NJIA NYEMBAMBA -- 03
Mtunzi: SteveMollel
No: 0685 758 123
Assessoko alihitimisha kisha akanyanyuka na kuondoka zake. Akamuacha Kessy akiwa na mawazo, amekaa akiwa kashika tama macho yake yakitizama chini. Kessy alikaa hapo mpaka akaanza kusinzia. Mwishowe alilaza kichwa chake juu ya meza usingizi ukampitia mpaka asubuhi.
*******
Baada ya mlango wa chimbo kufunguliwa, sauti ilisikika;
“Amadu, toka nje!”
Alikuwa ni General Kessy mlangoni akiwa ameshikilia mlango. Amadu akainua uso wake na kutizama kisha akaurudisha uso chini na kuuliza;
“Unahitaji nini, mkuu?”
“Toka nje!”
“Siwezi nikatoka humu ndani kama sitatoka na mwenzangu.”
“Amadu, unanibishia, ama?”
“Tangu lini nikakubishia, mkuu? Sijakataa kutoka ila tu kama nitatoka na mwenzangu.”
“Amadu, nenda tu.” Chui alishauri.
“Hapana. Sitoenda popote bila yako. Ni bora tukaendelea tu kukaa humu.” Amadu alitia msimamo. General akamtizama kwa dakika kama mbili kisha akasema;
“Tokeni nje.”
Amadu pamoja na Chui wakatoka wakaongozana na general kuelekea makao makuu. Wakaketi, General Kessy akaweka chupa ya kilevi na ramani juu ya meza kisha akaanza kuongea;
“Amadu, kwa sasa hali yetu si nzuri huko Sierra. Silaha na majeshi toka Liberia yanatudhoofisa zaidi. Una shauri nini kifanyike?”
“Mkuu, hapo hakuna cha kufanya isipokuwa haya yafuatayo; Mosi, lazima tujue na tuzibe njia zitumikazo kupitishia silaha hizi. Pili, lazima Liberia awe distracted, kwa vyovyote vile inabidi tuhamishe focus yake ya majeshi toka kwetu kwenda sehemu nyingine, na njia rahisi ya kufanya hivyo ni kwa kutumia kundi la Le tueurs.” Amadu akafafanua kwa kujiamini.
“Kuhusu hilo kundi hamna shida naweza nikawapa order wakatii. Ila sasa hizo njia tutazitambuaje?” General aliuliza. Chui akachukua nafasi kutoa maelezo;
“Eneo la Monrovia, Liberia, ndipo penye kambi ya kijeshi iliyokaribu na Sierra Leone. Kwa namna yoyote ndipo patakuwa panasambaza silaha hizi za kijeshi kuja Sierra. Kwahiyo, moja, tunaweza tukaharibu daraja lile la mpakani mwa Sierra na Liberia linalopokea barabara tokea Monrovia ili kukata mawasiliano. Kisha pili, kambi ile ya Monrovia ingeshambuliwa kwa kushtukiza. Na tatu, jeshi la Liberia lingepewa kazi kubwa ya kutetea nchi yake na kuachana kabisa na Sierra.”
“Sasa, hiyo kazi ya kwenda kufumua daraja na kushambulia hiyo kambi, inaweza ikachukua muda gani?” General aliuliza.
“Ndani ya juma moja tu endapo utanipa watu ninaowataka kufanya nao kazi.” Amadu akajibu.
“Unawataka wakina nani?”
“Wale nilioenda nao kuchukua silaha Sulima kasoro Talib.”
“Kingine?”
“Uwe kwenye mawasiliano mazuri na kundi la Le tueurs katika muda huu kwani tutawahitaji kumalizia kazi tutakayoianza huko. Zaidi ya hapo, ni kikosi changu tu.”
“Sawa. Niachie hiyo kazi, jioni wenzako watakuwepo hapa!”
Kweli wakati jua lazama, Mou, Ussein na Farah wakawa tayari wapo makao makuu kukutana na Amadu na Chui. Mipango ikaanza kupangwa juu ya kile cha kufanya, Chui na Amadu wakiwa waelekezaji.
Jua lilipopotea, wanaume wakajiweka kwenye gari na safari ya kuelekea mpakani mwa Sierra na Liberia ikaanza. Ndani ya gari zilipakiwa kreti za bia nne na bunduki za kila mmoja pamoja na maguruneti. Safari hii hawakutumia tena njia ya Sierra Leone, walishika njia ya Guinea wakilenga kuingia Sierra Leone baadae kwa kupitia mji wa Kangama.
Ndani ya lisaa bila ya kupumzika wakawa tayari wamefika mji wa Banian. Baada ya masaa mawili wakafika mji wa Kissidougou, hapo wakaweka kituo wapate kula na kuvuta pumzi. Walipaki gari lao wakaingia mtaani kunyoosha nyoosha miguu huku wakipiga simulizi za hapa na pale. Cheko na tabasamu vikitawala nyuso zao. Walitumia lisaa tu katika huo mji wakarudi kwenye gari na kuendelea na safari. Ilipofika saa sita ya usiku wakawa ndio wanaingia ndani ya nchi ya Sierra Leone ili sasa waambae kutafuta mji wa Sulima wakapate kuharibu daraja. Mita chache wakiwa wameacha mpaka wakakutana na wanaume watano wa uhamiaji, gari likasimamishwa.
“Naombeni pasipoti zenu.” Mwanaume mmoja alisema huku akiwa amekinga mkono wake. Chui akasonya.
“Hivi nyie hamjui hata wenzenu?”
“Wewe ni nani?”
“Mimi ni huyu!” Chui akasema huku akionyeshea kitambulisho chake cha jeshi.
“Mnaelekea wapi usiku huu?”
“Aaah ndugu yangu, kwani hujui kinachoendelea? Tunaelekea Liberia kubeba silaha. Huku Guinea tumetoka kwa shemeji zenu!” Chui alisema kwa sauti yenye utani, wenzake wakaangua kicheko. Wakaruhusiwa kuondoka wakaendelea na safari yao, ndani ya asubuhi ya saa kumi na mbili wakawa tayari wameshafika mji wa Sulima. Waliweka pozi hapo wasome mazingira kwanza. Waliacha gari lao kando sehemu ya kificho kisha wakaanza kutembea tembea maeneo ya Sulima, baadae wakazamia kuingia nchini Liberia kwa kupitia mto wa Mane, wakaenda mpaka Monrovia huko nako wakijifanya wazururaji tu lakini waliokuwa na macho makali kutizama na kukariri mazingira.
Walipotimiza haja zao za moyo, wakarudi nchini Sierra Leone. Walitafuta sehemu ya kupumzikia wakapata nyumba moja ya wageni ya hadhi ya chini, hapo wakakodi vyumba vitatu lakini wakakutania sehemu moja na kuanza kuteta;
“Inabidi tuyarejee hayo mazingira na usiku pia tupate kuona ulinzi wake unakuaje.” Amadu alinena.
“Ni kweli hiko unachokiongea. Sehemu ninazoziona zina shida ni pale kambini kidogo, na hata pale darajani.” Mou alitema neno.
“Ila mimi nina wazo kidogo.” Chui aligusia, wenzake wote wakamuazima macho na masikio.
“Itabidi tujigawanye na kupeana majukumu, sidhani kama itakuwa busara tukaenda wote hasa kipindi hiko cha usiku. Lakini cha muhimu ni kuwa na mawasiliano kati yetu.”
“Wazo zuri!” Amadu akadakia huku akitikisa kichwa. “Au mnaonaje?”
“Kweli, wazo jema.” Wengine wakaliunga mkono.
“Sasa basi tutakachokifanya ni hivi, mimi na Mou tutakwenda mpaka kule kambini, Farah na Chui mtazunguka maeneo ya mtoni na darajani, Ussein utatembelea zile njia za panya tulizozipitia na kuzitizama kwa muda ule. Alafu tutakutana hapa saa nne ya usiku.” Amadu alifafanua mgawanyo. Wenzake wakakubali.
Baadae giza lilipotanda, wanaume wakajigawa na kwenda kutimiza majukumu yao kama vile walivyopeana. Mida ya saa nne ya usiku wakakutana pale pale walipopeana maelekezo kuleta mrejesho.
“Kwangu safi, hakuna shida. Njia zipo vyema hakuna cha kutisha zaidi tu ya walevi walevi kukatiza.” Ussein alielezea eneo lake.
“Kwetu maeneo ya darajani kuna shida kidogo, magari ya jeshi yanapita pita yakielekea na hata kurudi toka Sierra Leone kila baada ya dakika kama kumi na tano.” Chui alitia neno, Amadu naye akatoa majibu ya eneo lao.
“Kwa eneo letu kuna doria ila si ya kutisha. Wanajeshi wanapita wawili wawili, wawili upande wa magharibi na wawili upande wa mashariki. Nadhani doria yao ni hafifu kutokana na kutokuwa na sababu ya kuhofia na eidha kwasababu wapo ndani ya uzio.”
Baada ya hayo maelezo, wakaulizana;
“Muda gani mnaona ni sahihi kufanya tukio?”
“Usiku!” Wote wakajibu. Mipango ikaelezwa na Amadu;
“Kama tulivyojigawa leo, na kesho vile vile. La muhimu sana ni mawasiliano si kingine. Mtabandika mabomu pale madarajani na sisi tutayabandika mule kambini. Tukikutana hapa ndipo tutakapoyafumua. Sawa?”
“Sawa!”
Ngoma inogile kesho yake usiku ilipowasili. Wanaume wakagawana majukumu, Chui na Farah wakawa wa kwanza kutekeleza kazi yao kwa kubandika mabomu chini ya daraja huku Ussein akiwa anang’aza macho yake kwenye vinjia vyake endapo kama kuna lolote litatokea.
Amadu na Mou wakaongozana kwenda kambini. Waliruka ukuta wakaingia ndani kwa tahadhari kubwa. Wakiwa wananyata wakaanza kusogelea maeneo kadha wa kadha na kubandika mabomu toka kwenye mabegi yao waliyoyabebelea mgongoni. Baada ya kubandika maeneo manne, wakakutana na wanajeshi wawili walio doria. Bila ya kutengeneza sauti waliwakaba wanajeshi wale wa doria na kuwaburuzia gizani kisha wakaendelea na kazi yao ya ubandikaji wa mabomu. Walipomaliza waliruka ukuta, walipotua tu wakakutana na wanajeshi wengine wawili, hapo kukawa hamna jinsi. Amadu na Mou wakaachia bunduki zao ziseme na maadui na kufanya sauti za risasi kuvuma! Kisha mbio zikaanza.
“Tunakuja haraka! Kila kitu kipo sawa … Over?” Amadu aliongea na radio call huku wakiwa mbioni na mwenzake.
“Kila kitu kipo sawa … Over!” Sauti ya Chui ikajibu.
“Tunakimbizwa. Nitakapokushtua tu hakikisha unalipua daraja, sawa?”
“Sawa!”
Baada ya lisaa wakiwa wanakimbia Amadu na Mou wakafika darajani na kutoa taarifa kwa Chui, daraja likalipuliwa. Hao wakashika njia ya panya na kutokea eneo lao la mapumziko, wakiwa hapo wakafyatua na mabomu waliyoyapachika kambini mwa jeshi la Liberia kisha wakapanda gari lao na kuanza safari ya kurudi kambini kwao, Guinea.
Njiani Amadu akatoa radio call yake na kumtafuta General akampasha habari kisha akamtaka afanye jambo;
“Mkuu huu ndio wasaa wa Le tueurs kushambulia. Waambie wavamie Monrovia sasa hivi na waiweke kwenye himaya yao. Kama sio sasa, si milele tena.”
Ni ndani ya dakika kadhaa tu, waasi wa kundi la Le tueurs wakajitokeza na kushambulia kambi ya Monrovia wakaiweka himayani. General Kessy akawatafuta wafuasi wake na kuwapasha habari ya mafanikio hayo. Furaha ikatanda miongoni mwao. Walipeana mikono ya kheri ikisindikizwa na macheko na matabasamu. Walifungua vinywaji wakanywa mpaka basi. Baada ya kuzidiwa na kilevi, Amadu ambaye ndiye alikuwa akiendesha gari aliamua apaki kando wapate kupumzika. Wakalala fofofo.
Jua lilipokucha safari ikaendelea na wakati jioni yawasili wakawa tayari wamefika kambini kwao. General akawapokea kwa uso wenye furaha na makumbato makubwa.
“Mmefanya kazi nzuri sana. Mkuu amenipigia simu ameona taarifa ya habari! Raisi wa Liberia amechanganyikiwa, sasa atatulia na yake!”
General alisema kwa bashasha ya furaha. Alileta chupa ya kileo akampa kila mmoja.
“Sasa huu ndio wakati wa kuongeza mashambulizi Sierra Leone, amekuwa yatima sasa.” General aliendelea kumumuya kifuraha. “Shambulizi letu limekuwa msaada mkubwa sana kwa Le tueurs, wamepata pa kuanzia. Hakika watatusaidia sana huko mbeleni tukiwa tupo ndani ya Sierra!”
Baada ya hayo maongezi na vinywaji kumalizika, wakina Amadu waliaga. Ila kabla hawajatoka, General akawapatia bahasha ya kaki. Walipotoka nje wakaifungua na kukuta pesa, wakagawana sawa kwa sawa kisha kila mtu akaelekea upande wake, Amadu pamoja na Chui wakaelekea hemani. Walihifadhi pesa zao na kujilaza kitandani wakawa wanateta;
“Nataka niwatumie wazazi wangu hizo pesa.” Chui alisema huku akimtizama Amadu.
“Usihofu. Kesho mida ya mchana nitakupeleka kwa wakala utume.”
“Nitafurahi sana.”
“Usihofu, ni jambo dogo tu hilo.”
“Nashukuru sana. Nimewakumbuka sana wazazi wangu, nataka tukienda Sierra nikawasalimie.”
“Tutaenda wote, natamani nikusindikize.”
“Nitafurahi mno.”
Baada ya hiyo kauli ghafla sauti ya kengele ikasikika kwanguvu, Amadu akashtuka.
“Kengele ya nini hiyo?”
“Sijui!” Chui alijibu huku naye akiwa na kauso kenye kabumbuwazi. Amadu alitizama saa yake ya mkononi akatikisa kichwa chake na kutabasamu kama vile ameona kitu cha kijinga.
“Ni wakati wa kula kumbe!”
Chui naye akatabasamu. Walinyanyuka wakaenda kupata msosi. Watu walikuwa wanmashangaa Chui, alikuwa ni mpya miongoni mwao. Wengine walishindwa kunyamaza wakamuuliza ni wapi alipotokea wakati wengine wakiyarushia hayo maswali kwa Amadu ambaye ndiye alionekana naye karibu.
“Huyu ni mdogo wangu!” Amadu alimjibu mmoja wa wa mtu aliyemuuliza kisha akatizamana na Chui na kucheka. Walipomaliza kula, Amadu akabebelea chakula kiasi na kumpelekea Ulsher pamoja na mzee Buruwani.
Asubuhi ya saa moja kamili ilipohitimu, kengele ya makutano ikagongwa. Wafuasi wote wakakutana kwenye uwanja wao, Kessy akatoka makao makuu na kwenda kukutana nao. Dhamira kuu ya mkutano ikawa moja tu, kumtambulisha Chui kama mfuasi wao mpya na apewe ushirikiano wote katika kila shughuli ya ukombozi. Lakini zaidi ya hapo, Amadu pamoja na Chui wakaitwa na Kessy waongozane naye kuelekea makao makuu, huko Kessy akawapa kazi mpya ya kufanya.
“Nataka mkavamie shule hizi tatu za msingi. Mkawateke watoto wa kutosha muwalete hapa. Tunahitaji kuongeza ukubwa wa jeshi letu, tumepoteza wanaume wengi.”
“Ila general, hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo?” Amadu alitia kaswali.
“Hakuna njia nyingine. Au wewe una wazo?”
“Ndio.”
“Niambie.”
“Mi nadhani tutumie tu njia zile zile tunazozitumiaga kuliko kuumiza hao watoto na kuwatenganisha na wazazi wao.”
“Hapana! Hakuna tena pesa ya kutosha kufanya hivyo. Pesa iliyobakia inatosha tu kuleta madawa ya kulevya kwaajili ya kuwazubaisha na kuwaingiza hao watoto kwenye mfumo. Hatuwezi tena kuwashawishi watu wazima. Kuwapata watoto ni rahisi, pia wanakuwa watii zaidi pale wanapopewa mafunzo ya kutosha kuliko watu wazima.”
“Ila general …”
“Sitaki tena maswali wala mawazo. Fanya nilichokuambia. Inabidi ujifunze kutii amri zaidi ya kupinga amri. Mnaweza mkaenda kwa sasa, kesho muda wa mchana mtakwenda huko Sierra kutimiza agizo.”
Kikao kikafungwa na hiyo amri. Amadu pamoja na Chui wakatoka makaoni na kwenda kujumuika na wenzao kwenye mazoezi. Walibeba vitu kupasha misuli. Walikimbia kwenye vilima kutafuta nguvu za miguu na stamina. Walifanya mazoezi ya kulenga shabaha kwa risasi wakifanya shindano miongoni mwao. Zoezi lilipokoma, Amadu pamoja na Chui wakaelekea mtoni kuoga. Na huko ndipo Chui akamuona Amadu hayupo sawa. Hakuwa na tabasamu lake lililozoeleka. Uso wake ni wazi ulimezwa na tafakuri fulani.
“Amadu, nini kinatafuna akili yako?” Chui aliuliza. Amadu akazamia ndani ya maji kwa muda wa dakika kama mbili kisha akainuka. Akamkuta Chui bado amesimama kama mtu amngojeaye mgeni akitokea safarini.
“Siko tayari kwenda kuteka wanafunzi.”
“Kwanini?”
“Sijaona haja ya kuja kuwatesa watoto huku. Wanahitaji kusoma, wanahitaji kukaa na wazazi wao. Kuwateka na kuwaleta huku ni sawa na kuwafanya wateseke. Si lengo letu ama langu kuwatesa wana Sierra wenzangu, bali kuwakomboa.”
Chui alitikisa kichwa chake kama mtu asikitikaye kisha kamuangalia Amadu.
“Hamna njia kaka. Sasa utafanyaje? … Cha kufanya ni kuwachukua hao watoto na kuwaleta hapa kwa amani. Wapatiwe mafunzo, baadae watakuja elewa.”
“Si rahisi kihivyo, Chui. Si watoto wote watakaoweza kustahimili. Wengine watakufa mazoezini wakati wengine wakiharibikiwa moja kwa moja na utumizi wa madawa, hata msongo wa mawazo.”
“Naelewa sana hiko unachokiongea. Ila general amebakiwa bila jinsi na hiyo ndio ameona njia pekee. Nadhani itabidi tufanye tu.”
Amadu hakusema tena jambo. Alizamia chini ya maji akakaa kwa muda wa dakika moja, alipoibuka alikuwa na tabasamu. Alimshika mkono Chui akamuambia;
“Tushindane kuzamia.”
Baada ya hilo neno, wakaanza kushindana nani akaaye muda mrefu kwenye maji kwa kuhesabiana muda. Amadu akashinda hilo zoezi kwa mara tatu akimuacha Chui kwa nyuma mno.
“Hatimaye na wewe umekaa nyuma. Si ulinishinda kwenye kulenga shabaha!”
Amadu alisema kwa bashasha la furaha wakaanza kumwagiana maji. tendo hilo likadumu kwa muda wa dakika zisizozidi dakika kumi. Wakatoka kwenye maji na kurudi kambini, wakati huo jua laenda kuzama ila bado miale yake inasema na uso wa dunia.
Wakiwa wanatembea kuelekea hemani, kwa mbali Amadu na Chui wakaona wafuasi wenzao wanajenga nyumba za miti. Walizitizama, Chui akauliza;
“Wanajenga nini?”
“Nyumba za hao watoto tutakao kwenda kuwakamata.” Amadu alijibu kwa sauti ya chini. Kwa muda wakatizama zoezi lile likifanyika, giza lilipoanza kudhoofisha uwezo wa macho yao, wakaondoka na kwenda hemani. Asubuhi ya mapema, wakaaamka na kuanza kujiandaa kwa zoezi lao lililo mbele. Walipakia bunduki kadhaa zisifike hata tano kwenye basi, lile walilowahi kuliteka Sierra hapo awali, wakabebelea na maji ya kunywa. Wakawasha basi tayari kwa kuhepa. Wakati wanatoka, general akawasimamisha kwa kusimama mbele yao.
“Nataka muende na hawa.”
General alinyooshea mkono wake mlangoni mwa makao makuu. Wakatoka Talib na Mohamed. Amadu akang’aka;
“Hayakuwa makubaliano yetu general.”
“Nilikuambia jana, jifunze kutii amri zaidi ya kupinga. Utaenda nao.”
Amadu alitaka tena kufungua kinywa alonge ila Chui akamshika mkono na kumminya kama ishara anyamaze.
“Ina mana hatuamini, au?” Amadu alimuuliza Chui kwa sauti ya kunong’oneza
“We tulia tu, kaka. Tufanye tu.” Chui naye alinong’oneza. Talib na Mohamed wakapanda basi na kuanza safari.
Kwa dakika kama kumi na tano wakiwa njiani hakuna aliyemuongelesha mwenzake. Safari ilikuwa ya kimya, kelele tu ya basi ikisikika. Lakini ilipohitimu dakika ya kumi na sita, Talib akavunja ukimya;
“Tunaanza na shule gani?”
Hakuna aliyemjibu. Kila mtu alikuwa na yake.
“Nimeuliza, tunaanza na shule gani we Amadu. Hunisikii?”
“Kwani mkuu hajakuambia?” Amadu alijibu kwa kuuliza.
“Nimekuuliza wewe!”
“Tulia, utaona.” Amadu alijibu kibabe. Chui akaingilia kati;
“Tunaanza na shule ya Devout.”
Talib akatabasamu kwa kebehi na kusema;
“Kwahiyo wewe ni kibaraka wake, sio?”
Chui akamtizama Talib bila ya kusema jambo. Akageukia mbele na safari ikajongea.
“General ameniambia niwatizame kwa makini. Na nihakikishe kila kitu kinaenda sawa. Kama mnabisha muulizeni Mudy hapa.”
Talib alijibaraguza. Bahati mbaya hakuna aliyehangaika naye tena, wote waliweka midomo yao kufuli. Walipokaribia eneo la shule wanayoivamia, Amadu akatoa maelekezo;
“Shule ina madarasa matano na ofisi mbili. Hatuwezi tukajigawanya kutosha kote huko. Tutakachokifanya ni kuwatoa wanafunzi wote nje wakusanyike eneo moja. Talib na Mudy, nyie mtaenda ofisini na kuwaweka walimu na wafanyakazi wote chini ya ulinzi.”
Baada tu ya hayo maelezo, basi la wakina Amadu likagonga geti la shule na kuingia ndani. Kabla hawajashuka, Amadu akatoa angalizo;
“Hakuna kuua!”
Walijigawanya kama vile walivyopena maelezo. Ndani ya dakika tano, wanafunzi wote wakawa wapo nje ya madarasa, mikono kichwani. Nyuso zao zikiwa zimetawazwa na hofu kubwa, wengine wakilia na hata kutiririsha makamasi. Amadu pamoja na Chui wakachagua wanafunzi wa kiume ishirini kwa kuwagusa na bunduki za na kuwataka wakajipakie kwenye gari. Waliwachagua wale wanafunzi walioonekana wameshiba na wana miili ya mapambano. Wakiwa katika hilo zoezi, ghafla wakasikia sauti ya milio miwili ya risasi toka ofisini mwa walimu. Amadu na Chui wakatahamaki kwa kutizamana. Upesi, Amadu akaelekea huko zilipotoka sauti za risasi, akakuta wanaume wawili chini wamelala damu zikiwa zikiwa zinawachuruza vichwani. Talib akiwa ndiye aliyeshikilia bunduki kama mtu aliyetoka kushambulia.
“Si nilisema hakuna kuua?” Amadu alifoka.
“Sasa kama analeta ubishi?” Talib alijibu na kuongezea, “najua ninachokifanya. Sihitaji kuelekezwa, sawa?”
Kabla Amadu hajajibu, mluzi uliita huko nje akaamua atoke na kumrudia Chui wakamalizia zoezi lao la kuchagua watoto kisha wakaondoka toka eneo lile la shule. Wakaacha simanzi pana na hofu ndefu kwa wanafunzi na walimu.
“Wamemchukua kakaaa!” Mwanafunzi mmoja mdogo mwenye makadirio ya umri wa miaka saba, alipaza sauti kwa kulia. Mwalimu alimbembeleza na kumtaka anyamaze. Lakini haikufua dafu, kwani wanafunzi wengine nao walianza kulia, na hata baadhi ya walimu ambao walishindwa kuvumilia kuona mizoga miwili ya wenzao imejilaza kinyama.
Palikuwa eneo la msiba ghafula. Nyuso zao za tashtiti ya majonzi ziliwalilia waliouwawa na wale waliobebwa. Hata pale taarifa zilizopotolewa kituo cha polisi, haikuwa tena na faida kwani watuhumiwa walikuwa tayari wameshayeyuka ndani ya nchi ya Sierra, sasa wakiwa ndani ya Guinea.
“Ndio mkuu … inasemekana wameelekea Guinea, sasa tunafanyaje?” Polisi mmoja akiwa na wenzake kama nane wakiwa na bunduki, aliongea na simu yake.
“Ok … sawa, mkuu tunarudi.”
Polisi alikata simu yake na kuwataka wenzake warudi kwenye gari wakayoyoma. Baada ya masaa matatu, kukawa na kikao ndani ya jengo la wizara ya ulinzi. Wanaume wanne na mwanamama mmoja wakiwa wamevalia nguo za kijeshi na polisi zikiwa zimechafuliwa na vyeo, waliketi wakikitizama kiti kimoja kilichokuwa tupu, ambacho baada ya muda kilikaliwa na mwanaume mmoja aliyevalia suti ya kaki baada ya kupewa salute na wengineo. Kikao kikafunguliwa.
“Sasa hatuna tena haja ya kukaa na kungoja. Ni wazi kabisa tena isiyopingika kwamba washenzi hawa wana makazi yao nchini Guinea. Hatuwezi tukakaa kungoja mpaka turuhusiwe, si jambo la mashaka raisi wa Guinea anawafichama hawa watu.” Mwanaume pekee aliyevalia suti alitamka.
“Ni kweli, mkuu. Ila kama tumeshindwa kupambana nao na kuwatoa mji wa Kabala, huko ndani ya Guinea tutaweza kweli?” Aliuliza mwanamama pekee kikaoni.
“Hapana! Si kwamba tumeshindwa.” Alidakia mjumbe mwingine wa kikao. “Endapo kama tukienda na kuvamia moja kwa moja Kabala, tutawaua wananchi wetu wengi mno maana wapo hapo kama mateka. Inabidi tutumie busara zaidi kuliko nguvu.”
“Kweli.” Mjumbe mwingine naye akadaka mada, “Tulikuwa tunaenda vyema sana kipindi kile tunapata msaada toka Liberia. Ila tokea na wao waanze kushambuliana na Le tueurs baada ya kuuweka mji wa Monrovia chini yao imekuwa tena vigumu. Ila kwa mimi, namuunga mkono mkuu. Tuna haja ya kwenda huko Guinea. Ila … Ila ni kwa siri kwa maana isipokuwa hivyo, tutakuwa tumetangaza vita na Guinea. Na hatutoweza kuwamudu pande zote mbili, waasi wa MDR na wanajeshi wa Guinea. Inabidi tuchague makomando kadhaa, wakapeleleze na hata kuteketeza kambi ya waasi huko.”
“Naunga mkono hoja.” Mjumbe mwingine akadakia. “Waasi waliokuwepo Kabala, wanapata msaada toka kwa wenzao waliopo Guinea. Kama tukifanikiwa kuwamaliza wa huko Guinea, hawa wa Kabala watakuwa yatima, na tutawamaliza kwa urahisi mno.”
Hoja hizo zikaonekana kukubalika. Ikadhamiriwa kupangwa kama ilivyotamkwa. Mkuu akaongezea kwa kuuliza;
“Kuna lolote zaidi ya hayo?”
Mwanamama pekee kikaoni akatoa picha tano na kuziweka juu ya meza. Mkuu akazichukua na kuzitizama.
“Hawa si ndio wale wale uliowahi kunionyesha?”
“Ndio mkuu. Hao watu watatu wamejirudia. Ni watu ambao wamefanya tukio zaidi ya moja sasa nchini. Nadhani ni muda muafaka wa kutangazwa ulimwengu mzima kama magaidi.” Mwanamama alimimina maneno bila kumung’unya mung’unya.
Zilikuwa na picha tano, sura ya Amadu ikijirudia kwenye kila picha, wakati sura ya Chui na Talib zikijirudia mara mbili na Mohamed yeye pekee akiwa katokea mara moja. Mkuu alizitizama kwa umakini zile picha kisha akamwambia mwanamama;
“Fanya hivyo kama ulivyosema, haraka.”
Mwanamama akaitikia kwa kupandisha kichwa chake. Kikao kikafungwa.
****
****
☆Steve