Kumbukumbu Zangu za Mtaa wa Kipata (Mtaa wa Kleist Sykes)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,266
KUMBUKUMBU ZANGU: MTAA WA KIPATA (SASA MTAA WA KLEIST SYKES)
Nimefika Mtaa wa Kipata leo majira ya asubuhi.

Siku zote nifikapo Gerezani na kupita mitaa yake kumbukumbu nyingi za utotoni hunijia.

Nyumba za ndugu na jamaa nilizokuwa nazijua, nyumba za kuezekwa na madebe na mjengo wa vyumba sita na ua nyumba na mbele kuna baraza nyumba hizi hazipo tena.

Badala yake yamesimama majumba ya ghorofa na maduka makubwa ya biashara na kwa Gerezani biashara kubwa ni maduka ya vifaa vya ujenzi.

Mtaa wa Kipata na Swahili naangalia Msimbazi na hapo niliposimama si mbali na nyumba niliyozaliwa mwaka wa 1952.

Nyumba hiyo haipo tena mahali pake imesimama ghorofa.
Hapo niliposimama kulia kwake kulikuwa na nyumba ya Mama Kilindi.

Huyu Kilindi alikuwa mwanae ambae mimi kwangu alikuwa dada mkubwa na Kilindi alikuwa na kaka yake Mbaraka.

Kiasi cha kama miaka 15 iliyopita, Mtaa wa Kipata haukuwa umachangamka kama nilivyoshuhudia leo kwani niliweza kuegesha gari yangu pembeni ya Mtaa wa Kipata na Swahili leo barabara imejaa watu na magari yameegesha ubavu kwa ubavu magari ya kubeba vitu vya ujenzi vinavyouzwa madukani hapo.

Siku hiyo wakati natoka ndani ya gari nilimuona mtu mzima wa makamo kasimama pembeni ya nyumba ya Mama Kilindi.

Akili yangu ikawa inaniambia kuwa huyu mtu mimi namfahamu lakini sikuweza kumtambua ni nani.

Nilimwemdea nikamtolea salam na akaniitikia.
Nilimwambia kuwa nadhani kama namfahamu.

Hakupendezewa na kauli yangu na hilo lilijionyesha katika uso wake.

''Mimi Mohamed mtoto wa Bi. Baya nimezaliwa nyumba ile pale.''

Nikaonyesha kidole nyumba niliyozaliwa wakati ule bado haijajengwa ghorofa.

''Mohamed, nimekuona mtoto leo tunakutana umekuwa mzee?
Mimi Mbaraka wa Mama Kilindi.''

Nilikumbuka nyimbo ya wakati ule ya Mwenda Jean Bosco ambao katika nyimbo ile akiimba maneno, ''We mbaraka.''

Nyimbo hii tukiimba sote miaka zaidi ya 50 iliyopita palepale mtaani Kipata.

Mama Kilindi alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu mama yangu.

Naiangalia nyumba hii naona tofauti kubwa iliyokuwapo baina ya nyumba ile ya Mama Kilindi ya miaka ya 1950 mimi nazaliwa na nyumba hii ya leo mbele yangu.

Pembeni ya nyumba hii upande wa Mtaa wa Swahili jioni kulikuwa na muuza chai maarufu akiuza pamoja na maandazi, chapati na maharage.

Ikiingia alasiri watu wanatoka makazini pale panajaa watu wengi kunywa chai na pembeni kulikuwa na akina mama wanauza smaki wa kukaanga.
Kulikuwa pia na bomba la kuteka maji.

Siku hizo nyumba chache sana zilikuwa na maji ndani na umeme.
Nimesimama pale nikamkumbuka kaka yangu Mbaraka na dada yake Kilindi.

Baada ya siku ile sikumuona tena Mbaraka ila niliambiwa ile nyumba ameuza na yeye kahamia Mbagala.

Mbaraka amezikwa Makaburi ya Kisutu na nilihudhuria mazishi yake.
Nimegeuka na kuangalia upande wa pili wa Mtaa wa Kipata.

Kuna ujenzi wa barabara magari hayapitiki mtaa mzima umechimbwa na mvua iliyonyesha imefanya mtaa mzima uwe haupitiki kirahisi.

Upande huu maduka si mengi sana lakini hapa mwanzoni yapo maduka makubwa yanauza tiles za kila aina.

Nimevuka barabara nakwenda nyumbani kwa Biti Hassani Machakaomo, mtoto wa Hassan Machakaomo mmoja wa viongozi wa Yanga katika miaka ya 1940 mimi sijazaliwa.

Machakaomo baba yake Hassan alikuja Germany Ostafrika na Herman von Wissman kama askari mamluki pamoja na Sykes Mbuwane na Afande Plantan.

Nimefika nyumbani kwa Biti Hassan Machakaomo.

Mwenyewe kafariki miaka miachache iliyopita na nakumbuka siku nilipokwenda kumjulia hali hapo nyumbani kwake miaka mingi sasa imepita na kumfahamisha kuwa mimi ni mtoto wa Baya bint Mohamed.

Nyumba ya Mzee Hassan Machakaomo picha ya pili ni kama vile haipo.
Nimemkuta mmoja wa wanafamilia kakaa kizingitini anauza karanga.

Akanifahamisha kuwa Biti Hassan kafariki na wajukuu zake wengi pia wametangulia mbele ya haki.

Sehemu hizi ndizo ilikuwa dunia yangu utotoni.

Mitaa ya Gerezani leo haipitiki magari yameshonana barabaara nzima kiasi watu wanatemebea huku wanagusana na magari.

Kelele za muziki wala hujui wapi zinatoka.

Miaka ya 1950 nakumbuka nyumbani kwa Mama Kilindi kulikuwa na duka la Muarabu.

Coca Cola yangu ya kwanza niliinywa kwenye duka hili.

Nalikumbuka duka hili kwa nyimbo zilizokuwa zikisikika kutoka radio iliyokuwapo, nyimbo za Abdulhalim Hafidh, Mohamed Abdulwahab, Feiruz na Um Kulthum.

Baadhi ya nyimbo hizi sisi watoto tukiziimba kwani ndiyo ilikuwa miziki ikipigwa katika Sauti ya Dar es Salaam.

Wakati ule sikuayajua majina ya hawa waimbaji hadi baada sana nilipokuwa mkubwa.

Mwaka wa 1991 niko Cairo ''transit'' naelekea Uingereza ndiyo siku Mohamed Abdulwahab alipofariki na nyimbo zake zikawa zinapigwa katika radio na televisheni mimi niko Movinpick Hotel Heliopolis nazisikiliza.

Hukutana na nyimbo hizi wakati mwingine katika YouTube na hunirudisha nyuma udogoni Mtaa wa Kipata.

Dar es Salaam ile haipo.

1706239679425.png

Mtaa wa Kipata 1970s
1706239756701.png

1706239795054.png

Kona ya Mtaa wa Kipata na Swahili ilipokuwa nyumba ya Mama Kilindi

1706239882482.png

Mtaa wa Kipata 2024 nilipopiga picha ya kwanza hapo juu 1970s

1706240145810.png

Nyumba ya Mzee Hassan Machakaomo




 
Historia ya Dar na kkoo kutika mzee Said....sijui nani amerithi mikoba yake ....hasa historia na mengine yoite na hata fitna ?
 
Mohamed Said Naomba kufahamu hili, ni kwanini mtaa wa Gerezani ulipewa jina hilo, je kulikuwa na ukaribu wowote na majengo ya wafungwa maeneo hayo au ilikuwa vipi.
 
Waislamu wameuza sana nyumba kariakoo, matokeo yake pesa wameenda kuongeza wake na kufilisika

Unamchokoza mzee sasa.

Sema wenyeji wa kariakoo. Usitaje dini zao.

Maana hata wakristo na wapagani na wao walikuwepo kariakoo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom