*NYUMA YAKO -- 10*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Tukachukua kama robo saa kufika. Nikagonga mlango na kuita. Kimya. Nikagonga tena na kuita kwanguvu, bado kimya! Kidogo mbeleni tukagundua kuwa bwana huyo hakuwapo tena hapo.
Tulivunja mlango na kusaka. Hakukuwa na kitu.
ENDELEA
“Atakuwa ametoroka,” akasema Daniele.
“hapana,” nikakataa. “sidhani kama huku ni kutoroka bali kujiepusha. Kama nilivyokuambia hapo awali, hakutaka haya mambo?”
“Kwani ni nini anachoficha?” Daniele akauliza akinishikia kiuno.
“Anaficha uhai na usalama wake,” nikamjibu na kisha nikatembea kuelekea gari. Naye Daniele akanifuata. Alipoingia tukajadili maswala kadhaa na kunifunza kuwa “Secret Service” hawakuwa wakihusika na upelelezi wa swala hili la upotevu wa Raisi.
“Kwa sababu za kiuwajibikaji, hawakuhusishwa ili kutoa mwanya wa mkono wa ziada kuwapeleleza hata wao endapo kutakuwa na mahusiano yoyote yale,” Daniele alisema akiwa anatazama mbele kana kwamba gari lipo kwenye mwendo.
Kisha akanitazama na kuniambia kiudadisi, “tunaweza kwenda Washington?” Sikujibu akaongezea, “inabidi tukatafute taarifa za huyo ajenti wa Secret Service ambaye akimletea ujumbe huyo mzee!”
Secret Service ni taasisi ya kiintelijensia inayohusika na ulinzi wa Raisi, Makamu wa Raisi na familia zao kwa ujumla. Wao ni chombo shurutishi cha kisheria kama ilivyo kwa FBI japo majukumu hutofautiana. Kwa ufupi taasisi hiyo huitwa USSS.
“Ni sawa,” nikamjibu Daniele. Niliona wazo lake linapendeza. Inawezekana kumpata ajenti huyo wa Secret Service ikawa ni hatua ya muhimu kwenye zoezi letu. Basi tukaenda huko kwa kutumia ndege. Tulipowasili, tukanyookea moja kwa moja kwenye makao makuu ya United States Secret Service (USSS). Huko tukakutana na Director, bwana Owen Allen, mwanaume mwembamba mwenye masikio mapana, macho madogo na lips nyembamba. Tukamweleza shida yetu.
Akiwa ameshikilia picha ya mtu tumtakaye, akasema, “huyu alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa zamu ya kumlinda Raisi.” Kisha akaminya lips na kufinya macho. “ila siku ambayo Raisi alipotea, hakuwa zamu. Hakuambatana naye.”
“Sasa yupo wapi?” akauliza Daniele akimtazama Director kwa umakini.
“Amefariki,” Director akajibu kisha akatupatia picha tatu toka kwenye droo yake. Zilikuwa ni picha za jengo linaloungua kuelekea majivuni.
“Tunaamini alifia humo. Mwili wake ulipatikana ukiwa umejeruhiwa sana, ngumu kutambulika. Hatukuwa na namnna zaidi ya kuufanyia taratibu za kuuzika.”
“Na vipi kuhusu familia yake?” nikamuuliza. “hana mke wala watoto?”
“Hakuwa na mtoto. Alikuwa anaishi na mwanamke ambaye aliachana naye muda mrefu kidogo kabla ya ajali hiyo kutokea.”
“Una picha ya mwanamke huyo?”
“Hapana.”
“Kuna habari yoyote ambayo aliwahi kufikisha kuu ya usalama wa Raisi?”
“Hamna habari ya kushtua. Zilikuwa ni habari za kawaida kutokana tu na majukumu yake.”
“Nino chanzo cha ajali yake hiyo? Mmechunguza mkajua?”
“Kwa mujibu wa wataalamu, ni ajali ya gesi. Bwana huyo alikuwa akitumia gesi kupikia.”
“Kabla ya ajali hiyo, hakuna dalili au mabadiliko yoyote ambayo bwana huyo aliyaonyesha?”
Director akabinua mdomo na kutikisa kichwa. Akaongezea, “alikuwa ni mfanyakazi mzuri sana. Sidhani kama anastahili kutiliwa shaka.”
“Vipi kuhusu bwana ---” nikasita. Niliona si stara kuntambulisha bwana O’neil. Kwa namna hiyo niliona ni kheri nikanyamaza kama ambavyo yeye alivyokuwa anahitaji. Faragha ya maisha yake.
Basi tukaaga na kwenda zetu.
***
Saa tatu usiku, Mgahawa wa Lemaire, Virginia.
Mezani nilikuwa na Jack Pyong na mchumba wake, Violette. Tulifika hapo muda si mrefu na hata bado hatukuwa tumeagiza chochote toka kwa mhudumu. Wakati Jack anaangaza macho yake, nikamuuliza, “kwanini mgahawa huu, Jack?”
“mzuri!” akanijibu kifupi na kisha akaniuliza, “kwani kuna tatizo bwana Tony?”
“Hapana, ila ni kama vile hamna mgahawa mwingine ndani ya jiji hili.”
“Tony, hapa kakuita nani?”
“Wewe!”
“Na mimi ndiye ntalipia bills, shida yako nini?”
“Kwani nilikuomba uniite?”
“Sasa mbona ukaja?”
Kabla sijajibu, jibu ambalo natumai lingemkera, mhudumu akawa amefika hapo. Mdada mrembo mwenye tabasamu usoni.
“Naweza kuwasaidia?”
Tukamuagiza chakula, nami angalau kinyongo changu kifuani dhidi ya Jack kikawa kimekauka.
“Nadhani sasa hivi ungekuwa kwenye kitanda chako cha baridi umejikunyata. Si ndiyo Tony?” Jack akan’chokoza. Sikutaka kumjibu. Chakula kilikuwa kitamu kuliko maneno yake ya kijinga. Huenda hii ndo’ ikawa sababu yake kupendelea mgahawa huu, chakula cha moto na kitamu.
“Maisha ya upweke mabaya sana Jack,” akaendelea kuhororoja. “inabidi ufanye namna uwe na pa kupumzikia!” hapa Violette akamwonya juu ya mdomo wake lakini nikijua ni kazi bure maana Jack hatosikia.
Uzuri sikujali, na kulikuwa na sababu nyingine ya kunifanya nimpuuzie. Chakula. Niliujaza mdomo wangu chakula, nikatafuna nikitazama wateja wengine waliofika hapo.
Sikukaa muda mrefu, nikasikia sauti ya mtu akikokota viatu vyake. Kabla sijageuka, sauti hiyo ikakoma na mara kutazama, mtu akaniangukia, nikawahi kumdaka! Naye Jack Pyong akainama kama aliyetaka kumdaka. Kumtazama mtu huyo, nikamkumbuka! Alikuwa ni yule mwanamke niliyekutana naye kule Hong Kong!
Nikiwa katika mshangao huo, mara nikashuhudia Jack Pyong akipiga magoti na kufunua kidude kidogo cha rangi ya zambarau. Akiwa amemtazama Violette, akamwambia, “Utakubali kuwa mke wangu?”
Violette alikuwa amepigwa na duwaa. Hakutegemea kile kitu. Hata mimi sikutaraji kabisa. Na hapa ndipo nilipofahamu ya kuwa mwanamke yule ambaye tulikutana naye Hong Kong, ndiye aliyeleta pete ile. Kwahiyo, Jack alikuwa ametufanyia surprise watu wawili kwa mpigo!
Akakumbatiana na Violette na sisi, mimi na yule mwanamke mgeni, tukaishia kupiga makofi na kuwapongeza.
“Jack, uliwezaje kuliweka siri hili hata kwangu?”
Akatabasamu. “Nilipanga kukwambia, ila niliona nawe uwe ni miongoni mwa watakaoshangazwa. Vipi? Nadhani umependa wazo langu sio?”
Nikamtazama yule mwanamke kando yangu. Alikuwa ndiye yuleyule. Macho makubwa, nywele nyeusi. Hakika alikuwa anavutia. Na kwa namna alivyokuwa ananitazama alinifanya nihisi maungio yangu ya mwili hayafanyi kazi.
“Umekuja kufanya nini Marekani?” nikamuuliza. Akan’tazama na kutabasamu.
“Kutalii.”
“Kweli?”
“Ndio! Kwani haiwezekani? Au Marekani si sehemu ya kutalii kama Hong Kong?”
“Ni majuzi tu umetoka Hong Kong, itawezekanaje uwe huku kutalii?”
Akamtazama mhudumu aliyekuwa amefika hapo, akamwagiza kinywaji na kisha akan’tazama kuendeleza soga.
“Nimekuja kusoma, Tony.”
“Na unajua jina langu!”
Akacheka kidogo akifunika kinywa chake. “kwanini nisijue. Uliniambia mwenyewe? .. aah sasa naamini siku ile ilikuwa ni pombe ipo kichwani sio?”
“Siku gani?”
“Kule Hong Kong kwenye party!”
“Tulitambushana mimi na wewe?”
“Maskini Tony. Ilikuwa ni mara yako ya kwanza kunywa?”
“Yah! Kama si huyu fala, nisingegusa kilevi!” nikasema nikimtazama Jack Pyong.
“Kwahiyo haukumbuki hata kama ulinibusu na kunikumbatia?”
“Nilifanya hivyo?” Nikauliza nikikodoa. Akacheka tena akifumba mdomo wake kwa kiganja. “Kipi sasa wakumbuka Tony?”
“Nadhani ni sura yako tu. Hiko kitu hakikutoka kichwani.”
“Kweli, naona.” Alisema hivyo kisha akanitazama akiwa kimya. Kwa muda nikahangaika kutafuta kauli yangu mdomoni. Na kama vile mtu aliyefahamu ‘struggle’ ninayopitia akatabasamu kwambali kisha akaniuliza, “vipi Tony, kuna kitu unataka sema?”
Kabla sijasema jambo, mhudumu akampatia juisi na mrija. Ilikuwa ni juisi baridi ya tufaha. Hapo akanywa mafundo kadhaa kabla hatujaendelea na maongezi yetu machache. Alijitambulisha kwa jina la Kelly na kama alivyoniambia hapo awali, yeye alikuwapo hapo kwa ajili ya kusoma, chuo kikuu cha Harvard kitivo cha sheria.
Nilipotaka kufahamu juu ya wapi alipotokea, akanisihi nisiwe na haraka. Kila kitu kitajulikana taratibu.
“Maisha yangu yapo ‘simple’ and ‘straight’, Tony. Utajua kila kitu ndani ya muda mfupi. Lakini ukiwa ‘interested’.”
Baada ya hapo, Jack Pyong na Violette hawakukaa sana, wakatuaga wanaenda zao. Jack akanikonyeza akiwa anaenda zake.
“Sasa,” Kelly akachokoza mada. “Wewe hauondoki? Unalala hapa nini?”
Nikatabasamu kisha nikatazama saa yangu. Yalikuwa ni majira ya saa tano sasa usiku. Kweli muda ulikuwa umeenda. Nilimtazama Kelly na kumuuliza juu ya makazi yake, akaniambia kuwa amefikia kwenye apartment moja ndani ya Virginia.
“Kwanini Virginia na si Massachusetts huko karibu na chuo cha Harvard?”
Akatabasamu pasipo kuonyesha meno. Mashavu yake yalituna na macho yake kujifinya.
“Kwasababu ndo’ sehemu ambapo nina mwenyeji!”
“Mwenyeji? Hapa Virginia?”
“Ndio.”
“Wapi huko?”
Kabla hajajibu akaingiza mrija mdomoni mwake na kufyonza juisi.
**