Nenda kapumzike Professor Assad wenye macho tumeona

chidy abidal

Member
Mar 4, 2015
6
4
Ilikuwa ni Jumanne tulivu kabisa iliyomshuhudia Prof. Mussa Juma Assad akichukua kila kilicho chake na kukabidhi vyote vya Serikali kwa Ndugu Charles Edward Kichere ikiwa ni ishara ya makabidhiano ya Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali nafasi aliyoihudumu kwa kipindi cha miaka mitano akichukua nafasi ya Ndugu Ludovick Utouh.

Profesa Assad kabla ya kuwa Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama vile Profesa mshiriki katika Idara ya Uhasibu katika Shule Kuu ya Biashara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mnamo mwaka 2013 pia Mhadhiri Mwandamizi wa masomo ya biashara hata huyu Charles Kichere alikuwa mwanafunzi wake.

Wakati naendelea kutafakari busara, hekima na misimamo ya Mzee huyu nadiriki kusema hiki ni ‘kisu cha bucha’. Ameiacha Ofisi akiwa katika ubora wake lakini akionyesha kila aina ya furaha na ukarimu kwa mrithi wake. Pengine labda ni kwa sababu ya ugumu na uzito wa kazi ya ukaguzi wa hesabu za serikali lakini kwa mila zetu Waafrika sijazoea kuona hivyo.

Mkulima huyu wa bamia hana makuu amekabidhi Ofisi ya Serikali kisha akapanda zake kwenye ‘IST’ akiwa na mkewe tu bila ya walinzi wala wasindikizaji akarejea zake nyumbani. Wazee wa kujimwambafai sasa mtu akimiliki mke tu tena aliyekuwa beki tatu wa familia yao anajaza walinzi wa kumlinda ama kweli ukiacha yale Mussa ya Firauni yanaendelea kustaajabisha.

Prof. Assad wakati anakabidhi Ofisi ya watu hakusita kututambulisha mkewe Bi. Ambaye ndiye mshauri mkuu wa Mzee wetu Prof. Assad huku akitanabaisha kuwa mengi anayoyafanya ni mawazo ya mkewe na mara zote alikuwa akimsihi atulie anapopitia vipindi vigumu ama kweli kuna watu wamependelewa aisee.

Ni ngumu sana kwa wakati tulionao kupata mke wa aina hiyo mke ambaye ana uwezo wa kumudu nyakati za furaha na huzuni. Sasa naanza kusadiki maandiko kuwa ‘Kila mtu atapata wa kufanana naye’ Prof. Assad amepata wa kufanana naye. Eti kuna mtu ananambia huyu Bibi yetu hajazaliwa kizazi hiki cha ‘tuma na ya kutolea’ ni wivu tu.

Sasa Prof. Assad anaenda kuwa mkulima mdogo mdogo kwa kizungu wanamwita ‘Peasant’ na kuwapa nafasi ya kupumua wale waliokuwa wameingia kwenye anga zake na wakapata cha mwana kuyataka. Nasikia kuna sauti inanielekeza niseme kidogo kuhusu kustaafu kwake nasemaje ‘mtego huo siuingii’

Sitaki hata kidogo kuzungumzia kuhusu kustaafu kwake maana mimi ni mdogo sana naanzaje kujadili stori za wakubwa huko juu? Ni mbaya mno kuingia kwenye mkumbo wa eti nasikia kastaafu kwa sababu ana ugomvi na mhimili fulani, eti ooh nasikia ni zile pesa za mheshimiwa kwenda kujitibia nje ya nchi na watu wanne. Hayo ya Kaisari nimemuachia kaisari acha nimuhubiri Mzee wangu Prof. Assad.

Profesa anaondoka Ofisini lakini kwa upendo mzito mno anawatetea wanaobaki kwa kumshauri mkaguzi mpya asifanye timua timua kama wafanyavyo viongozi wa vilabu vya soka la bongo. Profesa anaamini katika watu (Human resource) ili kuongeza ufanisi katika kazi ya ukaguzi wa hesabu za Serikali hivyo anamshauri mrithi wake kuwekeza katika kukuza uwezo wa watendaji wake (Capacity building).

Profesa naye ni binadamu hivyo naamini ana mapungufu yake lakini kwa ujumla itoshe kusema kwamba Wema wapo na wanaishi, Mungu huwapenda sana watu wema na kuwachukua mapema lakini hawa wachache anaotuachia wanatosha kuifanya dunia kuwa sehemu salama. Nenda Profesa nikipata namba yako nitaomba siku moja nije nikusalimie kijijini uendako.

RAJABU ATHUMANI
0715685395
Rajabuathumani123@gmail.com
 
Nenda salama mie mteja wako wa bamia nitakuwa nakuja kuchukua🤤🤤🤤🤤🤤
 
Nenda salama mie mteja wako wa bamia nitakuwa nakuja kuchukua
Ishara ya kukubalika kwake kwenye jamii ni ishara MUNGU naye anamkubali,pia na kinyume chake
Acha MUNGU aendelee kubaki katika sifa yake ,fikiria kama wewe ungepewa nafasi ya kuamua kama MUNGU ingekuweje? Au yeye,au Mimi .

Yote kwa yote MUNGU ameyaruhusu yatoke.
 
Back
Top Bottom