13--Bado wazazi wangu wasingejua nani anayehusika katika uchawi,
kujitokeza kwa mzee Manoni kulijidhihirisha wazi wasiwasi wao pengine nimewajua. Nilimuomba Mungu aniepushe na janga lile kwa kuamini kama wataendelea kunifuata, nitashindwa kusoma vizuri. Usingizi nao haukuchelewa kunichukua baada ya kitu kizito kunipitia na kunifanya nilale usingizi wa pono. Siku ya pili kama kawaida baba aliniamsha kujiandaa kwenda shule, niliamka nikiwa na nguvu kama kawaida. Nilijiandaa kuwahi namba shuleni, niliwahi namba na kufanya usafi kama kawaida. Muda wa kuingia darasani ulipowadia tuliingia. Ajabu siku ile wale wanafunzi niliowaota wakicheza ngoma ya wachawi katika ndoto na nilipoamka sikuwakuta darasani na kuwauliza kama walikuwepo darasani. Hata mwalimu aliyekuwepo kwenye ngoma alikuwepo siku hiyo shule, kila sekunde ya pumzi yangu nilijiona kama sipo katika dunia ya kawaida ambayo naishi peke yangu. Sikutaka kuhoji lolote nilikaa kimya na kuendelea na masomo kama kawaida.
Siku ile nilisoma kama kawaida hakuna kilichonitokea cha ajabu. Jioni ilipofika nikielekea nyumbani, mara nyingi nilipenda kuwinda ndege kila nikitoka shule. Niliacha njia ya kuelekea nyumbani na kuingia vichakani kuwinda ndege, nikiwa katikati ya kichaka, nilisikia sauti ya wale wasichana niliowaota wakicheza ngoma ya wachawi .
Shija. Kabla ya kuitika niligeuka kuwaangalia, nilishtuka kuwaona ni wale wale, nilijiuliza wamefuata nini kule porini.
Niliwaitikia huku nikitabasamu kuficha hofu yangu.
Naam, aah Helena na Sabina, Helena na Sabina walikuwa wakubwa kwangu kiumri.
Mbona uko huku peke yako?
Nawinda ndege.
Eti jana ulituulizia?
Eeh, kwani mlikuwa wapi jana?
Mmh, nyumbani.
Wote?
Kwani vipi mbona unauliza hivyo ?
Si rahisi wote muwe nyumbani kwa pamoja bila sababu, ikizingatiwa hamkai pamoja.
Kwani wewe wasiwasi wako nini?
Hakuna tatizo, ila niliwaulizia kama wanafunzi wenzangu.
Shija ilianza lini na jana iwe ya pili, ina maana mimi na Sabina ndiyo jana kukosekana kwa pamoja?
Tena nasikia sijui ulipitiwa usingizi na kuanza kukohoa na ulipopata fahamu watu wa kwanza tulikuwa sisi.
Tunaomba utueleze ukweli nini kilichokufanya utuulize.
Helena aliongezea.
Shija ataeleza nini, wenzie wamuelewe?
ITAENDELEA ASUBUHI..