Nchi haijengwi kwa ubazazi na visasi

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Sep 20, 2021
3,214
3,587

Aidha ripoti ya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2013 iliyozinduliwa na Umoja wa Mataifa, ilibainisha zaidi ya nchi 40 zinazoendelea zilifanya vizuri zaidi ya matarajio katika maendeleo ya binadamu ndani ya miongo iliyopita karibuni, huku mafanikio yao yakiserereka pasina kushuka kasi na viwango ndani ya miaka 10 iliyopita nyuma ya 2013. Lakini changamoto kubwa iliyopo kwenye hali hii ni kwamba unapochambua mafanikio haya hutaweza kuona uwiano wa mafanikio ya nchi hizi dhidi ya mafanikio ya nchi zilizochangia mafanikio hayo kwa njia za kutoa fursa za masoko, uzalishaji na ugavi wa malighafi na pengine hata na uhakikishwaji wa nguvukazi rahisi kwa ajili ya mitaji (investments) ya mataifa hayo yaliyofanikiwa; mitaji yao ambayo iko kwenye mataifa ambayo hayakufanikiwa kwenye maendeleo ya binadamu kwa viwango vya jumuiya za kimataifa, na hii inabaki kuwa ushahidi wa msingi pia wa kuthibitisha mfumo huu mpya usio sawia na usio haki wa dunia hii. Lakini pia ni dhahiri kuwa nyingi ya nchi hizo zilizotajwa kufanikiwa zimeshindwa kutafsiri maendeleo zilizopata ya chumi zao; yaani kuzitafsiri kwenye mabadiliko ya msingi na makubwa ya mifumo yao (broader structural transformation) kupitia uundwaji wa fursa mpya za ajira maridhawa na upunguzaji wa umasikini na utofauti wa viwango vya maisha ambavyo ni viashiria vya maendeleo jadidi katika sehemu zingine za dunia na badala yake zimeendelea kuwa na changamoto kadha wa kadha za maendeleo. Baghosha!

Wapinzani mnatakiwa mtusaidie kufikia ndoto ya 2025 na siyo kufisha ndoto hiyo kwa kutufarakanisha na dola. Ikumbukwe kuwa Mhe. rais Magufuli (hayati) alikuwa na kazi nzito sana kama Mungu angempa awamu ya pili tena; kazi ya kuandaa dira nyingine mpya ya taifa kama dira hii iliyopo ya 2025 ingefikia ukomo wa uhai wake bila kufanikisha malengo yake. Hili ni zoezi linalohitaji kila mtu pasina kujali itikadi za vikundi-maslahi; kuheshimu na kutekeleza falsafa ya kazi tu, na siyo kinyume chake. Hakuna nchi duniani imewahi kuendelea kwa porojo na propaganda za siasa kwa asilimia kubwa huku ikipuuza umuhimu wa kujituma kazini na kutanguliza maadili na tunu za taifa. Japan baada ya kupigwa bomu la atomiki, walipochukua hatua ya kujenga nchi iliyokuwa ikizaa mapooza ya bomu hilo, waliafikiana kufuta likizo wakabakiza zile za dharura, ugonjwa na labda uzazi tu hivyo watu wote saa 24 (kwa shifti), siku 7 za wiki, siku 30 za mwezi, siku 365 za mwaka wako kazini. Israel ile, maisha ni kazi tu kasoro siku za ibada (sabato na Ijumaa/masjid) tu, lakini wote wanakuwa standby kwa sababu wako vitani tangu uhuru mwaka 1948 (vita yenye umri wa miaka 73 sasa). Falsafa na sera ya ulinzi na usalama ya Israel imeweka msisitizo kuwa kila raia wa rika linalotambuliwa na sheria kuwa mtu mzima ni askari, na wako watu milioni 8,296,000 tu (sensa ya 2014).

Chapisho dogo la tume ya mipango liitwalo The Tanzania Development Vision 2025 ambalo utangulizi wake umeandikwa na Mhe. rais muasisi wa dira hii Ben Mkapa (Big Ben) kwenye uk wa v-vii huku dibaji yake ikiandikwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango Mhe. Nassoro W. Malocho (MB) kwenye uk wa viii-ix inabainisha kwenye uk wa 13 malengo makuu ya dira ya maendeleo ya taifa 2025 kuwa ni: kufanikisha viwango vya juu vya maisha ya watu wa Tanzania, utawala bora na utawala wa sheria, uchumi imara shindanishi. Haya hayawezi kufanikiwa ikiwa watu watajengewa tabia ya uasi ya kusubiri kulishwa na wachache wanaojituma huku wengi wakishiriki harakati laghai za kisiasa zisizoweza kuwapa mikate mikononi au fedha mifukoni mwishoni mwa maandamano na mikutano ya kisiasa na hata ela ya matibabu ya majeraha ya makabiliano na vyombo vya dola kwenye maandamano haramu. Wenzetu wa upinzani ambao pia kama viongozi wa kiroho na makundi-maslahi mengine pia katika jamii pana walishiriki kujadili na kutolea maoni dira hii ilipokuwa ikiandaliwa; hawaelekei kufanya chochote cha ama kuunga mkono au kufanikisha malengo hayo ya dira ya maendeleo ya taifa 2025 kwa vitendo isipokuwa tu wameng’ang’ania lengo namba mbili (utawala bora na utawala wa sheria) kwa kulibebea bango kuwa halitekelezwi ipasavyo.

Lakini ukisoma vizuri lengo hilo linasisitiza kuwa jamii ya Tanzania inatakiwa kuzingatia maadili na utamaduni sawia, kuheshimu kwa msisitizo utawala wa sheria, kuondoa ufisadi na maovu mengine, kuweka bidii ya kujifunza kutokana na uzoefu wa ndani na nje ya nchi na kudhihirisha na kumiliki agenda yake ya maendeleo. Sote wakiwamo wapinzani tunajuwa kuwa wenye uweledi na jukumu la kuhakikisha amani na utangamano ni vyombo vya dola kwa sababu vimejengewa uwezo wa upelelezi/ukachero na ulinzi wa amani na usalama.

Hili ni jukumu lao la kikatiba na kwamba hata wapinzani wanajuwa kuwa wao hawana uweledi huo na ndiyo maana hata vipindi vya kampeni za uchaguzi huwa wanajiundia vikosi vyao na kuvijengea uwezo huo ili kuziba mapengo ya Polisi wachache waliopo. Sasa kama hilo liko wazi kabisa, shida iko wapi pale dola inaposema kuwa mikusanyiko hairuhusiwi kutokana na taarifa wanazopata za ujasusi/ukachero? Kwanini tufanye vitendo na vitimbi vya kutupeleka mahakamani kila mara na kesi hizo kuendeshwa kwa spidi ya ambulensi na kutolewa hukumu huku raia wa kawaida kesi zao zikiendelea kucheleweshwa kwa miaka mingi na kuwasababishia mateso makali yaliyopitiliza viwango vya unyama? Haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa. Uzalendo tafsiri yake nyepesi ni kutokuvunja sheria za nchi.

Kwa mujibu wa chapisho hilo dogo la tume ya mipango uk wa 6, na ijulikane leo kuwa Tanzania imepitia dira mbili tu za taifa, ya kwanza ikiwa ni kuleta uhuru na hapa watu wote walipokea na kutekeleza dira hii hata kama ni kupitia makundi-maslahi mengine japo kulikuwa na baadhi waliokosa kuelewa umuhimu wa falsafa ya “Uhuru na Kazi” na hivyo kutoshiriki kikamilifu kutekeleza dira hii ambayo ilikuwa isikamilike disemba 9, 1961 tu bali ilitakiwa iendeleze kazi kama falsafa pekee ambayo ingeweza kuzaa matunda (mkate) ya uhuru huo ambao ulikuwa ni wa bendera tu (wa kisiasa).

Baada ya kutoonekana matunda ya uhuru kama ilivyotarajiwa, taifa lililazimika kubuni dira nyingine ya pili ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ambayo ilibeba falsafa ya ukombozi wa uchumi-jamii (socio-economic liberation) likiwa na mkakati wa kudhihirisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kuondoa makupe na manokoa na kuweka milki ya uchumi mikononi mwa umma. Azimio hili lilipozikwa na Azimio la Zanzibar, tangia hapo taifa lilikuwa likienda bila dira yoyote ya maendeleo hali ambayo ingetafsiriwa kinyume na dhamira ya kuhakikisha amani na utangamano wa nchi.

