Ni migomo, maandamano bila kikomo

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
2.jpg

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mh Freeman Mbowe

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza kuwepo kwa maandamano bila kikomo nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba waliloliita la kifisadi linaloendelea mjini Dodoma.

Pia, kimeazimia kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais ifikapo mwakani, lengo likiwa kuung'oa utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliowafanya watanzania kuwa maskini wa kutupwa.

Akihutubia mkutano mkuu wa uchaguzi, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alisema umefika wakati sasa wa kuacha kukaa na kuzungumza na kwani kinachoendelea Dodoma ni wizi na ukatili wa hali ya juu kwa wananchi wanyonge ambao ndio walipa kodi.

"Samahani maneno yangu ni makali na wala hapa sifanyi uchochezi…kinachoendelea Dodoma ni ufisadi na wizi, tumekaa Kinana, tumekaa na Mangula, tumekaa na Rais Kikwete tumekubaliana bunge lisitishwe lakini wanamwacha Sita afanye anachotaka kama utafikiri ndiye Rais…

"Anachakachua rasimu, anabadili kanuni, anavunja sheria anakusanya maoni utafikiri yeye ni Warioba…hiki hakivumiliki, naomba mkutano huu utoke na tamko," alisema Mbowe na kushangiliwa na wajumbe wakiafiki.

Mbowe akipendekeza maadhimio, alisema kinachotakiwa ni kuungana na kufanya maamuzi ya kuandamana nchi nzima kushinikiza kusimamishwa kwa Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma ambalo linafuja fedha za wanyonge ili hali katiba haitapatikana.

Mwenyekiti huyo, alisema Katiba haipatikani kwa kura au wingi wa watu, bali hupatikana kwa maridhiano na hivyo kuwataka wabunge wanaoendelea na vikao hivyo Dodoma kusitisha mara moja.

"Hatuwezi kukaa kimya huku maoni ya watanzania yakiwa yanachakachuliwa, hivyo basi tutashirikiana na taasisi mbalimbali, UKAWA kufanya migomo na maandamano nchi nzima bila kikomo… aidha kuwa na kibali cha Polisi au laa na kwamba kuna watu watakaokuwa mstari wa mbele watajeruhiwa, lakini lengo likiwa kufikisha ujumbe wenye sura ya wananchi," alisema Mbowe.

Alisema kila eneo lazima liwe na mkakati wake wa kuhakikishav
maandamano yanafanyika bila kikomo, hivyo mara baada ya mkutano huo mkuu viongozi watakaporejea maeneo yao waanze kuwandaa wananchi wakati wakisubiri maelekezo zaidi baada ya viongozi waounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi litakapokutana.

Pia, aliwataka wanasheria wa CHADEMA kukutana na kuangalia jinsi kufungua kesi kwa wabunge wanaoendelea kufanya mikutano ya katiba Dodoma, kwa kuwa ndio adui wakubwa wa taifa na kwamba, siasa ifanyike katika majimbo yao ambayo wametoka ili kuhakikisha mwakani hawarejei.

Aidha, alisema katika uchaguzi mkuu ujao, watahakikisha wanajipanga kusimamisha mgombea mmoja kutokana na UKAWA, ambaye wanaamini atawawakilisha vyema na kuhakikisha wanaiondoa CCM madarakani.

Aliongeza kuwa, umaskini unaonekana sifa ndani ya CCM na kwamba, wengine wanapata sifa kujitambulisha wao ni watoto wa wakulima na kujifanya maskini, jambo ambalo aliliita si sahihi kuwakashifu wakulima.

Alisema ni lazima watanzania kuuchukia umaskini na kila mmoja anatakiwa kupambana kuiondoa CCM iliyowafanya watanzania kuwa maskini wa kutupwa.

"Umaskini ni laana katika jamii… lakini hatuwezi kuwachukia maskini ila tunachukia umaskini na watanzania msikubali kurudi nyuma katika mapambano haya, ni vyema tukaungana kuhakikisha tunaupiga vita umaskini huo," alisema Mbowe.

Hata hivyo, alisema katika uchaguzi huu kulikuwa na propaganda kali, ambazo CHADEMA waliweza kuzizuia ikiwa moja wapo ni kufadhiliwa fedha na wazungu, jambo ambalo alisema si kweli na wengine walipandikiza wagombea ili mradi watumike katika kuharibu chama.

Alisema kuwa chama cha siasa si ofisi kubwa wala majengo na kwamba, siasa ni fikra njema itakayojengwa kwenye vichwa vya wananchi.

Hata hivyo, aliwatoa hofu watanzania kuwa kuogopa ni dhambi kubwa kwa sasa na kwamba, kinachotakiwa ni kupambana vilivyo.

Awali kabla ya kuanza kuhutubia, Mbowe alianza kwa kuwakumbuka viongozi na wanachama mbalimbali wa CHADEMA ambao wametangulia mbele kabla ya kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka.

Akizungumzia juu ya waliopoteza maisha, Mbowe aliwatia simanzi wajumbe na wageni waalikwa, pale alipoelezea tukio la Mwandishi wa Habari Daud Mwangosi aliyeuwawa na bomu la polisi Nyololo mkoani Iringa na tukio la bomu wakati akifunga mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa madiwani jijini Arusha.

"Wale watoto walinifia mimi…maana walikuja kunisikiliza na Msajili (Jaji Mutungi), naomba niseme hapa, narudia waliorusha bomu ni Polisi, walikuwa wametulenga mimi na mheshimiwa Lema, ila Mungu alitunusuru," alisema kwa uchungu Mbowe huku akiongeza kuwa;

Hata Mwangosi aliuawa kwa maelekezo ya Polisi na zawadi aliyopewa aliyekuwa wa Iringa ni kupandishwa cheo!

Kauli hizo ziliwafanya wajumbe kuwa kimya huku wengine wakishika tama kwa huzuni.

DK. SLAA

Naye Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk.Willbroad Slaa, awali akimkaribisha Mbowe, alisema kuwa hali ya watanzania ni ngumu kila kukicha kutokana na ufisadi mkubwa unaoendelea.

Alisema kutokana na viongozi wenyewe wa serikali kushiriki katika kufanya ufisadi huo, kumesababisha hata wahusika wakitajwa hawachukuliwi hatua yoyote.

"Watanzania ni maskini sana na ufisaidi unaofanyika kwa sasa ni mkubwa, umetoka kwenye ule wa EPA sasa umehamia kwenye akaunti ya Escrow ambao mkubwa zaidi na wakubwa wa serikali wanahusika kwa namna moja ama nyingine, ndio maana wanashindwa kutoa kauli," alisema Dk. Slaa.

Aliwaasa wajumbe wa mkutano huo mkuu wa uchaguzi, kwamba wasitegemee kura zao kwamba zitasimamiwa na CCM kwa sasa na kwamba, ifikapo mwaka 2015 kila mwanachama ahakikishe wanasimamia wenyewe kura ili kuing'oa madarakani.

Aidha, alisema nchi kwa sasa imekosa wazalendo kwa kuwa kila kukicha ni ufisaidi na kwamba, nguvu ya umma inahitajika.

"2010 CCM iligeuza akina mama kuwa mabango kwa kuwavalisha nguo za mgombea wao, lakini sasa wamewaacha kuwa maskini wa kutupwa hakuna tena maisha bora kwa kila mtanzania, bali maisha magumu kwa kila mtanzania," alisema Dk.Slaa.

Alisema CCM haina uwezo wa kurekebisha chochote na kwamba watanzania wenyewe wanatakiwa kufanya mabadiliko ya kweli bila woga, kwani ndani ya miaka 50 kimeshindwa.

Pia Dk.Slaa alikumbushia mauaji mbalimbali yaliyosababishwa na Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na yale ya Iringa ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi na jijini Arusha, ambayo alisema IGP alihusika na ushahidi wanao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, CUF, NCCR Mageuzi, NLD, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwakilishi wa Takukuru, mabalozi wa nchi mbalimbali na vyama rafiki vya CHADEMA kutoka Denmark na Ujerumani.

PROF. LIPUMBA

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba, akizungumza katika mkutano huo, alisema kwa sasa nchi ipo njia panda kutokana na rasimu ya katiba ya iliyokuwa tume ya Jaji Warioba kuchakachuliwa na CCM.

Alisema kwa sasa kinachofanyika Dodoma ni wizi na ufisaidi na kwamba, haiwezekani kupata katiba bora kwenye hali ya ufisadi na tamaa za fedha ambazo CCM wanazifanya.

Alisema vyama ni kama nyenzo na kwamba, kwa sasa wanachohitaji ni kuwepo kwa haki za kijamii, siasa, uchumi na rasilimali zitumiwe na wananchi wenyewe.

Lipumba aliwahakikishia wajumbe kuwa, wanasubiri maazimio yao na CUF watayaunga mkono.

Lipumba, alitia fora kwa vibwagizo vya salamu za vyama hivyo kuanzia Peoples Power, Haki…Sawa… Haki Sawa, Pamoja Tutashinda na kumalizia na ya UKAWA Tumaini jipya na kuamsha shangwe ukumbini.

MBATIA

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, mbali ya kumpongeza Mbowe kwa kuiimarisha CHADEMA hadi mafanikio iliyofikia na kubainisha kuwa si kazi rahisi, alisema UKAWA
wameanzisha historia mpya na ili kuweza kuwa na viongozi bora na makini, ni lazima kila mmoja aweze kumuamini mwenzake.

Alisema nchi ya Tanzania ni ya wote, lakini cha ajabu watu wachache wanataka kuvuruga amani huku akitolea mfano wa makubaliano yaliyofanyika na Rais Kikwete mjini Dodoma kuhusu katiba mpya.

Alisema wanashangaa wakiwa mjini Dodoma, walikubaliana Bunge la Katiba linaloendelea liahirishwe lakini baadaye linaendelea kinyume na makubaliano yao.

MAKAIDI

Naye Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, alisema UKAWA ni tumaini la watanzania ndani ya CHADEMA, hivyo aliwataka kufanya uchaguzi utakaozingatia demokrasia huku akiupongeza uchaguzi uliopita wa Baraza la Wanawake (Bawacha).

MANGULA

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula, licha ya kupata kigugumizi kutaja salamu ya Peoples Power, alisema siasa sio ugomvi bali ni tofauti katika sera na itikadi, hivyo kuwataka CHADEMA kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano.

Alivitaka vyama vya siasa kujenga utamaduni wa kuvumiliana kisiasa kwa kila chama na kila mmoja, ili kudumisha amani na upendo.

"Siasa ni kama Simba na Yanga na hapa mpo Simba Yanga…mkiwa uwanjani kule ni balaa lakini mbona hapa mko pamoja, hivyo hivyo siasa, lakini nashangaa kwenye siasa kwanini haiwi hivi, hivyo tubadilike na tuvumiliane huku tukiweka utaifa mbele," alisema Mangula ambaye alibainisha kuwa pia amemwakilisha Rais Kikwete.

Aidha, alipongeza mpangilio wa mkutano huo na kukiri kuna kitu kajifunza.

MKURUGENZI WA TCD

Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Daniel Loya, aliisifu CHADEMA kwa kufanya uchaguzi mara muda
unapofikia na kwamba, hiyo ni ishara tosha kuwa kuna demokrasia ndani ya chama hicho.

TAKUKURU

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maria Mosha, alisema kinachohitajika ni utulivu na mshikamano ili kudumisha amani ya nchi iliyopo.

MSAJILI WA VYAMA

Alianza kwa kubainisha kuwa, salamu ya CHADEMA anaijua, ila hatoweza kuwasailimia hivyo kwa kuwa ‘anabalance' kwani ni mlezi wa vyama vyote.

Alikipongeza chama hicho kwa kudumisha demokrasia na ni jukumu lake katika kuhakikisha vyama vinafanya mikutano pamoja na chaguzi mbalimbali.Aidha, alisema yeye anaamini vyama vya siasa vipo katika kuimarisha na kulinda amani nchini.

MWAKILISHI WA ODM

MWAKILISHI kutoka nchini Kenya, Mbunge wa Chama cha ODM, Injinia Nicholaus Gumbo, aliyemwakilisha Raila Odinga, alisema nchini Kenya wanajua tofauti zao za kikabila lakini wanaishi kama ndugu.

Pia, alisema wanafahamu watanzania wanahitaji katiba mpya, hivyo Kenya wanawaunga mkono na kwamba wapo bega kwa bega huku wakiwataka wasichoke katika kupambana.

UMOJA WA ULAYA

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Filiberto Sebregondi, aliipongeza CHADEMA na kuitaka kuendelea kufanya vizuri katika chaguzi zake mbalimbali.

MWENYEKITI IDU

Mwenyekiti wa IDU, John Howard, alisema siasa zina changamoto nyingi na kwamba vijana wengi wanahitaji mwongozo na kwamba bila kuwa na msimamo hawawezi kufanya maamuzi yoyote.


Chanzo: Tanzania Daima
 
hayo maandamano na migomo yaanzie moshi,yaende tengeru kisha yaende pemba halafu mbowe awe mbele
 
lipumba na akina mbatia leo wamegeuka lulu ya chadema kutaftia umaarufu wa upinzani, hamkumbuki mlivyowatukana mkawaita majina ya ajabu ajabu sasa yamewakuta Chadema mnatafuta pa kutokea. Tulia mfe na tai shingoni si mlijifanya mnaweza peke yenu hapo awali?
 


…kinachoendelea Dodoma ni ufisadi na wizi, tumekaa Kinana, tumekaa na Mangula, tumekaa na Rais Kikwete tumekubaliana bunge lisitishwe lakini wanamwacha Sita afanye anachotaka kama utafikiri ndiye Rais…

"Anachakachua rasimu, anabadili kanuni, anavunja sheria anakusanya maoni utafikiri yeye ni Warioba…hiki hakivumiliki, naomba mkutano huu utoke na tamko,"
Jamaa kajivalisha koti jipya la Ujumbe wa Tume ya Katiba - Sasa anakusanya maoni sijui mwezetu anatumia sheria ipi? Kwa hili CDM nawaunga mkono kuandamana bila ukomo kama watagoma kulisitisha Bunge hili!!
 
waje barabarani wakutane na virungu vya IGP MANGU
mna police wangapi, washawasha ngapi, mabomu mangapi kuzuia watu mil 20 barabarani kila wilaya? cha msingi waambieni walioko Dodoma kwamba Rais kashasema mchakato basi tena kwa awamu ya nne.
 
mna police wangapi, washawasha ngapi, mabomu mangapi kuzuia watu mil 20 barabarani kila wilaya? cha msingi waambieni walioko Dodoma kwamba Rais kashasema mchakato basi tena kwa awamu ya nne.

Hao watu mil 20 wapo wapi? na wanatoka wapi na kwenda wapi? mbona ni wengi mno?
 
Habari viongozi wa juu wa chama? Kwanza napenda kuwapongeza kwa kupitisha azimio zito lililoteka hisia watanzania wengi hata serikali na jeshi la polisi si haotu bali hata wajumbe wa BMK pia wamestushwa na azimio lenu la migomo na maandamano nchi nzima tena isiyo na kikomo. Najua madhara ya azimio lenu mnayajua na baadhi mwenyekiti aliyataja.

Sasa kwakuwa mkutano mkuu chadema ni kundi kubwa ambalo na kwa sasa mkopamoja Dsm kwanini msitupe hata mfano wa maandamano ya kupinga bunge hili ili mnaporudi katika maeneo yenu mnakuwa mmepata uzoefu wa vipi mtaendesha maandamano hayo bila kikomo. Na pia itawapa moyo wanainchi kuwa mko serious na azimio lenu. Wananchi wanatamani wapate mfano ili wajipange tena viongozi wakuu wawe mstari wa mbele angalau kwa siku 3 ili tu learn from you .
 
Maandamano ni haki ya kikatiba Duniani kote na hivyo ili kuwakumbusha watawala majukumu yao njia pekee ni maandamano na migomo. Mimi kama kiongozi nitayaunga mkono na nitakuwa msitari wa mbele, niungane na MBOWE ni bora kujitolea kufa ili kuandaa mazingira ya vizazi vyetu baadaye hata kama si kwa risasi nitakufa tu. Biblia inasema nimewapa mamlaka ya kukanyaga Ng'e na Nyoka na silaha yoyote itakayo inuka juu yako haitafanikiwa, lakini pia maneno ya Mungu juu ya Joshua yananitia moyo anasema "UWE HODARI NA MOYO WA USHUJAA HILO TU" so niko tiaria kufa kwa maslahi ya mtu mweusi. Nawaomba MBOWE na UKAWA kupanga haya maandamano na migomo kimkakati yaani kuwepo maeneo ya LEVEL SQURE ambayo yataunganisha watu katika maeneo yote nchini na siyo kuandamana na kulandalanda kwenye miji nchini. Masharika ya uma ambayo yatakubali kuungana na uma wote tukutane sehemu moja LEVEL SQURE na kupaza sauti zetu huku vyombo vya usalama na ulinzi vikitulinda. Mimi nitaandaa Mwanza na viunga vyake Ahsateni sana UMMA.
 
jina lako nani unaitwa?nakuchangia fedha ya kuhamasisha vurugu nitumie namba yako nikutumie tigo pesa
 
Kama kweli wanatupenda watanzania mbona sijawahi kuwaona wakisifia mafanikio yaliyofikiwa na serikali kama vile ujenzi wa barabara za lami, viwanja vya ndege, kivuko, sekondari, afya n.k badala yake wao hulaumu kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 6 usiku? Kama kweli ni waungwana na wanapingana mtu mmoja kuwa na kofia zaidi ya moja (kujilimbikizia madaraka), mbona ni wabunge, wenyeviti wa vyama vyao? WAPENDA AMANI, SALAAM!

