Siasa imepenya kila mahali. Imeingia hadi kwenye mimbari na madhabahu za makanisa. Vyama vya wafanyakazi ni moja ya taasisi ambazo CCM, kwa ustadhi mkubwa sana, wamefanikiwa kupenyeza mapandikizi wao kwa maslahi yao binafsi.
Kiongozi wa TUCTA aliyemaliza muda wake, ndugu Nicolaus Mgaya, ni kada wa CCM kindakindaki. Huyu bwana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alijitosa kugombea Ubunge katika jimbo moja la uchaguzi nchini lakini aligalagazwa vibaya na kada mwenzake katika kura za maoni. Mrithi wa Mgaya TUCTA, ndugu Tumaini Nyamhokya, ni kada maarufu wa CCM. Aidha, Katibu Mkuu wa TUCTA Dr Yahaya Msigwa ni kada maarufu wa CCM na anashikilia nafasi kubwa ya uongozi ndani ya CCM mkoani Iringa.
Uwepo wa makada hawa katika nafasi za juu za vyama vya wafanyakazi haijatokea kwa bahati mbaya. Huu ni mkakati maalumu uliosukwa na CCM kupenyeza makada wake ndani ya vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kupoza makali ya madai ya wafanyakazi, ambao mara nyingi hudai madai yao kwa mtindo wa migomo na maandamano. Kuthibitisha hili, tangu makada hawa waanze kuongoza TUCTA, hawajawahi kuonekana hadharani kuishinikiza serikali yao ya CCM kuwalipa wafanyakazi stahiki zao mbalimbali, ikiwemo nyongeza za mishahara za kila mwaka, malimbikizo ya mishahara, kupandishwa vyeo, na madai mengine lukuki ambayo wafanyakazi wanaidai serikali.
Chama cha Walimu (CWT) kimefanikiwa kwa kiasi fulani kutetea maslahi ya walimu. Ndio maana CWT kinaonekana kuwa na nguvu kuliko vyama vingine vya wafanyakazi. Hata hivyo, bado chama hiki kinapata upinzani mkubwa kutoka TUCTA, inayoongozwa na makada wa CCM..
Akitokea kiongozi wa chama cha wafanyakazi asiyekuwa na chembechembe za CCM hupata misukosuko ya hapa na pale ili kumkwamisha na ikibidi hata “kumpoteza”. Sote tunafahamu kilichomkuta kiongozi machachari wa chama cha TRAWU, ndugu Silvester Rwegasira. Serikali siku zote inajitahidi kuwapachika makada wake ndani ya vyama vya wafanyakazi ili kutimiza azma yake ovu ya kukandamiza maslahi na haki za wafanyakazi hapa nchini.
Nini kifanyike?
• Mwanachama yeyote anayejitokeza kugombea uongozi wa TUCTA na vyama vingine vya wafanyakazi achunguzwe kama ni kada au la. Na ikiwa itafahamika kwamba mwanachama huyo ni kada, basi hicho kiwe kigezo kikubwa cha kumnyima kura au hata kumuangusha kwenye kura za maoni ili asipenye uongozini na kusaidiana na serikali yake kukandamiza haki na maslahi ya wafanyakazi.
• Wafanyakazi wasikubali kukatwa fedha za michango ya uanachama kwa kuwa fedha hizo zinaenda kuwanufaisha makada wa CCM ambao wamewekwa pale kwa maslahi mapana ya chama na serikali yao ghairi ya maslahi ya wafanyakazi.
• Wafanyakazi waangalie uwezekano wa kuunda vyama vipya vya wafanyakazi na kuachana na vyama vilivyopo kwani vimeshindwa kutetea maslahi yao kwa muda mrefu sana.
• Wafanyakazi waadilifu waliopo wafanye mapinduzi ya kuwaangusha viongozi waliopo na kisha kuwachuja kwa misingi ya ukada, ambapo wale makada dhahiri waondolewe moja kwa moja na makada nyemelezi watupiliwe mbali pia.
Malisa, G.J