Naukumbuka mwaka wa 1957

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,915
30,259
NAUKUMBUKA MWAKA WA 1957

Alfajir.

Baada ya sala ya Alfajir wengi wetu tukirudi nyumbani kutoka msikitini kitu cha kwanza, Bismillah mkono unakwenda kwenye simu kuangalia kuna ujumbe gani.

Mimi simu yangu kuna program moja hata sijui imeingiaje lakini siichukii kwani hunipa mengi katika yale ambayo nina mapenzi nayo.

Alipokufa Natalie Cole, mtoto wa Nat King Cole taarifa ya kifo chake niliipata hapa.

Toka utoto wangu nikumuusudu baba yake, Nat King Cole.

‘’Ramblin’ Rose,’’ ‘’Nature Boy,'' ''The Good Times.''

Niko ndani ya KLM, Dar – London Heathrow mwaka wa 1991.

KLM tuliipa jina ''Keep Loving Me.''

Ndege ya usiku baada ya ''diner,'' wametuwekea movie.

Enzi hizo screen mbele si kila abiria na screen yake kwenye kiti.

Haya yamekuja baadae sana.

Taa zinawekwa ‘’dim,’’ anatokea Nat King Cole anaimba, ‘’Unforgettable.’’

Anaingia Natalie anampokea baba yake.

Hii ni ‘’duet’’ ya baba na mwana.
Raha juu ya raha.

Natalie Cole alikuja Uingereza mimi niko huko na akafanya show London Royal Albert Hall na alipiga baadhi ya nyimbo za baba yake.

Ukumbi ulijaa pomoni mimi sikuhudhuria niko mbali na London naishi kimji kidogo Wales.

Turudi 1957 nini kimenikumbusha mwaka huu?

Leo asubuhi nimefungua simu yangu taarifa iliyopo ni kuwa Don Everly kaka yake Phil Everly amekufa.

Hapo hapo akili yangu imerudi nyuma kwa kasi ya ajabu.

Nimerudi mtoto nina miaka mitano tunaishi Gerezani, Mtaa wa Kiungani nyumba ya tatu kutoka kwetu kona ya Kiungani na Mtaa wa Sikukuu kuna nyumba nzuri kushinda zote pale mtaani akikaa Mashado Plantan.

Kuna nyimbo za Kizungu nilikuwa nikizisikia kutoka nyumba hii zikipigwa, ‘’We Will Make Love,’’ ya Russ Hamilton na ‘’Devoted to You,’’ ya Everly Brothers wanamuziki ndugu wawili.

Nyimbo nyingine niliyokuwa nikiisikia ni, "Round the Bay of Mexico," ya Harry Belafonte.

Huyu Harry Belafonte nitakuja kukutanae na Sidney Poitier nje ya British Airways na nitawafata na kuwaomba, "Autograph."

Niko na mwenyeji wangu New York nakaa karibu ya Hudson River.

Mwenyeji wangu akanambia hapo nilipopanga mimi tukivuka mto tuko nje ya nyumba ya Belafonte.

Bahati mbaya mwenyeji wangu hafahamiani na Belafonte kwa hiyo hakuweza kunipeleka kwake.

Namkumbuka binti ya Mashado Plantan, Rita, mama yake alikuwa Mjerumani.

(Miezi michache tu iliyopita nimemuuliza dada yake Bi. Maunda Plantan Rita yuko wapi akaniambia amekufa miaka mingi nyuma).

Lakini sikuja kujua wapigaji wa nyimbo hizi hadi miaka mingi baadae sana.

Nyimbo hizi nikizipenda sana na dada yangu mkubwa wakati huo anasoma Girl School akiziimba pale nyumbani.

Yeye ni marehemu aliingia Form One Aga Khan Girls 1961 mwaka tunapata uhuru.

Dada yangu alikuwa mwanafunzi wa Mwalimu Blandina shoga wa mama yetu na akija hadi nyumbani.

Nawaona wote katika fikra zangu na wote wametangulia mbele ya haki miaka mingi sana iliyopita.

Mwaka wa 1957 mchana.

Nimekaa barazani nacheza peke yangu mara kaja kijana wa TANU kavaa shati la kijani anapita nyumba kwa nyumba anabisha hodi anachangisha sumni sumni kwa wananchi kwa ajili ya safari ya Mheshimiwa Julius Nyerere kwenda UNO kuleta uhuru.

Namuona mama yangu anatoa sumni anampa kijana wa TANU na aniingiza ndani ya kikopo kilichokuwa na tundu juu.

Watu wote wanaitana wanatoa kila mtu sumni wanazitia katika kikopo.

Huu ulikuwa mwaka wa 1957 safari ya pili ya Julius Nyerere UNO baada ya ile ya kwanza 1955.

Sikujua kuwa nilikuwa nashuhudia historia ya Julius Nyerere na uhuru wa Tanganyika kwa macho yangu na iko siku nitanyanyua kalamu yangu na kuiandika kwa wale ambao hawakupo kuisoma.

Sikujua pia kuwa nitakuja kumtafiti Mashado Plantan na nduguze na nitawatia katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

Ajabu ni kuwa kila kumbukumbu hizi zikinijia huwa zinakuja pamoja na nyimbo za wakati ule.

Nakumbuka katika gramafoni pale nyumbani kulikuwa na rekodi za Salum Abdallah bahati mbaya sikumbuki majina ila nyimbo chache kama, ‘’Nina Mpenzi Wangu Kibambawe,’’ ''Kawia Kawia Utamkuta Mtoto si Wako.'''

Lakini hadi leo kuna ‘’tune’’ za nyimbo za Salum Abdallah nakumbuka na maneno machache.

Iko siku nitakuahadithieni vipi nilivyokuwa nikicheza nyimbo za Septet Habanero ya Cuba na kuimba nyimbo yao moja nikiipenda sana, ''El Sonero,'' mama akinipigia makofi ya kunishadidisha nizidi kuonyesha staili zangu.

Naimba Kispanishi.

Mama yangu alikuwa na magazeti ya DRUM nilikuwa sijui kusoma lakini nikipenda kuangalia picha ndani ya gazeti hili za watu wamevaa suti nzuri na kofia za pama.

Wakati mwingine nikijaribu kuwachora.

Sikujua kuwa iko siku nitakuja kufahamiana na mwenye gazeti hili, Bwana Jim Bailey kwa karibu sana.

Wala sikujua wakati ule kuwa ile mitaa na majumba marefu ya ghorofa niliyokuwa nikiyaangalia katika DRUM nitakuja kuyaona Johannesburg kwa macho yangu.


Kubwa sana kupita yote ninayokumbuka katika miaka ile ya Kiungani ni mawili.
La kwanza ni ngoma ya kilua na la pili kupunga majini.

Mbele ya Mtaa wa Kiungani ni Mtaa wa Mbaruku.

Mtaa wa Mbaruku na eneo nyuma yake miaka ile ulikuwa uwanja mkubwa uliojaa miembe na minazi huu uwanja ukiuvuka unakutana na nyumba nyingi zilikuwa na mashine za kukoboa mahindi na mpunga.

Mbele ya hizi nyumba ni Arab Street sasa Nkrumah Road.
Neema inakaribisha israf.

Ilikuwa watu wakipeleka mahindi pale kusaga na punje nyingi za mahindi mengi zikimwagika chini.

Zilikuwa haziokotwi zitafagiliwa na kuja kuchukuliwa na gari la taka la Dar es Salaam Municipa Council kwenda kumwagwa dampo.

Sisi watoto hii ilikuwa moja ya sehemu yetu ya mchezo.

Tulikuwa tukienda kwenye zile sehemu za mashine tunaokota yale mahindi na tukirudi nyumbani tunawasha moto tunatengeneza bisi.

Hivyo hivyo ilikuwa kwa korosho.
Haziokotwi zikiwagika chini hizo zilikuwa tunaachiwa watoto tukachome tule.

Kama vile wale wenye mali hizi walikuwa wanajisemea kuwa hii tunawaachia watoto waokote.

Hii ni rizki yao hawa malaika wa Mungu.

Miaka mingi sijaona magunia ya mahindi wala korosho na sijui hii biashara inafanyiwa wapi.
Sehemu hii ndiko ilipojengwa SIDO (viwanda vidogo vidogo) hivi sasa lakini hapo zamani kulikuwa na malingo.

Hapa ndipo kilipokuwa kinapigwa kilua kila Jumapili ngoma ya Kimanyema.

Na ni siku ya Jumapili ndipo waganga walikuwa wanapunga majini katika mitaa mingi ya Gerezani.

Watoto tukipenda shughuli hii sana kwa kuwa ''kiti'' yaani anaepungwa akishapandisha shetani yule shetani analishwa vitu vitamu kama tende, halua, sukari guru kutoka kwenye chano.

Huwa hamalizi anakula kidogo na chano kizima tunapewa watoto.

Ikiwa kwenu kuna mgonjwa anataka kupungwa basi siku hiyo huchezi mbali na nyumbani.
Haya mambo sijayasikia kwa miaka mingi sana sasa.

Miaka imekwenda.
Ubongo unahifadhi mengi.

PICHA: Everly Brothers, Jim Bailey na Bi. Maunda Plantan na Mwandishi.

1629777077739.png


1629777126966.png

1629777159279.png


Huyo ni Bi. Maunda Plantan.

Mjukuu wa Chief Mohosh wa Kwa Likunyi, Imhambane Mozambique.

Chief Mohosh ndiye aliyeweka mkataba na Hermann von Wissman kuja Tanganyika na jeshi lake la mamluki wa Kizulu kuja kupigana na Bushiri bin Salim Al Harith wa Pangani na Chief Mkwawa wa Kalenga.

Bi Maunda ni mtoto wa Thomas Plantan aliyepata kuwa President wa TAA katika kipindi cha WW II.

Bi. Maunda alikuwa mwalimu na mwanamke wa kwanza radio announcer Sauti ya Dar-es-Salaam English Service.

Hawa ni ndugu na akina Sykes.
 
Mashallah!
Khabari kubwa!
Mzee Mohamed Said pongezi sana
Kwa makala zako nzuri zenye kuvutia na
Kufundisha mengi.

Kuna watu walikushauri uandike kitabu
Cha historia yako, mimi nakushauri
Tengeneza kitabu chenye mchanganyiko wa makala zako mbalimbali.
 
Sheikh Mohammed

Wallahi unatukumbusha mambo ya miaka ya khamsini na sitini na magramafoni, umeturudisha mbali.

Marehemu kaka yangu alikuwa nalo hilo basi akiweka santuri ya Miriam Makeba mimi zile nyimbo zote nilikuwa nikizijua kwa moyo (hata sijui nikisema nini).

Tulikuwa na muuza duka mbele ya nyumba yetu, siku moja alinipa zawadi ya peremende (siku hizo ilikuwa haiitwi pipi) kwa kufuatisha nyimbo ya Miriam Makeba vizuri kwenye redio.

Lakini wimbo wa Salum Abdulla ukiitwa 'chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako', au nimekosea?
 
Sheikh Mohammed,
Wallahi unatukumbusha mambo ya miaka ya khamsini na sitini na magramafoni, umeturudisha mbali.

Marehemu kaka yangu alikuwa nalo hilo basi akiweka santuri ya Miriam Makeba mimi zile nyimbo zote nilikuwa nikizijua kwa moyo (hata sijui nikisema nini).

Tulikuwa na muuza duka mbele ya nyumba yetu, siku moja alinipa zawadi ya peremende (siku hizo ilikuwa haiitwi pipi) kwa kufuatisha nyimbo ya Miriam Makeba vizuri kwenye redio.

Lakini wimbo wa Salum Abdulla ukiitwa 'chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako', au nimekosea?
Aiseee!
 
Sheikh Mohammed,
Wallahi unatukumbusha mambo ya miaka ya khamsini na sitini na magramafoni, umeturudisha mbali.

Marehemu kaka yangu alikuwa nalo hilo basi akiweka santuri ya Miriam Makeba mimi zile nyimbo zote nilikuwa nikizijua kwa moyo (hata sijui nikisema nini).

Tulikuwa na muuza duka mbele ya nyumba yetu, siku moja alinipa zawadi ya peremende (siku hizo ilikuwa haiitwi pipi) kwa kufuatisha nyimbo ya Miriam Makeba vizuri kwenye redio.

Lakini wimbo wa Salum Abdulla ukiitwa 'chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako', au nimekosea?
Biti...
Umepatia kabisa.
 
Nakushauri kasikilize nyimbo hizi mbili zikiwa zimeimbwa na Kenny Rogers. Ya kwanza ni Teenty years ago na ya pili ni Green green grass of home. Kisha safiri hadi Kilwa ukaangalie Msikiti wa zamani na historia yake
 
Mashallah!
Khabari kubwa!
Mzee Mohamed Said pongezi sana
Kwa makala zako nzuri zenye kuvutia na
Kufundisha mengi.

Kuna watu walikushauri uandike kitabu
Cha historia yako, mimi nakushauri
Tengeneza kitabu chenye mchanganyiko wa makala zako mbalimbali.
Dos Santos,
Kweli shinikizo linazidi kuwa kubwa kila uchao kuwa niandike kitabu cha maisha yangu.

Kinachonipa tabu ni kuwa nani atataka kusoma maisha ya Mohamed Said kafanya lipi?
 
Nakushauri kasikilize nyimbo hizi mbili zikiwa zimeimbwa na Kenny Rogers.Ya kwanza ni Teenty years ago na ya pili ni Green green grass of home.Kisha safiri hadi Kilwa ukaangalie Msikiti wa zamani na historia yake
Mig...
Green Green Grass of Home ya Tom Jones ni nyimbo naifahamu kwa miaka mingi.
Hiyo nyingine ya Kenny Rogers sijapta kuisikia.

Kilwa nimefika mara mbili.

1629833159764.png

Kilwa Kisiwani Msikitini mbele ya Kibla wa kwanza kushoto ni Prof. Issa Ziddy.
 
Dos Santos,
Kweli shinikizo linazidi kuwa kubwa kila uchao kuwa niandike kitabu cha maisha yangu.
Kinachonipa tabu ni kuwa nani atataka kusoma maisha ya Mohamed Said kafanya lipi?
Vitabu ulivyoandika kuhusu uhuru wa Tanganyika na vingine vingi, kila aliyesoma ana hamu ya kutaja kujua historia ya mwandishi wake.

Fahamu wengi tunataka kusoma historia yako kuna mengi tutajifunza.

Kuanzia kumbukumbu zako zilivyo kali, uandishi wako mzuri na ufahamu wa mambo mengi.

Wewe ni Role model wa wengi fahamu hilo. Twajua watu wakubwa huwa hawapendi kujikweza, hupenda kujishusha.

Tutafurahi sana kusoma historia ya mwandishi wa historia ya uhuru wa Tanganyika.
 
Back
Top Bottom