Ole wao mabilionea wa Kikwete | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ole wao mabilionea wa Kikwete

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, May 11, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  May 11, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,788
  Likes Received: 83,160
  Trophy Points: 280
  Ole wao mabilionea wa Kikwete

  Ansbert Ngurumo

  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  NAKUMBUKA kauli moja ya Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani. Alisema kwamba katika kipindi cha utawala wake, anakusudia ‘kutengeneza’ mabilionea wa Kitanzania.

  Waliokuwa karibu na ‘jikoni’ walijua anachomaanisha. Walijua msukumo wa kauli yake na matokeo yake.

  Na baadhi ya waliokuwa naye kwa muda mrefu katika harakati za kuitafuta Ikulu, hasa waliotoa mchango mkubwa kifedha, walikuwa wa kwanza kushangilia.

  Hata pale alipotoa kauli nyingine, kwamba anakusudia kuweka sheria itakayowazuia wafanyabiashara kufanya siasa, baadhi yao walishangilia pia.

  Maana walijua kuwa kauli hiyo ilikuwa tofali za nyongeza katika msingi wa ‘kutengeneza’ mabilionea wa Kikwete.


  Ndiyo maana, ingawa kuna watu wameingia kichwa kichwa kupongeza na kukubaliana na kauli hiyo, wapo wanaodhani kwamba msukumo wa kauli hiyo ndiyo kasoro yake.

  Baadhi ya hawa wanaozungumzwa kuondolewa kwenye siasa ili wafanye biashara ni wale ambao wametumia siasa kuchuma na kutajirika kwa kasi inayotisha, na kuiingiza serikali katika migogoro mikubwa.

  Na kwa kuwa ni mapapa wasioweza kukamatika, maana serikali inawaogopa au inafaidika nao; na kwa kuwa inajua kuwa matendo yao yamewajengea sura hasi kisiasa, wanaweza kupewa fursa ya ziada.

  Waonekane wameondolewa kwenye siasa, lakini watumie mitandao waliyoijenga kwenye mfumo wa kisiasa kuendelea kujineemesha. Si tu kujineemesha, bali kuwaneemesha wanasiasa wenzao wanaosubiri kukinga mabakuli wakati wa kampeni.

  Hivyo, hawa watakuwa ni mabilionea waliotengenezwa makusudi ndani ya serikali, wakawekwa nje ya chama na serikali ili wakifadhili kinapotembeza bakuli.

  Maana yake ni kwamba ingawa hawatakuwa wanasiasa, watakuwa na nguvu ya kuendesha siasa, na hata kutuamulia nani atawale; maana siasa zetu zimeshatekwa na pesa za matajiri – wakiwamo majambazi waliokubuhu wanaotegemea ulinzi wa dola.

  Kama pesa ya mabilionea hawa ndiyo itaendelea kununua urais, ubunge na udiwani wa watawala wetu, kuna neema gani itakuwa imepatikana katika ubilionea huu?

  Kama kuwatenga na siasa itakuwa ni njama ya kuwaokoa na zahama kutoka kwa wananchi, ipo wapi nia njema ya kisiasa kutoka kwa watawala hao?

  Kama watawala hawatajikata kutoka kwenye ufadhili mchafu wa mabilionea hao (ambao kwa hakika nao watalipa fadhila), zi wapi siasa za kistaarabu, na upo wapi msingi mpya wa uadilifu kisiasa?

  Walipofurahia kauli ya rais kutengeneza mabilionea, wenzetu hawa walijua fika kwamba mabilionea hao wasingekuwa miongoni mwetu. Waliamini sasa zamu yao ilikuwa imewadia. Waliridhika kwamba ‘mtaji’ waliowekeza kwenye kampeni ungekuwa umezaa faida.


  Ni wazi, baadhi yao walijua kuwa kauli ya rais ya kutengeneza mabilionea ilikuwa ya kisiasa zaidi. Lakini ilikuwa na uzito mkubwa ambao ungewahakikishia nia njema kisiasa na kijamii.

  Kwa sababu ya kiwewe na mbwembwe za wakati huo, baada ya ushindi wa kishindo, baadhi yao walipumbaa, wakaona hakuna haja ya kusubiri rais ‘atengeneze’ mabilionea wake.

  Wakadhani kwa kuwa yeye si mfanyabiashara, hana uwezo wa ‘kuwatengeneza.’ Wakaanza kujitengeneza wenyewe haraka haraka kuwa mabilionea wa Kikwete.

  Baadhi yao ndio waliompa ushauri wa kipuuzi wa kutawanya hicho kinachojulikana kama mabilioni ya Kikwete – kugawa shilingi bilioni moja kila mkoa, eti kuwaendeleza wajasiriamali wazawa.

  Nasisitiza neno ‘wazawa’ kwa sababu wasio katika tabaka hilo walishajikomboa kifedha. Si walengwa wa vijisenti hivi viliyorushwa mikoani.

  Kwa hesabu ya kawaida kibiashara, bilioni moja ni pesa kidogo mno; ni mtaji wa biashara ya mtu mmoja au kundi la watu wachache, si watu milioni nne.

  Maana kila mmoja wa mabilionea halisi wa Kikwete, fisadi na asiye fisadi, ana miradi binafsi ya mabilioni ya shilingi inayozidi jumla ya pesa zote ambazo serikali ilisambaza mikoani.

  Inasemekana yupo mmoja ambaye wakati wa kampeni alitoa mchango wa pesa ambao ni zaidi ya mara mbili ya mabilioni yote ya Kikwete yaliyosambazwa mikoani.


  Kwa maana hiyo, mtu mwenye uwezo mkubwa kifedha kwa viwango hivyo, – hata kama amezikwapua popote anapojua – anaweza kumpa mkubwa au chama tawala bilioni zaidi ya 26 kwa shughuli yoyote itakayokiwezesha kuimarisha madaraka yao kwa sababu mbili.

  Kwanza, anajua kuwa wakiondoka madarakani ubilionea wake uko hatarini. Pili, anajua kwamba, kwa kuwa yuko kwenye orodha ya mabilionea watarajiwa, fedha hizo zitarudi tu.

  Ufanisi wa biashara za mtu kama huyu hautegemei uwezo wake kibiashara bali ukaribu wake na serikali na ujanja ujanja wa kujua wapi panono, na kujiingiza humo.

  Watu wa aina hii ndio wamekuwa wanakerwa na kelele za vita dhidi ya ufisadi, kwa sababu wanajua zikiendelea wataibuliwa na ujanja wao au wenzao utagundulika.

  Baadhi yao ndio hao wanalalamika kwamba wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi ‘wanakwamisha jitihada za serikali kuwatumikia wananchi.’

  Wanachukia serikali inaposhikwa shati, maana ndani ya mfuko wa shati hilo, ndimo kuna masilahi yao wasiyotaka tuyagundue.

  Wanakerwa sana na maswali yetu juu ya zilikokwenda bilioni 26 zilizomwagwa mikoani. Wanaogopa tukiendelea kuhoji tutagundua waliozilamba, pia tutagundua kiini cha serikali kuendekeza uchumi wa kiupatu upatu wa kugawa fedha mikoani.

  Lakini baadhi yetu hatushangai hatua ya serikali kujaribu ‘kukuza uchumi wa mwananchi’ kwa kugawa pesa mikoani. Sijui ni misingi ya uchumi wa karne gani, lakini najua tabia ya kugawagawa pesa ndiyo iliwasaidia kupata kuungwa mkono na baadhi ya watu.

  Walinunua njaa za watu wakazitumia kufika hapo walipo na kupata walichonacho. Wanajua kuwa njaa ya pesa imekithiri nchini.

  Hivyo waliamini wakigawa vijisenti kidogo, watakuwa wamewafurahisha baadhi ya wananchi, na wataungwa mkono watakapohojiwa kuhusu utekelezaji wa ahadi zao!

  Wapo wanaojua kuwa hii ilikuwa danganya toto, na pazia la kufunikia mamia ya mabilioni yaliyokuwa yanaandaliwa kutoroshwa au yaliyokuwa yameshatoroshwa kuelekea akaunti za watu wachache sana walio karibu na watawala; kwamba hii ilikuwa janja ya serikali ya kuwatajirisha watu wachache, na kuwaziba wananchi midomo wasishtukie ‘dili’ maana wao walishapewa mgawo wao mikoani.

