Wild Flower
JF-Expert Member
- Jul 20, 2023
- 858
- 1,655
Aliyekuwa Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), marehemu Anastazia Mwamongi (72), aliyekutwa ameuawa kikatili ndani ya nyumba yake na watu wasiojulikana, amezikwa katika makaburi ya Igeleke, yaliyopo Kihesa Kilolo, Manispaa ya Iringa.
Maziko ya marehemu huyo yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji, wakiwemo wanachama wa CHADEMA ambao walitawala eneo hilo kwa sauti za “No Reforms No Election,” huku wakilaani tukio hilo na kudai haki itendeke juu ya tukio hilo. Mwili wa marehemu Mama Mwamongi uligundulika tarehe 20 Julai 2025, baada ya watoto wake kupata wasiwasi kufuatia kushindwa kuwasiliana naye kwa zaidi ya siku nne mfululizo.
Hata hivyo, walipofika nyumbani kwake walikuta nyumba imefungwa, hivyo wakatoa taarifa kwa uongozi wa mtaa ambao ulihusisha vyombo vya dola, ndipo mwili wake ulipokutwa ukiwa umefungiwa ndani ya nyumba hiyo. Akitoa salamu za pole katika maziko hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Iringa Mjini, Frank Nyalusi, amesema kuwa marehemu Anastazia Mwamongi alikuwa ni kiongozi wa mfano kutokana na msimamo na ujasiri wake katika kutetea demokrasia na haki za wananchi.
Marehemu Anastazia Mwamongi alizaliwa Machi 3, 1952. Aliwahi kuwa kiongozi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) mkoani Iringa akikumbukwa kwa ujasiri wake kisiasa na dhamira ya kuwatumikia wananchi. Hadi sasa, chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi.