Ninastahili Lawama

Ninastahili Lawama

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
34,080
Reaction score
79,478
NINA STAHILI LAWAMA.

Na. Robert Heriel.
Maandishi ya Robert Heriel, Kwa Lugha ya kiswahili

Kila kitu nilikiona cha muhimu. Hata yale niliyokuwa ninayachukulia kama mambo ya kawaida nilianza kuyaona ya muhimu. Kupitia dirisha lililokuwa pembeni ya kitanda nilichokuwa nimelala. Nilishuhudia Majani ya miti yakianguka. Nilihuzunika. Sasa nami nilijiona kama moja ya majani hayo yaliyotoka mtini na kudondoka chini. Nilijua siku zangu zilikuwa zinahesabika duniani.

Miale ya jua legevu ilinimulika machoni. Nilijisikia kutabasamu lakini nilishindwa mara nilipokumbuka kuwa muda mchache ujao sitauona tena mwanga wa jua. Machozi yalitoka na kutotesha Mashavu yangu. Midomo yangu ilianza kutetema kwa kilio. Kwa mbali mlango wa Koo uliachia sauti ya kilio cha mtu mwenye kwikwi. Loooh! Mtu mzima kulia bila kupigwa.

Watoto wangu walisikia sauti yangu ya Kwikwi, Walikuja upesi kujua nini kilikuwa kimenipata. Walinikuta nikiwa nimegeukia dirishani. Nikitazama nje ambapo kulikuwa na Kuku na vifaranga vyake vikichakura chakura chakula kwa maandalizi ya jioni. Pia huko nje niliwaona Wajukuu zangu wakicheza Mpira wa miguu.

Punde mawazo yangu yalikumbuka enzi za ujana wangu. Kipindi nikiwa Mchezaji mahiri wa mpira. Nikivaa jezi namba Saba. Nilikumbuka Jinsi kipindi kile nilivyokuwa na kasi huku nikikokota mpira. Yote hayo niliyakumbuka lakini yalikuwa kama kisu kikali kilichoukata moyo wangu. Hivi leo nipo kitandani siwezi fanya lolote zaidi ya kugeuza macho huku na huku. Siwezi lolote labda kutema mate. Masikini Mimi.

''Baba, Vipi unaendeleaje?''
Mwanangu Mkubwa aliniuliza huku akisogea katika dirisha kuona ninachokiangalia.
Wengine wote walibaki kimya wakisubiri kwa hamu jibu langu.

Kitambo kilipita jibu halikutoka. Walibaki wamenitizama mithili ya mtu aliyepima VVU amtazamavyo Daktari anayempa majibu.

Punde niliongeza sauti ya kilio jambo ambalo liliwachanganya kwa kutojua kwa nini ninalia. Kilio changu kiliwafanya mpaka wajukuu wangu waliokuwa wakicheza mpira kuja ndani. Kilio changu kiliwafanya waliojikoni kuja chumbani kwangu. Waliosebuleni, Kwenye vyumba vyao wote walikuja kuona nini kimetokea.

Sasa kundi kubwa lilikuwa limezingira kitanda changu na chumba chote kilikuwa kimejaa. Macho yote yalikuwa kwangu.

Ukimya ulitawala huku mapigo ya moyo ya kila mmoja yakionekana kwenda kasi. Jasho jepesi lililamba ngozi zao. Hakuna aliyekuwa anajitisha isipokuwa mawazo yao yaliokuwa yanakimbia kwa kasi sana. Kila mmoja aliwaza lake na hakuna aliyekuwa anajua mwenzake anawaza nini.

Niliwageukia na wote wakanitazama usoni kama watazamaji wa Luninga wanaotazama filamu ya kusisimua. Niliona hofu katika macho yao. Nyuso zao zilipoteza Matumaini na Mimi. Sijui ni nani aliwaambia kuwa muda mchache ujao nitakuwa nimekufa. Huenda walidhani hivyo kwa jinsi nilivyokuwa nimechoshwa na ugonjwa.

Tulisikia watu wakibisha hodi. Mke wangu akaitikia na kuufungua mlango. Liliingia kundi la watu ambao miongoni mwao walikuwa majira zetu. Kwa hali waliyoikuta walifuata utamaduni wa mule ndani wa kukaa kimya. Hawakuzungumza chochote.

Sasa chumba kilikuwa kimejaa haswa pasiwepo nafasi ya Kutemea mate. Hali hiyo ilifanya mule ndani kuwe na joto. Hivyo Feni iliwashwa ili kufukuza joto la mule ndani.

Sasa nilihisi baridi ikiingia mwilini. Mke wangu aligundua hilo akachukua shuka akanifunika. Hata hivyo bado baridi niliisikia. Nilikumbuka maneno kuwa Mtu akitaka kufa anahisi baridi kali hata kama kuna joto. Moja kwa moja nilijua zamu yangu imefika. Zamu ya kuikimbia dunia. Kwenda kwenye giza. Mahali kusiko na jua. Mahali penye ukungu na baridi. Huko ndiko nilikuwa naenda.

Nilisikia adhana ya waislam. Nikajua ni saa kumi na mbili. Hapo ndipo nikanyanyua mdomo wangu. Mdomo wa mgonjwa mahututi.

Nikakohoa kidogo kufukuza kimya kilichokuwepo awali. Na kuosha masikio ya waliokuwa wakinitazama. Wote walikaa mkao kusikia jambo. Wanasema, Neno la mwisho la marehemu.

''Kama kuna siku nitakayojivunia ni hii siku ya leo'' Nilizungumza nikameza fumba la mate. Kisha nikaendelea;
''Siku ya leo sikuijua. Ila leo nimeijua. Kwa nini nisifurahie mwisho wangu. Kwa nini nisifurahie Mauti yangu.....''
''Baba maneno gani hayo...''
Mwanangu mdogo alinikatisha. Mke wangu alikuwa akilia tuu. Wengine walikuwa kimya huku huzuni ikiwa pandisha bendera yake mioyoni mwao.

'' Mwanzoni niliweza, ila mwishoni siwezi. Mwanzoni nilikuwa hodari lakini mwishoni nimegeuka dhaifu. kohoo! Koo...!!''
Nilikohoa huku Mke wangu akinipiga kifuani akinipa pole.

''Mwili umesinyaa. Roho imenyauka. Nimeukosea huu Ulimwengu''
Nilimgeukia Mwanangu niliyemzaa kabla ya ndoa. Nikasema;
''Ninastahili lawama zote kwako. Sikukutendea haki. Hukula chakula kizuri kwa ajili ya ujinga wa mimi Baba yako. Mpaka ukaumwa magonjwa ya Lishe. Hukuvaa vizuri mwanangu. Yote ni Mimi Baba yako. Nakiri sikuwa Baba bora kwako. Umeishi kama mdudu wakati hukustahili kuishi hivyo.

Mwanangu, ninastahili lawama zako. Nisamehe nisije kufa na laana yako. Nisamehe Mwanangu''
Niliangua kilio cha nguvu nikiwa nimeushika kwa nguvu mkono wa mwanangu mtoto wa nje. Wote tulilia. Mwanangu ndiye alilia zaidi.

Niligeuza kwa tabu macho yangu yaliyolowa kwa machozi nikamtazama Baba J ambaye ni jirani Yetu.
''Baba J umekuwa Jirani mwema. Umekuwa Zaidi ya ndugu kwangu na familia Yetu. Siku zote tumeishi kwa kushirikiana''
Maneno hayo yalimfanya Baba J kuachia tabasamu jepesi la shukrani lakini Mama J uso wake ulizingirwa na Hofu.
''Baba J nina stahili lawama zako. Pamoja na wewe kuniheshimu lakini Mimi nimekulipa mabaya. Ninastahili lawama zako Baba J. Nimetoka na Mkeo kwa zaidi ya Miaka mitano. Nisamehe Baba J''

Maneno hayo yaliupasua Moyo wa Baba J. Baba J alidondoka chini na kupoteza fahamu. Mama J alibaki akibabaika tuu kama mwendawazimu. Walimtoa nje ya chumba na kumpeleka sebuleni.

''Ninastahili Lawama... Lawama.. Lawa..Kooh!.. Koo!''
Nilikohoa mfululizo mpaka mishipa ya uso ikajitokeza.

''Mke wangu, Umekuwa mke bora kwangu. Umekuwa kama Mama yangu. Ukinilea mimi na Wanangu. Lakini mimi sikustahili Mapenzi yote yale. Sikustahili!. Huyu binti nilimpa Mimba miaka saba iliyopita. Kwa kuhofia kufungwa nikamlazimisha aitoe. Nikaua mimi. Mimi....Nimu..u..aji''
Nililia kidogo kisha nikaendelea kwiki ikiwa imenibana.
''Kinachoniuma ni kuwa kwa sasa binti wa watu kaolewa lakini hazai. Mimi ndio nimefanya asizae. Mimi nilistahili nifungwe miaka 30. Watu wanamlaumu bure tuu huyu binti. Mimi ndiye ninastahili lawama''

Yule binti alilia sana. Alijitahidi aseme kitu lakini alishindwa. Mdomo ulikuwa mzito. Kilio chake kiliashiria kiu yake ya kutaka Mtoto. Looh!

''Nakumbuka kipindi kile nikigombea Ubunge.(navuta makamasi). Nilikuwa miongoni mwa watu tuliomteka na kumuua mgombea wa chama kile. Hivi nimepata nini mimi. Ona familia ya yule mgombea tuliyemuua inavyopata tabu. Ona. Oneni jamani. Mimi ndiye ninastahili lawama. Nilimuua Baba wa watu ili nipate madaraka. Nini faida niliyoipata. Nauliza ni ipi faida''

''Baba usiseme hivyo. Mungu atakusamehe''
Mwanangu mkubwa aliongea.

''Kwa niliyoyafanya Mungu akinisamehe hatatenda haki. Mimi sistahili Msamaha''

''Nimekumbuka..! Jamani nimekumbuka...! woyo.. woyo. Hiii..hiii..Mimi ni shetani jamani''
Walijaribu kunituliza lakini ni kama ndio walikuwa wanachochea kuni. niliongeza sauti.

''Mwaka ule niliiba pesa iliyotakiwa kununuliwa madawa ya hospitalini. Nikajenga ile nyumba ya ghorofa. Watu walikufa kwa kukosa madawa. Wakati Mimi ndiye niliyeiba pesa zao. Watoto wao wamebaki Yatima. Wake zao wamebaki Wajane. Hawakustahili lawama ya kushindwa kulipa ada kama Baba zao wangekuwa hai. Lakini Mimi nilivyoshetani nikaua Baba zao na mama zao. Jamani... eee
''

Kila mmoja alikuwa akilia mule ndani. Maneno yangu yalikuwa machungu kama shubiri. Iligeuka nyumba ya Maombolezo.

'' Mwaka mia tisini huko. Nilimfukuza kazi dada mmoja kisa na mkasa ati alikataa kunipa penzi lake. Masikini Binti wa watu kwao walikuwa masikini na yeye ndiye walikuwa wanamtegemea. Alihangaika sana. Hakustahili yote yale. Lakini tamaa zangu za kijinga jinga zikamsononesha. Alihangaika sana. Mtoto wake alikufa kwani alikosa hela ya kumpeleka hospitali. Ninastahili lawama''

''Nikifa waambieni Mashehe na Wachungaji. Wamuombe Mungu anipe adhabu kali sana. Tena wasijaribu kuniombea msamaha. Kwa maana sistahili msamaha. Ninachostahili ni lawama''

''Mke wangu, Watoto wangu
, na Wajukuu zangu. Kabla sijasahau. Ninataka kuwaambia. Lakini Angalieni kwenye hilo Sanduku hapo.......''

Kabla sijamaliza Nilikohoa mfululizo na kama umeme wa Luku roho iliacha Mwili. Nilikufa Kibudu.

Waliachia makoo yao kupiga mayowe. Walilia wakijigara gaza chini. Wakijipiga piga ukutani. Uchungu waliopata hausimuliki.

Wakiendelea Kulia Mke wangu alikumbuka maneno yangu kuwa aangalie kwenye Sanduku. Alienda kwenye sanduku nililomuagiza. Aliona shuka Jeupe lililoandikwa Maneno.mekundu yaliyosomeka; NINASTAHILI LAWAMA.

Alikuja kitanda nilipolala akanifuka Gubi Gubi. Toka Unyayoni mpaka utosini. Mwisho kukawa Kiza.

Niite Taikon wa Fasihi.

Robert Heriel
Taikon Wa Fasihi
0693322300.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom