Oparesheni Barakuda yarudi Afrika III

jijayetu

JF-Expert Member
Jul 15, 2016
722
549
MBINU za mabeberu zinatabirika, na kila wakati zinafanya kazi, kwa hiyo hawana haja ya kuzibadili, kwa vile sisi tunatabirika! Lumumba alijua ataishia kifo cha kikatili aliposema “Nikifa kesho, ni kwa sababu, mzungu kampa Mwafrika silaha!”

Vyombo vya habari duniani vilijenga taswira kwamba Lumumba ni mtu mwenye aina ya kichaa ambacho kinapotosha haiba ya mtu na kumfanya awe na chuki isiyo kikomo. Kichaa ambacho huwapata watu weusi tu. Umbile lake nalo lilieleza mengi hasa wembamba wake, urefu wa vidole vyake kwamba ni jitu lililopagawa na chuki ya kutisha na lingeweza kuteketeza dunia nzima kwa uroho wa madaraka.

Ni propaganda iliyokubalika kuwa Lumumba ni hatari, bora afe amani ipatikane. Baada ya kifo chake ukweli ukaanza kudhihiri na maelfu Ulaya, Asia na Afrika wakadai UNO itoke Kongo na kwamba Afrika ni ya Waafrika. Rais Nasser wa Misri alidai Katibu Mkuu wa UNO ajiuzulu kwani Afrika yote haina imani naye.

Nkurumah Rais wa Ghana aliomboleza kwa kusema “ndugu zetu, wapigania uhuru (Lumumba umri wa miaka 35), Mpolo (umri miaka 32, Waziri wa Vijana na Michezo), Okito (50 Makamu wa Spika) wameuawa mahali pasipojulikana huko Katanga, Kongo.

Kilicho wazi ni kwamba wameuwa kwa sababu, UNO ambayo Lumumba akiwa Waziri Mkuu aliwaomba waje kulinda amani na usalama, walishindwa kutimiza wajibu wao. Kifo cha Lumumba na wenzie ni cha pekee katika historia, kwamba kiongozi halali wa nchi ameuawa kwa kusaidiwa na UNO ambayo iliwaunga mkono waasi.

Kwa kukosa msaada wa UNO, Lumumba aliposaidiwa magari na Urusi akazomewa kuwa ni mkomunisti na waasi wapolimbikiza silaha na wajeshi kutoka Ulaya, UNO ilinyamaza. Vituo vya Radio nchini vilifungwa ati kwa sababu za kiusalama. (Badala yake matangazo yakupinga serikali yalitangazwa kutoka Kongo Brazaville nchi ambayo Rais wake alikiri anatumikia wazungu) UNO ilishindwa kuzuia Lumumba na wenzie wasichukuliwe na mahasimu wao kwenda Katanga kuuawa.”

Waafrika tulifichwa ukweli kuhusu machafuko ya Kongo na mauaji yaliyofanyika. Wakongo walidhulumiwa uhai na haki ya kujitawala. Inauma kujua UNO ilitumika kukidhi matakwa ya Ulaya na Marekani na hata wanapofanya makosa ya wazi, hakuna aliyekemea.

Msimamo wa Lumumba ulikuwa rasimali za Kongo zijenge uchumi imara wa Kongo na Afrika kwa faida ya vizazi vyake. Msimamo huu ulikuwa tishio kwa wazungu na vizazi vyao. Inatisha kiongozi wa taifa kubwa kama Marekani Eisenhower na Macmillan Waziri Mkuu wa Uingereza, wakitamka kwa vinywa vyao; “Kwa nini tusimwondoe Lumumba sasa? Kama atarudi madarakani atatuletea tatizo kuhusu Katanga suala ambalo litatutia hatiani kisheria”. Walijua kilichokua kinaendelea lakini nani atawahukumu mpaka leo vizazi vyao bado vinatutambia.

Waliohujumu Kongo wanajulikana, ushahidi upo na wenyewe wanakubali, lakini mpaka leo wanadunda si kama Nduli wala Hitler. Mbona UNO iko kimya kuhusu Kongo na inaendelea kuficha ukweli, wanaendelea kutenda maovu ? Sisi wenyewe tuko wapi?

Lumumba, Mpolo, Okito na wengine wengi waliteseka na hatimaye kuuawa kwa ajili yetu. Akina Tshombe, Mobutu na wengine waliokubali kuwasaliti, wamepata nini na wamewaachia nini vizazi vyao?

Wale waliofurahia kumpiga vibaya, kumwekea vijiti katika kucha zake, kumfunga kamba, kumlaza kwenye unyevunyevu bila kuoga wala kubadili nguo kwa zaidi ya siku 30, na kuwapa chakula ambacho hata mbwa koko hangekula na kumdhalilisha, wako wapi? Wako wapi walioshuhudia Lumumba akimiminiwa risasi kwa usongo na mamluki wa kibelgiji kama mhalifu sugu?

Dhambi na laana ya kusaidia mipango ya wazungu ya kuua vuguvugu la ukombozi Afrika kwa vitendo vya kikatili dhidi ya Lumumba na wenzie bado tunayo Waafrika wote. Baada ya kuuawa waliwafukia kisha wakafukua, maiti zao zikakatwa katwa vipande na kutiwa kwenye pipa lenye tindikali, mifupa ikachomwa moto, majivu kutawanywa porini ili wasirudi tena. Vidole viwili vya Lumumba na mfupa kwenye uume wake vikakatwa na ‘wachawi’ hao kwa lengo lisilojulikana na baadaye kutupwa baharini! Damu yao bado iko juu yetu hadi nasi tutakapoacha usaliti!

Jamani waliteswa kwa kuthubutu kutekeleza matakwa, mahitaji na matarajio ya Wakongo! Ili kuzima vuguvugu la ukombozi kote Afrika wakoloni wakaanza kutawala kupitia vibaraka wanaoingilika. Kifo cha Lumumba kilikusudiwa kuwa fundisho kwa wanaojitia kimbelembele.

Wakoloni hawataki serikali imara ambayo itabinya uhuru wa kampuni zao kubwa kufanya watakavyo pasi kuingiliwa na serikali au sheria zinazokinzana na matakwa yao. Lawama kwa maovu ya kampuni hizo itabebwa na serikali zetu ambazo zimelazimishwa kutoa ulinzi kimkataba.

Katibu Mkuu wa UNO, Dag Hammarskjold, kutoka Sweden alificha ukweli kuhusu machafuko Kongo. Alijidai hajui kuwa Lumumba aliuawa Januari 17, mwaka 1961 huko Katanga kwa kuandika Januari 19, 1961 “… kupelekwa kwa Lumumba Katanga kuzingatie azimio la UNO la haki za binadamu…” UNO ilimsalimisha Lumumba kwa adui zake akauawe. Januari 1961, UNO ilitambua kazi ya Tshombe katika kujenga mazingira mazuri ya kuinyonya Kongo na Baba Mtakatifu John wa 23 pia alibariki juhudi za Wabelgiji.

Septemba 1960, UNO iliingilia kati raia wachache walipouawa wakati wa machafuko. Lakini haikuchukua hatua yoyote Januari hadi Machi 1961, wakati Lumumba na maelfu ya raia walipouawa, kuchomewa nyumba zao na jeshi la waasi,
Mwandishi Hempastone Smith anasema; “…Lumumba alikua hajui atendalo, hana sifa za uongozi, fisadi, mbaguzi wa rangi. Kama kifo cha mtu mmoja kilihitajika kuokoa maisha ya Wakongo, basi Lumumba alistahili heshima hiyo!”

Munongo msaidizi wa Tshombe alisema; “ Nitakuwa nadanganya nikisema kifo cha Lumumba kinanihuzunisha, ni mhalifu wa kawaida yule, aliyesababisha vifo vya wengi Katanga na Kasai. Katibu Mkuu wa UNO mwenyewe kasema yalikua mauaji ya kimbari.”

Gazeti la Ubelgiji liliandika; “Yaliyotokea Kongo yanathibitisha kwamba huko Afrika upatikanaji wa demokrasia ni suala la mauaji.” Gazeti jingine likasema; “ uhai wa Lumumba ni kama jipu ambalo lilikua linahatarisha nchi nyingine. Ni vigumu kwetu kusikitika.”

Baada ya kumuua Lumumba walewale walioanzisha vita Kongo na kuwasaidia waasi wakaanza kutumia lugha ya umoja wa kitaifa. Walijua kwa vile vibaraka wao wamejaa bungeni na kuunda serikali basi ajenda ya kuikamua Kongo itafanikiwa. UNO ikatuma askari wake kumlazimisha Tshombe arudi kundini.

Mamluki wote wakizungu na kiafrika walizawadiwa kwa kazi nzuri. Kosa kubwa alilofanya Lumumba ni kuamini kwamba ana marafiki wa kutegemewa, Afrika, Asia, Urusi, UNO na baadhi ya viongozi wachache nchini kwake.

Tumefichwa ukweli na kumbukumbu kuteketezwa ili tusijue mawazo ya Lumumba yakuendeleza vuguvugu la kuunganisha Afrika na kujenga uchumi imara kwa faida ya Afrika. Damu ya Lumumba inatembea ndani ya mishipa yetu! Tukiungana tutapona, tukitengana wote tutaangamia!
 
Baba hatari, lakini yote uliyoyasema watu watayapitisha kwenye masikio yao kama vile hukusema chochote. Ni Ukoloni Mamboleo na kibaya zaidi HAWA wazungu wameshatuBRAINWASH kiasi kwamba chochote watakachosema na kufanya wengi wetu tutajionea sawa tu sababu tunawahusudu na kutaka KULWA kama wao. Piga MOYO ndugu endelea KUELIMISHA JAMII NA TAIFA KWA UJUMLA.
 
Baba hatari, lakini yote uliyoyasema watu watayapitisha kwenye masikio yao kama vile hukusema chochote. Ni Ukoloni Mamboleo na kibaya zaidi HAWA wazungu wameshatuBRAINWASH kiasi kwamba chochote watakachosema na kufanya wengi wetu tutajionea sawa tu sababu tunawahusudu na kutaka KULWA kama wao. Piga MOYO ndugu endelea KUELIMISHA JAMII NA TAIFA KWA UJUMLA.
kitu kibaya hiki kwa jamiii ya sasa, watu wakobize kutafta umbea na vitu vya kijinga kuliko mambo ya msingi,

wazungu wako makini sana na mambo ya msingi lakini waswahili tuko bize na vitu vya kuambiwa.

juzi ndg makamba alisema vijana wengi wanataka taarifa lakini siyo maarifa.
 
Ukweli mtupu Democracy ya wamaghalibi haiwezi kumkomboa mwafrika.vibaraka wana someshwa na hawa watu kuleta fujo.hapa Tanzania tunao sikuchache zilizopita walijazana kwa balozi wa umoja wa ulaya.
 
Back
Top Bottom