PAYE
JF-Expert Member
- Jun 19, 2025
- 386
- 492
View: https://www.youtube.com/live/a3BDmRIzhv0?si=JH8Q9Wvv6d01j_Gq
Ijumaa, tarehe 10 Aprili 2026, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles Kichere, aliwasilisha Bungeni taarifa ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kwa mwaka wa fedha 2024/25, baada ya kuikabidhi kwa Rais tarehe 30 Machi 2026. Sisi, ACT Wazalendo tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini.
Katika uchambuzi wetu, tumeona zipo hoja nyingi za ukaguzi zinajirudiarudia mwaka hadi mwaka. Aidha, katika kipindi cha miaka mitano ya uchambuzi wetu, yaani mwaka wa fedha 2020/21, 2021/22, 2022/23, 2023/24 na 2024/25 tuliibua hoja 50 kutoka katika ripoti za CAG, ambapo tumeona nyingi zikijirudia bila kuchukuliwa hatua za msingi za kuwawajibisha wahusika.
Wakati ambapo Bunge lipo kwenye mgogoro wa uhalali kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya uwakilishi wa wananchi na usimamizi wa Serikali, ACT Wazalendo tunaendelea kutekeleza wajibu wetu wa kuwawakilisha wananchi kwa kuitumia ripoti ya CAG kuanika uozo, ubadhirifu na uzembe.
Uchambuzi wa Ripoti ya CAG mwaka 2024/25 ACT Wazalendo, kupitia uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG mwaka 2024/25, tumebaini hoja/ mambo kumi (10) muhimu ambayo tumekusudia kuwaeleza Watanzania na kuyatolea mapendekezo na miongozo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
1. Ubadhirifu na Upotevu wa Fedha za Umma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2024/25, imebainisha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha ubadhirifu, upotevu wa fedha, matumizi yasiyofuata sheria, na udhaifu wa usimamizi wa fedha za umma wenye thamani ya Sh. trilioni 7, sawa na ongezeka la asilimia 173.4 ikilinganishwa na ubadhirifu wa mwaka wa fedha 2023/24 ambao ulikuwa shilingi trilioni 2.56. Fedha hizi zenye hoja ya ubadhirifu ni sawa na asilimia 13.7 ya bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2024/25.
Katika uchambuzi wetu wa Ripoti nne (4) za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaani; Ripoti ya Serikali Kuu (MDA), Miradi ya Maendeleo, TAMISEMI na Mashirika ya Umma, hoja kuu za ubadhirifu na upotevu wa fedha zimeainishwa kama ifuatavyo:
ii. Upotevu mkubwa wa mapato kwasababu ya kuibwa au kutokusanywa kwa ushuru, ada, kodi na mapato yasiyo ya kodi. Jumla ya upotevu huu ni takribani Sh. trilioni 3.21 Fedha maalum zilizokusanywa lakini hazikuwasilishwa kwenye mifuko husika zenye thamani ya takribani Sh. trilioni 1.48, zikiwemo fedha za matengenezo ya barabara kupitia Mfuko wa Bodi ya Barabara, Fedha za maendeleo ya miundombinu ya reli kupitia Shirika la Reli (TRC), fedha za miradi ya maji kupitia Mfuko wa Taifa wa Maji, na fedha za nishati vijijini kupitia REA.
iii. Matumizi yasiyoidhinishwa, malipo bila nyaraka, matumizi yasiyo sahihi na malipo yasiyokidhi viwango vya kisheria. Jumla yake ni Sh. bilioni 115.25
iv. Ukiukwaji wa sheria, taratibu za manunuzi na usimamizi wa fedha (Zabuni kutofuata sheria, mikataba bila idhini, single sourcing isiyo halali, na udhaifu wa mifumo ya udhibiti). Hoja hii ina jumla ya thamani ya Sh.bilioni 243.77
v. Ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi yasiyo na tija. Jumla fedha zilizoliwa kwa ushahidi wa wazi ni Sh. bilioni 500.9 vi. Ucheleweshaji, utelekezaji na kusuasua kwa miradi ya maendeleo (Miradi ya maji, miundombinu, afya, elimu, reli na ujenzi kuchelewa au kushindwa kukamilika kwa wakati). Hasara ya jumla ni Sh. bilioni 783.60 Aidha, Upotevu wa mapato, ubadhirifu, matumizi yasiyo sahihi, ucheleweshaji wa malipo na udhaifu wa usimamizi wa fedha kwa jicho la kisekta; Serikali Kuu imepoteza au kuwa na ubadhirifu wa– Sh. trilioni 2.86; Miradi ya maendeleo ni ubadhirifu wenye thamani ya Sh. bilioni 658.11; Ubadhirifu katika Serikali za Mitaa sawa na– Sh. bilioni 386.35; Na Ubadhirifu katika Mashirika ya Umma – Sh. trilioni 2.42.
Inastaajabisha kwamba badala ya kuhakikisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, katika wakati ambao nchi ina upungufu wa makusanyo ya trilioni 1.45, CCM imeamua kukumbatia ubadhirifu. Ni ubadhirifu kwenye mauzo, manunuzi, mikataba, makusanyo, ruzuku, matumizi, malipo; ni ubadhirifu kila kona. CCM inafanya makusudi kuhakikisha kunakosekana ufanisi katika ukusanyaji wa mapato haya, ili mradi kujitengenezea mianya ya rushwa na ufisadi, unaolenga kuwaneemesha wao na kuwafukarisha watanzania wengi.
Pamoja na kumulika na kuainisha ubadhirifu na upotevu, ACT Wazalendo tunasisitiza mambo yafuatayo:
i. Tunataka watumishi wote wanaohusika na kuwezesha kuwepo na kushamiri kwa vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa mapato wakamatwe na hatua kali za kisheria na kiutawala zichukuliwe;
ii. Tunatoa rai kwa vyombo vya habari na AZAKI kutekeleza wajibu wao wa kimapambano wa kuangazia, kumulika na kuweka hadharani vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma;
iii. Tunaitaka TAKUKURU ishughulike na makosa makubwa ya ufisadi na rushwa kwa uwazi;
iv. Serikali ihakikishe kwamba mifumo ya kielektroniki inafanya kazi kwa ufanisi na wakati wote;
v. Tunautaka umma wa watanzania kutumia ripoti ya CAG kuwahoji kuwakosoa, kuwazomea viongozi wabadhirifu, kupinga ufisadi na kulinda kila shilingi inayotokana na kodi zetu. ACT Wazalendo hatutokaa kimya na kubaki kuwa mashuhuda wakati fedha za umma zinaliwa, miradi ya maendeleo inatelekezwa na Watanzania wanaumia na kuteketea.
2. Kasi Hatari ya Kuongezeka kwa Deni la Taifa na Athari Zake kwa Maendeleo ya Wananchi Katika ripoti ya mwaka 2024/25, deni la taifa limefikia Sh. trilioni 110.55 kutoka Sh. trilioni 97.35 mwaka uliopita, ongezeko la zaidi ya Sh. trilioni 12.70 (asilimia 13.04) ndani ya mwaka mmoja tu. Hata hivyo, tathmini za karibuni zinaonesha kuwa hadi Februari 2026 deni limepanda zaidi na kufikia takriban Sh. trilioni 115.2. Hii ni kasi hatari ya kukua kwa deni ambayo inaweka mzigo mkubwa kwa uchumi na mustakabali wa taifa.
Kwa miaka mitano sasa ya uongozi wa Rais Samia, serikali imekopa jumla ya Sh. trilioni 58.18 kati ya hizo Sh. trilioni 38.7 ni mikopo ya msingi na Sh. trilioni 19.48 ni riba. Hii ina maana taifa linaingia kwenye mzunguko wa kukopa ili kulipa madeni ya zamani, badala ya kuwekeza kwa tija kwa wananchi. Viashiria muhimu vya uchumi vinaonesha uwiano wa kulipa deni kwa mapato unaelekea kufikia viwango vya juu vinavyotambuliwa kimataifa kama hatari. Uhalisia wa hali hii unaonekana moja kwa moja kwenye matumizi ya kila mwezi ya serikali.
Kwa mfano, Januari 2026 serikali ilikusanya takribani Sh. trilioni 2.8, lakini karibu Sh. trilioni 1.2 zilitumika kulipa deni. Kwa wastani, kati ya Sh. trilioni 1 hadi 1.3 hulipwa kila mwezi kwa ajili ya deni. Hii ina maana sehemu kubwa ya kodi za wananchi inaishia benki na wadai, badala ya kuboresha maisha yao. Takwimu za ukaguzi zinaonesha picha hiyo hiyo kati ya Sh. trilioni 30.4 za mapato ya ndani, Sh. trilioni 18 zilienda kwenye kulipa deni na matumizi mengineyo, huku Sh. trilioni 10.35 zikienda kwenye mishahara. Wakati Sh.trilioni 2.05 pekee inaenda kwa wananchi.
Kwa lugha rahisi, kila Sh. 100 inayokusanywa, Sh. 93.3 inaenda kulipa deni na matumizi ya serikali, na Sh. 6.7 pekee ndiyo inaelekezwa kwenye maendeleo. Kutokana na mapato ya ndani yote kuelekezwa kwenye kugharamia deni na matumizi. Fedha kwa ajili ya Miradi ya maendeleo ilitengewa Sh. trilioni 15.6 kwa mwaka 2024/25 ilitokana na mikopo.
Athari za mzigo huu wa madeni ni kubwa kwa wananchi wa kawaida; Fedha zinazopaswa kwenda kujenga shule, hospitali, maji safi na barabara zinamezwa na kulipa riba ya madeni. Serikali kwa kutumia sehemu kubwa ya mapato kulipa madeni, inashindwa
kuwekeza katika huduma za kijamii zinazogusa maisha ya kila Mtanzania. Badala ya kutoa huduma bora, tunajikuta tukilipa kwa makosa ya maamuzi ya kifisadi na matumizi holela ya serikali iliyojiweka madarakani kwa mabavu. Kutokana na uchambuzi wetu katika suala hili nyeti, ACT Wazalendo tunasisitiza yafuatayo:
i. Serikali izibe mianya ya upotevu fedha na matumizi mabaya yanayongeza ukuaji wa deni na maumivu kwa wananchi.
ii. Serikali iache kuhadaa wananchi kuhusiana na hali halisi ya deni la serikali kwa kuwa deni halitoshi kutazamwa katika jicho la kiuchumi wa jumla jumla pasipo kuangalia hoja za kina za siasauchumi na kijamii.
iii. Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ufanisi katika makusanyo ya ndani, ili kujiwekeza zaidi katika uchumi unaojitegemea. iv. Nidhamu ya matumizi na mipango ya fedha lazima izingatiwe, na kuachana na tabia ya kukopa kupita kiasi bila mkakati madhubuti. ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba serikali ya CCM imeshindwa kutoa suluhu na mbadala wa kiuchumi.
3. Hatari ya Kupotea kwa Mapato kutokana na Mrundikano wa Rufaa za Kodi zenye thamani ya Sh. Trilioni 10.75 Uchambuzi wetu katika ripoti ya CAG 2024/25 umeonesha kuwa Serikali inakabiliwa na hatari kubwa ya kupoteza mapato ya umma kutokana na ongezeko la kasi la migogoro ya kodi ambayo haijatatuliwa. Jumla ya mapato yanayobishaniwa katika rufaa za kodi yamefikia takribani Sh. trilioni 10.75 kiasi kikubwa ambacho