Ndipo ilipotimu mwaka 1995, Big Ben akalazimika kubuni dira ya maendeleo ya taifa yenye lengo la kulifanya kuwa taifa la uchumi wa pato la kati ifikapo 2025 ambayo ndiyo Big Ben kaibuni na kuitekeleza, akampa rais JK kijiti naye akaitekeleza na kumkabidhi kijiti rais JPM ambaye kama Mungu angemrefushia uhai basi dira hii ingetimia mikononi mwake 2025. Nafikiri msomaji sasa unapata mantiki, picha na ramani kamili pale rais JPM aliposisitiza falsafa ya kazi, ukusanyaji kodi, ujenzi wa viwanda, ulinzi na usalama nk kuwa alimaanisha kuwa tunatakiwa tupae na siyo kukimbia kuelekea 2025. Taifa haliwezi kuingia uchumi wa pato la kati kama hakuna sekta ya viwanda, kama kodi haikusanywi ipasavyo ili kuondokana na kuombaomba na kukopakopa na kama ufisadi unalitesa taifa na kama falsafa ya kazi (Uhuru na Kazi) haipo au kama ipo basi haitekelezwi pia kama ulinzi na usalama hauhakikishwi; badala yake maandamano, mikutano ya siasa isiyoisha, utoro bungeni ambako ndiko bajeti na mipango ya kufanikisha dira hiyo inakojadiliwa, ujambazi, vibaka, ufisadi, ulawiti na ubakaji, mimba zisizotarajiwa, mfumo wa fedha na uchumi usiojumuishi, uwanja wa siasa kutokuwa sawia ndani na nje ya vyama nk.

Ni budi Watanzania wakajuwa kuwa Neema yoyote ile lazima kwanza itanguliwe na mapito. Kipindi cha mapito ya nchi ni hiki, baada ya hapa kama sote tutajitambua na kutoa ushirikiano kwa serikali yetu basi nina ujasiri wa kudiriki kutamka kwamba ni zamu ya Wazungu sasa kututamani kama ambavyo tumekuwa tukiwatamani kwa enzi na enzi. Mtu awaye yote yule anayejuwa kuwa haki huinua taifa lazima atauzuia ulimi wake kutoa malaumu dhidi ya hatua alizochukuwa Mhe. rais JPM wa awamu ya 5. Yeye mwenyewe Mhe. rais alikuwa akisisitiza kuwa hiki ni kipindi cha mpito (transition) na kwamba Watanzania wanatakiwa kubadilika fikra zao (change of mindset). Tutawezaje kuwa washindani wazuri katika Afrika Mashariki, SADC, Maziwa Makuu, COMESA, PTA na hata AU kama tuko tayari kupinga kila jambo jema lililofanywa na serikali ya awamu ya tano na kutaka kuendelea na uzembe, uvivu (ukiwamo wa kufikiri), ufisadi, upotofu wa maadili na tunu za taifa?

Imetupasa kukumbuka kwamba mgawanyiko wa dunia (polarization) ulioleta makundi ya kujihami kiulinzi na usalama (NATO na WARSAW PACT) uliletwa na migawanyiko midogomidogo ya madaraja ya maisha (stations of life) kwenye jamii na mataifa ya dunia na kuzaa makundi ya kujihami yaliyopewa majina UNIPOLAR na PIEPOLAR ambayo haya nayo yakaja kuzaa NATO na WARSAW PACT baada ya Amerika iliyokuwa ikijiita UNIPOLAR kugundua kuwa haiwezi kujihami yenyewe pasina kuwa na ushirika (NATO ikazaliwa). Amerika iligundua umuhimu wa ushirikiano kwa jambo liwalo lote lile chini ya jua, ndiyo maana haiendi vitani bila kuwa na mdau/mshirika chini ya mwamvuli wa NATO. Iliwahi kupata fundisho la hasara ya kupigana mwenyewe kule Vietnam ambako ilipoteza medani.

majwalaoriko@yahoo.co.uk
 
Huwezi kuwa mtu mwenye akili nzuri kwa kumsifia Magufuli mtu aliyetuharibia taifa letu kwa maamuzi mabovu, uonevu na ubaguzi mkubwa
 
Huwezi kuwa mtu mwenye akili nzuri kwa kumsifia Magufuli mtu aliyetuharibia taifa letu kwa maamuzi mabovu, uonevu na ubaguzi mkubwa.
Umesema ukweli kabisa. Anaye msifu Magufuli anastahili kupimwa akili.
 
Labda aliwaharibia nyie vyeti feki, mafisadi, walaji rushwa, wapiga madili, wavivu, wahujumu uchumi

Kiongozi anayetumia rasilimali za taifa kuendeleza kijiji alichozaliwa kamwe hawezi kuitwa mzalendo labda kama neno mzalendo lina maana tofauti.

Kiongozi anatumia vyombo vya usalama kunyanyasa raia wanaomkosoa ana stahili kuitwa jina moja tu “Dictator uchwara”
 
Back
Top Bottom