  Wakati mabilioni ya Kikwete yameshindwa kuwaneemesha wananchi mikoani, miradi minono na tenda kadhaa za serikali, vikiambatana na mikataba mibovu inayohusu rasilimali za umma, vimewaneemesha na kuwatajirisha wachache kwa muda mfupi mno.

  Naamini miaka mitatu ya utawala wa Kikwete tayari imetengeneza mabilionea wachache. Lakini hawatoshi.

  Tungehitaji mabilionea wengi wazalendo – weusi, weupe, wekundu, wa kijani, bluu na kadhalika. Lakini tunahitaji walio safi.

  Hatutaki wanaotutumia sisi au wanaomtumia rais kupalilia umaskini miongoni mwetu, huku wakiibuka na utajiri wasiostahili kuwa nao. Hatukupata uhuru kwa ajili ya kuwaneemesha wajanja wachache.

  Na ahadi ya rais kutengeneza mabilionea haijatimia, maana haijatekelezwa vizuri. Na sasa katika sokomoko hili la ufisadi, papa na nyangumi, ipo hatari kwamba ahadi hii inaweza kukwama kabisa.

  Maana kama wananchi watagundua kwamba wazalendo wanarushiwa makombora ili mafisadi watengenezwe kuwa mabilionea kwa jasho la kodi ya wanyonge, nchi itawaka moto.

  Kama ahadi ya rais kutengeneza mabilionea itagundulika kuwa kichocheo cha ufisadi, papa au wa jina lolote, ahadi hiyo na ipotelee mbali, iuawe na kufukiwa kwa mawe mazito.

  Na kama ubilionea wa hao walionao ni sababu ya jeuri, dharau na kiburi dhidi ya wananchi wazalendo maskini; eti kwa sababu wanatoa ajira na kuwarushia mabaki ya ufisadi, ni heri ahadi ya rais isitekelezeke.


  Mbinu ya kuondoa umaskini wa Watanzania, si kujenga tabaka dogo la mabilionea fisadi linalokuza utajiri wao kwa kuchochea umaskini wa mamilioni ya walipa kodi na wapiga kura wa Tanzania.

  Wao wanajua, na sisi tunajua. Utajiri wa haraka haraka hautokani na biashara halali. Ni dhahiri kwamba waloitajirika kupindukia katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hawafanyi biashara halali tu. Wanazo nyingine tunazopaswa kuzitilia shaka.

  Kauli ya rais ilikuwa njema. Sijui nia yake. Kutengeneza mabilionea ni jambo la heri. Mchango wao unaweza kusaidia katika harakati za kulikomboa taifa kiuchumi.

  Lakini tunataka watengenezwe mabilionea safi. Watoe ajira safi. Walipe kodi yote. Na watuambie waliupataje ubilionea wao ili na wengine wahamasike.

  Na baada ya miaka mitano, tutamuuliza Rais Kikwete atueleze vema jinsi alivyotengeneza mabilionea wake.

  Atuambie ni wangapi, kina nani, na wako wapi? Ni hao hao wafadhili wa CCM wanaolalamikiwa kila siku? Ni hao wanaosemekana waliwekeza sana kwenye kampeni za 2005? Ni hao wanaohusishwa na miradi kibao ya kifisadi?

  Ni hao hao wanaofahamika kwa kukwepa kodi kubwa kubwa? Au ni wawekezaji raia wa kigeni wanaofaidika na misamaha ya kodi ambayo wenyeji hawawezi kuipata? Au ni wananchi wa kawaida waliojikwamua kwa mabilioni ya Kikwete mikoani?


  Au ni watu waliojibidisha kuendeleza na kukuza biashara zao zilizokuwapo kwa mitaji mipya na mbinu mpya? Tuwajue.

  Lakini ole wao, na ole wake, kama mabilionea hao ndio hao wanaosemekana kuiweka serikali mfukoni, wanaojifanya serikali ndani ya serikali.
   
Loading...