Nimefuatilia kwa karibu sana juu ya uelekeo wa nchi yetu katika mukitadha wa kisiasa hasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Nimepata kuwatafakari pia kwa karibu akina Mbowe, Lipumba na Mbatia nikagundua kwamba wanajifanya kupigania watanzania katika majukwaa na mbele ya vyombo vya habari ikiwa ni janja ya njani kutaka waaminiwe kisha wahujumu mali za taifa. Ili kufikia maamuzi haya nijiuliza na kuuliza watu wenye akili maswali yafuatayo:


  • Kama kweli Lipumba, Mbowe na Mbatia ni watu wenye uzalendo wa kisiasa ulijengwa juu ya misingi ya kidemokrasia, mbona wanaogopa ushindani ndani ya vyama vyao?


  • Kama kweli wanatupenda watanzania mbona wanahamasisha maandamano badala ya kuhamasisha wananchi kujitafutia kipato kupitia shughuli zao za kila siku?


MAONI:
Tusipopuuza huu ujinga na miwasho ya kutaka kuandamana naamini roho za watanzania wenzangu zitakuwa ni kafara za akina Mbowe, Lipumba na Mbatia. Niko tayari kuandamana kama viongozi hao wako tayari kuachia nafasi zao na kubaki na kofia moja. Aidha, niko tayari kuandamana kama familia zao zitatangulizwa mbele kwani ndizo zitakazofaidika na kile kinachotafutwa leo.

Naomba watz mpuuze huu mpango wa kiwendawazimu.
 
Kama kweli wanatupenda watanzania mbona sijawahi kuwaona wakisifia mafanikio yaliyofikiwa na serikali kama vile ujenzi wa barabara za lami, viwanja vya ndege, kivuko, sekondari, afya n.k badala yake wao hulaumu kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 6 usiku?

sasa wakisifia kitabadilika kipi? kama ni barabara zitabaki vilevile. ila kama hamna barabara wakiponda ndo vizuri ili serikali ishtuke.
 
Kama kweli wanatupenda watanzania mbona sijawahi kuwaona wakisifia mafanikio yaliyofikiwa na serikali kama vile ujenzi wa barabara za lami, viwanja vya ndege, kivuko, sekondari, afya n.k badala yake wao hulaumu kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 6 usiku? Kama kweli ni waungwana na wanapingana mtu mmoja kuwa na kofia zaidi ya moja (kujilimbikizia madaraka), mbona ni wabunge, wenyeviti wa vyama vyao? WAPENDA AMANI, SALAAM!

Nimefuatilia kwa karibu sana juu ya uelekeo wa nchi yetu katika mukitadha wa kisiasa hasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Nimepata kuwatafakari pia kwa karibu akina Mbowe, Lipumba na Mbatia nikagundua kwamba wanajifanya kupigania watanzania katika majukwaa na mbele ya vyombo vya habari ikiwa ni janja ya njani kutaka waaminiwe kisha wahujumu mali za taifa. Ili kufikia maamuzi haya nijiuliza na kuuliza watu wenye akili maswali yafuatayo:


  • Kama kweli Lipumba, Mbowe na Mbatia ni watu wenye uzalendo wa kisiasa ulijengwa juu ya misingi ya kidemokrasia, mbona wanaogopa ushindani ndani ya vyama vyao?


  • Kama kweli wanatupenda watanzania mbona wanahamasisha maandamano badala ya kuhamasisha wananchi kujitafutia kipato kupitia shughuli zao za kila siku?


MAONI:
Tusipopuuza huu ujinga na miwasho ya kutaka kuandamana naamini roho za watanzania wenzangu zitakuwa ni kafara za akina Mbowe, Lipumba na Mbatia. Niko tayari kuandamana kama viongozi hao wako tayari kuachia nafasi zao na kubaki na kofia moja. Aidha, niko tayari kuandamana kama familia zao zitatangulizwa mbele kwani ndizo zitakazofaidika na kile kinachotafutwa leo.

Naomba watz mpuuze huu mpango wa kiwendawazimu.

full of nonsense
 
Back
Top Bottom