Octoba 14 na kumbukumbu ya nyerere na nasaha zake | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Octoba 14 na kumbukumbu ya nyerere na nasaha zake

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mbunge, Oct 12, 2012.

 1. M

  Mbunge Senior Member

  #1
  Oct 12, 2012
  Joined: Aug 7, 2008
  Messages: 104
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Friday, October 12, 2012
  OKTOBA 14

  (Kwa ajili ya kumbukumbu ya Mwalimu na

  Usia wa Hatma ya Tanzania.)  NAMSHUKURU Karimu, kwa kunipa itihari,

  Amri nimesalimu, nakukubali kadari,

  Ili siku ya hukumu, janibu isiwe nari,

  Kwa nafsi kuidhulumu, kwa yasokuwa na kheri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Katika siku adhimu, ya kufariki amiri,

  Inaifaa kaumu, kadhaa kutafakari,

  Tukayapa umuhimu, kuyapima kwa urari,

  Ili lililo rahimu, kwa wazi likadhihiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Alituonya mwalimu, tukadhihaki bashiri,

  Na kinachotakadimu, kwetu sote sio siri,

  Wenyewe twajidhulumu, tuendako ni hatari,

  Mapema tusipojihimu, afriti kuajiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Uovu wanakirimu, wasiomo kwenye gari,

  Nje bado kuhitimu, iweje wakidhihiri?

  Ndani wakitakadamu, kuwa ni kubwa hatari,

  Roho watatudhulumu, yakatoweka ya kheri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Anayefunga gidamu, mbele akatasawari,

  Kabla adhana kukimu, ibada huiathiri,

  Amedamka kujihimu, binafsi yake safari,

  Huyo ni mwanaharamu, nchi ataihasiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Kazungumza mwalimu, hata leo ni habari,

  Huko aliko kuzimu, anaiona hatari,

  Mwaritadi waadhimu, chama kufa ni dhahiri,

  Mkijitia wazimu, mtaipata habari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Kama yao walikimu, kitaifa si muhuri,

  Yawahusu kitimutimu, kinyamkera chagairi,

  Na umma yote kaumu, hawakubali kabari,

  Tunamtaka adhimu, asiye nayo dosari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Udini sio kutimu, tunamtaka mzuri,

  Watu asiyedhulumu, na dunia kaabiri,

  Uzoefu si admu, kimataifa mahiri,

  Wa kuzika uhadimu, nchi ikawa fahari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Miradi wanaoazimu, ya wizi na ukafiri,

  Hata kama Islamu, ibiisi adhihiri,

  Iliyo bora hukumu, ya kwao ni kughairi,

  Jitambue waadhimu, twapelekwa kwenye shari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Huwakusanya wazimu, wakaicheza kamari,

  Pata potea kitimu, chaguo kujitahiri,

  Tumbo akiwasalimu, watamuona mzuri,

  Ije sie kugharimu, yasiyokuwa na kheri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Nchi wakaihujumu, na kuitia kabari,

  Ikulu wakijihimu, damu kumwagwa dahari,

  Na uchumi kudhulumu, mifupa ikadhihiri,

  Baba hakuwarehemu, hao kwetu si nadhiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Taasisi ya Mwalimu, kwayo haina hiari,

  Lazima kutakadamu, kuitangaza hadhari,

  Paka nimemtuhumu, kengele namkasiri,

  Nyoyo zisiwe ni ngumu, kuitangaza athari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Mapadri na maimamu, hutuba nazitabiri,

  Wala sio kuhukumu, ni ukweli kuajiri,

  Kwa insha kutuhumu, nyimbo pia mashairi,

  Taifa kutohasimu, kwa teuzi za hatari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Dhuluma kufa vigumu, hadi ulipwe jeuiri,

  Ajiuza binadamu, ili kuivuna shari,

  Urithi hii awamu, mfuasi tahadhari,

  Hao wanaokirimu, kesho kwako ni hatari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Wamezuka madhulumu, watu wasio na kheri,

  Watangaza umuhimu, na kuwa kwao tayari,

  Kaumu iwaheshimu, kwa mazazi ni mahiri,

  Ni rahisi mahakimu, ninawahofu Jibari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Watu hawa baragumu, mwalimu alikariri,

  Ukiwaona wadumu, Ikulu kuifikiri,

  Na kwenda wanajihimu, wasukumwa na kafiri,

  Wana lao la msimu, la faragha na usiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Pesa zatia wazimu, akili zimewaathiri,

  Sifa zao si adimu, kila mtu kakariri,

  Ovu wanalo jukumu, wanapanga na washari,

  Nchi wakaihasimu, na damu naitabiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Chama tulichokifahamu, asili kimeghairi,

  Wajifungia beramu, wanunuliwa kwa shari,

  Na njaa yawahukumu, hawaioni hatari,

  Kamati wanahujumu, kwa kuabudu matajiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Nafasi kimedhulumu, kufukuza mafakiri,

  Wajitia chakaramu, kwenye mengi yaso kheri,

  Sasa twaona kwa zamu, nchi wanavyoiadhiri,

  Ikisha hii awamu, ije bahari ya damu ?

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Ya Syria natuhumu, hapa kwetu kujajiri,

  Ishara zote za sumu, naweza kuzitabiri

  Nadhani mwazifahamu, kusema si itihari,

  Wajumbe watudhulumu, kujiuza kwa mudiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Alituonya mwalimu, wapo wasio na kheri,

  Nchi waliihijumu, kwa dhahiri na shayiri,

  Cheo mkiwarehemu, wanazo kubwa athari,

  Taifa watagharimu, kwa amani na urari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Watajitia karimu, wakayafanza mazuri,

  Ila yote ya haramu, na nia zao za shari,

  Kuna kitu waazimu, kwa wengi kisicho kheri,

  Mkiwaachia hatamu, kilio kitadhihiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Hatujapangia zamu, wenye uchu na shubiri,

  Kama yao waazimu, kwetu yao si kadari,

  Ndio nasema muhimu, haya kuyatafakari,

  Tuzungumze kaumu, tumpate mushawari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Ningependekeza Salimu, awe ni wetu urari,

  Ana sifa za kutimu, japo walimhasiri,

  Bure tukamtuhumu, asiyekuwa na shari,

  Na Zanzibar muhimu, urais kudahiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Hao wake madhulumu, wa kwanza kwneye mstari,

  Mara mbili kumdhulumu, ninaona kubwa shari,

  Atagoma Muntakimu, nchini asidhihiri,

  Tukajaogea damu, na mengi yaso na heri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Akipita ni alimu, kilingeni nitajiri,

  Chama nikakikirimu, kwa tungo na ushairi,

  Na ushindi si mgumu, kila kitu ni tayari,

  Ila vingine adimu, nahofia tahayari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Pinda naye ni hatamu, kwa ukimya na usiri,

  Watu wangemfahamu, anayo mengi mazuri,

  Nchi ataikirimu, pasijekuzuka shari,

  katikati kujihimu, haki kutoihasiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Amri hajasalimu, Membe naye ni mahiri,

  Makundi kayatuhumu, yanaubeba ushari,

  Wala hayajifahamu, shilingi ikidhihiri,

  Huja kutia wazimu, hata palipo na shwari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Wanawake yao zamu, wasafi waliodhihiri,

  Sio wale wa fremu, kubeza wanaokariri,

  Kitu wasiofahamu, wakajifanza hodari,

  Bora tusiwadhulumu, fursa ikidhihiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Kuna wasio na hamu, wala hawayafikiri,

  Waendelea hudumu, changamoto kuabiri,

  Kama tukijifahamu, hao ndio wenye kheri,

  Ogopeni baragumu, wana yao nzito siri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Yaoneni ya kalamu, yao waliyoyakiri,

  Na kama wajifahamu, na kuenziwa mazuri,

  Na sio wapenda utamu, na rafiki wa hatari,

  Nchi waliodhulumu, na kuifanza fakiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Sio waliotakadamu, hisa zikawa futari,

  Ukubwa wanaoazimu, kuabudiwa kafiri,

  Wa chini wanaodhulumu, na juu kuwapa dari,

  Wajifanyao mahakimu, kudhani ni wenye kheri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Vyama vitajidhulumu, vikichagua hatari,

  Yanayochoma mabomu, kwa tuhuma msumari,

  Ikulu waloazimu, kwenda ifanya bohari,

  Mambo mengi ya haramu, kwenda kuyasetiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Tupate aso na hamu, ya dunia kaghairi,

  Utumwa kuuhudumu, ni mtumwa wa fakiri,

  Dunia anayefahamu, na asoma na kukariri,

  Sio wasiojifahamu, japo waogelea shari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Tuogopeni madhulumu, wazaini wahariri,

  Habari kuwa muhimu, ili sura zidhihiri,

  Ila yao kubwa hamu, waonekane wenye kheri,

  Haya yanaihujumu, tasnia ya habari,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Wajumbe wawakirimu, bidhaa halmashauri,

  Wamenunuliwa hirimu, wala hii sio siri,

  Umeingia wazimu, utajiri wa kiburi,

  Wanasepa wanajimu, vigumu kuyatabiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Wasomi pia walimu, mashehe na mapadri,

  Oktoba kuazimu, kumi na nne lijiri,

  Kongamano la kaumu, kubashiri yenye kheri,

  Makosa kujidhulumu, kwenye nchi yenye kheri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Tupambanue rahimu, nje wasiodhihiri,

  Waliojificha sehemu, mtu asiyeabiri,

  Mema waliyokirimu, nje sasa yadhihiri,

  Mdahalo wahitimu, wao nasi mafakiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Naachia milizamu, kilio chenye ghururi,

  Katika sintofahamu, sijui litadhihiri?

  Ukikubali haramu, ujue wakosa kheri,

  Naikataa dawamu, jioni na alfajiri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Mifumo tuikasimu, kutafuta waso shari,

  Kila kundi kujihimu, na vyama kutafsiri,

  Rais mtu muhimu, kwa heri ama kwa shari,

  Uchama kutotakadamu, wananchi walikariri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Hizi ni zangu Salamu, kwa umma zikadhihiri,

  Naitakia kaumu, heri wala sio shari,

  Najua kitu muhimu, nahodha kumuajiri,

  Huyu ni wetu imamu, kupata yalo mazuri,

  Na moja la kuazimu, ni sifa za urais.  Tunu ya kumbukumbu ya Mwalimu,

  Mtwara. Tanzania.

  Oktoba 12, 2012.


  Posted by KWETU KUPENDWE KWANZA at 12:40 AM No comments:
   
 2. Takalani Sesame

  Takalani Sesame JF-Expert Member

  #2
  Oct 12, 2012
  Joined: Jun 24, 2008
  Messages: 588
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  RIP Mwalimu. Tutakukumbuka daima.
   
 3. Malaria Sugu

  Malaria Sugu JF-Expert Member

  #3
  Oct 12, 2012
  Joined: Jul 7, 2009
  Messages: 2,653
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  baada ya kusikiliza redio imaan, leo nimegundua mwalimu ndie adui yangu number 1
   
 4. Takalani Sesame

  Takalani Sesame JF-Expert Member

  #4
  Oct 12, 2012
  Joined: Jun 24, 2008
  Messages: 588
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Kila la heri mkuu.
   
Loading...