Jamani hii nchi visiasa vitatuangamiza. Angalia taarifa ya hatari ya kufilisika mifulo ya jamii.Na kutokana na madeni ndio maana serikali inawazuia watu wasipate mafao kabla ya muda wa kustaafu. Chadema na vyama vya wafanyakazi jipangeni kupinga
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uko hatarini kufilisika na
kupoteza fedha za wanachama wake.
Hii inatokana na serikali kushindwa kurejesha katika mfuko huu, mabilioni
ya shilingi iliyokopa au kudhamini katika miradi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) ya 2010/2011, fedha za wanachama, hata katika mifuko mingine ya
jamii, ziko hatarini kupotea.
Mbali na NSSF, mifuko mingine inayotajwa kuwa katika hatari hiyo ni Mfuko
wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF); Mfuko wa Wafanyakazi wa Serikali
Kuu (PSPF), Mfuko wa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa
Bima ya Afya (NHIF).
Kulingana na taarifa ya CAG, sehemu kubwa ya fedha za wanachama ambazo
hazijarejeshwa, zilikopeshwa kwa serikali kwa ajili ya ujenzi wa Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Katika chuo hiki, NSSF peke yake iliingiza Sh. 234.1 bilioni. Mifuko
iliyosalia ilitoa jumla ya Sh. 181.3 bilioni.
Katika ujenzi wa UDOM, PPF ilitoa Sh. 39.99 bilioni, PSPF (Sh. 105.9
bilioni), LAPF (Sh. 22 bilioni) na NHIF (Sh. 13.4 bilioni). Fedha hizo na
riba yake hazijarejeshwa.
Ripoti ya CAG, Ludovick Utouh, inasema kutorejeshwa kwa mikopo hiyo,
iliyochukuliwa au kudhaminiwa na serikali, ni kinyume cha sheria ya
udhamini ya mwaka 1974.
Kutolipika kwa mikopo hii iliyodhaminiwa na serikali kunaiweka mifuko
hii ya hifadhi katika hatari ya kupoteza fedha za wanachama na kuhatarisha
uwezo wa mifuko kufanya uwekezaji zaidi, anasema na kuongeza:
Kushindwa kulipa madeni taasisi hizi ambazo baadhi yake zilipata
udhamini wa serikali, kunatia shaka iwapo upembuzi wa kina wa wakopaji
ulifanywa na mifuko ya kijamii kabla ya kutoa mikopo hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau hakupatikana kwa maelezo kuwa
alikuwa kwenye mkutano mkoani Mbeya.
Lakini Meneja Kiongozi Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume amesema mikopo kwa
serikali imetolewa kwa uangalifu na inalipwa bila matatizo na kwa misingi
ya kibiashara.
Mikataba ya kisheria imesainiwa kukidhi mazingira mbalimbali ikiwa ni
pamoja na iwapo itacheleweshwa
. Hakuna hatari yoyote ya fedha kutolipwa
wala kupoteza fedha za wateja, amesema Chiume.
Lakini CAG katika taarifa yake ya kurasa 183, anasema, Ukubwa wa
kibiashara kati ya serikali na mifuko unatia shaka kutokana na kusuasua
kwa serikali katika ulipaji madeni yake. Hii inahatarisha uendelevu wa
mifuko hii.
Katika ukaguzi wake, CAG amebaini kuwa NSSF ilitoa Sh. 234.1 bilioni kwa
mradi wa UDOM, lakini mkataba uliosainiwa ni wa Sh. 35.2 bilioni tu. Hii
ni hatari kwa fedha za wafanyakazi na wastaafu.
Akifafanua suala la fedha kwenye mkataba kutofautiana na fedha
zilizotolewa, Chiume alisema mkataba ulitakiwa kuwa mmoja ambao ulisainiwa
wakati wa awamu ya kwanza.
Chiume alisema kwa awamu ya pili, kilichotakiwa ni kusaini addendum
(makubaliano ya nyongeza), ambayo yako mbioni kukamilika.
Utouh anaripoti, Majengo kwa ajili ya awamu ya kwanza yalikamilika na
kuwekwa katika matumizi mwezi Septemba 2008. Mpaka wakati wa ukaguzi
2010/2011, mfuko ulikuwa haujafanikiwa kukusanya malipo ya pango kutoka
serikalini.
Kwa msingi huo, hadi sasa limbikizo la riba limefika thamani ya Sh. 14
bilioni, anasema Utouh.
Mkopo huo ulitolewa kwa utaratibu wa kubuni, kujenga, kumiliki na
kuhamisha ambapo mfuko ungepokea kodi iliyokokotolewa kwa riba ya asilimia
15 kwa kipindi cha miaka kumi.
Vilevile CAG amebaini kuwa majengo yaliyojengwa kwa mkopo huo, hayako
kwenye vitabu vya UDOM wala katika vitabu vya NSSF, kutokana na uelewa
tofauti uliopo kati ya pande mbili zinazohusika.
Kuna mikanganyiko katika uelewa kwa serikali na mifuko ya hifadhi,
ameeleza CAG. Wakati mifuko inasema fedha zilizotumika kujenga majengo
hayo zilikuwa mikopo kwa serikali, yenyewe serikali inadai fedha hizo ni
uwekezaji wa kawaida wa mifuko hiyo.
Mbali na UDOM, serikali pia haijalipa jumla ya Sh. 19.77 bilioni
zilizotumika katika ujenzi wa ukumbi wa bunge, ambazo hazilipwi kulingana
na makubaliano. Hadi wakati wa ukaguzi, NSSF ilikuwa inadai Sh. 8.96
bilioni, PPF (Sh. 7.9 na LAPF Sh. 2.91.
Pia upo mkopo mwingine wa NSSF wa Sh. 5.33 bilioni na riba ya asilimia 15
kwa miaka kumi, uliotolewa kwa ajili ya ujenzi wa taasisi ya serikali
ya kiusalama mwaka 2007.
Mfuko mwingine uliowekeza katika mradi huo ni PSPF uliotoa Sh. 6.4 bilioni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NSSF kwa udhamini wa serikali ilikopesha
taasisi kwa shughuli mbalimbali.
Kwa mfano, ujenzi wa nyumba za polisi kwa Sh. 20 bilioni na Sh. 12. 9
bilioni kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 2007 kwa ajili ya
ujenzi wa Machinga Complex, Ilala.
Hadi sasa hakuna malipo ya riba wala sehemu ya mkopo hiyo yaliyofanywa.
Hii ni kinyume cha mkataba, inasema sehemu ya ripoti ya CAG.
Kwa upande wa Machinga Complex, hadi tarehe 30 Juni 2011, mkopo na riba
yake ulikuwa umefikia Sh. 15.3 bilioni.
Ripoti ya CAG imeainisha pia mikopo mingine ambayo hailipwi kulingana na
mikataba ya mifuko hiyo, bila ya kutaja viwango vyake.
Mikopo hiyo ni iliyotolewa kwa Continental Venture (T) Limited, Meditech
Industrial Co. Ltd, General Tyre (GT), Kiwanda cha Sukari Kagera, Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani
Mbeya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio amesema hajaona
ripoti ya CAG na yuko safarini Tanga.
Hata hivyo amedokeza kuwa hivi karibuni walikaa na CAG kujadili suala hilo
na kubaini makosa ya kifundi katika uhasibu baina ya mifuko na serikali
katika ujenzi wa UDOM; hivyo CAG kuahidi kuyashughulikia kwa upande wa
serikali.
Alipoulizwa ni makosa yapi hayo, Erio alimtaka mwandishi awasiliane na
kaimu wake, Stephen Alfred ambaye ilielezwa kuwa yuko kwenye mkutano. Hadi
tunakwenda mitamboni, Alfred hakupatikana.