Natamani Bunge lingekuwa linakaa vikao kila siku

nice 2

JF-Expert Member
Aug 10, 2011
747
520
Nilikuawa napitia hii habari iliyoandikwa baada ya kikao cha nne cha Bunge kuahirishwa mwezi uliopita, ndipo hapo nilipotamani kama vikao hivi vingekuwa vinakaa kila siku, labda Serikali yetu ingejirekebisha kiutendaji japo kidogo! Maana saizi wanafanya mambo jinsi wanavyojiskia wakijua hakuna wa kuwapigia kelele na wananchi wanaweza wasijue mambo wanayoyafanya.

‘Bunge lilikuwa kama Ze Comedy’

Imeandikwa na Basil Msongo; Tarehe: 6th September 2011 @ 01:40 Imesomwa na watu: 248; Jumla ya maoni: 0KUNA mambo mengi yalitokea wakati wa Mkutano wa Nne wa Bunge, uliomalizika Agosti 26 mjini Dodoma, na nimeshawishika kuyasema japo machache, ambayo ninaamini yatabaki katika kumbukumbu za wananchi wengi.

Kwanza unahitajika ujasiri kwa Mbunge, kusimama katika Bunge na kuwaponda wenzake, wanaosimama bungeni na kudai waongezwe mishahara na posho. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amefanya hivyo katika mkutano uliopita wa Bunge, na kama ilivyotarajiwa, wenzake walimpinga.

Zitto anasema, ni makosa kwa Mbunge hivi sasa kudai nyongeza hiyo, kwa kuwa Taifa linakabiliwa na matatizo mengi, ukiwemo upungufu wa umeme na upungufu wa fedha. Ametoa msimamo huo bungeni, wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012.

Zitto anawataka wabunge wawe na mtazamo wa kiuongozi, na waonyeshe wanaguswa na matatizo yanayowakabili Watanzania. Anawaeleza wabunge kuwa, hata kama wapingana na msimamo wake hivi sasa, ni makosa kutaka nyongeza ya mishahara na posho za wabunge.

Si hivyo tu, nathubutu kusema kuwa, kama mkutano wa Bunge ungekuwa ni mchezo wa soka, Zitto angekuwa nyota wa mchezo, kwa kuwa pia ndiye aliyesababisha wabunge waijadili kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kama jambo la dharura.

Mbunge huyo alitoa hoja, kabla ya kipindi cha maswali na majibu, Kamati ya Bunge ya Uongozi ikalazimika kukutana kwa dharura katika ukumbi wa Spika, baadaye Zitto akaifafanua, na wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao, wakaiunga mkono.

Zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwa ukumbini, wakiwemo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliunga mkono hoja ya Zitto. Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, anasema hoja ya Zitto ya kupinga Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, kurudishwa kazini kabla ya wabunge kuijadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni ya msingi, kwa kuwa Bunge limedharauliwa.

“Kwa sababu Bunge ni mhimili, hatuwezi kudharauliwa kirahisi,” anasema Ndugai na kusisitiza kwamba Wabunge hawawezi kukaa kimya wakati Waziri Mkuu anadhalilishwa.

“Kama dharau inaweza ikatokea, basi huko huko, lakini sio ndani ya Bunge hili”, anasema Ndugai baada ya wabunge kuijadili hoja ya Zitto na anasisitiza kwamba, kwa kuwa suala hilo lilianzia bungeni, taarifa ya CAG ingepelekwa kwanza kwenye mamlaka hiyo kabla ya uamuzi wa Serikali.

Ukiacha suala la Jairo, jambo lingine ambalo bila shaka lilivuta hisia za wengi ni kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, aliyoitoa bungeni kuwa Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu ni mchochezi na anawapotosha Watanzania.

Kombani amemtuhumu Lissu kuwa ana usongo na suala la Urais wa Tanzania, na anavuka mipaka katika baadhi ya mambo anayozungumza. Kombani anamtuhumu Lissu, kwamba amewasilisha bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Katiba bila idhini yake, na amemuuliza Spika wa Bunge kama Kanuni za Bunge zinaruhusu mawaziri vivuli kufanya hivyo.

Kombani anasema, hana uhakika kama aliyoyasema Lissu kwenye hotuba ya kambi ya upinzani ni maoni ya kambi hiyo au ni mawazo yake binafsi. Amemshauri Mbunge huyo awe mwangalifu anapozungumza kama walivyo majaji.

Amesema hana uhakika kama kambi ya upinzani, ilipata fursa ya kuipitia hotuba aliyoisoma Lissu bungeni, na kama ingekuwa hivyo wasingemruhusu aisome hotuba hiyo. “Upande wa Upinzani muwe mnapitia hizo hotuba kabla”, anasema Kombani na kwamba wasipofanya hivyo, mtu anaweza kusoma madufu yake bungeni.

Waziri Kombani amesema, Mungu amempa kila mtu karama, hivyo ‘tuzitumie vizuri hizo karama zetu”. Agosti 17 mwaka huu ilikuwa ni zamu ya Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kupondana bungeni.

Serukamba anamponda Mdee, kuwa ni muongo na anapeleka siasa uchwara bungeni. Mdee anamjibu Serukamba, kwa kumweleza kuwa anamuonea huruma, kwa kuwa hajui kama mwaka 2015 Mbunge huyo atarudi bungeni.

