Ndugu zangu,
KAMWE huwezi kukausha maji yatokanayo na chemchemi kwa kumwagia mchanga.
Na kuna namna mbili za mwanadamu kuula mkate, ama aukate slesi ( Slices) kwa maana ya vipande vipande, au aufakamie. Hilo la mwisho hufanywa na mtu mlafi, mtu mchoyo. Mtu mbinafsi.
Watanzania tuna bahati mbaya ya kuwa na baadhi ya viongozi wenye hulka za kibepari miongoni mwa jamii ya watu wengi wanaoishi maisha ya kijamaa. Viongozi wenye kuendekeza tamaa ya mali na hata kufikia kuwatelekeza wananchi wanaowaongoza.
Naam. Kwa Serikali kubinaifsisha yaliyokuwa mashamba ya taifa ya mpunga; Kapunga na Mbarali, kisha waziri mhusika, mwaka 2006 kujibu manunguniko ya wananchi kwa kuwaambia Serikali imeuza chake, ni sawa kabisa na kujaribu kuzuia maji ya chemchemi kwa kumwagia mchanga. Manunguniko ya wananchi hayakupungua, yanaendelea kutolewa. Ni chemchemi ya ukweli, haikaushwi kwa kumwagia mchanga.
Juzi hapa nilikuwa Mbarali. Nilifika hadi kijijini Nyeregete. Pale nikutana na kuongea na wananchi wenye kusikitishwa na namna Serikali inavyoshindwa kuwaelewa. Inahusu ardhi ya mashamba yao. Serikali imeyauza mashamba ya mpunga ya Kapunga na Mbarali kwa Wafanyabishara wawili kupitia makampuni yao; yaani Highlands Estates Limited kwa shamba la Mbarali, na Export Trading Company Limited, kwa shamba la Kapunga.
Kilimo kina falsafa yake. Mkulima ni shamba lake. Pale kijijini Nyeregete nilielewa zaidi, kuwa hakuna faraja na heshima kubwa kwa mkulima kama kurudi nyumbani akiwa ametoka shambani kwake. Na hakuna fedheha kubwa kwa mkulima kama kurudi kutoka kwenye kibarua cha shamba la mtu mwingine. Kwamba hana shamba. Kwa mkulima kutokuwa na shamba analolimiliki , hata kwa kukodi ni sawa na kupoteza sehemu ya uhai wake.
Mkulima hatachoka kupambana kulinda hadhi, heshima na utu wake. Kamwe, hukaushi chemchemi kwa kumwagia mchanga. Na hilo ni Neno langu la Leo.
( Hii ni sehemu ya makala yangu ya Raia Mwema ikichapishwa juma hili)
Maggid,
Iringa
Novemba 16, 2010
mjengwa