Nimeamua kuja mwenyewe. Nashangaa wakati mwingine maana ni hapa ndo watu walisema Nape kashazibwa mdomo kama vile yale ni maamuzi ya Nape binafsi.
Jana nimewakumbusha tu watuhumiwa na wapambe wao si busara kujifariji kuwa maamuzi yatabadilishwa nje ya vikao, na vikao vyenyewe ni lazima iwe ama NEC au Mkutano Mkuu(Congres) na si vinginevyo.
Kuna hoja hapa eti kwamba Nape anabwabwaja tu, hakuna vitendo, let's be objective, hivyo vitendo ni vipi? Taarifa ya utekelezaji wa maamuzi haya itatolewa kwenye kikao kijacho cha NEC na si siku 90 kama wanavyojaribu kueleza hapa.
Tumelieleza sana hili la siku,WAANDISHI TENA BAADHI ndo walitafsiri siku tisini kutoka kwenye ratiba ya vikao vya NEC ambavyo Dodoma tulikubaliana tentively tunaweza kukutana July ndo wakahesabu na kusema siku tisini. Lakini hakuna kikao kinakutana exactly kwa muda ulopangwa,kuna flexibility.
Ushauri subirini NEC ikutane mtuseme tukishindwa kufukuza.
Nape, sitaki wala sitajaribu kuutilia shaka uwezo na upeo wako wa kupambanua siasa za Tanzania na haswa za ndani ya CCM. Hata hivyo, nataka kutilia shaka kauli zako hapo juu, hususani zilizokolezwa na rangi nyekundu.
1. Kauli ya kwanza kuhusu "...maamuzi kubadilishwa nje ya vikao...", inaashiria yale ambayo wengi hapa tumekuwa tukisema kuwa maamuzi ya kikao kilichopita yameelekea kubadilishwa na sasa hayatekelezeki. Kwa kauli yako, unajaribu tu kutetea kuwa ni kinyume kwa maamuzi kubadilishwa nje ya vikao, lakini hausemi wazi kuwa maamuzi ya awali hayajabadilishwa na yanasimama jinsi yalivyo. Yamkini hata hausemi ni maamuzi gani hayo unayozungumzia hapa.
Katibu Mkuu Mukama alikwenda mbele ya vyombo vya habari na kusema mengi, lakini nukuu moja ni kuwa "..hakukua na uamuzi au azimio lolote la kuwafukuza.....". Kama ambavyo yeye na wewe hamutaji nani anafukuzwa au la, je ni vipi umma utajua uamuzi huo ni ndiyo au siyo.
2. Vitendo vinavyoongelewa hapa ni vile ambavyo wewe mwenyewe ulijiwekea mipaka. Umenukuliwa mara kadhaa na vyombo mbalimbali ukitoa kauli kuwa "...barua zao ziko tayari na zitatolewa hivi karibuni...". Yamkini ulienda mbali na kusema kuwa zitatotelewa baada ya Pasaka, hata kutaja siku kuwa ni jumatano baada ya Pasaka.
Labda kwa kuwa hukuwa makini na kusema ni jumatano ipi baada ya Pasaka, na kwa kuwa sasa unasema kuwa kikao ni July, basi pengine tuendelee kubuni kuwa itakuwa mojawapo kati ya hizi jumatano nyingi kati ya wakati huu hadi July.
Pungufu ya hayo, nikuelekeze tu kuwa kauli zako zina walakini au upungufu wa 'vitendo' hivyo.
3. Unaposema "...subirini NEC ikutane mtuseme tukishindwa ku(m/wa)fukuza", nachelea kuona kuwa hii ni njia nyingine ya kujaribu kutafuta pa kutokea.
Mosi, hakuna hata siku moja CCM kwa uwazi au usiri imewahi kutamka kuwa kuna mafisadi ndani ya CCM na majina yao ni haya. Hakuna, kama ipo nikumbushe mdogo wangu. Chadema imetangaza orodha ya mafisadi hadharani Mwembeyanga (2006) na Tabora (2011). Baadhi ya hao waliotajwa na Chadema ni viongozi ndani ya CCM na wengine ni watendaji ndani ya Serikali ya CCM, na wengine ni wafanya biashara wenye ukaribu na CCM.
Sasa ni akina nani mta(m/wa)fukuza na kwa vigezo vipi, umma hautaweza kupima usahihi wa huo uamuzi wenu.
Pili, mnaposema kuwa CCM NEC inawapa nafasi wajitoe wenyewe la hasha w/atafukuzwa, ina maana kuwa kwa undani fulani huyo mtu au watu tayari wamejulishwa kwa njia moja au nyingine, vinginevyo inaamaanisha kuwa vikao vya CCM vinategemea tu 'hisia' za hao watuhumiwa kujichukulia hatua wenyewe. Hapo sioni umakini wa taasisi kubwa kama CCM kutumia mbinu za Abunuwasi kuwa wezi wa pamba utawajua tu maana wana nyuzi kwenye videvu vyao.
Kama wapo wataje, si umesema vikao vimeamua, na kama hawapo basi jaribu hata kuwa shujaa wa uongo na kusema kuwa hamuwajui ila vile vile hamkubaliani na wale waliotajwa na Chadema.
July ikitokea mkafukuza mwenyekiti wa kijiji huko Nkasi au Mfaranyaki kwa madai ya ufisadi, msitegemee kuwa mtageuka na kujigamba kuwa mmejivua gamba. Umma utacheka, lakini hautacheka nanyi, bali utawacheka nyinyi.
Zidumu Fikra Za Mwenyekiti.