Serukamba anasema wabunge waache kutafuta umaarufu kwa kusema uongo bungeni na kwamba, wananchi wa Kigoma ndiyo wanaofahamu hali halisi ya mambo yao. “Huo uzalendo uchwara unaoletwa leo, hatuutaki Kigoma, tunataka maendeleo,” anasema Serukamba alipoomba kutoa taarifa, wakati Mdee anachangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mdee anasema, hatafuti umaarufu kwa kuwa yeye tayari ni maarufu, anataka kufanya kazi. Mbunge huyo amesema, hazungumzi kitu ambacho hana ushahidi nacho na hafanyi uchochezi.

“Hatutafuti umaarufu wa kisiasa, upo tayari, tunataka kuijenga nchi yetu” anasema Mbunge huyo kijana, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mdee anataka haki itendeke kwa wananchi wa Kwembe na Mabwepande mkoani Dar es Salaam na atakuwa na wananchi hao hadi mwisho.

“Sisi tutakufa na wananchi wetu, liwe jua, iwe mvua,” anasema Mbunge huyo na kusema, Serikali inapaswa kuweka utu kwanza, iache siasa zifanywe na vyama. Anadai kuwa, maeneo ya wazi yakiwemo yaliyotengwa kwa shughuli maalumu yanauzwa, na kwamba, wakubwa wanajenga ‘mabangaloo’.

Amesema, ardhi ndiyo mhimili wa nchi na kwamba, sekta hiyo ikipuuzwa baadaye wananchi watachinjana. “Sekta hii ikipuuzwa watoto wetu, wajukuu wetu watakuja kuchinjana, hatutaki kutengeneza Tanzania ya Watanzania kuja kuchinjana,” anasema Mdee.

Takribani wiki moja kabla ya kauli za Mdee na Serukamba, kuna jambo lingine lilijitokeza bungeni, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, Agosti 11 alikataa kutoa mwongozo kuhusu hoja ya Mbunge yeyote kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 133, inayosema kwamba, Mbunge yeyote anaweza kupeleka hoja kwa maandishi kwa Spika wa Bunge, kumweleza kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Ndugai anamruhusu Mnyika aisome kanuni hiyo mara mbili na akatoa uamuzi kuwa shughuli za Bunge ziendelee, kwa kuwa kanuni hiyo inamtaka Mbunge awasilishe hoja hiyo kwa maandishi.


Kwa kuzingatia mantiki ya mwongozo aliouomba Mnyika, bila shaka, kama kanuni ingemruhusu atoe hoja hiyo bungeni, angetamka kuwa hana imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa sababu ambazo angezitaja.

Ndugai anawaeleza wabunge mjini Dodoma kuwa, Mbunge anayetaka kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, lazima awe amejiandaa vizuri kwa kuwa jambo hilo si dogo.

Kwa mujibu wa Ndugai, Mbunge akisema kuwa hana imani na Waziri Mkuu, ina maana kuwa hana imani na Serikali, hivyo ina maana serikali inapaswa ijiuzulu. Ndugai anasema bungeni kuwa Mbunge anaweza kutumia Kanuni za Bunge, kuwasilisha hoja za kutokuwa na viongozi akiwemo Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Naibu Spika wa Bunge na hata Rais wa Tanzania.

Anasema, Mbunge akiwasilisha hoja hiyo, Bunge litaipokea, lakini lazima iwe imewekwa saini na asilimia isiyopungua 20 ya wabunge wote. Bunge la sasa lina wabunge 357, hivyo ili kuifikia asilimia hiyo, lazima wabunge wasiopungua 72 wawe wameweka saini.

Kwa mujibu wa Ndugai, Mbunge akitekeleza sharti hilo, wabunge wataijadili hoja yake, na watapiga kura za siri, na kwamba matokeo ya kura, utakuwa ndiyo uamuzi wa Bunge la Tanzania.

Si hivyo tu, Agosti 26, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Kabwe Zitto alilieleza Bunge kuwa, endapo itabainika kwamba, mjumbe yeyote wa kamati hiyo alipewa rushwa katika suala la kuiongezea muda taasisi ya Serikali inayosimamia ubinafsishaji wa mashirika ya umma (CHC), si tu atajiuzulu uenyekiti wa kamati hiyo lakini pia atajiuzulu ubunge.

Zitto ametoa ahadi hiyo bungeni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2011/2012. Amemtaka Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo naye aliahidi Bunge kuwa ikibainika viongozi wa Serikali walipewa rushwa ya shilingi milioni 60 ili CHC waruhusiwe kufanya kazi hiyo moja kwa moja atajiuzulu.

Mkulo hajatoa ahadi ya kujiuzulu, amesema kwanza uchunguzi ufanyike ndipo lije suala la kujiuzulu au la. Siku hiyo hiyo Makinda aliwasifu wabunge kwa kufanya kazi nzuri katika mkutano wa Bunge uliokwisha Agosti 26 mjini Dodoma, na kwamba walivumiliana, walisikilizana na kufanya kazi pamoja.

Kwa mujibu wa Makinda, Bunge hilo lilipoanza lilikuwa kama Ze Comedy, lakini linaelekea kuwa imara, na litafanya kazi ipasavyo kuisimamia Serikali. Amewataka wabunge wasiwe na chuki au uadui na wanaoongoza vikao vya Bunge, kwa kuwa hakuna aliye na chuki na yeyote.

“Chuki na hila mziache hapa, na ziozee humu. Mkiwa hapa mwenzio akisema, usijenge uadui. Kwa waliokwazwa, naomba tusameheane” amesema Makinda kabla ya kusitishwa kwa shughuli za Bunge hadi Novemba 8 mwaka huu.

 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom