mkitakacho.” Alisema yule mwanajeshi wa kike. Huku akiwa amemkumbatia mmoja wa wale wanaume. Wasichana watatu hawakuwa na la kujibu. Yule mwanajeshi wa kike na yule mwanaume hawakuishia kukumbatiana tu wakaanza kunyonyana ndimi. Milka, Hellen na Vivian wakabaki wamesimama wanashangaa. Wawili hao hawakuishia hapo wakaanza kufanya ile michezo yao ya kimahaba yenye kutia ashki. Walipozidiwa wakavutana hadi chumba kingine huko miguno ya mahaba na makelele ya kudai na kuridhika vilisikika.

***********

Jenerali Mmbando au JM kama vijana wake wa jeshi walivyozoea kumwita alikuwa ofisini kwake asubuhi hii. Tofauti na siku nyingine, leo alikuwa amevaa kiraia jambo ambalo liliwafanya MPs wengi wabaki na maswali ya kujiuliza kuwa kulikoni, haikuwa kawaida yake kuonekana akiwa hajavaa sare za jeshi saa za kazi. Muda pekee ambao alionekana akiwa hajavaa sare za kazi ni kuanzia saa mbili na nusu usiku hadi saa nne na nusu, muda ambao huwa kwenye chumba maalum cha mazoezi ya mbinu za kulinda mwili na kushambulia kwa kutumia mwili. Muda huo alivalia mavazi yake maalum kwa ajili ya mchezo huo na hujihusisha kikamilifu katika kuwaongezea uzoefu askari maalum walioko kwenye kambi aliyokuwa akiishi. Akishatoka kwenye hayo mazoezi huvaa tena mavazi yake ya kijeshi na kuelekea ilipo maktaba na hujifukia huko kusoma vitabu na majarida mbalimbali. Tofauti na wakuu wengine wa kijeshi waliokuwa wamepewa nyumba za kifahari uraiani na kuishi maisha ya kifahari, Jenerali Mmbando hakutaka kuishi namna hiyo. Hakuwa na mke, hakuwa na mtoto, hakuwa akikaa na ndugu yeyote. Yeye mwenyewe ndiyo alikuwa kila kitu kwake. Mtu pekee ambaye waliwahi kuishi pamoja kwa muda mrefu alikuwa ni msichana wa kazi aliyekuwa akiitwa Sophia. Aliishi na msichana huyo kwa miaka tisa hadi pale siku moja alipotoweka na hakuwahi kuonekana tena. Kuondoka kwa Sophia maishani mwake kulimfanya asiwe na mpango wa kuishi na mtu yeyote. Mambo mawili ambayo kila alipokuwa akifikiria kuhusu Sophia yalimfanya asiwe na mpango wa kuishi na mtu yeyote. Moja ni vile alivyokuwa amemuamini Sophia na kumfanya kuwa mtu wake wa karibu sana. Hawakuwa wakiishi tena kama bosi na mfanyakazi wa ndani bali waliishia kuishi kama marafiki wakubwa, hivyo hakutegemea Sophia angeweza kuondoka kwa staili aliyoondoka. Katika muda wote alioishi na Sophia, Jenerali Mmbando alikuwa amemfundisha Sophia mambo ambayo yalimfanya kuwa mpiganaji wa kutisha. Alianza kwenda naye mazoezi, kisha wakawa marafiki katika mazoezi. Ile kasumba iliozoeleka miongoni mwa watu kuwa wasichana ni wepesi sana katika kujifunza ilithibitika kwa Jenerali Mmbando kwani kasi ya Sophia kuchukua mazoezi na kwenda mbele zaidi ilimshangaza sana.
“Sikiliza Sophia, hivi vitu unajifunza ni kwa ajili ya kujilinda mwili wako pale inapolazimika. Kwa namna yoyote usitumie kuwatisha watu wala kuharibu amani ya sehemu yoyote.” Ilikuwa ni sehemu ya onyo ambalo Jenerali Mmbando alikuwa akimpa Sophia kila mara walipokuwa wakimaliza hatua fulani ya mafunzo na kuingia kwenye hatua nyingine. Onyo hilo lilimfanya msichana Sophia kuwa mpole zaidi, alikuwa na tabia ya upole, ila upole wake uliongezeka mara dufu kwa kadiri alivyokuwa akizama kwenye mazoezi na mafunzo aliyokuwa akipewa na Jenerali Mmbando.
Jambo la pili lilomfanya jenerali Mmbando kujiapiza kutokuishi na mtu au kutoa mafunzo kwa raia ni tetesi ambazo alikuja kuzipata miaka michache baadaye kuhusu Sophia. Inasemekana wakuu wachache wa jeshi walikuwa wametengeneza timu fulani ya siri kwa ajili ya kutafuta taarifa za siri kwa manufaa yao binafsi. Hilo lilikuwa likijadiliwa ndani ya jeshi lakini kilichomshangaza ni kuwa mmoja kati wa watu wa juu katika kuendesha operesheni hiyo ya siri alikuwemo msichana Sophia.
Hivyo asubuhi hii alikuwa katika nguo za kiraia, ndani ya ofisi yake. Hakuwa na faili lolote zaidi ya kompyuta laptop yake na CD kadhaaa. Aliiweka kompyuta hiyo juu ya meza kisha akaanza kuangalia kwa makini kilichokuwa kikitokea. Aliendelea kufanya hivyo kwa saa kadhaa huku kadri muda ulivyokuwa ukitoweka moshi wa Sigara uliendelea kukijaza chumba huku Sigara kadhaa zikiwa zimeshateketea.

* * *

Siku hii nyingine, Makamanda hawa walikuwa katika mkutano wa siri kwenye moja ya nyumba za siri za jeshi. Walikuwa watu watatu, wote wakiwa na vyeo vya juu sana katika jeshi. Katika kikao hicho, Jenerali Mmbando alitakiwa kutoa taarifa moja nyeti kwa Mkuu wa Majeshi ambaye alikuwa ameandamana na Mzee mmoja wa makamo. Kikao kilikuwa kimepamba moto.
“Ukweli ni kuwa miaka zaidi ya ishirini iliyopita ilikuwa ya wasiwasi mkubwa na giza kwa upande wangu. Kama mnavyofahamu kuwa kazi ya kuandaa operesheni niliiweka chini ya KAPTEN, ambaye nilimwondoa kwenye shughuli zote za kawaida ili awe na nafasi nzuri ya kushughulikia hilo. Kutokana na sababu za kiufundi, baada ya tukio la kulipuliwa ile Wodi ya Wazazi ya Hospitali ya Bugando Mwanza, KAPTEN alipendekeza kuwachukua, Luteni Mwasumbi na Luteni Paul.
 
PATASHIKA - 17

Mtunzi: Japhet Nyang'oro Sudi


Hasa kwa vile wao walkuwa wanahusika na wale watoto waliozaliwa, huku dalili za awali zikionyesha kuwa yule mtoto wa kiume angeweza kuwa amewekewa kitu na yule Daktari wa Kiyahudi. Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa chochote alichowekewa Maganga yule mtoto wa Paul ingechukua miaka zaidi ya ishirini na minane kuweza kuonekana na hakukuwa na namna nyingine ya kusoma alama hizo mwilini mwake. Kutokana na unyeti wa jambo hili na utaratibu wake kuwa mrefu sana sikutaka kuwa na mawasiliano ya karibu sana na KAPTEN, ili kutoamsha maswali vichwani mwa watu. Nasema imekuwa miaka migumu sana kwa sababu miaka saba baadaye nilipoteza mawasiliano na KAPTEN, si hilo tu, nilipoteza hata nyendo zake na mahali alipokuwa. Nadhani mnaelewa kuwa kupoteza nyendo na mawasiliano na KAPTEN ilimaanisha kupoteza mawasiliano na Paul na Mwasumbi ambao sasa ndiyo walikuwa kwenye uwanja wa matukio. Ni wazi kuwa KAPTEN atakuwa alipata watu au mtu ambao watakuwa wamemwahidi maslahi makubwa na hivyo kwa sasa anawafanyia kazi. Ili kuimarisha timu yake, ndipo KAPTEN akamchukua Sophia, nadhani mkuu unaelewa namaanisha nini, nikiongelea Sophia.
Pamoja na jitihada zote za makusudi, lakini sikuwa nimefanikiwa kujua hawa watu wako wapi hadi wiki chache zilizopita nilipopata mawasiliano ya Luteni Mwasumbi. Mwasumbi alinieleza kuwa kwa miaka yote hiyo wamekuwa wakifuatilia kwa karibu sana maisha ya kijana Maganga. Mwasumbi aliniambia kuwa Maganga ana alama mwilini mwake ambayo alichorwa na yule Daktari wa Kiyahudi wakati wa kuzaliwa, alama hiyo inaonyesha mahali ambapo Myahudi huyo alikuwa ameficha karatasi zilizokuwa na kanuni ya kutengenezea silaha ya kudhibiti bomu la Atomic. Mwasumbi alinitaarifu kuwa ilikuwa imebaki wiki moja tu ambapo KAPTEN na kundi lake wangeenda kwenye Kijiji ambacho Paul alikuwa akimlea Maganga ili kumchukua na kufanya utaratibu wa kuzisoma hizo alama mwilini mwake kisha kuendesha operesheni ya kuzichukua karatasi hizo. Sikuwa na hiari, maana sikuwa na muda, ilibidi nimuamini Mwasumbi na kumwamuru kumtorosha Maganga kabla KAPTEN na kundi lake hawajafika Kijijini pale. Niliona heri nusu shari kuliko shari kamili, kama nisingekubaliana na Mwasumbi nisingekuwa na njia mbadala ya kuweza kumfikia huyo Maganga kwa muda nilikuwa nao mkononi. Mwasumbi alifanikiwa kumchukua Maganga siku moja kabla vijana wa KAPTEN na kumpeleka kwenye kituo chetu maalum cha uchunguzi. Kwa msaada mkubwa wa wataalamu wetu tuliweza kufanikiwa kujua eneo ambapo karatasi hizo zimehifadhiwa. Hivyo nikatuma timu ya wataalamu ili kwenda kuangalia uwezekano wa kuzichukua. Katika hilo kundi la wataalamu hakuna aliyekuwa anajua walikuwa wanakwenda kuchukua nini. Nasikitika kusema kati ya vijana ishirini waliokwenda, walirudi vijana watatu tu wakiwa hai. Wengine wote walifia eneo la tukio.” Jenerali Mmbando aliweka tuo na kuruhusu mate kupita kooni.
“Ulituma watu wa namna gani?” Aliuliza yule Mzee aliyetambulishwa kama Mtaalamu wa Ufundi.
“Nilichukua vijana sita kutoka AK218, wanne toka CA10 na waliobaki walikuwa Makomandoo toka mbegu maalumu.” Jenerali Mmbando alieleza.
“Khaaaah!, haiwezekani. Watu uliowasema wana uwezo wa kupambana na jeshi kubwa sana sasa ilikuwaje wakabaki watatu tu?” Mkuu wa Majeshi aling’aka.
“Labda kama walikuwa wanapambana na mizimu!” Aliongeza yule Mzee Mtaalamu wa Ufundi.
“Myahudi huyo amezihifadhi hizo karatasi ndani ya pango lillilokaa kama shimo. Pango hilo liko kwenye pori moja, kwa mujibu wa video camera ambazo tulikuwa tumewafunga wale vijana walitumbukia pangoni mule, ni dhahiri kuwa Myahudi huyo ameamua kutumia kila alichonacho kuhakikisha karatasi hizo haziangukii katika mikono asiyoitaka. Video camera zinaonyesha kuwa ndani ya shimo hilo kuna joka kubwa sana, joka hilo ni mbegu ya kipekee sana, lina kasi na shabaha ya ajabu. Hivyo yeyote anayetaka kuzifikia hizo karatasi ni lazima kuliangamiza hilo joka. Mnaweza jiuliza na kushangaa kuwa inawezekanaje ikawa shida kuua nyoka mmoja. Hakika kuua lile joka si kazi ngumu ila kuna kitu cha ziada, kuta za pango hilo zimechomekwa mashine fulani kuzunguka shimo lote, mashine hizo hufyatua mishale kutokea pande zote na mishale hiyo husambaa kulenga pande zote za shimo. Inavyoonyesha ni kuwa chuma kinachotengeneza ncha ya mishale hiyo ina madini maalum ambayo husukumana na mfumo wa mwili wa yule nyoka na hivyo kila ile mishale inapokuwa inamkaribia yule nyoka hubadilisha mwelekeo. Mashine hizo, huamshwa na mtikisiko wa moyo wa binadamu. Hivyo kuna umbali fulani ambao mashine hizo mfumo wake huamshwa na mapigo ya moyo wa binadamu yaliyo jirani na hizo mashine. Moja ikishafyatua, na nyingine huendelea kufyatua michale hiyo midogo kama misumari ya inchi mbili. Wataalamu wanadai kuwa inawezekana mishale hiyo ikawa na sumu maana video zilionyesha kuwa, haimchukui mtu dakika nyingi kuendelea kuwa hai mara baada ya kuchomwa au hata kukwaruzwa na mishale hiyo. Kwa ilivyo sasa hakuna namna mtu anaweza kuingia akapona. Baada ya kugundua hilo tukafikiria kutumia mabomu, ili kuharibu hizo mashine na kuliua lile joka. Hapo tena tukakabiliana na kikwazo kingine. Kwa mujibu wa zile video camera walizokuwa wamevaa wale watu walioingia shimoni na baadae kuuawa ama na ile mishale au lile joka, inaonyesha kuwa hizo karatasi ziko kwenye boksi ambalo kuta zake zimetengenezwa kwa baruti maalum ambayo italipuka mara ipatapo moto au joto kali sana. Hivyo kupiga bomu kuna maanisha kuziteketeza zile karatasi.
Hivyo baada ya harakati hizo kwa wiki nzima iliyopita, tumeamua kuwa wapole na kwenda taratibu. Ni wazi kuwa Myahudi huyo kaamua kutumia ubunifu wa hali ya juu kuweza kufanya hivyo, haijulikani kama kafanya mwenyewe au kasaidiwa na Wayahudi wenzie, maana kinachotushangaza ni jinsi mtu ambaye ni Daktari kuweza kufanya ufundi wa namna ile. Kwa hali ya siasa ilivyo Duniani kwa sasa, hasa kwa upande wa mahusiano ya Israeli na nchi za Kiarabu iko wazi kuwa Wayahudi wanajua kuwa kuendelea kuishi kwao hapa duniani haitakiwi kuwa hiari bali lazima. Wamejivika umiliki wa siri muhimu na ujuzi ambao Dunia nzima inabidi iende nao kwa makini. Nadhani mnaelewa kuwa Marekani mara zote imekuwa upande wa Wayahudi kwa kila jambo, na siri ni moja tu kuwa katika zile silaha tatu ambazo Marekani inajivunia kuwa nazo zote zimebuniwa na Wayahudi, na inasemekana watu hao kwa kila silaha kali wanayobuni wanatengeneza na Silaha mbadala wa kuidhibiti. Kinachofanya Marekani na mataifa makubwa washindwe kuwatowesha hawa Wayahudi ni hii mbinu yao ya kuficha hizo silaha mbadala. Kanuni ya silaha mbadala hukabidhiwa kwa Myahudi asiyejulikana aliyeko sehemu isiyodhaniwa wala kufikiriwa Duniani. Kwa hivyo huwezi kujua nani salama na nani hatari. Mara nyingine binafsi simlaumu Nyerere kwa maamuzi aliyoyachukua, hawa watu ni hatari sana." Jenerali Mmbando alielezea kwa makini na utaratibu mkubwa.
“Mmmmh!, hii kitu imekaa vibaya sana makamanda, kabla sijauliza maswali ya ufafanuzi hebu tuambie una mkakati gani kuhakikisha tunaweza kuzifikia hizo karatasi kabla ya KAPTEN na wowote walio nyuma yake, maana wasiwasi alionao Mkuu wa Nchi, ni kama zikiangukia mikononi mwa watu wasio salama, amani ya Dunia inaweza vurugika ndani ya miezi michache na kushuhudia mauaji ya kutisha. Lazima ieleweke kuwa kwa hali ilivyo duniani kwa sasa, ni vema kukawa na nchi zenye nguvu kuliko nchi nyingine. Hii inaweka usawa duniani, na nchi zenye nguvu ndizo ziwe na hasara kubwa pindi amani ya dunia ikipotea. Ikitokea kuwa uwezo wa kijeshi ukaangukia mikononi mwa nchi ambayo haina hasara kubwa kwa kupotea kwa amani duniani, au nchi ndogondogo tu isiyo na uongozi imara ikapata umiliki wa silaha hizi za kutisha lazima tujue kuwa dunia haitokalika tena. Sasa hebu tuambie unafanya nini ili kuhakikisha tunafanikiwa?”
Mkuu wa majeshi aliuliza huku akimwangalia Jenerali Mmbando na yule Mzee Mtaalamu wa Ufundi aliyeonekana kuwa na umri mkubwa.
“Kuna mambo matatu hapa; kwanza ni Mwasumbi, ninaamini bado anaweza kuwa na namna ya kunisaidia kufikia mwisho wa suala hili, pili Maganga wakati wanaendelea kumpa mafunzo ya kujihami na mbinu za mapigano, wataalamu waendelee kuuchunguza mwili wake kuona kama kuna lolote linalohusiana na namna ya kutuwezesha kuzichukua zile karatasi, tatu nataka kujua KAPTEN yuko katika hatua gani juu ya hili, maana kwa sasa nina kila sababu ya kumwita muasi, labda kama wewe mkuu una taarifa mbadala, maana wewe ndiye unajua karibu kila jambo ndani ya jeshi. Najua na yeye anazitafuta hizo karatasi, kwa hivyo nataka nijue ana taarifa gani, kwa vyovyote tutakuwa tumemvuruga sana kwa kitendo cha kumchukua Maganga. Nataka kujua kama tofauti na Maganga ana mtu yeyote ambaye huenda anaweza kuwa na alama nyingine mwilini kama alivyokuwa Maganga. Maana ikumbukwe kuwa wakati wa ule usiku ambao ile wodi ya kujifungulia inalipuliwa kulizaliwa watoto wengi, sasa inawezekana yule Myahudi aliamua kutawanya taarifa kwa watoto tofauti. Tatu, nataka kujua Paul yuko wapi na anajua nini kuhusu Maganga, maana yeye ndiye amekuwa kama mzazi wa Maganga kwa miaka yote hiyo, lakini lengo kuu ikiwa ni kusubiri wakati wa kuweza kuzipata taarifa toka mwilini mwa Maganga. Kama ujuavyo kuwa wataalamu wamebaini kuwa kabla ya wiki ile iliyokusudiwa isingewezekana kusizoma zile alama na herufi zilizokuwa mwilini mwa Maganga. Hivyo tulimchukua kwa wakati muafaka maana matumizi yake ndiyo yalikuwa yamewadia." Alisema Jenerali Mmbando taratibu na kwa uhakika. Mkuu wa Majeshi alimwangalia Jenerali Mmbando, kisha akamgeukia yule Mzee ambaye yeye alimtambulisha kama Mtaalamu wa Ufundi, alimwangalia kwa ule mtindo wa kama anamwuliza una lolote.
“Asante kijana wangu!”
“Kijana wako? Mkuu wa Majeshi unamwita kijana wako? Mbona siwaelewi?” Jenerali Mmbando alihamaki mara baada ya kumsikia yule Mzee, Mtaalamu wa Ufundi akimwita Mkuu wa Majeshi - kijana wangu.
"Jenarali, achana na hilo, niachie mimi, haya tuendelee.” Mkuu wa Majeshi alimtuliza Mmbando, ambaye baada ya kuambiwa hivyo na mkuu wake akatulia na kushusha pumzi ndefu.
“Kwa nini unahisi kuwa Mwasumbi anaweza kuwa na taarifa za ziada dhidi ya Maganga? Je, unahisi KAPTEN na Paul bado wako shirika? Unadhani nani anaweza kuwa nyuma ya KAPTEN, namaanisha nchi gani?” Aliuliza yule Mzee kwa sauti ya kutetemeka.
“Siku ile wakati Paul akiliandaa kundi lake kwenda Kijijini kwa ajili ya kumchukua Maganga, nilimsihi sana Mwasumbi aondoke kwa sababu alikuwa ameshafanya alichotakiwa kufanya.” Mmbando alianza kujibu taratibu. Kisha akaendelea.
“Lakini alikataa kwa madai kuwa kuna mambo alitakiwa kuyaweka sawa. Tulivutana sana, maana sikutaka aonane na Paul au KAPTEN kwa ajili ya usalama wake na operesheni kwa ujumla, lakini hata hivyo alikataa akidai ni kwa faida ya nchi na damu yake pia. Nilipomtaka kufafanua hilo akaniambia, next time. Kwa hivyo ninahisi kuna la ziada. Ila hakuwa na muda wa kunieleza na alionekana kutokuwa mtu aliyetulia. Pia, labda niseme hili linaweza kuwa la muhimu, Maganga ni mtoto wa damu wa Mwasumbi.
Kapteni na Mwasumbi bado wana mawasiliano, kwa mujibu wa Mwasumbi, mmoja kati ya vijana waliokuwa kwenye gari lililoenda kumchukua Maganga na Paul pale Kijijini lilikuwa la kijana wa KAPTEN, Mwasumbi aliweza kumtambua. Hivyo kwa vyovyote vile Paul yuko na KAPTEN. Paul ni mpiganaji mzuri sana ila hawezi kuwa na kundi la kuendesha operesheni, kwa vyovyote, KAPTEN alipewa tenda na akamshirikisha Paul na Sophia.
Na kuhusu ni nani anaweza kuwa anahusika katika kuwatumia KAPTEN na kundi lake hapo naweza kuihusisha Japan. Utakumbuka ile miaka baada ya Nyerere kuwatimua Wayahudi kwa sababu za kisiasa. Lakini jeshini tunajua kuwa hii sababu ya kuwepo hizi karatasi hapa nchini ilikuwa sababu kuu, China, Japan na Urusi zilijisogeza karibu sana na Nyerere. Usiku ule kabla ile wodi haijalipuliwa na yule Daktari wa Kiyahudi kuuawa kama walivyodai japo sasa tunajua kuwa yupo hai, balozi wa Japan alikuwa ameomba kwenda kutembelea Hospitali ya Bugando. Balozi huyo aliweka wazi kuwa yeye na timu yake walikuwa wamepanga kwenda kwenye wodi ya watoto. Mnakumbuka jinsi ile ndege ya kutisha ya Japani ilivyokuwa imekuja na watu wa kazi, ni wazi kuwa walikuwa wanalenga kwenda kumchukua yule Daktari wa Kiyahudi. Nadhani kwa namna moja ama nyingine taarifa za kijasusi zilitembea haraka zaidi na hivyo Daktari yule akachukuliwa na kusingiziwa kufa. Hivyo tangu hapo Japan imekuwa mstari wa mbele kuhusu suala hili na nadhani kuanzia hapo walianza upelelezi wao kwa kasi zaidi.
Itakumbukwa kuwa hadi sasa, Japan ndiyo nchi pekee ambayo imewahi kupigwa kwa bomu la Atomic, wanajua machungu na madhara ya bomu hilo kuliko nchi yoyote. Na itakuwa shangwe kwa nchi yao kusikia kuwa nchi yao ina silaha ya kuweza kuwakinga na bomu la Atomic." Jenerali Mmbando alisema huku akionyesha kuwa amechoka kutoa maelezo.
“Sikiliza Jenerali, hili suala ni nyeti mno kuweza kuchukuliwa kwa mzaha, maana madhara yake yanaweza kusababisha dunia nzima kutoweka, sasa ninachotaka kusema ni kuwa, fanya mambo yako ukijua kuwa huna nafasi ya kufanya mzaha hata kidogo. Pia, ukae ukijua, mimi na Mkuu wa Nchi, tunalifuatilia suala hili kwa makini sana. Tunajua kuwa majasusi wa Nchi za Magharibi wako hapa nao wanahitaji sana hizo karatasi, tena wao wanazihitaji kwa udi na uvumba. Hivyo uyafanyayo yafanye kwa kasi na usahihi mkubwa. Ukihitaji msaada wowote usisite kutuambia. Ila nina ushauri kwako, fikiria kumwangamiza Mwasumbi, kama kweli Maganga ni mwanae na kuna mambo anayahusisha na damu yake, basi huyo mtu si salama kabisa katika hii operesheni. Damu nzito kuliko maji, heri nusu shari kuliko shari kamili. Mmalize Mwasumbi. Labda la mwisho ambalo ningependa ufafanuzi kidogo na kutaka kujua kwa vipi unamhusisha Sophia na KAPTEN?” Mkuu wa Majeshi alimalizia maelezo yake kwa swali.
“Kuna siku KAPTEN alikwenda Hospitali ya Bugando kuchunguza mambo fulani ayajuayo yeye, mkanda wa camera wa siku hiyo unamwonyesha akiwa na Sophia. Si hiyo tu, kuna wakati mwingine yeye na vijana wake walivamia nyumba moja iliyokuwa ikikaliwa na Majasusi wa Kihindi, camera ya ulinzi pia, inamwonyesha Sophia na KAPTEN wakiwauwa majasusi hao huku wote wawili wakiwa wamevalia Sare za Jeshi. Na kila Sophia alipotaka kuua alimrushia mtu ua jekundu. Mara kadhaa KAPTEN alisikika akimwita Sophia kwa jina la UA JEKUNDU." Jenerali Mmbando alieleza huku akikabidhi faili la maelezo yake mkononi kwa Mkuu wa Majeshi, ambaye alilikabidhi kwa yule Mzee, Mtaalamu wa Ufundi.
“Kwa zaidi ya miaka 40, huyu ndiye amekuwa mtunza siri mkuu wa jeshi letu, siri ambazo hazitakiwi kujulikana na wakuu wengine ndani ya jeshi, huhifadhiwa na huyu Mzee. Hajulikani sana na watu lakini kila Mkuu wa Jeshi, mpya anapokuja lazima Rais amtambulishe kwa huyu mtu na kila Rais mpya akija lazima Mkuu wa Majeshi amtambulishe kwa huyu Mzee. Hivyo jisikie salama kabisa hili faili kuwa mikononi mwake. Na baada ya hiki kikao huwezi kumwona tena labda kama nitamhitaji.” Mkuu wa Majeshi alisema. Baada ya hapo yalifuata mazungumzo ya kawaida na vicheko vya hapa na pale.

*************

MAGANGA ALIJIANGALIA TENA, hakuamini kuwa ule ulikuwa ni mwili wake kwa jinsi ulivyokuwa umeharibika kwa mikwaruzo na usugu uliokuwa umetokea mara. Alijiangalia mikono yake, ilikuwa kama ya wale waponda kokoto aliyekuwa kwenye kazi hiyo kwa miaka mingi, aliangalia vidole vyake, akaviinua, akavichezesha, vikatoa mlio kama wa mti uliovunjwa, vilikuwa vimekakamaa sana. Alipojiangalia miguuni hakutaka kukubali kuwa ni yeye, alipoangalia nyayo za miguu yake akasahau kuwa alikuwa yeye lakini alipojiangalia kwenye kioo kilichokuwa mle bafuni alikutana na sura yake ambayo ilimthibitishia alikuwa bado ni Maganga, Maganga Paul au Maganga Mwasumbi, hakuwa na hakika ni jina gani la pili ajipe. Hakuwa na namna ya kuthibitisha, ila jambo moja alikuwa na hakika nalo, yeye alikuwa Maganga. Alifungulia maji ya bomba na kuyaruhusu yapite mwilini kwake, aliyaacha kwa muda huku akiwa anapumua taratibu akisikiliza jinsi yale maji yalivyokuwa yakitonesha majeraha yaliyotokana na kuchubuliwa na miti na mawe wakati akiwa kwenye kile kilichoitwa ‘Mafunzo.’
Mafunzo, kama wenyewe walivyoyaita na alivyoambiwa na Askofu Alphonso kwa njia ya ujumbe uliokuwa kwenye ile karatasi siku ya kwanza alipoingia humo ndani yalikuwa yamemfanya awe mtu tofauti kabisa. Zilikuwa zimepita siku nyingi tangu aingie kwenye hiyo himaya, kwa akili yake alikadiria kuwa zingekuwa zimeshapita siku zaidi ya arobaini. Kutoka na mambo yalikuwa yakifanyika hapo, Maganga alikuwa ameshajikinai, hakuwa anajali tena kuhusu maisha yake wala kesho, hakuwa na haja yoyote ya kujua majibu ya maswali mengi aliyokuwa nayo kichwani wiki ya kwanza aliyokuwa ndani ya hiyo himaya.
Hakuwa anajua chochote katika eneo hilo zaidi ya hicho chumba alichokuwemo na kuwa usiku wote ulitumika kwa ajili ya mazoezi ambayo aliyafanya gizani na watu asiowajua, wasio na huruma wala utu. Watu waliokuwa wakifanya vitendo zaidi kuliko kuongea. Watu waliojua kutoa amri na kusimamia utekelezaji wake.
Mchana kuna watu walikuwa wakija kuufanyia uchunguzi mwili wake, Maganga hakujua walikuwa wakitafuta nini mwilini mwake, lakini ilikuwa wazi kuwa kile walichokuwa wakikitafuta kilikuwa na umuhimu mzito sana, maana aliwaona jinsi walivyokuwa wakitumia vifaa vya kisasa na walionekana kuwa walikuwa watu wenye ujuzi mkubwa katika walichokuwa wakikifanya. Walitumia saa nyingi katika kuupekua mwili wake, mwili ambao usiku ulikuwa ukichubuliwa kwa maumivu ya mazoezi na mazingira ya mazoezi hayo, mchana ulikuwa ukitomaswa tomaswa na kuminywa minywa na watu wengine walioonekana kutafuta kitu toka mwilini mwake. Wakati mwingine walichukua damu yake na kuifanyia uchunguzi mkubwa. Waliulizana wakajibizana, wakakubaliana, wakabishana, wakakataliana ili mradi tu ulikuwa uchunguzi ambao ulileta kero kubwa kwa Maganga ambaye alikuwa akihitaji kupumzika kwa ajili ya mikiki mikiki ya usiku.
Kitu kimoja tu ambacho alishindwa kuamua kama achukie au kukifurahia ni uwezo wake wa kufanya mambo fulani fulani ulikuwa umeshabadilika kwa kiasi kikubwa. Alikuwa na uwezo wa kukimbia kwa namna ya ajabu sana, alikuwa na uwezo wa kupigana kwa namna ambayo yeye mwenyewe hakuelewa ni ipi maana haya kuwa mafunzo rasmi ila alijikuta akilazimika kuyajua kutokana na mazingira yenyewe ya mafunzo na waalimu walivyokuwa. Hakuelewa kama ndiyo kuchanganyikiwa au la, alijikuta ana uwezo wa kuhisi kwa kiwango cha juu sana. Kwa vile mafunzo yake kwa sehemu kubwa yalifanyika gizani, ilibidi ajifunze kutegemea hisia zake badala ya macho kumwezesha kuona. Hivyo akiwa gizani hisia zake zilikuwa na uwezo wa kuona sawa na anavyotumia macho akiwa nuruni. Hofu kwake ilikuwa msamiati, ila kilichochukua nafasi badala ya hofu ni kutotaka kukosea maagizo, hakuwa anaogopa ila badala yake hakuwa anataka kukosea maana kukosea kulimsababisha apate kipigo kikali kwa mwalimu yeyote aliyekuwa anamfundisha siku hiyo.
 
PATASHIKA - 18

Mtunzi: Japhet Nyang'oro Sudi


Wakati wanaingia kwenye nyumba, Vivian, Hellen na Milka walikuwa wamechoka sana, hakuna kitu walikuwa wakikihitaji zaidi ya kupumzika. Ndiyo maana miili yao haikuhisi chochote walipoona na kusikia makelele ya yule askari wa kike alivyokuwa akifanya mapenzi na yule mwanamume waliyemkuta kwenye hiyo nyumba. Wangehisi vipi wakati miili yao na akili vilikuwa taabani kwa uchovu. Vivian mara ya mwisho kulala usingizi wa maana ilikuwa ni wakati anamuuguza mama yake Maganga Hospitali ya Sengerema.
Lakini tangu mwanamke yule alipofariki, mambo mengi yalitokea na tangu hapo hakuwa amepata nafasi ya kupumzika. Hivyo mwili wake na akili yake vilikuwa vimechoka sana. Milka ni kama ilivyokuwa kwa Vivian na Hellen. Walikuwa na hamu ya kusimuliana yaliyowakuta na kujua kwa nini walikuwa mahali pale lakini uchovu wa akili na mwili havikuwaruhusu kufanya hivyo.
Baada ya kila mtu kuwa amekabidhiwa kitanda chake, waliletewa chakula kizuri sana, wakala. Kilichofuata kikawa ni kukalala usingizi. Walilala hadi wakachoka. Alikuwa ni Milka aliyefanya jaribio la kutoka chumbani kwake, baada ya kuwa ameoga na kubadilisha nguo alizokuwa amevaa. Lile furushi walilokuwa wamepewa kila mmoja yeye na Hellen lilikuwa na nguo, hivyo alichagua moja iliyomuenea vemaa akavaa. Baadaye ndipo akajaribu kitasa cha mlango, ulikuwa wazi. Kwanza alianza kutembea kwa wasiwasi, lakini alipogundua kuwa ilionekana hakukuwa na mtu alitembea kwa kawaida. Hakujua alikuwa akienda wapi maana nyumba hiyo ilikuwa na vibaraza vingi na vyumba vingi. Hakuwa na jingine zaidi ya kutaka kuonana na Vivian na Hellen, alijua wazi kuwa wangekuwa kwenye moja ya vyumba vilivyokuwa kwenye hiyo nyumba. Hivyo taratibu akaanza kujaribu kitasa cha kila mlango, ni katika kufanya hivyo mlango mmoja ulifunguka. Akachungulia ndani, macho yake yalikutana na yule mwanajeshi wa kike na jamaa yake wakiwa fofofo huku wakiwa kama walivyozaliwa. Aliurudishia ule mlango. Akaendelea na ziara yake hadi alipofikia chumba kingine kilichofunguka, alichungulia, humo alipokelewa na macho ya Hellen na Vivian, Hellen ndiyo alikuwa anavaa.
"Hamjambo warembo?” Milka alisabahi baada ya kuwa ameingia ndani.
"Hatujambo hofu kwako." Vivian alijibu.
"Mimi nimeota ndoto mbayambaya tu." Hellen alisema huku akiwa anajaribu nguo ya ndani kati ya zile zilizokuwa kwenye furushi alilokuwa amepewa na yule mwanajeshi wa kike.
"Utaachaje kuota baada ya haya yote yaliyotokea?!” Milka alisema huku macho yake yakikagua mwili wa Hellen.
"Khaa!, mnaniangalia hadi naona aibu, acheni hizo.” Hellen alisema baada ya kuona Milka na Vivian walivyokuwa wakimwangalia kama wanaomkagua.
"Eeeeh!, bibie nina kaka mimi, unajuaje labda kanipa kazi ya kumtafutia." Milka alisema
"Mmmmh! Padri yule hayawezi haya." Hellen alijibu.
"Hata angekuwa anayaweza, yule ni kaka yako." Vivian alidakia. "Aaaaah!, hakuna ajuaye kwa sasa maana mchanganyiko huu wa habari naweza jikuta nafaa tu kula na Padri." Hellen alisema huku akiwa ameshamaliza kuvaa.
"Hebu tuacheni ujinga hapa, nadhani inatakiwa tuulizane na tujuzane nini kinaendelea na nanmna ya kujinasua hapa. Na kwa jinsi mambo yalivyo kwanza nataka tufahamiane maana nimekuja kugundua inawezekana hata hatujuani hapa!” Milka aliwagutua wenzie.
"Shiiiiiii!” Vivian alisema. "Hadi tutakapoona kuna usiri na usalama wa kuongea." Neno hilo alilisema kwa kunong'ona katika Lugha ya kisukuma. Milka alielewa lakini Hellen hakuelewa.
"Sijaelewa…!” Hellen alisema. Harakaharaka kwa vile alikuwa jirani naye, Vivian alimvuta Hellen na kumnong'oneza kile alichokuwa amesema. Wote watatu wakatazamana, wakanyamaza. Baadae wakaendelea na maongezi ya kawaida ya wasichana wakutanapo lakini kwa makubaliano kuwa wasiongelee kabisa mambo yaliyotokea Kijijini Katunguru. Onyo alilokuwa amepewa na Mwasumbi bado lilikuwa kichwani mwa Vivian hivyo hakutaka kuongelea lolote pasipo kujua nani mwingine angekuwa anasikiliza.
Waliongea wakachoka, walienda sebuleni wakaweka mikanda ya video, wakaangalia wakachoka. Jambo moja lililowashangaza ni kuwa hawakumwona tena yule mwanajeshi wa kike aliyewaleta wala wale wanaume wawili waliowakuta, mtu pekee aliyekuwa akiwahudumia alikuwa Bibi mmoja, ambaye mwanzoni walijitahidi sana kumwongelesha na kumuuliza maswali kadhaa lakini hakuonekana kuwajali kabisa. Mwishoni walikuja kugundua kuwa Bibi yule alikuwa bubu na kiziwi. Bibi huyo alikuwa akipika chakula na kufanya usafi wa aina zote kwenye hiyo nyumba. Walipojaribu kutoka nje waligundua kuwa nyumba ilikuwa imefungwa na hakuna ambaye angeweza kutoka nje.
Hawakuwa na mawasiliano ya aina yoyote na ulimwengu wa nje. Walipohakikisha kuwa hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba hiyo ndipo walipoamua kuongelea mkasa uliokuwa umewapa.
Alianza Milka, alisimulia yote yaliyokuwa yametoke siku ile walipokuwa Kijijini Katunguru ambapo walishuhudia Paul na wanaume wengine wawili wakiteketeza eneo zima kwa sababu tu ya kumtafuta Maganga. Kisha wakaelezea jinsi kwa namna ya kimiujiza walivyoweza kuokolewa na Askofu Alphonso.
"Sitaongea mengi sana, ila kuna mambo ambayo najua mkiyajua yanaweza kuwasaidia. Askofu Alphonso mnayemsema, hakuwa Askofu Alphonso yule wa siku zote, bali yule alikuwa ni Mzee Mwasumbi aliyekuwa amevaa sura ya bandia iliyokuwa inafanana na sura ya Askofu Alphonso...." Vivian alisema lakini kauli yake ilikatwa na Hellen.
“Eheee!, umesema Mwasumbi umenikumbusha...” Hapo Hellen akasimulia wakati yeye na Maganga walipokuwa kwa Mwasumbi na yote waliyokuwa wameyasikia. Milka na Vivian wakabaki vinywa wazi. Lakini Vivian akawa na picha kubwa zaidi kichwani mwake. Alikuwa na maswali kadhaa aliyokuwa akijiuliza, kama Milka na Maganga ni watoto wa Mwasumbi, ina maana hao watatu ni watoto wa mtu mmoja - Mwasumbi. Sasa ilikuwaje akaishia kwenye mikono ya wazazi anaoishi nao sasa.
“Kwa kweli sielewi kwa nini hawa watu wametufungia hapa?” Hellen alisema.
“Kwa vyovyote ilivyo, watu hawa watakuwa wanajuana na Mwasumbi, maana hadi sasa mkombozi wetu sote hapa ni mmoja na nadhani mnajua ni kwa nini ametuokoa, sababu iko wazi nayo ni kuwa Mwasumbi anajua sisi ni watoto wake. Na kwa mujibu wa maelezo ya Hellen inaonyesha japo anajua kuwa Hellen si mwanae ila anamjua vizuri sana, mama yake Hellen..." Milka alieleza. Wote wakatingisha vichwa kukubaliana naye.
“Kama Mwasumbi na Paul walikuwa marafiki, mnataka kuniambia kuwa watu hawa urafiki wao ulivunjwa na wanawake tu au kuna kitu kingine nyuma ya hayo? Na kwa nini Mwasumbi aliendelea kufuatilia maisha ya Paul kwa siri? Msiniambie kuwa ni kwa sababu tu alijua kuwa Paul alikuwa anaishi na wanawe. Maana jinsi Mwasumbi alivyotuokoa inaonyesha wazi kana kwamba alikuwa anajua nini kingetokea na alikuwa amejiandaa siku nyingi kutuokoa. Vyovyote ilivyo nahisi kuna haja ya kuwa na mazungumzo na Mwasumbi, inaonekana ana mengi anayojua kutuhusu, hasa asili yetu na kwa nini tuko kwenye hali hii...” Milka alisema huku akiwaangalia wenzie kwa zamu. Wote walikuwa wakiongea kwa sauti za kunong'ona.

*****************************
Kitabu hiki cha PATASHIKA Unaweza kipata kwa sh 10,000 tu. 0762204166
******************************
Vivian alikuwa anashindana na nafsi yake kama ama awaeleze wenzie yale aliyoambiwa na Mwasumbi ama asiwaeleze. Lakini mwisho wa siku akawa amekata shauri kutowaambia.
“Kabla sijaachana na Mwasumbi, alivuta kwa nguvu nywele chache toka kichwani kwake na kunipatia, alisema ana hakika ipo siku nitazihitaji.” Vivian aliamua kuwaambia hilo maana hakuona kuwa lilikuwa na taarifa yoyote kuhusiana na habari ya silaha aliyokuwa ameambia na Mwasumbi.
“Ziko wapi hizo nywele? Yule Mzee ana akili sana, sasa nakubali kuwa anaweza kuwa baba yangu, sikuwahi kumpenda Paul, hakukuwa na mvuto wowote wa baba na mwana kati yangu mimi na yeye. Huyu Mwasumbi kwa namna mnavyonisimulia na matendo yake huyu anaweza kuwa ni baba yangu huyu...” Milka alisema, lakini akakatizwa na Vivian.
“We, Milka hebu angalia hicho kinywa chako hicho kisije kikaponza kichwa, watu hawachaguagi baba, baba huchaguliwa na mama pale mama anapoamua kuzaa na mwanaume alomridhia...” Vivian alisema, kwa namna ya kumuonya Milka juu ya kauli aliyokuwa ameitoa kuhusu Mzee Paul.
“Ziko wapi hizo nywele?!” Hellen alimkatiza Vivian kuonyesha kuwa hakuwa amezingatia onyo lake. Japo kutokana na maelezo yote ilikuwa inaelekea kuwa yeye peke yake ndiyo mtoto halisi wa Paul lakini tangu siku ile aliponusurika kunyongwa kule shambani, Hellen amekuwa na chuki ya ajabu dhidi ya Mzee Paul. Hivyo lolote baya lililosemwa au kupangwa dhidi ya Mzee Paul lilikuwa likiifurahisha na kuiburudisha nafsi yake. Hivyo onyo la Vivian kwa Milka kuhusu kauli mbaya ya Milka juu ya Mzee Paul hakulipenda hata kidogo.
“Hizi hapa!” Vivian alisema huku akiwa anafungua saa yake ya mkononi. Alizitoa zile nywele na kuwakabidhi wenzie.
“Sikilizeni, kama nilivyosema hapo awali, huyu Mzee Mwasumbi ana akili sana na kweli anastahili kuwa Luteni wa Jeshi. Unajua inawezekana hakuwa na hakika juu ya maisha yake, na alijua kuwa Vivian angetaka kuthibitisha kama kweli yeye ni mtoto wake. Hivyo hizi nywele zinaweza kutumika kupima vinasaba vya yule Mzee na kulinganisha na vya mtoto..." Kabla Milka hajamaliza maelezo yake, Hellen akadakia.
“Nakubaliana na wewe Milka, naona na wewe una akili kama baba yako Mwasumbi. Kweli hilo ndiyo lengo halisi la yeye kukupatia hizi nywele. Ila nami nina wazo la kuchangia...” Hellen alisema kwa sauti ya kushadadia
“Sema tu.” Milka alijibu kwa haraka kwa ile sauti ya kushabikia pia. Vivian alikuwa akiwaangalia na kuwasikiliza.
“Hakuna ajuaye hatima yetu, inawezekana sote tukatoka salama na kuendelea na maisha yetu ya kawaida au pia inawezekana hatutoka hapa salama. Lakini pia, inawezeka baadhi tukatoka salama na wengine tukaishia hapa.” Hellen aliongea lakini kauli yake ilikatishwa na Milka aliyelalamika.
“Aaaah! shostito, acha kutuchuria basi, we sema unalotaka kusema hayo mambo ya kufa wakati wengine ndiyo tunataka tukitoka hapa tukaanze kuyafaidi maisha wala halikubaliki. Sema unachotaka kusema, kama kufa tungekufa siku ile kule Kijijini.” Milka aliongea.
“Ninachotaka kusema ni kuwa, wote tufanye kama Mzee Mwasumbi alivyofanya, tutoe nywele zetu na tuziweke kwenye mafungu matatu kama tulivyo, kila unywele mmoja wa mmoja wetu tuuweke na kipande cha nywele ya Mzee Mwasumbi. Halafu kila mmoja awe na hayo mafungu matatu, ili akifanikiwa kutoka hapa salama afanye hivyo vipimo. Manaonaje?” Hellen alimalizia maelezo yake.
“Wazo zuri Hellen, nadhani tufanye hivyo.” Vivian aliafiki.
“Wewe naye una akili sana usije kuwa mtoto wa Mwasumbi pia, maana anaonekana alikuwa kiwembe sana yule mtu.” Milka alisema.
“Aaah! mimi bwana nimechukua akili za mama yangu, alikuwa na akili sana yule, ndiyo maana nadhani alishindwa kuishi na mtu kama Mzee Paul.” Hellen alisema kwa kujitapa.
“Unamaanisha nini? Ina maana mama Maganga aliyeweza kuishi na Mzee Paul alikuwa mjinga?” Vivian alihoji kwa sauti ya kuonya kwa mara nyingine. “Utamuweza huyu, si anaongea tu bila kufikiri saa nyingine.” Safari hii Milka lilimgusa kwa vile mama yake alikuwa amesemwa, hivyo akaunga mkono onyo la Vivian.
“Haya tuyaache hayo, tusijeanza rushiana ngumi wenyewe kwa wenyewe bure.” Vivian alisema tena. Baada ya hapo walizigawa zile nywele katika mafungu matatu na kuziweke alama ili kujua ipi ilikuwa ya nani. Kisha kila mmoja wao akapewa aina tatu za nywele ili azitumie pindi ikihitajika.
Maisha yao yaliendelea hivyo kwa wiki kadhaa, wakajikuta wamezoeana. Waliongea wakamaliza yakuongea, waliangalia muvi hadi wakachoka. Hatimaye maisha ndani ya nyumba hiyo yakawa mchoko mkubwa kwao. Yule Bibi aliendelea kuwapikia na kuwapa huduma. Jambo moja liliwashangaza, hawakujua ni saa ngapi na namna gani yule Bibi aliletewa chakula cha kuwapikia. Ila walikuta tu yule Bibi anabadilisha mapishi kila siku na vinywaji vikiongezeka kwenye friji.
Kitabu cha riwaya hii sasa kinapatikana duka la kona ya riwaya reloaded kwa Dar es salaam. Kwa mikoani wasiliana na mtunzi wa riwaya akuelekeze namna unaweza kipata kitabu hiki mkoani kwako. leo hii kinaweza kuwa mkononi kwako!

Hapo vipi?
 
Riwaya: PATASHIKA - 19

Mtunzi: Japhet Nyang'oro Sudi

“Unamaanisha nini? Ina maana mama Maganga aliyeweza kuishi na Mzee Paul alikuwa mjinga?” Vivian alihoji kwa sauti ya kuonya kwa mara nyingine. “Utamuweza huyu, si anaongea tu bila kufikiri saa nyingine.” Safari hii Milka lilimgusa kwa vile mama yake alikuwa amesemwa, hivyo akaunga mkono onyo la Vivian.
“Haya tuyaache hayo, tusijeanza rushiana ngumi wenyewe kwa wenyewe bure.” Vivian alisema tena. Baada ya hapo walizigawa zile nywele katika mafungu matatu na kuziweke alama ili kujua ipi ilikuwa ya nani. Kisha kila mmoja wao akapewa aina tatu za nywele ili azitumie pindi ikihitajika.
Maisha yao yaliendelea hivyo kwa wiki kadhaa, wakajikuta wamezoeana. Waliongea wakamaliza yakuongea, waliangalia muvi hadi wakachoka. Hatimaye maisha ndani ya nyumba hiyo yakawa mchoko mkubwa kwao. Yule Bibi aliendelea kuwapikia na kuwapa huduma. Jambo moja liliwashangaza, hawakujua ni saa ngapi na namna gani yule Bibi aliletewa chakula cha kuwapikia. Ila walikuta tu yule Bibi anabadilisha mapishi kila siku na vinywaji vikiongezeka kwenye friji.

********
MWASUMBI ALIREJEWA na fahamu taratibu kama zilivyokuwa zimemtoka. Aliweza kuyasikia mapigo ya moyo wake jinsi yalivyokuwa yakilazimishwa taratibu na mzungunguko hafifu wa damu. Alifumbua macho na kujaribu kutambua alikuwa wapi, lakini nguvu ya giza lilokuwa limetanda kila mahali ilimzidi macho yake. Hakuweza kuona chochote. Alijaribu kujitingisha, hapo akasikia ule mlio wa mbao kusuguana. Mlio wa kitanda kilichochoka. Alijaribu kupapasa aligundua kuwa alikuwa amelala juu ya mkeka. Akataka kuinuka, lakini maumivu makali toka kila sehemu ya mwili wake ilimzuia kuinuka. Baada ya dakika chache macho yake yakawa yameshazoea giza, alikodoa kwa nguvu zaidi huku akidhani kuwa kukodoa sana ndiyo kuona. Hatimaye akagundua kuwa alikuwa ndani ya chumba au nyumba. Aliweza kuona mwanga hafifu ulioweza kupenya kwa wembamba kama michirizi kwenye kuta za nyasi za chumba au nyumba aliyokuwa. Hatimaye alikuwa na hakika kuwa alikuwa ndani ya chumba cha nyasi baada ya kujitahidi na kufanikiwa kugusa sehemu ya ukuta wa chumba hicho – vidole vyake vilikutana na nyasi.
“Khoo khoo...aaaar!” Ilikuwa ni sauti ya kukohoa toka upande wa nje wa sehemu aliyokuwepo. Sauti ilionyesha dhahiri kuwa aliyekuwa anakohoa alikuwa na umri uliokwenda sana. Mwasumbi alijaribu kukumbuka tukio la mwisho wakati akipambana na Sophia.
Alichokumbuka ni kuwa, mara baada ya kuwa ameachana na Vivian, alibana sehemu huku akiwatayari kwa lolote. Nia yake ilikuwa ni kupambana na yeyote yule, alijua wazi kuwa KAPTEN na Paul wangecharuka kama nyuki mara baada ya yeye kuwawahi na kumchukua Maganga. Kwao ilikuwa kama kupokonywa tonge mdomoni.
Akiwa amejituliza kwenye kichaka fulani kilichokuwa jirani na nyumba moja ya nyasi eneo lile, aliweza kumwona Mzee mmoja aliyekuwa akiendesha baiskeli kuelekea barabarani. Ilikuwa inaelekea kuwa saa tisa alasiri wakati hayo yalipoanza kutokea. Wakati Mzee yule alipokaribia kuingia barabarani lilitokea tukio ambalo lilimsisimua Mwasumbi. Kwa nukta ya kwanza aliona Ua Jekundu likianguka mbele ya baiskeli ya yule Mzee, wakati yule Mzee anatafakari nini kilikuwa kinatokea na kuliangalia lile ua jekundu pale chini. Ghafla alikuja mtu aliyekuwa anajiviringisha kwa sarakasi kama kimbunga cha kiangazi. Mwasumbi alifanikiwa kutambua kuwa yule mhusika alikuwa ni mwanamke kwa jinsi mtikisiko wa nyonga zake na makalio ulivyokuwa pindi alivyokuwa akiruka. Lakini alishindwa kutafsiri jinsi yule msichana alivyompiga yule Mzee, kwani alipofikia mahali pale yule Mzee alipokuwa amesimamisha baiskeli yake akitaka kuokota lile ua, yule msichana alisimamia mikono na kwa kutumia miguu aliishika shingo ya yule Mzee na kuivunja. Hata risasi zilizotoka kwenye Bastola ya Mwasumbi ziliishia kuzikosakosa buti za yule msichana. Awali Mwasumbi alikuwa amejiandaa kumtetea yule Mzee, alijua fika kuwa yule mtu aliyekuwa akienda kumshambulia yule Mzee angetumia moja ya staili zilizozoeleka, hivyo shabaha yake ilikuwa imekadiria eneo ambalo kichwa kingekuwepo wakati huo. Staili hiyo ya uuaji ilimfanya Mwasumbi mara moja amkumbuke Sophia. Mwasumbi alijiweka sawa kwa pambano. Wakati macho yake yakiwa kwa Sophia maarufu kwa jina la Ua Jekundu, mara akasikia mchakacho tokea mgongoni kwake. Akahisi kitu kinakuja, alikwepa kwa kasi na kulipisha teke lililokuwa limepigwa na mtu tokea nyuma. Mwasumbi alijipindua na kuachia teke kali lililompata yule mtu ubavuni. Akaongeza jingine ambalo lilimpeleka chini. Hapo hakutaka kusubiri, aliachia risasi iliyolenga moyo na kumuua yule jamaa. Kabla hajakaa sawa walitokea wengine wawili. Mwasumbi alichomeka bastola kwenye mkanda wake. Akawa tayari kukabiliana nao, kitendo cha yule wa kwanza kumnyatia bila kummaliza ilikuwa taarifa tosha kwa Mwasumbi kuwa watu hao walimtaka akiwa hai. Hivyo alijua kuwa yeye alikuwa na nafasi na uhuru mzuri wa kuwamaliza kuliko wao, alielewa kuwa walikuwa na wakati mgumu kuliko yeye. Ndiyo siri ya mchezo, mtu anayetakiwa kumshika mwenzie huku kukiwa na sharti la kumbakiza hai huwa na wakati mgumu zaidi kuliko yule anayewindwa. Hapo likatokea pambano moja safi sana, lilibadilika toka mpango wa kutekana nyara na kuwa kufa na kupona. Kila mmoja alitumia uwezo na mbinu zake. Hadi mpambano unakwisha wale jamaa walikuwa maiti ambazo bado zilikuwa za moto zikiwa zinalilia pumzi iliyozitaliki. Mwasumbi alikuwa hoi lakini alijua hakuwa na muda wa kujipooza wala kupumzika. Wakati akitembea taratibu toka sehemu aliyokuwepo, mara akasikia mlio wa kitu kama jani likidondoka. Hakutaka kugeuka kuangalia, alishajua huyo angekuwa nani na kama akigeuka tu angekuwa ameshaingia kwenye mahesabu ya adui, alijirusha pembeni wakati pigo la aina yake la mkono wa Sophia likipita kwa kasi kama upanga uliopiga hewa. Mwasumbi aliachia mapigo manne mfululizo, mawili yalimpata Sophia, lakini mawili yalikwepwa.
“KAPTEN anakuhitaji, sijatumwa kukuua, ila ukinilazimisha unajua nini naweza kufanya.” Alisema Sophia kwa sauti ya kike ya kikatili.
“Haiwezekani, ama nife au ufe, maana kwa vyovyote nitaishia kufa au kuua.” Mwasumbi alisema huku akijiweka sawa tayari kwa mpambano. Alikuwa anamjua Sophia, alijua nguvu zake na udhaifu wake. Akakumbuka kuwa walianza hii kazi pamoja mara baada ya kufanikiwa kumshawishi ajiunge na kundi lao la kuzitafuta karatasi zilizo na kanuni ya kutengenezea silaha. Sophia akabaki kwenye upande wa kuua na kushambulia wakati yeye Mwasumbi na Paul wakiwa kwenye upande wa kimkakati zaidi huku wote wakitumiwa na KAPTEN bila kujuana. Kapten alikuwa bosi wao wote wawili walipokuwa Dar es salaam na aliwaweka Katunguru makusudi. Alijua uwezo wa Sophia kuwa hakuwa mtu wa masihara hata kidogo.
“Okay, chukua au acha…!” Sophia hakumalizia kauli yake, alijipindua kwa staili ya kipekee na kuachilia mapigo mfululizo kwa Mwasumbi. Mwasumbi alitumia uwezo wake wote kuyaona na kujikinga lakini hatimaye mengi yakaanza kumwingia.
“Hebu niambie, Maganga umempeleka wapi?” Sophia aliuliza huku akiwa amejaa ghadhabu.
Japo alikuwa taabani, Mwasumbi alijua fika kuwa kama angesema tu angehalalisha kuuawa na Sophia. Maana sababu pekee ambayo ingewafanya watu hawa waendelea kumuacha hai ingekuwa ni kutaka kujua Maganga alipo.
“Si..si..sijui..muulize Mr M” Mwasumbi alisema. “Hebu acha kunichezea, unajua fika kuwa Paul hajui lolote na kwa uzembe alioufanya na yeye anakabiliwa na kifo huko aliko!” Sophia alisema huku akiongezea vipigo kuelekea kwa Mwasumbi.
Mwasumbi sasa alikuwa taabani kabisa. Lakini Sophia aliendelea kutoa kipigo kikali. Alijua fika kwa mtu mzoefu kama Mwasumbi ili aweze kutoa siri lazima umpeleke katikati ya hali ya kifo na uzima, huku nafsi ikiachiwa nguvu ndogo sana ya kuamua, ndipo angeweza kuropoka.
Wakiwa katika hali kama hiyo, Mwasumbi akajikuta anapoteza uwezo wa kufikiri na akawa hajielewe elewi, mara akaanza kuropoka vitu asivyovijua. Wakati hali hiyo ndiyo ambayo Sophia alikuwa akiisuburi, maana alijua katika hali hiyo angeweza kuyapata mawazo yaliyoko sirini mwa Mwasumbi maana midomo yake sasa ilikuwa ikiropoka yaliyoko moyoni. Kumbukumbu ya mwisho kabisa ambayo Mwasumbi aliweza kuidaka kwa mbali aliweza kusikia sauti kama ya inzi wengi sana, hakuelewa walitoka wapi. Hiyo ndiyo ilikuwa kumbukumbu ya mwisho, hakuweza kukumbuka kilichofuata. Sasa alijikuta yuko kwenye hiyo nyumba ya nyasi. Akiwa bado yuko pale kitandani, aliweza kuona kitu kama mlango kikifunguka, lakini ukubwa wa mwanya huo haukutosha kuitwa mlango wala dirisha lakini kwa vile ulikuwa ardhini na kuunganika na sehemu ya paa, Mwasumbi aliamua kuutambua kama mlango. Mara akaingia mtu, alijua ni mtu kwa vile aliona miguu miwili na mikono, lakini giza halikumruhusu kuweza kuiona sura ya mtu aliyekuwa ameingia. Mtu huyo alisogea hadi pale alipokuwa amelala. Aliingiza mkono chini ya uvungu, akatoa kiberiti, akawasha koroboi ambayo mwanga wake sasa ulifanikiwa kulifukuza giza lililokuwa limetanda. Sasa aliweza kuiona vema sura ya mtu aliyekuwa mbele yake, alikuwa Mzee aliyekuwa na nywele na ndevu nyingi nyeupe. Yule Mzee alipomsogelea Mwasumbi karibu zaidi huku vidole vyake vikavu vilivyokuwa vikitetemeka vikiwa vinatomasa majeraha ya Mwasumbi kwa mtindo wa kuyakagua, ndipo alipoweza kusikia harufu kali toka kwa huyo Mzee. Mzee huyo alikuwa akitema mate mara kwa mara. Aliendelea kutomasa majeraha ya Mwasumbi baada ya dakika kadhaa, alichukua mkoba fulani na kutoa mikebe midogo midogo. Mwasumbi aliendelea kujifanya hajui kinachoendelea ili kujipa nafasi ya kujua nini kilikuwa kikiendelea. Yule Mzee alifungua baadhi ya mikebe na kuanza kuchukua ungaunga toka kwenye hiyo mikebe na kuyapaka majeraha yaliyokuwa mwilini mwa Mwasumbi. Maumivu yaliyoletwa na zile dawa, yalimfanya Mwasumbi ajinyonge nyonge kwa uchungu.
“Oooooh umeshaamka!” Alisema yule Mzee kwa sauti ya kukoroma.
“Niko wapi hapa?” Mwasumbi aliuliza badala ya kujibu.
“Usiogope uko salama, maana yule mwanamke siku ile alikuwa anataka kukua kabisa!” Alisema yule Mzee.
“Mwanamke yupi?” Mwasumbi alijifanya kuuliza japo alijua yule Mzee alikuwa akimwongelea Sophia.
“Yule uliyekuwa unapambana naye. Alikuzidi nguvu kabisa, sema nikaingiwa na huruma nikaamua nikuokoe.” Alisema yule Mzee huku akiwa anafungasha dawa zake na kuzirudisha kwenye mkoba wake.
“Unajua sikumbuki chochote kilichotoke, naomba uniambie Mzee!” Mwasumbi alisema ili aweze kuunganisha matukio.
“Nilimwona jinsi alivyomuua Mzee Magesa, yule Mzee aliyekuwa akiendesha baiskeli. Nikaona jinsi ulivyopambana na wale wengine, kisha ulivyojaribu kupambana naye lakini akakuzidi nguvu. Sikupenda jinsi alivyokuwa akikutesa, nikaamua kukusaidia.” Alisema yule Mzee.
“Sasa ulinisaidiaje, maana siamini kama uliweza kukabiliana na yule muuaji?” Mwasumbi alihoji kwa mshangao.
“Ha ha ha ha!, nilituma askari wangu, askari wangu huwa hawashindwi kabisa.” Alisema yule Mzee huku akicheka na kukenua meno yake ambayo yalikuwa ya njano huku fizi zake zikiwa zimefunikwa na ukoko mzito wa njano.
“Una askari wewe Mzee?” Mwasumbi alihoji kwa mshangao zaidi.
“Ndiyo, hata hapa tulipo ndiyo wanaotulinda, maana baadaya kufanikiwa kumfukuza siku ile alipotaka kukua, yule mwanamke amerudi hapa Kijijini zaidi ya mara tano, ameshakagua kila mahali na kuua watu kadhaa lakini wiki ya pili hii sasa askari wangu hawajamruhusu kukaribia hili eneo hadi amekata tamaa maana sijamwona kwa hizi siku nne.” Alisema yule Mzee kwa kujitapa.
“Sikuelewi Mzee, ni kweli inaonekana umenisaidia maana nipo hapa na nimeona ukiwa unanipa dawa, ila suala la askari wako hapo sikuelewi, labda kama utafafanua kidogo.” Mwasumbi alikuwa mpole.
“Unajua shida yenu ninyi vijana mnadharau sana jadi yenu. Kwa namna nilivyoona mnapambana kwa ustadi mkubwa, kama mngechanganya ule uwezo wenu na uwezo wetu wa jadi hakuna ambalo lingeshindikana. Hebu tulia halafu sikiliza kwa makini uniambie unasikia nini?” Mzee alisema huku safari hii akiwa anamenya kipande cha Muhogo. Mwasumbi alijituliza na kujitahidi kusikiliza kama alivyoambia. Naam! Alisikia mlioa wa kitu kama nzi, na mara hiyo akakumbuka kuwa alisikia mlio kama huo mara ya mwisho kabla hajapotelewa na fahamu.
“Nasikia mlio kama wa nzi wengi, nakumbuka siku ile kabla sijapoteza fahamu nilisikia huo mlio pia. Sasa huo mlio una uhusiano gani na wewe kuniokoa miye au askari unaosema?” Hatimaye Mwasumbi alisema. Huku akisikia kichwa kikiwa kinagonga kwa mbali.
“Hao ni nyuki na ndiyo askari wangu. Hao ndiyo niliowatuma kumfukuza yule mwanamke siku ile. Kwa jinsi alivyokuwa anapigana hakuna mtu angeweza kumshinda, ila hakuna mtu anaweza kusimama na kupigana na askari wangu. Unajua kwa nini Nyerere alifanikiwa kwenye utawala wake na hata kwenye vita yake dhidi ya Idd Amini?” Alisema yule Mzee huku akijitapa.
“Sijui, ila nashangaa unaposema nyuki ndiyo askari wako, wewe uliwezaje kuwaamuru nyuki?” Mwasumbi alisema kwa mshangao.
“Ndiyo maana nimekuuliza…” Kauli ya yule Mzee ilikatizwa na sauti ya mlio wa bati tokea nje. “Ingia!” Yule Mzee alisema. Mara akaingia binti mmoja akiwa na ndoo kichwani. Aliingia kimyakimya, akaitua ile ndoo, halafu akapiga magoti, akainama mbele ya yule Mzee. Mzee hakujibu kitu aliendelea kutafuna muhogo wake huku mlio wa mmeng’enyo wa ule mhogo ukifika hadi kwenye masikio ya Mwasumbi. Yule binti alitoa vyungu vinne toka ndooni. Kisha akatoka nje ambapo alikuwa ameacha kikapu kingine, alikiingiza ndani. Toka ndani ya kile kikapu alitoa sufuria iliyokuwa imejaa vipande vya papai lililomenywa. Kisha akatoa kidumu cha maji. Aliinua kile kidumu cha maji akapiga magoti akiwa amejiweka tayari kumnawisha yule Mzee. Yule Mzee alipukuta mikono yake, kisha akanawa. Binti aliondoka.
“Inabidi ule vizuri, hapa kuna samaki aliyechemshwa, chungu kingine kina uji wa mtama, kingine kina supu ya mlenda iliyochangwanywa na majani ya maboga na maharage mabichi, hiki kingine kina ugali wa ulezi uliopikwa kwa maziwa. Kwa vile tunakula ulezi ni vema tukamaliza kwa haya mapapai ili kuweka tumbo sawa tusije hangaika tukienda chooni. Kumbuka hujala kwa uhakika kwa muda mrefu, nimekuwa nikitumia njia za kienyeji kukupa chakula, ila sasa unatakiwa ule ili upate nguvu.” Alisema yule Mzee huku akisogeza vile vitu jirani na kilipokuwa kichwa cha Mwasumbi. Akaanza kumlisha na kumnywesha.
“Nilikuwa nasema unajua nini kilimsaidia sana Nyerere kwenye uongozi wake na Vita ya Kagera? Nyerere alikuwa jirani na viongozi wa dini na wataalamu wa jadi kama sisi. Wewe unadhani kwa nini viongozi wengi walikuwa wakimwogopa Nyerere na kuwa waadilifu? Wengi waliogopa ile fimbo yake, ndiyo maana walimwita Mzee Kifimbo. Lakini pia kwenye ile vita ya Kagera, silaha kama hii niliyo nayo hapa vilitumika sana, ndiyo maana hadi leo Waganda huamini kuwa Watanzania ni wachawi sana, kumbe ni ufundi tu kama huu.” Alisema yule Mzee huku akiwa anajitafuna. Alikuwa akila na wakati huohuo kumlisha na kumnywesha Mwasumbi. Baada ya maelezo hayo ya yule Mzee, Mwasumbi alikuwa kimya tu akitafuna chakula. Ilikuwa wazi kuwa alikubaliana na wazo la yule Mzee kuhusu umuhimu wa yeye kula ili arejewe na nguvu zake za kawaida. Hivyo alijitahidi kufanya kila awezavyo kula ule mchanganyiko wa chakula aliokuwa ameletewa. Wakati huo huo alikuwa akiwaza mambo mengi yaliyokuwa yakipita kichwani kwake. Alimuwaza Maganga, alimuwaza Vivian, hakuwa na hakika kama alifanikiwa kufika mikononi mwa watu waliokuwa wakimsubiri. Lakini pia, alijisikia faraja alipokumbuka jinsi Sophia alivyokuwa amesema kuhusu Paul, ina maana KAPTEN alikuwa ameamua kumuua Paul baada ya kugundua kuwa ameshindwa kazi aliyokuwa amepewa.

* * *

Mwasumbi aliendelea kuwa hapo kwa siku kadhaa akiwa anapata matibabu. Sasa alikuwa na uwezo wa kutembea mwenyewe na kufanya mazoezi mepesi. Kibanda walichokuwepo, kama alivyosema Mzee kilikuwa kikilindwa na nyuki wengi sana waliokuwa wakiruka hapo muda wote. Mbali kidogo na hicho kibanda kulikuwa na vibanda kadhaa ambavyo walikuwa wakiishi wake wa Mzee na watoto. Aliyeleta chakula siku ile alikuwa ni mmoja kati ya wake zake. Umri wa yule msichana ulitosha kuwa mjukuu wake.
Cha kushangaza familia ya yule Mzee iliweza kuja na kufanya chochote katika eneo la kile kibanda bila nyuki kuwasumbua. Huo ndiyo ufundi ambao muda wote yule Mzee alikuwa akijisifia mbele ya Mwasumbi kuwa nao.
Siku moja wakiwa katika maongezi ya kawaida na mambo mbalimbali mara yule Mzee akauliza swali.
“Treni senta echi ndiyo nini?” Mzee alimgutua Mwasumbi toka katika mawazo yake.
“Unasemaje Mzee?” Mwasumbi alihoji maana hakuelewa.
“Dakika za mwisho kabla sijatuma nyuki wangu kumfukuza yule mwanamke ulikuwa ukipiga kelele huku ukisema hayo maneno. Sasa sielewi ulikuwa ukimaanisha nini. Pia, ulipokuwa ukizindukazinduka ulikuwa ukisema train…sijui treni…sijui trening senta echi...”
“Ooooh my God! Ndivyo nilivyosema! Tayari Maganga yuko hatarini. Lazima nielekee huko Training Centre H. Maana kama Sophia alinisikia nikisema hivyo na akamwambia KAPTENI mara moja watajua Maganga alipo.” Mwasumbi alisema huku akiwa ameshasimama. Alikuwa amehamaki sana.
“Maganga ndiyo nani na KAPTEN ndiyo nani?” Mzee alihoji. Mwasumbi hakuonekana kuwa tayari kuongelea yale mambo.
“Halafu kuna redio yako hapa ila miye imenishinda kuiwasha.” Mzee alisema huku akiinama chini ya kitanda. Alivuta kitu kama boksi, kisha akatoa kitu na kumkabidhi Mwasumbi. Mwasumbi alikipokea, ilikuwa ni Redio Call. Mwasumbi aliiwasha na kutafuta chaneli fulani.
“Ndiyo Afande!”
“Luteni Mwasumbi hapa.”
 
Riwaya: PATASHIKA - 20

Mtunzi: Japhet Nyang'oro Sudi

“Sema Afande, nilikuwa nimeanza kupata wasiwasi sasa.” Ulijibu upande wa pili.
“Nilipata dhoruba kiasi. Vipi vipusa viko salama?” Mwasumbi alihoji.
“Yap Comrade, viko salama, nimevihifadhi Section 14 M, hadi hapo nitakapopata maelekezo yako zaidi…” Mwasumbi hakutaka kusubiri kusikia zaidi. Ile kujua kuwa wale wasichana walikuwa salama ilikuwa ahueni. Alizungusha na kuhama ile chaneli. Akaipata chaneli nyingine.
“Mwasumbi hapa!” Mwasumbi alijitambulisha baada ya kuwa ameipata chaneli aliyoitaka.
“Mmbando hapa!”
“Afande inatakiwa kuimarisha ulinzi Training Centre H, kuna uwezekano mkubwa KAPTEN na timu yake wameshapajua na wanaweza kushambulia muda wowote toka sasa!” Mwasumbi alitaarifu.
“Uko wapi Luteni?”
“Niko sehemu moja inaitwa Kasomeko katikati ya Katunguru na Kamanga!” Mwasumbi alisema.
“Asante Luteni, nitafanyia kazi hiyo sasa hivi!” Jenerali Mmbando alisema kisha akazima ile Radio Call na kuacha upande wa Mwasumbi ukikoroma.

******

“Okay, kama mlivyosikia, watu wetu wako Section 14 M, Sophia sasa hivi chukua vijana wako nataka ukawachukue wale wasichana halafu uwapeleke nyumba salama, Kawekamo, hapo wataalamu wetu watawafanyia kazi. Mimi na Paul tutaelekea Training Centre H. Hii ni nafasi ya Paul kurekebisha makosa na kumpata Maganga. Nina imani bado watakuwa hawajamsafisha kichwa na hivyo anajua kuwa wewe ni baba yake mzazi. Na kama Mwasumbi alishapata fursa hiyo basi haina shida, yule Padre mwanafunzi hawezi kuwa na madhara yoyote. Kama mjuavyo Training centre H haina mawasiliano yoyote ya kwenda nje. Hivyo Jenerali Mmbando analazimika kutuma taarifa hii kwa njia ya mtu na labda kuongeza ulinzi zaidi au kumhamisha Maganga toka pale. Hakuna namna nitakubali makosa safari hii, tunachotakiwa ni kuwa mbele ya Jenerali Mmbando kivitendo, akifika akute tumeshamaliza kazi.” KAPTEN alisema mara baada ya kuwa amesikia ile sentesi ya mwisho ya Mwasumbi wakati akiongea na Jenerali Mmbando.

* * *

Wakati KAPTEN akitoa maagizo hayo kwa vijana wake, Jenerali Mmbando naye alikuwa akifanya vivyo hivyo kwa mtu wake wa siri aliyeko Mwanza.
“… Mambo mawili, tuma watu wakammalize Mwasumbi. Sihitaji uniulize sababu, hii ni amri na ni kwa usalama wa Taifa. Halafu Kesho asubuhi nataka unipe orodha ya vijana wako safi kumi na tano. Watu hao nataka waelekee Training Centre H, kwa ajili ya kuongeza ulinzi na mimi nitakuja kesho jioni nitaelekea huko kadhalika. Sikiliza, hakikisha unafanya hii kazi kwa siri ya hali ya juu na umakini mkubwa.” Mmbando alipomaliza maelezo hayo hakutaka kusubiri maswali. Alikata simu kisha akaminya namba nyingine. “Ndiyo afande!” Ulijibu upande wa pili.
Akabonyeza namba nyingine “Ndiyo Comrade!” Ulisema upande wa pili. “Sikiliza kwa makini, kesho jioni nataka uende Training Centre H, kuna kipuri nataka ukakichukue halafu ukipeleke sehemu salama. Kipuri kiko white room, neno la siri ni Maganga.” Kadhalika kama hapo awali, alipomaliza maelezo yake alikata simu. Kisha akashusha pumzi ndefu na kuwasha sigara yake.
“Kazi imeanza!” Mmbando alijisemea huku akipuliza moshi wa sigara hewani.
* * *
Siku moja majira ya jioni wakati Vivian, Milka na Hellen wakiwa sebuleni, walisikia sauti za vishindo vikitokea nje, mara wakasikia mlio wa risasi. Wote wakakimbia kila mmoja kwenda kujificha alipojua. Milka hakujificha mbali sana na ilipokuwa sebule, hivyo aliweza kuona yule mwanajeshi wa kike akiingia pale sebuleni kwa stahili ya sarakasi huku akikwepa risasi kadhaa zilizokuwa zikimwandama. Risasi moja iliyomkosa yule mwanajeshi wa kike ilitua jirani na mguu wa Milka na kumfanya atoe ukelele wa hofu. Alipopiga kelele risasi zilikoma, halafu ghafla akaona Ua Jekundu, likianguka sakafuni jirani na alipokuwa amesimama. Kisha akamwona msichana mmoja akitokezea akiwa amevalia sare za jeshi. Yule msichana aliyetupa Ua aliendelea kutembea taratibu kwa kujiamini kuelekea sehemu ambayo kulikuwa na korido iliyokuwa ikielekea viliko vyumba vya nyumba hiyo. Alipofika kwenye kona ili aingie kwenye ule uwazi uliokuwa unaelekea vilipo vyumba, alipigwa teke la shingoni. Akageuka kwa kasi huku akijipangusa pale alipokuwa amepigwa.
Alijikuta anatazamana na yule mwanajeshi wa kike. Huyu msichana mwingine alikuwa ni Sophia ama Au Jekundu kama alivyozoeleka. Sophia alimtazama yule mwanajeshi wa kike halafu akaanza kuachia mapigo mazito ya kung-fu ambayo yule mwanajeshi wa kile yalimshinda kabisa. Ikawa wazi kichwani kwa Sophia kuwa alikuwa anapambana na mtu ambaye hakuwa kwenye ngazi yake. Hivyo hakutaka kupoteza muda, alifyatua teke la kupeleka na kurudisha yule mwanajeshi wa kike alitoa mlio wa maumivu na kuanguka chini kama gunia ambalo halijajazwa vema maharage.
“Njooni hapa kabla sijaanza kuwauwa mmoja mmoja!” Sophia alitoa amri. Kwanza kilipita kimya kabla ya Hellen kujitokeza, alikuwa akitetemeka kwa woga. Milka alifuata, Vivian alikuwa wa mwisho.
“Nifuateni, mkileta tabia za kike mtamfuata huyo mnayemwona hapo chini!” Sophia alisema huku akipiga hatua kutoka ndani. Alitembea hivyo hadi walipofika nje ambako walikuta gari limepaki. Waliingizwa ndani na gari likaondolewa. Sophia alikuwa ameandamana na wanaume wengine wawili, Milka na Hellen waliweza kuwatambua wale wanaume kuwa ndiyo wale waliokuwa wakiteketeza Kijiji chao siku ile ya mwisho walipokuwa Kijijini kabla ya wao kupoteza fahamu kutokana na moto ule mkubwa.
Mara hii walijua wazi kuwa walikuwa kwenye mikono hatari zaidi, walitazamana wakabetuliana midomo, hawakuwa na muda wa kuongea.
“TAFUTA.” Sophia alisema huku akiwa ameweka radio ya upepo. Alikuwa amekaa kwenye kiti cha abiria, mwanaume mmoja alikuwa akiendesha gari na mmoja alikuwa nyuma ya viti walivyokuwa wamekaa Hellen, Vivian na Milka. Lilikuwa gari aina ya Noah.
"Niko na warembo wako hapa, ndiyo tunaelekea safe house." Sophia alisema.
“Kazi nzuri.” KAPTEN alisema na kuizima ile redio.
Baada ya kuizima ile Redio Call, alitoa simu yake ya kiganjani, akaminya namba kadhaa kisha akasubiri kuongea.
“Kuna bidhaa zetu muhimu sana katika hii operesheni, kuna hisia kuwa zinaweza kuwa na ufunguo wa kutufikisha sehemu ambayo tunaitaka. Hivyo kwa siku hizi tatu wataanza kulishwa dawa ili kama wana alama zozote mwilini ziweze kujitokeza. Hivyo tuonane pale safe house baada ya siku tatu toka leo ili kuchunguza miili yao…” Hiyo ilikuwa sehemu ya maelezo ya KAPTEN alipoongea na mtu aliyekuwa upande wa pili wa simu. Alimwangalia Mzee Paul aliyekuwa amekaa kiti cha pembeni na pale alipokuwa. Walikuwa kwenye gari wakielekea Section Centre H. Walikuwa wakifukuzana na muda ili kuwahi kumchukua Maganga kabla timu ya Jenerali Mmbando haijaenda kumchukua kama alivyokuwa ameshauri Luteni Mwasumbi akiwa kule kwenye ile nyumba ya Mzee mfuga nyuki. Kama alivyokuwa amemwambia, KAPTEN alikuwa akimpa Mzee Paul nafasi ya mwisho ili kufanikiwa kukamilisha kazi yake ya kumkabidhi Maganga, kazi ambayo alikuwa ameshindwa dakika za mwisho kule Kijijini ambapo alizidiwa ujanja na Luteni Mwasumbi. Gari hili lilikuwa la kijeshi na wao walikuwa wamevalia kijeshi.
Eneo hilo lilikuwa porini sana, ukifika sehemu kilipo Chuo cha Ualimu Butimba, unaingia kwa ndani zaidi, ni sehemu ambayo ilisemwa kuwa ni hifadhi maalum ya miti adimu kwa ajili ya utafiti wa madawa yaani Medical Research. Kulikuwa na walinzi wa siri, ambao waliweza kuona hiyo gari likiwa linaingia kwenye hilo pori, lakini kwa vile lilikuwa la kijeshi hawakulitilia shaka sana. Gari lilizidi kukata msitu kuelekea sehemu ambapo kulikuwa na jengo kubwa la kijani. Walipokuwa umbali fulani walisimamisha gari.
Wakati gari hilo likiwasili, Maganga alikuwa ametoka kuoga, alijikagua mwili wake kama alivyokuwa akifanya siku zote. Alivaa nguo nyepesi kisha akaenda kujilaza kitandani. Ilikuwa ni saa tano na nusu asubuhi. Maganga tayari alikuwa ni mtu aliyejikinai, mwili wake ulikuwa umeshakufa ganzi na nafsi yake kuota kutu. Ile hali ya kujali na kuzingatia mambo aliyokuwa amejijengea kwa muda mrefu kutokana na mafunzo ya Upadri ilikuwa imeshamtoka, alikuwa ameshakaa katika jengo hilo kwa siku zaidi ya arobaini. Ilikuwa ni sehemu ambayo ilikuwa imeshamkinai kuwepo kama ambavyo Milka, Vivian na Hellen walivyokuwa wamekinai kukaa kwenye ile nyumba waliyokuwa wamepelekwa na yule mwanajeshi wa kike.
Akiwa amejipumzisha kitandani mara akasikia vishindo vya watu vikija upande ule wa chumba. Kutokana na ratiba yake, ulikuwa ni muda wa yeye kupumzika hadi hapo saa nane na nusu muda ambao wangekuja madaktari maalumu kwa ajili ya kuuchunguza na kuupekua pekua mwili wake. Hivyo kusikia vishindo vya watu ilimshangaza sana, katika jumba hilo wahusika walioneka kujua na kujali muda. Akiwa bado anawaza mara mlango ukafunguliwa.
 
PATASHIKA - 21

Maganga tayari alikuwa ni mtu aliyejikinai, mwili wake ulikuwa umeshakufa ganzi na nafsi yake kuota kutu. Ile hali ya kujali na kuzingatia mambo aliyokuwa amejijengea kwa muda mrefu kutokana na mafunzo ya upadri ilikuwa imeshamtoka, alikuwa ameshakaa katika jengo hilo kwa siku zaidi ya arobaini. Ilikuwa ni sehemu ambayo ilikuwa imeshamkinai kuwepo kama ambavyo Milka, Vivian na Hellen walivyokuwa wamekinai kukaa kwenye ile nyumba waliyokuwa wamepelekwa na yule mwanajeshi wa kike.
Akiwa amejipumzisha kitandani mara akasikia vishindo vya watu vikija upande ule wa chumba. Kutokana na ratiba yake, ulikuwa ni muda wa yeye kupumzika hadi hapo saa nane na nusu muda ambao wangekuja madaktari maalumu kwa ajili ya kuuchunguza na kuupekua pekua mwili wake.
Hivyo kusikia vishindo vya watu ilimshangaza sana, katika jumba hilo wahusika walioneka kujua na kujali muda. Akiwa bado anawaza mara mlango ukafunguliwa.
Wa kwanza kuingia alikuwa ni KAPTENI, ambaye alibaki kwenye mwimo wa mlango, alimtazama Maganga kwa muda bila kusema wala kufanya lolote. Macho yao yalipokutana, aliyaangalia macho ya Maganga kwa jinsi yalivyokuwa mekundu na kuonekana kuchoka, huku kukiwa na kitu fulani katika macho hayo ambacho mtu ambaye ni Padri mtarajiwa asingeweza kuwa nayo.
Uso wa KAPTENI ulikuwa kama una mshangao fulani, lakini hakuuliza, alipiga hatua tatu mbele, ndipo Mzee Paul naye akajichomoza. Alipomwona Maganga, Paul alitabasamu kisha akapiga hatua kukimbilia pale alipokuwa Maganga, kuona hivyo Maganga alijiinua pale kitandani.
Mzee Paul alipofika pale kitandani alimkumbatia Maganga kwa nguvu, lakini haikuchukua muda mrefu alimwachia. Alitambua mabaidiliko, hakuwa amekumbatia ule mwili wa Maganga anayemfahamu, huu ulikuwa mwili wa jitu na si Padri mtarajiwa.
“Maganga, pole sana kwa yote yaliyokupata.” Mzee Paul alisema.
“Yapi hayo!?’ Maganga alihoji kama asiyewajua watu wote waliokuwa mbele yake na wala hakujua nini kilikuwa kimetokea.
“Wewe hujui, jinsi ulivyochukuliwa Kijijini na kuwekwa kwenye hii nyumba?” Mzee Paul alisema.
"Hatuna muda zaidi, watafika muda si mrefu kutoka sasa, mchukue mwanao tuondoke. Imekuwa jambo jema tumemkuta akiwa hai." Sauti ya KAPTENI iliunguruma. Maganga aligeuka akamwangalia KAPTENI.
“Huyu ni nani?” Maganga alimuuliza Paul.
“Ni mtu aliyejitolea kunisaidia kukutafuta wewe baada ya kupotea.” Paul alijibu.
“Hana jina?” Maganga aliuliza tena kwa sauti kavu, sauti ambayo ilimshangaza Paul na kumkera kwa wakati mmoja. Alihisi ile sauti ilikuwa na dosari fulani lakini hakuwa na muda wa kuchunguza zaidi.
“Hayo majibu yenu mtajibishana tukishatoka hapa, kwa sasa hebu tuondokeni haraka.” KAPTENI alisema tena, wakati huu sauti yake ikiwa na amri ndani yake. Sauti hii Maganga aliifananisha na wale watu ambao huja usiku na kumfanyisha mafunzo magumu na ya kikatili.

Akajikuta ameanza kumchukia huyo mtu na mara hiyo maneno aliyosoma kwenye ile karatasi aliyoandikiwa na mama yake aliyoichukua chini ya mtungi yakamjia kichwani kwa kasi "Paul na Mwasumbi wako kwenye misheni moja japo hawajui....sijui yupi aliye upande wako.”
Maneno hayo yalimfanya awe na hadhari na Paul. Alisimama, akavaa mavazi yake ya mazoezi ambayo yalikuwa mazito kisha akaongozana nao kuanza kutoka mule ndani.
Maganga alishangaa kukuta maiti za wanajeshi waliokuwa na silaha zikiwa zimetapakaa maeneo waliyokuwa wakipita. Walipofika nje walikimbia kuelekea pale walipokuwa wameegesha gari lao. Hata kabla hawajafika lilipokuwa gari lao, mara wakasikia mlio kama wa Inzi.
“Nyuki, tukimbie kurudi ndani hadi wapite, ni hatari sana hawa,” KAPTENI alisema, ilibidi wakimbie kurudi ndani japo walikuwa wamebakiza hatua chache kulifikia gari lao.
Kwa vile gari lao lilikuwa la wazi hawakuona kuwa ni busara kuliondoa huku wakiwa wanafukuzwa na nyuki, hivyo ingemaanisha kujitakia vita ambayo hawakuwa wanajua kuipigana.
Walikimbia kwa kasi, wakati wanakimbia, nyuki wakiwa wanawakimbiza walishangaa jinsi Maganga alivyokimbia kwa staili ya ajabu sana na kuwaacha wao wakiwa wanafukuzana na wale nyuki. KAPTENI na Paul walikuwa ni wanajeshi safi sana, ambao wamekuwa kwenye misheni na kazi kwa muda sasa lakini namna Maganga alivyokuwa mwepesi na kukimbia iliwaacha vinywa wazi.
Walifanikiwa kuingia ndani na kufunga mlango, waliendelea kusikia sauti ya wale nyuki kwa dakika kadhaa. Baadaye kukawa kimya. Walitoka tena kuelekea lilipokuwa gari lao.
Hapo walishikwa na mshangao mwingine, walikuwa wamewaacha vijana wawili kwenye lile gari, lakini walikuta maiti zao zikiwa na mishale iliyowauwa.
"Daaah! hawa wameshambuliwa saa ngapi tena!” Alihoji huku akipanda kwenye gari. Aliliwasha, Maganga na Paul waliingia viti vya nyuma kisha KAPTENI akaliondoa gari kwa kasi.
Moja kwa moja safe house Kawekamo. KAPTENI aliwaza huku akiingiza gia kwa fujo.

Safe House - Kawekamo

ILIKUWA siku ya pili, usiku wa saa moja na nusu, Vivian, Lilian na Hellen walikuwa wamejilaza kando ya bwawa la kuogelea ndani ya safe house ambayo inamilikiwa na KAPTENI ikiwa maeneo ya mlima wa Kawekamo nje kidogo ya jiji la Mwanza. Hawakuwa na la kuongea, hawakuwa na la kuulizana, walishaongea yote, walishaulizana na kujibizana yote walipokuwa kwenye ile nyumba waliyokuwa wamewekwa na yule mwanajeshi wa kike.
Kwa sasa hawakuwa wanajua majaaliwa yao, tangu wameingia kwenye hii nyumba walikuwa wakichomwa sindano asubuhi na jioni. Miili yao ilikuwa imeanza kubadili rangi na kuwa ya ajabu ajabu tu.
Ulinzi ulikuwa mkali sana, walinzi walikuwa wakibadilishwa kila baada ya saa sita. Wakiwa kando ya hilo bwawa mara Hellen alishtuka kama aliyeona kitu, alijiinua akamwangalia kwa makini mlinzi mmoja aliyekuwa akitembea kuja upande huu waliokuwepo. Ndiyo alimkumbuka.
“Haaaah!, namjua yule mwanaume!” Hellen alimwambia Vivian aliyekuwa amejilaza kando yake.
“Yupi?” Vivian aligutuka.
“Yule pale!” Alisema huku akitaka kuinua mkono ili kuonyesha.
“Wewe hujajifunza tu, hapa hutakiwi kupayukapayuka wala kunyooshea watu mikono, utakuja kukatwa hiyo shingo, shauri zako. Kwani huwezi kusema bila kuonyesha kidole?” Vivian alisema huku akiusukumia chini mkono wa Hellen.
“Usimwangalie wala usijifanye unamjua, nisimulie kwanza,” Vivian alionya.
“Nakumbuka huyu mwanaume nililala naye usiku mmoja kabla sijaja Mwanza. Yeye ndiye niliongea naye kwa mara ya mwisho juu ya hamu yangu na kiu yangu ya kutaka kumjua baba yangu.
“Jamani kumbe na yeye yuko kwenye huu mtandao? Ukweli ni kwamba huyu mwanaume hakuwa tu mteja wangu wa kawaida, tulikuwa tunapendana sana alikuwa ananiridhisha sana kitandani," Hellen alisema huku akijishika shika.
“Kweli?” Vivian alisaili.
“Haswa! Hata siamini kwa kweli kama Machumu anaweza kuwa kwenye kundi hili la hatari,” Hellen alisema.
“Kwa nini usiamini, kwani alikuambia anafanya kazi gani?” Vivian alihoji zaidi wakati huo yule mlinzi alikuwa ameshapita na walikuwa wakimtazama mgongo wake tu. Alikuwa amebeba silaha nzito.
“Mimi nilikuwa najua kuwa yeye ni askari polisi. Sasa ndiyo napata mwanga, maisha anayoishi Machumu, vitu anavyofanya si vya mtu anayelipwa mshahara wa askari, anaishi maisha ya kifahari sana, khaa!” Hellen alisema kwa mshangao.
“Ngoja, si anazunguka kwa hivi, akipita hapa tena mwite kwa sauti ya chini halafu tuone kitakachojiri,” Vivian alishauri.
“Akhaa! mimi nimeshamwogopa siwezi bwana asijenipiga risasi bure!” Hellen alisema kike-kike.
“Hawezi, hawajawekwa hapa kutuua wamewekwa hapa kutulinda, muite tu tuone! Kama tumepangiwa kufa tutakufa tu, kama tumepangiwa kupona tutapona tu,” Vivian alisema kwa sauti ya kusisitiza.
“Haya nyamaza huyo hapo amekaribia.” Hellen alinong'ona.
“Machumu…” Hellen aliita.
Yule mlinzi akageuka akamwangalia Hellen huku bado akiwa anatembea. Hakusema neno japo uso wake ulionyesha mshtuko na mshangao fulani, lakini hata hivyo aliendelea kutembea. Vivian na Hellen wakabaki wametazamana.
“Amekutambua unaona alivyoshangaa!” Vivian alisema.
“Mmh! inawezekana, au kashindwa kuelewa yupi ni yupi, si unajua jinsi mimi na wewe tunavyofanana,” Hellen alisema.
“Kwa kweli lazima kuna kitu, maana mnavyofanana, hata mimi siku ile nimekuona kwa mara ya kwanza pale kijijini tukiwa na Maganga nilidhani u Vivian, mnafanana sana. Kwa kweli kuna haja sana ya kuutafuta ukweli toka katika maelezo ya Mwasumbi,” alisema Milka ambaye alikuwa kimya muda wote akiwasikiliza Hellen na Vivian.
Yule mlinzi aliendelea kutembea bila kugeuka, wale wasichana waliendelea kumwangalia huku wakijifanya kuwa hawana habari naye. Kulikuwa na walinzi wengine sita, wote wakiwa na silaha.
Hatimaye mzunguko wa yule mlinzi ukawa unamleta tena sehemu waliyokuwa wamejilaza wale wasichana pembeni ya bwawa. Akiwa anatembea kwa mwendo uleule wasichana wote watatu walikuwa wakimwangalia.
Taratibu alinyanyua mkono hadi kinywani kwake kwa kutumia kidole cha shahada akawaonyesha ishara kuwa wanyamaze kimya. Ishara hiyo aliifanya kwa kuweka kidole juu ya kuta za mlango wa mdomo. Kama ilivyokuwa mwanzo hakusimama akaendelea na mwendo wake uleule.
“Unaona, amekutambua, ametuambia tunyamaze,” Milka alisema kwa kunong'ona.
“Tufanye kama alivyotaka,” Vivian alisema.
Hellen hakuwa na la kusema alikuwa kimya akiwa ameshikwa na butwaa. Hiyo mada ikaishia hapo wakaendelea na mambo mengine.
Giza lilipoanza kuingia, kila mmoja alienda kuchukua nguo zake wakavaa. Wakatoka eneo hilo la bwawa la kuogelea wakaingia ndani. Usiku huo kuna jambo likawa limetokea, Vivian alikuwa ameenda chooni, katika shughuli za chooni ndipo kwa bahati mbaya au nzuri aliingiza mkono mfukoni, huko vidole vyake vikagusa kitu.
Karatasi!
Aliivuta na kuifunua, ilikuwa ndogo tu na yenye maandishi machache. “Nimekutambua, hakikisha hulali, saa nane usiku.”
Mapigo ya moyo ya Vivian yakabadilika, vidole vikaanza kutetemeka. Aliona hii ndiyo ilikuwa nafasi pekee. Alielewa kuwa ujumbe ule kwa vyovyote ulikuwa umeandikwa na yule mlinzi-Machumu na mlengwa alikuwa ni Hellen. Alishindwa kuelewa kama amshukuru Mungu au la. Hakutaka kujua hiyo karatasi iliwekwaje na muda gani, hilo halikuwa na maana kwa wakati huo. Alikifinyanga kile kikaratasi na kukitupia mdomoni.
Akakitafuna taratibu, aliondoka chooni, hakutambua kuwa hakuwa amejisaidia haja ndogo wala kubwa. Maana baada ya kukipata kile kikaratasi na kukisoma, alivuta suruali na kuivaa. Haja zikawa zimetoweka.
Asubuhi ya siku iliyofuata ilikuwa ya patashika kubwa kwenye hiyo nyumba. Walipoamka Milka na Hellen hawakumwona Vivian, kwanza walianza kutafuta kimyakimya hawakumwona. Hawakujua wamwulize nani hadi pale walipoulizwa. Waliamriwa kuingia kwenye chumba fulani ambako walikutana na KAPTENI na Sophia wakiwa wanawangoja, Milka na Hellen hawakuchelewa kujua kuwa watu waliowaita walikuwa ni wenye hasira nyingi.
"Nataka mniambie yule mwenzenu amekwenda wapi. Kushindwa kufanya hivyo mtauawa kifo cha mateso sana!" KAPTENI alisema kwa sauti isiyokuwa na chembe ya utani.
“Nadhani sisi ndiyo tuwaulize mmempeleka wapi mwenzet....” Kabla hajamaliza kusema Milka alipokea kofi kali sana tokea nyuma yake. Alienda chini huku akitoa kilio kikali cha maumivu na hofu.
“Shenzi, huko kwenye mafunzo ya usista ndiyo mlifundishwa kuwajibu watu hivyo?” Sauti ilisema toka nyuma yake.
Milka aliitambua ile sauti, akageuka. Uso wake ukawa unatazamana ana kwa ana na Mzee Paul.
“Baba una....” Kabla hata hajamaliza kauli yake, mlio mkubwa wa bunduki ulisikika wote wakatazamana.
“Mr M, hebu kaangalie kuna nini?” KAPTENI aliamuru.
“Sawa Afande!” Mzee Paul alijibu.
Milka na Hellen wakatazamana huku Milka akiwa bado anatomasa shavu lake kwa sababu ya lile kofi. Mara milio zaidi ya risasi ilisikika. KAPTENI na Sophia walikimbilia nje toka kwenye kile chumba walichokuwa.
“Mwasumbi yuko hapa, Maganga haonekani.” Sauti ya Mzee Paul ilisikika ikipiga kelele.
“Sophia, Mwasumbi asitoke hapa hai. Mr M, hakikisha Maganga hapotei.” KAPTENI alitoa amri. Kisha milio ya risasi ikaendelea kurindima, vilio vilisikika, sauti za kutisha na kutukana kwa hasira vilisikika pia.
 
Wakuu samahan hii riwaya mimi sio mwandishi wala mtunzi nilikua nakopi tu baada ya kuipenda na mwandishi ameishia sehemu ya 21 hatoendelea kitabu kinauzwa 10,000/= na namba yake iko juu hapo....mimi nimeisoma yote maana nimenunua kitabu chake na moto sana.


Shuka na riwaya hii yake nyingine faya nipo na sehemu hadi ya 24 inaitwa saa 72 za kufa na kupona.
 
SAA 72: 01

Februari 25, 2003

Bogoro – Buni, DRC

Msichana wa miaka 15 hivi, akiwa na majeraha mazito mwilini alizidi kujilazimisha kupiga hatua kwenye mtaa uliojaa maiti. Majeraha yake yaliyokuwa bado mapya yalifanya ausikie mwili wake kuwa kama ganda la kidonda kilichooza ambacho kilikuwa kikingoja mkasi kutumbuliwa ili kirushe usaha mzito. Kwa hali ilivyokuwa hakuwa na wakati wala namna ya kuyapooza majeraha yake hayo.
Kila kitu kilikuwa kimeharibika, nafsi yake ilikuwa imechafuka, akili yake ilikuwa imevurugwa vibaya, uwezo wake wa kufanya maamuzi ulishakufa ganzi.
Hali yake ya utu ilikuwa imeng’olewa kwa vile alivyokuwa amelazimika kuua bila kujali ili kupigania maisha yake, maana maisha huwa na thamani kubwa sana mtu anapokuwa kwenye mdomo wa mauti, ndio maana hata mgonjwa aliyedhoofu sana utashangaa anapata wapi nguvu anazotumia kupigania pumzi ya mwisho. Ni wakati mtu anapotakiwa kutoa pumzi ya mwisho ndipo huwa tayari kufanya chochote ili pumzi hiyo isimtoke!
Hakuwa akijali kitu sasa, bunduki aina ya SMG ikiwa inaning’inia begani kwake alishitushwa na mlio mkali wa ndege aina ya Tai aliyekuwa akiruka kwenye anga la eneo alilokuwepo.

Ndege huyu aina ya Tai alikuwa amefungua mabawa yake na kuyaachia yamiliki anga lililo juu ya kijiji kidogo kilichoko kwenye vilima vya Ituri, kijiji hicho kinaitwa Bogoro. Kiko kilomita kama 25 hivi toka mji wa Buni, Congo DRC. Tokea angani, macho yake makali yalikuwa yakiangalia juu ya barabara za mitaa ya mji huo, maiti kadhaa zilionekana zikiwa zimetapakaa mitaani. Ndege huyo fundi na mbabe wa anga, alitikisa mkia wake kwa furaha huku akitoa ukelele wa kusheherekea hali aliyoiona mitaani. Maiti zilizotapakaa, hali ya baridi na unyevunyevu kufuatia mvua iliyokuwa imekatika punde, ilileta upweke kwenye mitaa hiyo ya Bogoro.

Kwa kawaida mji wa Ituri hufunikwa na mvua kubwa tangu mwezi wa pili hadi mwezi Juni. Mji huu ambao una lile pori kubwa na maarufu lenye mvua nyingi sana lijulikanalo kama msitu wa Ituri huwa wa kijani kibichi muda wote wa mwaka. Ndege walikuwa wenye furaha, mijibwa ya mitaani ilikuwa imetulizana huku ikiwa imeshiba. Mlio wa maji yaliyokuwa yakitiririka baada ya mvua kubwa ulisikika. Hali ilikuwa kimya kabisa huku magari kadhaa-machache sana ya jeshi yalionekana kuzunguka kila baada ya dakika kadhaa. Magari hayo yalikuwa yameandikwa FRPI kifupi cha Patriotic Resistance Force in Ituri. Kwa ujumla hali ilikuwa ukiwa sana. Katikati ya hali hiyo Tai huyo aligeuza kichwa chake kumtazama binti mdogo aliyekuwa akikatiza kwenye mitaa pweke ya eneo hilo. Mitaa iliyokuwa imejaa maiti nyingi, zilizokuwa ama na majeraha mabaya ya risasi au visu. Hii ilikuwa ni masaa machache tangu yalipohitimishwa yale mauaji ya kikabila ya Bogoro ambayo wenzetu waliyabatiza jina ‘Bogoro massacre’. Msichana huyu, alitembea taratibu huku akitetemeka kutokana na jinsi hali ilivyokuwa. Alitembea hivyo huku akijificha ficha. Tai yule alijikuta akimshangaa binti huyo, hivyo akawa akiruka anga hilo na kutoa milio ya kipekee huku macho yake makali yakimdhihaki.
Binti mwenyewe alimuangalia yule Tai kwa jicho baya, alitamani angekuwa na uwezo wa kumnyamazisha lakini alijua hilo lilikuwa nje ya uwezo wake, alizidi kwenda kwa kujificha ficha huku akijitahidi kujificha kwenye macho ya yule Tai, kutokana na uzoefu wake binti huyo, Tai huyo alikuwa wa hatari kama ambavyo magari ya wanajeshi yaliyokuwa yakipita yalivyokuwa ya hatari. Akiwa na umri wa miaka 15, tayari alikuwa amefunzwa vema kama mwanajeshi kamili, alikuwa na uwezo huo japo hakuwa na muonekano huo, akiwa anatokea kwenye kabila la Lendu, kabila ambalo hujishughulisha na kilimo kwenye eneo hilo la Ituri, kufunzwa vita ilikuwa sehemu ya lazima kwenye jamii, hii iliwawezesha kuwa tayari kwa vita ya kikabila kati ya kabila lake yaani Lendu na ile ya Hema. Makabila yote haya mawili yalikuwa yakipatikana kwenye jimbo hilo la Ituri, huku Lendu wakijihusisha zaidi na kilimo na kabila la Hema wao wakifanya zaidi ufugaji. Ufugaji na ukulima ndio ilikuwa chanzo kikubwa cha kupigana kwao, hawa wakitaka sehemu za malisho na hawa wakitaka sehemu za kulima.
Yeye akiwa kati ya watoto waliokuwa wamekamatwa kwa nguvu na kufundishwa mapigano na kundi la kijeshi la FRPI lililokuwa likiongozwa na Joseph Katanga. Ilikuwa dhahiri kichwani mwake kuwa mlio wa yule Tai, ungetuma ujumbe tosha kwa mwanajeshi yeyote kuwa eneo lile kulikuwa na mtu aliyeonekana wa ajabu ajabu, ndio maana hakupenda kuona yule Tai akiendelea kuzunguka eneo lile na kutoa aina ya mlio aliokuwa akitoa. Baridi kali, ubichi-ubichi, maiti za watu, upweke, majeraha aliyokuwa nayo na njaa vilifanya aonekane kiumbe wa ajabu katikati ya uwanja wa mauti.
Huku akiwa anachechemea, mara hii akaingiza mkono wake tena kuelekea sehemu za siri. Alipoutoa bado aliweza kuona damu mbichi kabisa ikiwepo, alisimama, akavua chupi aliyokuwa amevaa, aliiangalia ile chupi jinsi ilivyokuwa imechanwa kwa fujo na mtu aliyekuwa katika zoezi la kumbaka. Hapo machozi yakaanza kumtoka kwa mara nyingine tena, aliitupa chini ile chupi na kuendelea kutembea taratibu huku akichechemea kufuatia majeraha mwilini, baridi lakini pia kitendo cha kubakwa na mtu aliyekuwa amemuamini sana. Joseph Katanga. Hakutegemea kuwa siku mmoja kiongozi wao wa kundi la kijeshi, mtu aliyekuwa akihubiri kuwa alikuwa anapigania na kutafuta haki ya kabila la Lendu na jamii ya wakulima kwa ujumla angembaka kinyama namna ile. Khajat, huku silaha yake aina ya SMG ikiwa begani, silaha ambayo ilionekana kumzidi umri, alikuwa akikatisha upande mmoja wa barabara kwenda mwingine wakati aliposikia muungurumo wa gari ukija. Wakati huo huo yule Tai alizidi kupiga kelele, alikimbia na kwenda kujibanza nyuma ya kibanda fulani cha mbao. Ni wakati akiwa na hakika kuwa amejificha vema ndipo aliposikia sauti upande mwingine ikisema ‘Khajat, not safe, run this way! (Khajat, siyo salama, kimbilia huku!). Ilikuwa ni sauti ya mtu aliyemjua, lakini haikuwa sauti ya mtu aliyetegemea kukutana naye.

*********
Riwaya hii imeandikwa na Japhet Nyang’oro Sudi ambaye anapatikana kwa namba 0762204166.

************

Aliangalia kule ilikotokea ile sauti, akamuona mtu aliyemuita, alimuangalia jinsi alivyokuwa taabani, akajikuta anashawishika kwenda kumsaidia, wakati anakwenda akasahau kuwa alikuwa amesikia mlio wa gari hapo kabla, kutokana na ukaribu wa yule mtu aliyemuita na jinsi alivyokuwa amejeruhiwa akakimbia tena kuvuka barabara. Wakati huo huo akasikia mvumo wa gari ukiwa jirani kabisa na alipokuwa, lakini kabla gari ile haijamfikia, ulitokea mlipuko mkubwa toka kwenye kile kibanda alichokuwa amejibanza. Mlipuko uliomrusha hewani, akiwa hewani, msichana yule alitoa ukelele mkubwa wa hofu na maumivu “Jooooaaan!!”

“Noooo, Khajat!!” Huyu aliyejulikana kama Joan alipiga kelele baada ya kuona Khajat ametua chini kama mzigo baada ya kuwa amerushwa juu. Wakati anataka kukimbilia pale alipokuwa ameangukia Khajat, Joan alishikwa na mshangao alipomuona mzee mmoja wa makamu akienda pale alipoangukia Khajat na kumchukua. Ilikuwa ni kitendo cha kasi na wepesi sana. Ilikuwa kama vile Mwewe amchukuavyo kifaranga. Yule mzee alitowekea kwenye majengo yaliyokuwa jirani. Kuona hivyo Joan akakimbilia sehemu ambayo mzee yule alikuwa ameingia na Khajat. Vilikuwa ni vitendo vya haraka, hivyo wakati Joan naye akiwa anapotelea kwenye lile jengo ndipo gari la jeshi la FRPI lilipopiga breki kwa fujo eneo hilo. Wanajeshi kadhaa walishuka na kuanza kukimbilia alipokuwa ameelekea Joan.
“Shiiiiiiii!” Yule mzee alisema mara baada ya Joan kutokezea kwenye chumba ambacho alikuwa amemlaza Khajat na kuanza kumpa huduma ya kwanza.
“Mzee Kasheba!” Joan alisema.
“Kaa hapo Joan, huyu anahitaji huduma ya haraka kama kweli tunataka aendelee kuishi!” Alisema mzee Kasheba.
“Wako wanakuja huko nje!” Joan alisema. Punde kidogo wakasikia mlango wa jengo hilo ukigongwa kwa nguvu.
“Oooooh shiiit!” Mzee Kasheba alisema kwa mshituko.

* * *

“Wote wako hapa isipokuwa watu wawili tu ndio wanakosekana!” Alisema askari huyu mwenye cheo cha juu jeshini huku jicho lake moja la kushoto likiwa na bandeji nyeupe iliyochafuka damu.
“Umeshajua ni nani wanaokosekana? unajua inatakiwa tukamilishe kazi hii ndani ya masaa machache yajayo!!” Alisema Joseph Katanga, ambaye alikuwa amechafuka sana, mavazi yake ya kijeshi yakiwa na matone na michirizi mingi ya damu.
“Kwa orodha iliyokuwa imetolewa mwezi wa nne siku chache kabla operesheni hii haijaanza wanaokosekana hapa ni Khajat na Joan!” Alisema huyu mwanajeshi mwenye jicho lenye bandeji.
“Watafutwe, hii ni sumu ambayo hapo baadaye itatuathiri, halafu nataka kujua kwa nini wao hawakuwa na watu wa kuwachukua wakati mambo yalipoanza?” Alisema Joseph Katanga. Wakati wakiongea hayo mara akaingia mtu mwingine aliyekuwa amevaa kiraia, wote wakampigia saluti. Hakujisumbua kuitikia saluti zao, alikuwa jamaa mrefu, mzungu, mwenye kipara kinachong’aa, aliwaangalia kwa muda bila kusema neno, halafu akatoa tabasamu la dhihaka. Hapo meno yake yaliyoungua na jino moja la dhahabu pembeni vilionekana.
“Nasikia kuna wasichana wawili wamekosekana, jitahidi watafutwe haraka, nataka hili jambo limalizike ndani ya muda mfupi ujao ili tumiliki mambo kama tulivyopanga” Alisema huyo mtu mwenye meno machafu kwa ghadhabu.
“Tayari tumeshawaombea hifadhi Tanzania, hivyo tunangoja hao wawili wapatikane ili malengo yetu yatimie, nawapa masaa kumi na mbili muwe mmekamilisha” Alisema huyo mzungu aliyejulikana kwa jina la KK na kutoka nje ya chumba kile huku nyuma akiwaacha Joseph Katanga na askari mwingine.
“Tumeua zaidi ya watu 200 usiku wa kuamkia leo, hebu hivi vitoto visituharibie kazi, huyo Joan ni mjukuu wa mzee Kasheba. Hebu nenda kaangalie, kama wako kwake muue yeye halafu walete, sitojali ukweli kuwa ni rafiki yangu lakini kama hafuati nisemacho sheria hufuata mkondo wake. Fanya haraka nataka kufunga kazi hii haraka iwezekanvyo, halafu nianze kuangalia kwenye TV jinsi suala hili litakavyoongelewa!” Katanga alisema huku macho yake yakionekana kuwa machovu na mekundu, hii ni kutokana na kazi aliyokuwa ameifanya usiku kucha. Kazi ya kuongoza jeshi la FRPI kuwaua watu wote wa jamii ya Hema na kuhakikisha hakuna mfugaji anabaki eneo hilo. Lilikuwa ni zoezi kubwa na gumu, waliua kadiri walivyoweza na kwa namna yoyote ile.
Yule askari alipiga saluti na kuondoka na vijana wengine kumi, walielekea nyumbani kwa Mzee Kasheba kuona kama wanaweza kuwapata Joan na Khajat.

Punde nitakuletea sehemu ya pili
 
Saa 72 za Kufa au Kupona
Mtunzi: Japhet Nayng’oro
Mfululizo wa: 02


“Tayari tumeshawaombea hifadhi Tanzania, hivyo tunangoja hao wawili wapatikane ili malengo yetu yatimie, nawapa masaa kumi na mbili muwe mmekamilisha” Alisema huyo mzungu aliyejulikana kwa jina la KK na kutoka nje ya chumba kile huku nyuma akiwaacha Joseph Katanga na askari mwingine.
“Tumeua zaidi ya watu 200 usiku wa kuamkia leo, hebu hivi vitoto visituharibie kazi, huyo Joan ni mjukuu wa mzee Kasheba. Hebu nenda kaangalie, kama wako kwake muue yeye halafu walete, sitojali ukweli kuwa ni rafiki yangu lakini kama hafuati nisemacho sheria hufuata mkondo wake. Fanya haraka nataka kufunga kazi hii haraka iwezekanvyo, halafu nianze kuangalia kwenye TV jinsi suala hili litakavyoongelewa!” Katanga alisema huku macho yake yakionekana kuwa machovu na mekundu, hii ni kutokana na kazi aliyokuwa ameifanya usiku kucha. Kazi ya kuongoza jeshi la FRPI kuwaua watu wote wa jamii ya Hema na kuhakikisha hakuna mfugaji anabaki eneo hilo. Lilikuwa ni zoezi kubwa na gumu, waliua kadiri walivyoweza na kwa namna yoyote ile.
Yule askari alipiga saluti na kuondoka na vijana wengine kumi, walielekea nyumbani kwa Mzee Kasheba kuona kama wanaweza kuwapata Joan na Khajat.

*******
Goma, DRC – 2017

Alhamisi, Saa 4:30 usiku

NDEGE maalum iliyokuwa imebeba makomandoo watano, ilikuwa ikipita juu ya anga la Goma - Congo DRC, anga lililokuwa limefunikwa na mawingu mazito, meusi ambayo mara kwa mara yalikuwa yakimulikwa na mwanga wa radi. Ndege hiyo ilikuwa na jumla ya abiria sita pamoja na rubani, japo ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria kumi na mmoja. Makomandoo wote walikuwa na vifaa vyao tayari kwa kuruka toka kwenye ndege hiyo hadi kwenye kambi maalum ya jeshi la serikali ambayo ilikuwa eneo hilo la Kivu Kaskazini.
Ilipofika eneo fulani, ndege hiyo maalum ilitoa mlio maalum, hivyo makomandoo wote wakajua walikuwa wamefika sehemu waliyotakiwa kudondoshwa, kila mtu akaanza kuweka sawa begi lake wakati ndege hiyo ilipokaribia sehemu ambayo makomandoo hao wangedondoshwa kwa miavuli.
“Haya makamanda tuko eneo husika. Nitahesabu hadi tano, kisha nitafyatua mlango nanyi mtaruka, mlango utakuwa wazi kwa sekunde thelathini halafu nitaufunga. Kila la kheri makamanda!” Kapteni Ambrose ambaye ndiye alikuwa rubani wa ndege hiyo alisema kwa sauti ya juu.
Makomandoo walikuwa kimya kila mmoja akiwa tayari kwa tukio.
“Moja…mbiliii…tatuuu…nnneeee… Tano twendeeee!”
Mlango ulifyatuka makomandoo wakajiachia hewani.
Ilitokea kama ghafla tu neno “shiiiiiit!” likasikika.
“Nini tena?” Kapteni Ambrose alihoji kwa hamaki baada ya kusikia komandoo mmoja akisema shiiiit!
“Limechanika, anyway ngoja niende, see you Captain!” alisema komandoo huyo aliyekuwa amesema shiit hapo awali, baada ya kubaini kuwa parachuti lake lilikuwa limechanika sehemu ya katikati.
“High risk (ni hatari sana), ngoja kidogo!” Kapteni Ambrose alipiga kelele kumzuia yule komandoo asiruke, lakini alikuwa ameshachelewa, yule komandoo alikuwa ameshajiachia angani!

* * *



Alhamisi, Saa 5:15 usiku

Komandoo wa kwanza alitua kwa kukimbia kwenye shamba kubwa la kahawa, zao ambalo ni maarufu eneo hilo. Dakika tano baadaye makomandoo wote isipokuwa mmoja tu walikuwa wameshafika sehemu waliyokuwa wakitarajiwa kutua. Hapo walipokelewa na wanajeshi watatu wenye vyeo vya juu wa jeshi. Makomandoo waliopokelewa ni Twaha Mchopa, Musa Buti, Mark Muga na Emily Otieno.
“Poleni kwa safari!” alisema afisa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Meja Jean Francis Kabananga.
“Asante. Ila tuna wasiwasi na mwenzetu sijui amepatwa na madhila gani!”
“Nilitaka kuuliza, maana tuliambiwa mko watano!?” Meja Kabananga alisema
“Tulimsikia akilalamika akiwa angani, nadhani alipata changamoto ndogo, ila yeye ni muhitimu bila shaka atafika tu,..” Luteni Musa Buti, mmoja wa wale makomandoo alisema. Yeye ndiye kiongozi wa wenzie kwenye misheni hii.
“Kwani hapatikani kwenye mawasiliano?” Meja Kabananga alihoji wakati wakielekea kwenye magari matatu ya kijeshi yaliyokuwa yamepaki eneo hilo.
“Dakika tatu baada ya kutua tulikuwa na mawasiliano naye, akatuambia kwa sababu ya kuharibika parachuti lake amedondokea mbali na sehemu iliyokusudiwa, na kama unavyoona hali hii ya upepo mkali na mvua hizi bila shaka unaweza kuelewa mtu akikutwa na ajali ya kuharibikiwa parachuti angani!” alisema Luteni Musa Buti.
“Okay, maadam ana ramani tutamngoja hapo kambini, ni kilomita kumi toka hapa, twendeni maana mnasubiriwa kwa hamu kubwa sana na mkuu!” Meja Kabananga alisema kwa Kiswahili chake cha Kikongo. Mvua nzito ilikuwa bado ikiendelea kunyesha, milio ya bunduki na risasi vilisikika kwa mbali, kitu kilichowaambia wale makomandoo kuwa walikuwa wameingia kwenye uwanja wa vita.
“Nasikia milio ya mashine huko!” Mchoppa alisema
“Nakwambia hapa limeshakuwa swala la kawaida wakati wote ni wakati wa mapambano, hali iliyofanya raia na askari wazoee tu sasa!” Alisema afisa mmoja wa jeshi. Ardhi ilikuwa imelowa chepechepe.


Alhamisi, Saa 5:15 usiku.

Kilomita nane toka mahali ambapo Meja Kabananga alikuwa anawapokea wale makomandoo, huyu naye alikuwa amepokelewa kwa namna yake. Baada tu ya kutua chini, Komandoo Pablo Mahene alishtukia anamulikwa na mwanga mkali sana usoni. Wakati bado anahangaika namna ya kujitoa kwenye parachuti alishtukia anachomwa na kitu kama sindano shingoni. Fahamu zikamtoka.
“Ndio mkuu, kama tulivyotarajia, aliangukia eneo lilelile,” alisema jamaa mmoja mrefu sana, mweusi sana, mwenye jicho moja bovu, wakati huu walikuwa kwenye gari moja la jeshi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi sana kama wako kwenye barabara ya lami.
“Vema, kazi nzuri! Sasa watajua kuwa Jose Katanga karudi, watafidia muda wote ambao nilikuwa nje ya uwanja!” Ulisema upande mwingine kwenye redio ile ya mawasiliano.
“Haya ndio mambo tulikuwa tunayakosa bosi, huu msisimko umerejea tena!” Alisema yule jamaa mrefu, mweusi, mwenye jicho bovu.
“Mwiteni mzee Kasheba amuhoji huyo jamaa!” Joseph Katanga alisema.
 
Saa 72 za Kufa au Kupona
Mtunzi: Japhet Nayng’oro
Mfululizo wa: 03

“Ndio mkuu, kama tulivyotarajia, aliangukia eneo lilelile,” alisema jamaa mmoja mrefu sana, mweusi sana, mwenye jicho moja bovu, wakati huu walikuwa kwenye gari moja la jeshi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi sana kama wako kwenye barabara ya lami.
“Vema, kazi nzuri! Sasa watajua kuwa Jose Katanga karudi, watafidia muda wote ambao nilikuwa nje ya uwanja!” Ulisema upande mwingine kwenye redio ile ya mawasiliano.
“Haya ndio mambo tulikuwa tunayakosa bosi, huu msisimko umerejea tena!” Alisema yule jamaa mrefu, mweusi, mwenye jicho bovu.
“Mwiteni mzee Kasheba amuhoji huyo jamaa!” Joseph Katanga alisema.

******

SAA kumi kamili asubuhi, kikao cha dharura kilikuwa kimeanza eneo la Pugu jijini Dar es Salaam. Mada ilikuwa moja tu; kujadili hatua za kuchukua kutokana na taarifa zilizopatikana usiku kuhusu timu yao maalum waliyoituma Goma kwa kazi maalum.
“Makamanda, bila shaka mmeshtushwa na taarifa kuwa makomandoo wetu watano wako Congo DRC,” alisema Meja Jenerali Obed Mahenda, huku nyuso za makamanda waliokuwa kikaoni hapo zikionesha ubaridi uliotokana na hali halisi kuzunguka suala lenyewe. Hapo akajua kuwa kwanza alikuwa na kazi kubwa ya kuwatuliza wajumbe wale na kuwashawishi wakubaliane na kilichofanyika hadi sasa kabla ya kutaka maoni yao juu ya nini kifanyike zaidi.
“Uamuzi wa kupeleka makomandoo hawa ulifanyika kwa ombi toka ngazi za juu, na ulifanywa na watu wachache sana kwa upande wa ndani, hivyo itanilazimu kuelezea kwa kifupi kwa nini viongozi walituomba sisi kupeleka makomandoo watano, halafu ndipo nitawaeleza kile ambacho inatakiwa tukifanyie uamuzi baada ya taarifa za usiku huu.”
Akazungusha kichwa kuwaangalia wajumbe tisa waliokuwa wamehudhuria kikao hiki. Mmoja kati ya wajumbe hao ni Kapteni Ambrose, rubani aliyekuwa ametumika kuwapeleka wale makomandoo. Watu wote walikuwa kimya kabisa.
“Iko hivi,” aliendelea, “nchi kadhaa zenye mapenzi mema na nchi ya DRC zilifanya kikao cha dharura, hii ilitokana na hali iliyokuwa imejitokeza katika wiki za hivi karibuni, kama mjuavyo kiongozi wa nchi hiyo kwa kushauriana na nchi hizo aliridhia kuitisha uchaguzi mkuu. Pamoja na Tume ya Uchaguzi, Jumatatu wiki ijayo anatarajiwa kutoa tangazo la tarehe ya uchaguzi, kila kitu kilikuwa kimepangwa vyema hadi pale ambapo ICC walipotangaza ghafla kuwa wameamua kumwachia Joseph Katanga siku kumi zilizopita.
Bila shaka wote mlizipata taarifa hizi, Katanga alitumikia kifungo chake cha muda mrefu na sasa alikuwa amebakiza miaka michache ili kumaliza, lakini kwa maelezo kuwa amejutia na kusikitikia vitendo vyake, ICC imeamua kumwacha huru na kumrejesha DRC. Lakini pia, ICC inadai kuwa amebadilika sana kitabia, taarifa hii ilikuwa ya kushangaza na kuchanganya. Kiufundi, kwa muda ulivyo na mazingira, Katanga akishasikia tangazo hili bila shaka atatangaza kugombea. Taarifa za kijasusi zinadai kuwa Katanga ameshaanza kufufua lile kundi lake la waasi na anakusudia kulifanya kuwa chama cha siasa, kurudi kwa Katanga kumeharibu zaidi hali ya usalama huko Goma. Taarifa tulizonazo ni kuwa watu wengi sana wameuawa Goma na kupelekea kuenea kwa magonjwa ya mlipuko eneo hilo hasa kwa vile maiti zimetapakaa mitaani na mvua kubwa bado inaendelea kunyesha, hivyo ili kuweka hali ya usalama na kuhakikisha uchaguzi huu hauingiliwi na Katanga, kazi yetu ikawa ni ‘kumnyamazisha’!
Wenzetu wa DRC hawakutaka kuhusika kwa namna yoyote na huyo Bwana Katanga, hivyo wakaomba msaada, ikiwa kama sehemu ya kutafuta amani ya DRC. Adui wa rafiki yako ni adui yako, na adui wa adui yako ni rafiki yako. Tunaunga mkono serikali halali, ndio maana tumepeleka nguvu yetu kule kukabiliana na waasi, hivyo hii nayo ni sehemu ya kukabiliana na waasi.
Lakini tukiachana na ombi la serikali, mtakumbuka kuwa kwenye mafaili yetu tuna faili lililo wazi dhidi ya mtu huyu, yaani Joseph Katanga. Mnakumbuka ile kashfa ‘Mapandikizi’ ambayo yeye alikuwa mhusika mkuu, hivyo ili kufunga faili lile hatakiwi kuendelea kuishi.
Sasa ni kwamba, makomandoo wanne wamefika salama na tayari wako kwa ajili ya kazi. Ila komandoo wetu mmoja inawezekana akawa amekamatwa na waasi wa Goma, hii ina maana kazi imeongezeka na kuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa. Kazi imekuwa kubwa kwa namna hii; Moja tunatakiwa tuendelee na operesheni yetu ya awali, yaani ‘kumfuta’ Katanga. Pili, inabidi kufanya utaratibu wa kumuokoa komandoo wetu ambaye inaaminika yuko kwenye mikono ya waasi hao ambao wanaongozwa na Joseph Katanga hapohapo Goma. Tatu, ni kufanya uchunguzi wa ndani kujua ilikuwaje parachuti likawa limetoboka kabla ya kutumiwa.
Kwa mujibu wa Kapteni Ambrose ambaye ndiye aliyeongoza ndege na kuwadondosha wale makomandoo kwenye anga ya Goma, komandoo aliyetoweka alilalamika kuhusu parachuti lake kuwa na ubovu, hata kabla hajatoka kwenye ndege, ina maana kulikuwa na parachuti bovu, jambo ambalo si la kawaida, hasa ukizingatia namna utaratibu wetu wa manunuzi ya vifaa vya jeshi ulivyo madhubuti na umakini mkubwa. Haliwezi kuwa kosa tu, siamini kuwa ni bahati mbaya, hivyo nataka kujua undani wa jambo hili kwani inaonesha kuwa mpango wa kukamatwa kwa komandoo wetu ulipangwa tokea hapa. Hiyo itamaanisha kuwa kuna ‘pandikizi’ mwingine wa Katanga, na hii inathibitisha ni jinsi gani mtu huyu alivyo wa hatari sana.”
Meja Jenerali Obed Mahenda alipofika hapo alishusha pumzi ndefu kuashiria kuwa alikuwa amehitimisha maelezo yake ya awali. Hapo ukafuata mjadala mkali sana toka kwa wajumbe wa kikao. Ilipofika saa kumi na moja na robo Meja Jenerali Obed Mahenda alipiga makofi kusitisha mjadala mkali.
“Nikiwasikiliza wajumbe wote naona kimsingi tunakubaliana kufanya haya mambo matatu,” alisema.
“Nimeona watu mmekwenda mbali zaidi namna ya kuyatekeleza, mawazo ya awali yanaonesha kuwa ile timu ya makomandoo walioko Goma igawanywe.
Wawili wamtafute Luteni Pablo Mahene, komandoo wetu aliyetoweka.
Wawili wamtafute Katanga.
Leo ni Ijumaa asubuhi, Tangazo kuhusu uchaguzi linatakiwa kutolewa Jumatatu, ina maana wana saa 72 tu za kukamilisha kazi zote mbili, au niseme tuna saa 72 tu za kufanya kazi hii. Nitawafikishia ujumbe huu ili asubuhi hii ya leo waanze operesheni zao, tunakubaliana hapo?”
Wote waliafiki.
“Sasa kazi ya ndani, mnadhani tufanyeje ili kuchunguza suala hili? Tupate mtu wa ndani au?”
Hapo tena ukazuka mjadala mkubwa sana, wengine wakisema mpelelezi wa ndani hatakuwa huru hasa ikitokea anawachunguza waliomzidi cheo, wengine walisema sheria za ndani haziruhusu mambo kwenda nje.

* * *

Jabir Omari Makame alikuwa jikoni wakati aliposikia simu ya mezani kwake ikilia sebuleni. Si kawaida yake kuamka asubuhi sana na kwenda jikoni, ila kwa ombi la mpenzi wake aitwaye Juliana Owima ilibidi aende jikoni. Mpenzi wake huyo alikuwa mjamzito, ujauzito mkubwa tu, hivyo alimkurupusha asubuhi na kumuomba amtengenezee mayai ya kukaanga.
Hivyo wakati simu ile inaunguruma, yeye alikuwa jikoni. Aliondoka haraka kuelekea sebuleni, hata kabla hajaipokea alishajua kuwa simu ile ingekuwa inatokea ofisini. Ni ofisini pekee ndio humpigia simu ile ya mezani wanapokuwa na hakika kuwa yuko nyumbani, lakini marafiki ndugu na jamaa hutumia zaidi simu ya mkononi.
“Jabir hapa,” alisema baada ya kuweka sikioni kiwambo cha kusikilizia.
“Bila shaka hujambo Jabir, ninakuhitaji haraka iwezekanavyo!” sauti ya mwanamke wa makamo ilisikika.
“Duuh, ofisini siyo?” Jabir Omari Makame aliuliza.
“Hapana, nitakueleza ukiwa njiani unakuja!” ilisema ile sauti ya kike.
“Tuonane hapo ndani ya dakika arobaini zijazo!” Jabir Makame alisema na kuibamiza simu kwenye sahani yake.
 
Back
Top Bottom