Nyimbo za taifa zagoma tena mbele ya rais!

Lipumba ashangazwa Wimbo wa Taifa kugoma Monday, 11 October 2010 08:09
Ray Naluyaga, Sengerema
TUKIO la kutopigw akwa wimbo wa taifa kwenye mechi ya nyumbani baina ya timu ya taifa na Morocco jana kulimgusa mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Prof Ibrahim Lipumba, ambaye alisema ni ishara ya ombwe kubwa la uongozi nchini.
Mechi hiyo ya mashindano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2012, ilichelewa kuanza kutokana na tatizo lililoelezwa la kiufundi baada ya timu zote mbili kusubiri nyimbo zao za taifa kwa muda mrefu, kabla ya refa kuamua mchezo huo uanze.

Mashabiki walioonekana kukerwa na tukio hilo ambalo pia lilitokea wakati wa mechi ya kirafiki baina ya Taifa Stars na Brazil, waliamua kuimba wenyewe wimbo huo.
Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi kwenye mechi hiyo na alionekana kukerwa na kitendo hicho kilichotokea kwa mara ya pili mbele yake. Baadaye, afisa habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Florian Kaijage alitangaza kuwa tatizo hilo lilikuwa la kiufundi na hivyo nyimbo hizo mbili kupigwa mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sima wilayani Sengerema, Prof Lipumba alisema kuwa wimbo huo wa taifa haukupigwa pamoja na rais kuwepo uwanjani kutokana na ombwe la uongozi nchini.

“Kwa sababu ya kuwepo kwa ombwe la uongozi, hakuna mipango madhubuti ya uendeshaji wa nchi... CUF imekua ikizungumzia kwa muda mrefu sasa tatizo hili. Serikali ya CCM ilishindwa kulielekeza Jeshi la Polisi kwamba katika shughuli kama ile wimbo wa taifa ulitakiwa kupigwa,” alisema Lipumba.
Awali wimbo wa taifa ulikuwa ukipigwa na bendi ya brass kutoka Jeshi la Polisi au Jeshi la Wananchi, lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia wimbo sasa huchezwa kwenye kaseti au CD, ambazo zimekuwa zikikwamakwamba na kuwa karaha mbele ya wageni.

Prof Lipumba aliongeza kuwa Kikwete bado ni rais wa Jamhuri ya Muungano hadi Oktoba 31, hivyo ni jambo lisilo la kawaida kwa wimbo wa taifa kutopigwa wakati rais amehudhuria shughuli kubwa kama hiyo.
Huku akitumia mapungufu hayo kama moja ya sababu za yeye kuamua
kugombea tena urais, Prof Lipumba alisema kuwa kwa kutopigwa Wimbo wa Taifa ni kuwadhalilisha Watanzania na utaifa wao na ni sababu tosha ya kutoipigia kura CCM na Kikwete.

Lipumba aliwaeleza wakazi wa kijiji hicho kilichoko katika Kata ya
Sima kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) inapashwa imchunguze mgombea ubunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja akituhumu kuwa mazingira ya kubaki kwake pekee kugombea kiti hicho yana kila dalili za rushwa.
Aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF, Mbaraka Sadi aliiambia Mwananchi kuwa kuenguliwa kwake kunatokana na hujuma alizodai alifanyiwa na mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Erika Msika.

Sadi alisema kuwa pingamizi alilowekewa na Ngeleja linahusu yeye kutojaza fomu ya maadili na liliwekwa wakati mkurugenzi huyo wa
uchaguzi alipokuwa ameshapokea fomu zake na kuweka sahihi kwamba
zimekamilika na kujazwa kikamilifu.

“Nilipopata batua ya pingamizi niliijibu kwa kuweleza kwamba kitendo
cha yeye mkurugenzi wa uchaguzi kuzipokea na kuweka sahihi yake ni ushahidi tosha kwamba fomu hizo zilikuwa zimekamilika,” alisema Sadi.
Nililalamika pia katika barua yangu ya majibu ya pingamizi kuwa jinalangu ni Mbaraka Sadi na si Mbaraka Saidi kama alivyokuwa ameandika
Ngeleja, lakini sikusikilizwa na mwisho wake maelezo yangu yalitupiliwa mbali na pingamizi la Ngeleja kupitishwa.

Hata hivyo, Sadi alisema kuwa sheria na kanuni za uchaguzi zinaelekeza
kwamba iwapo mgombea hatajaza fomu ya maadili, adhabu yake ni
kulipa faini ya Sh100,000 au kucheleweshwa kuanza kampeni.Sadi aliendelea kusema kuwa alikata rufaa kwa Tume ya Uchaguzi (Nec)
kuhusu kuenguliwa kwake na kwamba alitumia hoja ile ile ya fomu zake kupokelewa na kuwekwa sahihi na mkurugenzi wa uchaguzi.

Alilieleza Mwananchi kuwa baada ya kujaza fomu zake za rufaa,
mkurugenzi huyo alimshawishi asitumie hoja ya kupokelewa na kukubaliwa kwa fomu zake kama msingi wa rufaa yake bali akubali kwamba hakujaza fomu za maadili na yeye angemsaidia rufaa yake ishinde Nec.Kwa mujibu wa Sadi, alikataa kufanya hivyo jambo ambalo lilimchukiza
mkurugenzi huyo na kuahidi kuwa hatoshinda rufaa yake.

“Pamoja na kwamba barua ya kunijulisha kuwa nimeshindwa katika rufaa hiyo ilifika mapema, ilimchukua mkurugenzi huyo wiki tatu
kunifahamisha matokeo ya rufaa hiyo,” alisema Sadi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom