Not in our name | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Not in our name

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mwiba, Nov 12, 2008.

 1. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #1
  Nov 12, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  •Zanzibar ni nchi ndani na nje ya Tanzania
  •Hatukuchanganya utaifa bali uraia
  •Mjadala haujafungwa, bado unaendelea
  •Zanzibar daima…jana, leo na kesho

  Na Mohammed Khelef Ghassani


  Kuelekea uvamizi wa Uingereza na Marekani dhidi ya Iraq, mwaka 2003, waandamanaji waliokuwa wakipinga uvamizi huo jijini London walibeba bango linalosomeka: “No, Blair. Not in our name!”

  Waandamaji hawa walikuwa wakimkana aliyekuwa Waziri Mkuu wao, Tony Blair, ambaye alikuwa ameshirikiana na Rais wa Marekani, George Bush, kushinikiza kwamba uvamizi huo ungelikuwa ni kwa maslahi ya kiulinzi na kiusalama si kwa mataifa yao tu, bali pia kwa dunia. Walikuwa wakipeleka ujumbe wao kwamba wao – kama Waingereza – hawampi idhini ya kufanya uvamizi huo.

  Hata hivyo, Blair hakusikia. Akaiingiza Uingereza vitani, vita ambavyo hadi sasa vinaendelea vikiwa na hasara kubwa ya kijamii. kisiasa na kiuchumi kwa Iraq, Uingereza, Marekani na kwa ulimwengu mzima. Na yeye mwenyewe, Blair, sasa si tena Waziri Mkuu maana alilazimika kuondoka madarakani kabla ya wakati wake kumalizika kwa kile kinachoaminika kuwa ni dhima yake kwenye uvamizi huo. Blair aliiaibisha hishima ya Uingereza!


  Mimi leo naandika kama muandamanaji katikati ya kundi la maelfu ya Wazanzibari wenzangu nikiwa nimeshikilia bango linalosomeka: “No Nahodha, not in our name!” Ndiyo, Wazanzibari tunaandamana; na lengo la maandamano haya ya amani ni kulikana tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) lililotolewa na Waziri Kiongozi wake, Shamsi Vuai Nahodha, kwenye Baraza la Wawakilishi Ijumaa Oktoba 24, 2008. Tunalikana kwa kuwa haliwakilishi mtazamo wetu, Wazanzibari, halina maslahi nasi na, kwa hivyo, tumeameamua kutokulitambua. Natazamia kuwa, kama walivyofanya Waingereza, na sisi tutaiadhibu serikali hii kwa kutuendea kinyume!


  Katika tamko lake, SMZ kupitia Waziri Kiongozi Nahodha, inasema kwamba inakubaliana moja kwa moja na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Bungeni Agosti 21, 2008, ambayo iliitaja Zanzibar kama nchi ndani ya mipaka ya Tanzania, lakini siyo nchi nje ya mipaka hiyo. Tamko linasema pia kwamba, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, Zanzibar na Tanganyika (tamko linaitaja kama Tanzania Bara, ingawa mwaka huo hakukuwa na nchi yenye jina hilo) zilichanganya utaifa wake katika Muungano wa 1964 na hivyo katika uso wa kimataifa, kuna utambulisho wa Tanzania tu na sio wa Zanzibar wala wa Tanganyika. Tamko linasema, kwa hivyo, kauli hii ya Rais Kikwete inajitosheleza na hakuna haja ya kuongeza la ziada. Hilo ndilo tamko la SMZ!


  Lakini, kama nishavyotanguliza kusema, hilo si tamko letu, Wazanzibari. Sisi, kwa wingi na umoja wetu, tunasema kwamba, pamoja na mapungufu ya kimuundo na kikatiba, nchi yetu ni nchi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nje ya mipaka hiyo kwa yale mambo yote yasiyokuwa ya Muungano. Hili ndilo tamko letu.


  Kwa nini hatulitambui tamko la SMZ na kwa nini tutoe tamko letu wenyewe? Kwa uchache, sisi Wazanzibari tuna sababu tatu za kutokulitambua tamko la SMZ. Ya kwanza ni kwa kuwa limedanganya kwa kusema kuwa Zanzibar na Tanganyika zilisalimisha utaifa wake kwa Jamhuri ya Muungano na hivyo hakuna lolote kati ya mataifa hayo linalotambulika sasa kimataifa. Si kweli kwamba mwaka 1964 Zanzibar ilichanganya utaifa (nationality) wake na Tanganyika. Mkataba wa Muungano, ambao unatajwa na tamko hilo la SMZ kama kigezo cha hoja yake, hausemi hivyo. Badala yake tulichochangiana katika Muungano huu ni uraia (citizenship). Kwa tafsiri ya taifa, utaifa hauwezi kuchanganywa – au angalau tuseme kwa mfano wa kwetu, hatukutaka kuuchanganya.


  Taifa ni eneo lenye mipaka inayotambulika na ambayo ndani yake muna watu wanaotambuliwa kwa utamaduni na historia yao kuwa wamoja. Zanzibar ilikuwa, imeendelea kuwa na itaendelea kuwa taifa kwa tafsiri hiyo; na Tanganyika hali kadhalika. Maana watu wa pande zote mbili, wanatambulika na wenyewe wanajitambua kwa tamaduni na historia zao. Wanauhisi uwapo (essence) wao na kuwapo (existence) kwao kama wao.


  Tunajua kuwa pana tafauti katika kuzielezea hisia za utaifa kati ya Watanganyika na Wazanzibari. Kutokana na sababu ambazo sisi Wazanzibari tunazitilia shaka, Watanganyika wengi hawako wazi kuhusu Utanganyika wao. Hata wanapofanya sherehe za Uhuru wa 1961, husema kwamba wanaadhimisha siku ya uhuru wa Tanzania! Lakini Tanzania haikuwapo mwaka 1961. Tanzania haijawahi kutawaliwa na hivyo haijawahi kupata uhuru! Sisi Wazanzibari tuko wazi panapohusika utaifa wetu. Tunazisema waziwazi hisia zetu na hatutafuni maneno kwamba sisi ni Wazanzibari na tunataka tuendelee kubakia hivyo.


  Sababu ni kuwa utaifa ni hisia za kujinasibisha na watu na mahala fulani – kile wanachokiita Waingereza feelings of belongingness – na hisia hizo mahala pake ni katika nyoyo za watu. Hazichukuliki wala hazichanganywi kwa mbinu na hila kama hizi zilizomo kwenye Muungano huu, ambao kila ushahidi wa kihistoria unaonesha kuwa kuundwa kwake kulikusudiwa kuidhibiti Zanzibar na sio kushirikiana nayo kama mwenza mwenye haki sawa kwenye Muungano huu.

  Dhana ya uraia ni tafauti na ya utaifa maana uraia unaweza kusanifiwa kwa hila za kisiasa na hata kijeshi na mwishowe ukawekewa mipaka ya kikatiba. Watu wa mataifa kadhaa ulimwenguni wameshawahi kutenzwa nguvu ili wakubali kuwa raia wa dola fulani. Historia imejaa mifano ya aina hiyo. Falme nyingi za Ulaya, kwa mfano, kabla ya mwaka 1640, zilijitanua na kulazimisha majirani zao kuzitii tawala zao na hivyo kuwafanya kuwa raia zao. Huo ndio mfano wa zilivyokuwa na kutanuka kwa dola za Ufaransa, Ujerumani, Ureno na Ugiriki kwa kutaja mifano michache. Kwa hivyo, uraia unaweza kulazimishwa - na kwa hakika mara nyingi ndivyo inavyokuwa - na dola yenye nguvu kwa watu wa mataifa dhaifu. Katika mfano unaokaribiana na huo, ndipo nasi tukachangiana uraia kwenye Muungano huu.


  Hata hivyo, pamoja na ukungu wa shaka na shukuki uliotawala nia na dhamira iliyopo nyuma ya Muungano huu, sisi Wazanzibari tumeendelea - kwa miaka yote hii 44 - kuuhisi na kuukumbatia utaifa wetu wa Zanzibar, yaani Uzanzibari. Kwa hivyo, kwa mfano, mimi na hawa wenzangu tunaoandamana leo tunajitambulisha kwa utaifa wa Uzanzibari, japokuwa hatukatai kwamba kwa uraia sisi ni Watanzania. Kwa kufupisha maneno ni kwamba Uzanzibari wetu tumepewa na Mungu Muumba nchi na mataifa ya wanaadamu na uraia wetu tumepewa na Mkataba wa Muungano wa Sheikh Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere kama unavyosomeka katika kifungu chake cha iv (f).


  Sababu ya pili ya kutolitambua tamko la SMZ ni vile kujengwa kwake juu ya msingi wa hotuba ya Rais Kikwete ya Agosti 21 Bungeni, ambayo mara tu baada ya kuitoa tulisema kwamba ilikuwa imepotea njia. Kwa mfano, katika hotuba hiyo, Rais Kikwete aliitaja Tanganyika kuwa nayo ni nchi ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, jambo ambalo si kweli katika udhahiri wake. Tanganyika haipo hata ndani ya mipaka ya Jamhuri hiyo, maana ni bunge la Tanganyika ndilo lililopitisha Azimio la kuifuta (?) mwaka 1964, siku chache tu baada ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano.


  Kwa hivyo, hadhi ya Zanzibar (nchi iliyo hai) si kama hadhi ya Tanganyika (nchi mfu) katika Muungano huu. Si Mkataba wa Muungano wala Baraza la Mapinduzi, ambalo lilikuwa ndicho chombo cha juu cha kisheria kwa wakati huo kwa upande wa Zanzibar, lililoiua Zanzibar. Kwa hivyo, ikiwa tamko hili limejengwa juu ya msingi uliopotea, ni wazi nalo litakuwa limepotea na sisi hatuwezi kukubali tamko lililopotea liwe ndio mtazamo wetu.


  Na sababu ya tatu ya kutokulitambua tamko la SMZ ni njia ambayo limewasilishwa kwetu. Baraza la Wawakilishi ndicho chombo pekee chenye madaraka makubwa ya kisiasa kwa Zanzibar na ambacho kinawakusanya Wazanzibari wa vyama vyote viwili vikubwa katika nchi ya Zanzibar. Kwa lugha ya kisiasa, tunaweza kusema kwamba Barazani humo ndimo Wazanzibari tunamowakilishwa kama Wazanzibari. Tamko hili limesomwa na mkuu wa shughuli za serikali Barazani, Waziri Kiongozi, katika siku ya mwisho na katika saa za mwisho za kikao cha Baraza hilo, ikijuilikana wazi kwamba wawakilishi wetu wasingelipata muda tena wa kulichangia.


  Kwa nini SMZ ikafanya hivyo? Kwa sababu inajua kuwa hilo si tamko letu Wazanzibari na, hivyo, wawakilishi wetu wangelilipinga kwa nguvu zao zote kama vile walivyoipinga ile kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliyoitangaza nchi yetu kuwa si nchi. Ikiwa kuna chochote kilichopatikana kutokana na tamko hili la SMZ, basi, ni muakisiko wa khofu, woga na kutokujiamini ilikonako SMZ na ambako nako hitimisho lake ni kuwa serikali haituwakilishi sisi, Wazanzibari. Sisi tunakataa kuwa sehemu ya khofu na woga huu usiokuwa na maana, na hivyo tunakataa kulitambua tamko hili la SMZ. Tunasema “Not in our name!”


  Baada ya kuyataja mapungufu hayo ya tamko la SMZ, sasa tuje kwenye ufafanuzi wa tamko hasa la Wazanzibari wenyewe, ambalo kama nilivyolitanguliza ni kuwa Zanzibar yetu ni nchi ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, kwamba sisi hatukuchanganya utaifa na Tanganyika na kwamba mjadala huu bado haujafungwa, na unaendelea.


  Kwa nini Zanzibar iwe ni nchi? Jibu rahisi na la pekee ni kuwa hayo ndiyo matakwa ya sisi wenyewe, Wazanzibari, na ndivyo tulivyoyaeleza kupitia Katiba yetu – ambayo SMZ haina hiari ya kutokuifuata na kuiheshimu, maana viongozi wake waliapa kuilinda – na pia ndiyo matakwa ya msingi wa uhusiano huu baina ya Zanzibar na Tanganyika, yaani Mkataba wa Muungano. Mote muwili humo, Zanzibar inatambuliwa na inasimama kama nchi ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka hiyo kwa yale mambo yote yasiyokuwa ya Muungano.

  Na, kwa hakika, kimsingi mambo hayo yasiyokuwa ya Muungano ni mengi - au yalitakiwa yawe mengi zaidi - ya hayo ya Muungano. Elimu ya msingi na kati, afya, miundombinu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo, na mengineyo mengi, si ya Muungano; na kwayo Zanzibar ina haki na wajibu wa kuyasimamia na hivyo kujiwakilisha kwenye uso wa kimataifa kama Zanzibar inapoyazungumzia.

  Ni bahati mbaya sana ikiwa uongozi wa Zanzibar umeshindwa kufanya hivyo huko nyuma na unashindwa kufanya hivyo sasa, lakini si kwamba ikijiwakilisha kama nchi kwenye masuala hayo Zanzibar itakuwa inakwenda kinyume na Makubaliano ya Muungano, ambayo ndiyo sheria kuu ya Muungano huu!


  Kwa hivyo, Zanzibar ni nchi kwa kuwa ina sifa za kuwa nchi kwa maana ya nchi. Kwa kutumia maneno ya Ismail Jussa, nchi ni “eneo ambalo mipaka yake inafahamika, kwa Kiingereza wangeliita geographical area, ambayo ina wananchi wanaofahamika, population, na ina serikali ambayo inafanya kazi, yaani yenye madaraka – tunazungumzia hapa a functioning government.”


  Zanzibar ina sifa hizo: ina eneo lake linalofahamika, kama lilivyoelezwa katika Ibara ya 2, kifungu kidogo cha 1 cha Katiba ya Zanzibar: “Eneo la Zanzibar ni eneo lote la visiwa vyote vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo vilivyovizunguka na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Zanzibar pia ina wananchi wake, ambao ni sisi Wazanzibari tunaoandamana hapa. Sisi tunajitambua kuwa ni wananchi wa nchi ya Zanzibar na tunaunganishwa na historia na utamaduni wetu. Na vile vile Zanzibar ina serikali inayofanya kazi – au ambayo ilitakiwa ifanye kazi – ya kulinda hadhi, heshima na mipaka ya Zanzibar na kuwaendeleza Wazanzibari. Ikiwa serikali iliyopo inatimiza au haitimizi jukumu hilo ni kitu cha mjadala, lakini nguvu hizo inazo na imepewa na Katiba yetu.


  La kuwa Zanzibar yetu ni nchi, limo Tamko la Kuitangaza katiba yenyewe (Preamble), ambapo inasemwa: “Na kwa kuwa sisi, wananchi wa Zanzibar, tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katka nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya haki, udugu na amani… tumeunda Katiba hii.”


  Kwa hivyo, ikiwa tamko la SMZ linakubaliana na Rais Kikwete ambaye naye alikubaliana na Waziri Mkuu Pinda, basi sisi tunachukulia kuwa wote watatu (Pinda, Kikwete na SMZ) wamekosea. Alianza kukosea Pinda kwa kuitangaza Zanzibar si nchi akitumia Kifungu cha 1 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambacho kinasema kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano” bila ya kuzingatia Katiba ya Zanzibar, ambayo inaitangaza Zanzibar kuwa nchi yenye sifa zote za unchi. Akafuatia kukosea Kikwete kwa kumuunga mkono Pinda na kushadidia kuwa Zanzibar ni nchi kwa ndani na si nchi kwa nje. Na sasa imefuatia kukosea SMZ kwa kumuunga mkono Kikwete na kutokuheshimu Katiba yake yenyewe. Wote kwa pamoja, hoja yao inaporomoka kama mlima wa karata; na sisi tunakataa kuwa sehemu ya kuporomoka huko.  Tunasikitika sana kwamba SMZ, serikali yetu tuliyoipa dhamana ya kuilinda nchi yetu ya Zanzibar na katiba yake, imekubaliana na hoja ya Waziri Mkuu Pinda kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano iko juu ya Katiba ya Zanzibar. Tunasikitika kwa kuwa hivyo si kweli. Ukweli ni kuwa Katiba zote mbili ziko sawa sawa, kila moja ikiongoza taasisi zake katika eneo lake na kwa mamlaka yake. Na juu ya yote, Muungano huu hautawaliwi na katiba hizi mbili, bali Mkataba. Kilichotakiwa kufanywa na Katiba hizi, kwa hivyo, kilikuwa ni kuutafsiri tu Mkataba wa Muungano na sio kuukosoa ama kuurekebisha. Na Mkataba wa Muungano umetangaza kuwepo kwa Jamhuri (republic) moja na sio nchi (country) moja. Kinachoifanya jamhuri kuwa jamhuri hakiizuii nchi kuwa nchi.

  Mkataba haukuzifuta nchi za Zanzibar wala Tanganyika; na wala haziwezi kufutwa na Pinda, Kikwete wala Nahodha, maana kwa kuwa huu ni Mkataba wa Kimataifa, wanahitajika kuwepo wale wale waliokubaliana, ndio waufanyie marekebisho. Katika hali ya sasa ambapo Serikali ya Tanganyika inaambiwa kuwa haipo, maana yake ni kuwa tayari mwenza mmoja wa Mkataba huu hayupo na hivyo mabadiliko hayawezekani - kwa lugha ya kisheria.


  Ikiwa hivyo ndivyo, basi ilivyovisema SMZ katika tamko lake sivyo na wala haviwakilishi ukweli unaotambuliwa na sisi, Wazanzibari, na basi tunakataa kujinasibisha na kosa lililofanywa na serikali iliyopo madarakani hivi sasa Zanzibar. Hatulitambuwi tamko la SMZ kwa kuwa si letu!


  Nimalizie maandamano haya kwa kusisitiza mambo matatu. Kwanza, viongozi wa sasa wa SMZ wamejidhihirisha kwamba hawapo kwa maslahi ya Wazanzibari. Wamefeli kuilinda na kuitetea Katiba ya Zanzibar na hatima ya Uzanzibari. Kufeli huko, kwa hivyo, kunatupa Wazanzibari sababu ya kutosha ya kudhamiria kuwaondoa madarakani kwa kutumia njia tulizokubaliana katika taratibu na sheria zetu, yaani kura. Itakuwa aibu kwa Wazanzibari kuwarudisha tena viongozi hawa hawa katika uchaguzi wowote utakaofanyika kuanzia sasa. Badala yake tuwaweke madarakani watu ambao wana bwana mmoja tu wa kumtumikia, na bwana huyo awe ni sisi Wazanzibari. Tutafanya kosa la makusudi kuwaweka madarakani watu ambao wanaonekana kutumikia mabwana zaidi ya mmoja!


  Pili, kwa kuwa hao waliopo sasa madarakani wametusaliti na wamezisaliti nguvu tulizowapa kusimama kwa ajili yetu na badala yake wamejawa na woga matumboni mwao, basi sisi Wazanzibari wenyewe tunapaswa kuwa imara zaidi sasa kuliko wakati mwengine wowote ule kuilinda na kuitetea Zanzibar yetu. Wakati umefika kwa Mzanzibari kujinasibisha na kujilindia kwa Uzanzibari wake. Tuungane pamoja na tusimruhusu tena adui kusimama katikati yetu na kutuchagulia namna ya kuangaliana wenyewe kwa wenyewe. Mpemba na Muunguja ndiye mmiliki wa Zanzibar na wasifitinishwe tena.


  Na tatu, kwa kuwa tunapaswa kujilinda wenyewe kama Wazanzibari – bila kutegemea serikali iliyopo sasa madarakani – basi tusikubali hata kidogo kuuwa mjadala huu unaondelea wa hadhi na nafasi ya Zanzibar ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Licha ya kuwa Waziri Kiongozi amechagua kuibwaga mada hii kavu kavu na kuepuka kujadiliwa na wawakilishi wetu Barazani, sisi Wazanzibari huku nje ya Baraza tusikubali kufungwa kwa mjadala huu.

  Mjadala upo wazi na tuendelee kuuchangia kwa maslahi ya Zanzibar yetu. Kwamba hatuwezi kuwa na Tanzania imara, kama tuna Zanzibar dhaifu. Mzanzibari hawezi kuipenda Tanzania ikiwa mapenzi yake kwa Zanzibar ni mapungufu. Zanzibar ndipo petu, wala hatuna pengine, katu asitudanganye mtu!

  Hili ndilo tamko la Wazanzibari.

  Zanzibar daima. Jana, leo na kesho.
   
 2. Kibunango

  Kibunango JF-Expert Member

  #2
  Nov 12, 2008
  Joined: Aug 29, 2006
  Messages: 7,639
  Likes Received: 185
  Trophy Points: 160
  Vizuri... si ungeunganisha na ile mada kukuu kuhusu hili
   
 3. Kaizer

  Kaizer JF-Expert Member

  #3
  Nov 12, 2008
  Joined: Sep 16, 2008
  Messages: 24,664
  Likes Received: 1,506
  Trophy Points: 280
  mmmh...napata hisia kuwa hao wanaojiita wazanzibari kuliko waliotoa tamko, hawamtambui hata Rais wa Muungano kwa sababu ametoa tamko linaloend akinyume na ufahamu wao wa utaifa...

  tunarudi kule kule..huu muungano bora uvunjwe tu....
   
 4. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #4
  Nov 13, 2008
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  Sio uvunjwe uvunje kitu kipo,nikimaanisha haupo, lakini tuliokuwa nao sio Muungano kwa faida ya WaTanganyika na WaZanzibari bali ni kwa faida ya wanaolindana walioshika hatamu za nchi na chama chao. Jaribu kuutazama kwa kina Muungano utaiona hio hali.
  Mfano hai siku za chaguzi kuu batalioni za kijeshi hupelekwa Zanzibar kuteka ushindi,na uraisi wa Muungano hutumika wahafidhina kuweka mtu wao ,hapo utaona hata ndani ya CCM huwezi kupata tiketi ya kugombea Uraisi wa Tanzania kama hujulikani ndani yao.Na hadi sasa utaona walio na tamaa ya kuukwaa Uraisi wa Tanzania utaona wamo ndani ya mtandao unaokizunguuka chama na serikali yake.
   
Loading...