Niliua kwa Kukusudia -6-
ILIPOISHIA:
"Unaona kile kijumba kibovu pale?," alinielekeza mama mmoja wa makamo baada ya kumuulizia kama anamfahamu Mama Shufaa.
"Ahsante sana mama," nilimshukuru mama huyo na kuelekea kwenye kijumba hicho.
Baada ya kufika, nilimkuta Mama Shufaa japo alinishangaa kutokana na hali yangu lakini alinipokea na kunipa hifadhi ndani ya kijumba hicho kibovu.
SASA ENDELEA…
Nilimuelezea hali halisi ya maisha yetu baada ya wazazi kufariki dunia na kwamba nipo hapa Dar es Salaam kutafuta vibarua.
Mama Shufaa ambaye kiukoo ni shangazi yetu, alinipa pole na kunishauri kuwa nijaribu kutafuta kazi za ndani maeneo ya Sinza na Kijitonyama wanakoishi watu wenye uwezo kifedha.
Kesho yake asubuhi niliamka, baada ya kujiandaa nikapanda basi la kuelekea Sinza ambapo nilianza kazi za kugonga kwenye mageti ya watu kutafuta kazi za ndani.
Niligonga mageti mawili lakini sikufanikiwa.
Nikiwa nimekata tamaa kabisa, niliona nyumba moja iliyokuwa na geti kubwa, nikajiambia nijaribu kuulizia hapo, nikishindwa basi nirudi Buguruni hadi kesho tena.
Nikiwa najiandaa kugonga kwenye nyumba hiyo, ghafla lilikuja gari kwa kasi na kufunga breki karibu kabisa na miguu yangu, nilipoliangalia vizuri, alikuwa ni yule mwarabu aliyenigonga siku chache zilizopita.
Haraka akashuka na kuja hadi karibu yangu, tukasalimiana.
"Habari yako," alinisalimia huku akijaribu kuniangalia kwa umakini sana.
"Nzuri tu, za kwako."
"Salama, sijui wewe."
"Aah, salama lakini kama nakufananisha hivi, tuliwahi kuonana Chalinze?," yule mwarabu aliniuliza akijaribu kuvuta kumbukumbu.
"Ndiyo, mimi si ndiye ulinigonga yaani umenisahau mara hii?," nilimjibu na kumuangalia usoni, tayari alijawa na aibu kwa mbali japo hakutaka kuonesha dhahiri.
"Kumbe niko sahihi, maana nilikuwa nakufananisha tu!"
"Ni mimi bwana."
"Ehe sasa mbona uko hapa, ni kwa ndugu yako?"
"Hapana, niko hapa Dar tangu jana natafuta kazi," nilimjibu kwa kumkazia macho na kumuuliza kwani na yeye yupo Dar?"
"Mimi naishi hapa Dar, kule Chalinze kuna biashara zangu kama sheli za mafuta na nyinginezo.
Sasa unatafuta kazi gani?," aliniambia kisha akanitupia swali hilo.
"Yoyote, niko tayari kufanya," nilimjibu kwa ujasiri uliochanganyika na hofu kwa mbali.
"Oke, mimi nina hoteli yangu lakini kwa sasa hakuna nafasi kabisa, sijui nitakusaidiaje?," alisema yule mwarabu lakini kwa sauti ya upole na ya chini mno.
"Mmh!," niliishia kuguna huku nikiinamisha uso.
"Sasa sikiliza, naomba kesho uje hotelini kwangu," alisema na kuchomoa waleti yake ambapo alinipa shilingi elfu kumi kama nauli.
"Sawa, sasa huko hotelini ni wapi?," nilimuuliza kwa utulivu huku moyo wangu ukinienda pupa, sijui ni kwa minajili gani.
"Unapafahamu Mwananyamala?"
"Hapana, ni wapi?"
"Wewe kesho panda basi lolote la Mwananyala, waambie wakushushe Kwakopa, ukifika ulizia hoteli inayoitwa Riyama Hotel, ni hapo."
"Sawa."
"Lakini naomba uje kuanzia saa nne hadi sita, kwa muda huo utanikuta, sawa?"
"Sawa," nilimjibu kisha tukaagana.
Baada ya kuachana naye, sikuwa na ajizi zaidi ya kurudi Buguruni kwa shangazi mama Shufaa. Sikuona sababu ya kuendelea kutafuta kazi kwani nilikuwa na matumaini ya kupata kibarua cha riziki kwa mwarabu yule ambaye niliamini kabisa asingeweza kunitosa.
Nikapanda basi kuelekea Buguruni, njia nzima nilikuwa kimya. Kichwa changu kilijawa na mawazo mengi sana. Kuna wakati nilimfikiria mdogo wangu Inana, lakini sikuwa na jinsi ya kumjulia hali na kumjuza ninavyoendelea. Sikuwa na simu, iliniuma sana.
Nilifika majira ya adhuhuri na kumkuta shangazi akifua.
"Za huko utokako?"
"Salama tu."
"Vipi maendeleo, umefanikiwa?"
"Mungu amesaidia, unakumbuka jana nilikuambia niligongwa na gari kule Chalinze siku za hivi karibuni?"
"Ndiyo, nakumbuka ulinisimulia imekuwaje?"
"Nimekutana na aliyenigonga," nilimjibu na kuketi karibu naye.
"Hee, imekuwaje?," Shangazi aliuliza kwa hamaki na kunitazama kwa shauku ya heko.
"Tulisalimiana tu, nikamueleza shida yangu ndipo akaniambia niende kwenye hoteli yake Mwananyamala kesho."
"Mungu ni mkubwa sana."
"Kuna chakula humo ndani, waweza kulituliza tumbo lako."
"Ahsante."
Siku hiyo nilishinda kwa furaha kubwa nikiamini kuwa hatimaye mwanga wa mafanikio ulianza kuonekana japo kwa mbali sana.
Usiku sikupata usingizi mapema. Nilikuwa nawaza na kupanga mambo mengi sana, lakini kubwa nililoliwaza ni kwenda kumfuata mdogo wangu huko kijijini nikishafanikisha kazi.
Sijui nililala saa ngapi, nilishtuka asubuhi na kumsaidia shangazi kazi kidogo, kisha nikajiandaa kwenda huko Mwananyamala. Nilipanda basi hadi Ubungo ambako niliunganisha hadi Mwananyamala eneo moja linaloitwa Peace.
Nikaulizia Kwakopa na kuoneshwa. Nikauliza pia hoteli hiyo ya Riyama. Nayo nikaoneshwa na kwenda nikiwa na hofu.
Nilipofika, nikamuulizia yule mwarabu ambaye hadi wakati huo sikuwa nimelikariri kabisa jina lake. Hata hivyo, nilikuwa sikumbuki kama aliwahi kunitajia jina.
"Ndiyo, yupo nimwambie nani?," alikuwa ni mhudumu wa mapokezi hotelini hapo.
"Mwambie yule msichana wa Chalinze," nilimjibu huku nikiendelea kushangaa uzuri wa hoteli hiyo ya kifahari.
"Haya, twende nikupeleke ofisini kwake," yule dada alisema nami nikamfuata.
Tulifika hadi ofisini kwa huyo mwarabu na kumkuta akiwa bize nyuma ya kompyuta.
"Oh! Karibu sana," aliniambia lakini sura yake ikiwa imepoteza kabisa uchangamfu.
"Ahsante sana," niliitikia kwa unyenyekevu mkubwa.
Baada ya kusalimiana, niliketi kwenye kiti kizuri na cha thamani kilichokuwepo ofisini hapo.
Zilipia karibu dakika tano bila kusemeshana chochote na huyo mwarabu, nikaanza kuingiwa na wasiwasi juu ya msaada wa kazi nilioahidiwa.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia leo usiku.....