Nilikutana na Saddam mara mbili baada ya kupinduliwa

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
“Nilikutana na Saddam mara mbili baada ya kupinduliwa”

Maelezo ya picha. Mwandishi wa makala haya, Ahmed Rajab (kushoto), akisalimiana na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Kaimu wa Mkuu wa Jeshi la Mgambo la al-Hashd al-Sha‘abi nchini Irak mnamo mwaka 2017.

Na Ahmed Rajab

MWANZONI mwa Oktoba, 2017, nilialikwa kuhudhuria mkutano jijini Baghdad, Iraq, kuujadili ugaidi wa kimataifa. Baada ya kuisoma barua ya mwaliko, akili yangu ilizileta machoni mwangu kumbukumbu za miaka tisa kabla ya hapo.

Nilijikuta Dubai nikiwa mkuu wa chumba cha habari cha IRIN, Shirika la Habari la siku hizo la Umoja wa Mataifa. Tulikuwa na dhamana ya kukusanya, kuhariri na kuchapisha ripoti na insha kutoka nchi za Mashariki ya Kati na za Asia zilizokuwa zimekumbwa na nakama na majanga ya kibinadamu. Zilikuwa nchi zilizozongwa na vita au zilizoathirika kwa maafa ya kimaumbile.

Kumbukumbu zangu za Dubai zilinikuta nikimsaili Sinan Mahmoud, aliyekuwa miongoni wa waandishi wetu wa Irak. Sinan angali akiyafanyia kazi mashirika ya habari ya kimataifa.

Kwa vile takriban waandishi wetu wote walikuwa wakifanya kazi katika mazingira mazito na ya hatari tulikuwa na mpango wa kila baada ya muda kumleta mmojawao Dubai kwa mapumziko ya wiki mbili. Wakati huo wa kumbukumbu zangu ilikuwa zamu ya Sinan.

Baada ya kumdadisi kwa kina kuhusu hali ilivyokuwa Baghdad, ghafla ilinijia fikra ya kutaka kujua kwa nini nisende mwenyewe? Umoja wa Mataifa ulitukataza tusende Baghdad, ukisema ni hatari.

Nilipomuuliza Sinan kwani itakuwa nini nikenda? Alinitumbulia macho akanitazama, juu chini, utadhani akimuangalia mwendawazimu halafu akanambia kwa mkazo: “Wewe, watakuteka nyara.”

Sikutaka kujua ni nani wataoniteka nyara na kwa nini? Niliamua kuyaacha hapo.

Siku hizo jiji la Baghdad lilikuwa halikaliki. Watu wakiuliwa kwa misimu. Kulikuwa msimu wa kuwaua vinyozi; msimu wa mauaji ya warembo; msimu wa kuwaua wanaume wasio na ndevu; hata madaktari, wauguzi, na waalimu hawakunusurika. Masunni, Mashi‘a, Wakristo wote walikuwa na zamu za kuuliwa.

Wauaji walikuwa Waislamu waliokuwa wakijinata kwamba Uislamu wa mrengo wao ndio pekee uliokuwa sahihi.

Kumbukumbu zote hizo zilinirudia Oktoba 2017. Oktoba ile hali ya hewa London haikuwa mbaya. Kweli mawingu yakinunanuna lakini, kwa jumla, jiji langu lilikuwa kavu na halikugubikwa na baridi ya kuudhi. Nami, mshipa wa kusafiri ulishanipiga; nikitamani kuiona tena Baghdad. Nikajiambia wacha nende, naliwe liwalo.

Ilikuwa mara yangu ya pili kufika Baghdad. Mara ya awali ilikuwa 1971 wakati wa Rais Ahmed Hassan al Bakr. Saddam Hussein alikuwa makamu wake. Kwa hakika, muda wote wa miaka 11 ya urais wa al Bakr, mtu aliyekuwa na nguvu za utawala alikuwa Saddam.

Hatimaye, Saddam aliushika rasmi urais mwaka 1979 baada ya kujiuzulu al Bakr. Saddam naye alitawala kidikteta hadi Irak ilipovamiwa na Wamarekani. Alipinduliwa rasmi Julai 9, 2003 siku Wamarekani walipoiteka Baghdad na kuanza kuikalia ardhi ya Iraq.

Safari yangu ya pili Baghdad ya mwaka 2017 haikuwa ya utulivu kama ya mwanzo. Hata hivyo, jiji hilo halikuwa na umwagaji damu kama aliokuwa akiuelezea Sinan na wenzake kwenye ripoti walizokuwa wakituletea. Baghdad lakini ikitetemeka; hofu ilitanda jiji zima.

Mimi na wenzangu tuliohudhuria mkutano wa ugaidi tulijikuta tukilindwa kwa hadhari kubwa walizochukua wenyeji wetu. Miongoni mwetu walikuwako waandishi na wachambuzi maarufu wa siasa za kimataifa kina Sharmine Narwani, Ahmed Versi, Patrick Cockburn na Pepe Escobar.

Tulipata fursa ya kukutana na baadhi ya viongozi wa Iraq waliotueleza kwa kina jinsi walivyowashinda magaidi wa Da’esh (waliokuwa wakijiita Dola la Kiislamu). Tulibahatika kupokewa na kuzungumza na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa kaimu wa mkuu wa jeshi la mgambo la al-Hashd al-Sha‘abi. Jeshi hilo, kwa hakika, na sio Wamarekani, ndilo lililowashinda nguvu magaidi wa Da‘esh. Jeshi lenyewe liliyajumuisya makundi 67 ya wapiganaji. Wengi wao walikuwa Mashi‘a, lakini pia walikuwemo Masunni, Wakristo na wafuasi wa madhehebu ya Yazidi.

Majira ya saa saba za usiku tarehe 3 Januari 2020, Wamarekani walimuua Abu Mahdi al Muhandis karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Walimuua kwa droni pamoja na Jenerali Qasem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa majeshi ya kimapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi mwengine aliyetualika kwa mazungumzo Baghdad Oktoba, 2017 alikuwa Dkt. Ibrahim al Jaafari, waziri wa mambo ya nje. Al Jaafari aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya mpito iliyoundwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2005 na iliyodumu hadi 2006. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa Iraq waliokuwa uhamishoni London wakati wa utawala wa mabavu wa Saddam Hussein. Ingawa aliipinga Marekani kwa kuivamia nchi yake, hata hivyo alirudi kwao mwaka huohuo wa 2003 Wamarekani walipoingia Iraq na kumpindua Saddam.

Hivi karibuni gazeti moja la kimataifa la Kiarabu liitwalo Asharq al-Awsat (yaani Mashariki ya Kati) lilichapisha maelezo ya bwana mmoja aliyekuwa na usuhuba na Saddam na aliyewahi kufanya naye kazi.

Bwana huyo, asiyetaka jina lake litajwe kwa sababu za usalama, ameeleza mambo yenye kushangaza kuhusu siku za mwisho za utawala wa Saddam. Kwanza, amesema kuwa baada ya Saddam kupinduliwa alikutana naye mara mbili. Mara ya mwanzo, ilikuwa mjini Fallujah siku mbili baada ya Baghdad kutekwa. Mara ya pili walikutana Baghdad miezi minne baadaye. Saddam alikuwa mbioni baina ya miji hiyo akiwaongoza wapiganaji dhidi ya Wamarekani.

Bwana huyo pia amesema kwamba pale sanamu la Saddam lilipokuwa likiangushwa na kifaru cha jeshi la Marekani katika Uwanja wa Firdous, Baghdad, mwenyewe Saddam hakuwa mbali na hapo.

Usiku ule Saddam aliongoza shambulizi la mwanzo karibu na hapo dhidi ya Wamarekani waliokuwa wameuzunguka Msikiti wa Abu Hanifa katika mtaa wa Adhamiya.

Msikiti huo umelizunguka kaburi la Abu Hanifa, anayejulikana kwa lakabu ya Imam al A’dham yaani Imamu Mkuu. Imamu huyo ndiye aliyeyaanzisha madhehebu ya Kisunni ya Hanafi.

Mapambano yalipopamba moto wasaidizi wake Saddan walishtuka walipomuona akilikaribia eneo la mapigano akiwa amebeba kombora. Wasaidizi wake walimzuia asijitose kwenye mapigano. “Tunataka uendelee kutuongoza,” walimwambia. Baadhi yao waliamini kwamba Saddam akitaka afe usiku ule ili awe shahidi. Mapigano yaliendelea hadi alfajiri ya Aprili 10.

Halafu Saddam akaelekea Heet katika jimbo la al Anbar ambako alilala kwenye nyumba ya mwanachama wa chama chake cha Ba’ath mpaka siku ya pili alipoelekea kwenye viunga vya mji wa Fallujah.

Aprili 11, Saddam aliitisha mkutano wa watu watano akiwemo huyu bwana aliyeyatoa maelezo haya. Saddam aliuliza kuhusu hali ya Fallujah na kuwapo kwa wanajeshi wa Marekani katika Anbar.

Alipoambiwa kwamba Wamarekani walikuwa wakiingia katika nyumba za watu Fallujah, Saddam kwa ukali alisema: “Watoweni.”

Lakini Saddam aliwataka wafuasi wake wawe wavumilivu kwa vile, alisema, vita vitadumu kwa muda mrefu. Aliwaambia lilikuwa jukumu lao kuwachosha Wamarekani na kuwashambulia kila mahala. “Wawekeeni mitego barabarani muwashambulie wajuwe kwamba Iraq si ya kuchezewa,” aliwaambia.

Wakati wa mkutano huo mtu mmoja alisema kwamba baadhi ya wapiganaji wa Kishi‘a walianza kuwashambulia wale wenye kuwapiga vita Wamarekani. Saddam haraka alimkatiza akisema kuwa Mashi‘a ni Wairaqi kama wao na kwamba wasilaumiwe kama jamii nzima kwa vitendo hivyo.

Halafu Saddam akaondoka.

Siku ya pili yake asubuhi Saddam alikutana na wahasibu wa ofisi yake kwenye viunga vya Dora, Kusini mwa Baghdad. Walimpa pesa za Kimarekani dola milioni moja na laki mbili na hamsini. Saddam alishikilia lazima atie saini karatasi iliyothibitisha kwamba alipokea fedha hizo zikiwa mkopo wa kugharimia mashambulizi dhidi ya Wamarekani.

Julai 18, kijana mmoja alimwendea huyu jamaa aliyetoa haya maelezo kwenye gazeti la Asharq al Awsat, akampa miadi afike mahala fulani Adhamiya baada ya sala ya alfajiri. Alipokwenda alimkuta Saddam na wenzake wanne. Saddam alikuwa na bastola. Alisikitika kwamba baadhi ya majimbo ya Iraq hayakupambana na wavamizi wa Marekani kama yalivyoahidi.

Saddam pia aliuponda msimamo wa mataifa ya Kiarabu na alisema alivunjwa moyo na Syria.

”Bashar al Assad aliniahidi kwamba Syria itaiunga mkono Iraq risasi ya mwanzo itapofyetuliwa. Lakini alighairi.”

Kuporomoka kwa Saddam kulianza saa nne na nusu za usiku wa tarehe 6 Aprili, 2003. Hapo ndipo vifaru vya kijeshi vya Marekani vilipofika Ikulu na mbele ya Rashid Hotel.

Simu ya Jenerali Tahir Habbush, mkurugenzi wa usalama, ililia. Upande wa pili alikuwa Luteni Jenerali Abid Mahmud, katibu muhtasi wa Saddam. Mahmud ndiye pekee aliyekuwa akipokea amri za Saddam na akimfikishia ujumbe.

Aliyoyasema Mahmud yalitisha.

Alimuamrisha Habbush afanye upelelezi kwenye barabara mbili — ya kutoka Baghdad kuelekea Salahuddin na ya kutoka Baghdad kuelekea Diyala na aseme ipi iliyo salama kuondokea Baghdad pakitokea dharura.

Habbush akamjibu hivi: “We unadhani nina vikosi vya kijeshi vitavyoweza kuzidhibiti barabara hizo mbili?”

Mahmud naye akamjibu kwa kumtisha na akaibwaga simu.

Habbush alimtajia mkurugenzi wa makao makuu ya usalama kuhusu kadhia hiyo. Wote wawili walishangaa. Wakasema kwamba lazima Saddam ataondoka Baghdad akaongoze mapigano dhidi ya Wamarekani kutoa nje ya jiji hilo.

Jenerali Habbush hakuwa na hila ila kutekeleza amri ya Saddam. Alijua kitachomfika akimkasirisha Saddam.

Habbush aliondoka usiku kuelekea mji wa Tarmiyah katika jimbo la Salahuddin kufanya mwenyewe upelelezi. Aliikuta barabara iko wazi na salama.

Kwa vile simu zilikuwa haziingii Baghdad alimtaka mwenzake Kanali Mahmoud arudi mji mkuu na atumie simu ya ofisini mwake kumuarifu katibu wa Saddam kwamba barabara ya kuelekea Diyala ilikuwa wazi na hapakuwa na hatari. Alitaka pia amwambie kwamba yeye mwenyewe atarudi Baghdad katika muda wa saa chache.

Alipofanya upelelezi katika ile barabara nyingine, Jenerali Habbush aliona mlolongo wa magari, na kulikuwa ishara kwamba ndege za Marekani zilitupa mabomu kwenye barabara hiyo. Kwa hivyo, safari ya kwenda Baghdad ilikuwa ya hatari kubwa.

Majira ya saa sita za usiku, Habbush alikata shauri asirudi Baghdad kwa vile Saddam mwenyewe alikuwa analihama jiji hilo. Aliizima simu yake akamua kwenda kujiunga na mapigano dhidi ya Wamarekani.

Yaliyomfika Saddam hayahitaji maelezo; sote tunayajuwa.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Mwandishi ni mwanahabari mwandamizi aliyefanya kazi hiyo kwa takribani miongo mitano.

Screenshot_20230606-115435_Chrome.jpg
 
Ahmed Rajabu, moja ya tunu za kitanzania kwenye tasnia ya habari, ni kati ya wanahabari wa kuaminika sana. Anapolieleza jambo, hujenga picha ya kueleweka kwa haraka na kama msomaji akitazama filamu.

Nimekuwa nikimfuatilia sana kama mchambuzi redioni na runingani; mwandishi magazetini na hata sasa anabakia kuwa Mchambuzi mahiri wa siasa za Mashariki ya Kati. Anajua anachokisema. Mungu amjaalie zaidi na zaidi!
 
Back
Top Bottom