Nafasi ya Zanzibar katika Katiba Mpya ikoje?

GHIBUU

JF-Expert Member
Jan 13, 2011
4,432
3,006
Na Maisory Chacha
APRILI 26 kila mwaka tunasheherekea kumbukumbu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar na mwaka huu ilikuwa miaka 47 ya Muungano. Waasisi wa nchi za Tanganyika na Serikali ya Zanzibar kwa kuheshimu tamaduni zetu, kuenzi umoja na undugu uliokuwepo waliamua kuziunganisha nchi hizi mbili. Ni jambo la kujivunia sana kwani ni nchi pekee barani Afrika zilizothubutu kufanya hivi.

Hata hivyo, pamoja na mazuri mengi yanayohusu muungano wetu, changamoto bado ni nyingi na ukosefu wa dhamira ya kisiasa kuzishughulikia wauweke muungano wetu katika dhoruba kali. Kelele nyingi za "Kero za Muungano" zimepigwa na zinaendelea kupigwa ila kwa makusudi au bahati mbaya zinaendelezwa kusikilizwa tu huku juhudi kubwa zikitumika kushughulikia kero ‘ndogo ndogo' za muungano bila kutatua ‘kiini' cha matatizo hayo yote.

Elimu itolewayo juu ya muungano wetu ni ile ile ya miaka yote. Huzungumzia historia za nchi hizi mbili, kwanini waliungana na umuhimu wake. Kero hizi huwezi ambiwa.
Ni jambo la kushangaza sana kwani ni kero nzito, nyingine ni za kikatiba. Nikiri tu, mimi mwenyewe sikuzijua kero hizi hadi Aprili mwaka jana. Je, wananchi hufahamu "Kero za Muungano"? Je, serikali iko wapi kutoa elimu ya uraia kuzifahamu? Je, wananchi wanafahamu changamoto zinazoikabili muungano?

Kero hizi zimeendelea na wiki kadhaa zimepita sasa tangu kukataliwa kwa Muswada wa Marejeo ya Katiba. Muswada huo una udhaifu mwingi. Umeshindwa kuangalia mambo ya msingi ambayo wananchi wanahitaji. Umeshindwa kuweka vipaumbele vya nchi kwanza. Udhaifu huu umezidi kuwa ni kawaida ya viongozi wetu kwani ni mara nyingi sana wamekuwa wakitanguliza siasa mbele ya mambo ya kitaifa. Wakati harakati za kupinga katiba mpya zikiendelea Tanzania Bara, Zanzibar wao wameukataa, tena na kuchanwa chanwa na kuchomwa moto. Hili ni suala zito sana.

Kelele nyingi zilizosikika ni Wazanzibari wamechokwa "kuburuzwa" na wenzao wa Tanzania Bara. Kelele hizi si za leo, si za "kikundi cha watu wachache wahuni", ni kelele za muda mrefu. Kauli kama hii inasikitisha sana na inatia doa muungano wetu.

Hivi ni gharama gani inayosubiriwa kuingiwa ili kuondoa kero zinazoleta manung'uniko haya? Kwanini serikali ya muungano haichukui hatua kushughulika matatizo haya nguli ukizingatia karibu nusu ya Wazanzibari walikuwa hawaafikiani na kuwepo kwa muungano hata kabla ya kuundwa?
Ushiriki wa Wazanzibari katika kupatikana kwa katiba mpya umekuwa mdogo mno hadi kuzua maswali kama mabadiliko haya ni kwa katiba ya muungano au ni katiba ya Tanzania Bara. Wazanzibari ama kwa makusudi au kwa kujisahau wameachwa kuzingatiwa maoni yao na kero zao katika mchakato huu mzima. Hili ni jambo la kusikitisha sana. Kama tulikubali kuungana basi matendo yetu yaonyeshe dhamira za kweli za muungano huu. Mchakato huu uwe wa pande zote na nafasi ya Zanzibar katika kupatikana kwa katiba mpya ijulikane na ieleweke.

Labda kwa wale wanaodhani mbona Zanzibar ni nchi dogo na inapewa nafasi nyingi sana katika muungano na hata uwakilishi wake ni mkubwa kulingana na Wananchi wake ikifananishwa na Tanzania Bara. Naweza kuwapa jibu moja tu; hakuna kitu kama nchi ndogo ndani ya muungano. Katika Umoja wa Ulaya, nchi ndogo kabisa ya Malta hufaidi matunda yote ya muungano ikiwemo ushiriki sawa katika mambo yanayohusu umoja huo na nchi nyingine kubwa, kama Ukraine ambayo ni kubwa kuliko zote kwenye umoja huo.

Napenda kusisitiza umuhimu wa kutambua "Kero za Muungano" sasa na kuzishughulikia kabla ya kuanza mchakato wa kuandika katiba mpya. Nafasi ya Zanzibar katika mchakato huu kamwe isidharauliwe, isiondolewe uzito kama kweli tunataka kuuenzi huu Muungano wetu. Maswali la kujiuliza; Hivi ni kwanini kusiwe na tume itakayoratibu maoni ya Wananchi wa pande zote mbili kujadili mustakabali wake na kero zilizopo na kuzishughulikia kabla hatujazungumza katiba ya muungano? Kwanini nafasi ya muungano imepewa mzito mdogo sana katika mchakato huu muhimu?
Kama kero hizi zinavyowasumbua sana Watanzania wa visiwani, vivyo hivyo kwa wa bara. Wananchi wengi wana malalamiko juu ya kero ambazo huziona katika muungano na wangependa kuona zinajadiliwa kwa kina na kutatuliwa ili Muungano uwe wa kuridhisha pande zote mbili. Kama la, basi ieleweke mchakato huu unaoendelea ni wa kuandika katiba na kufufua serikali ya Tanganyika.

Kama ni ya muungano, kwa upepo unaondelea kwa sasa, nafasi ya Zanzibar kutoeleweka, kutojulikana, kutothaminiwa; kama Jamhuri ya Muungano tunawanyima washirika wetu katika muungano nafasi sawa ya kujadili yale yanayohusu mustakabali wa nchi yao.
Ni vyema sasa, kero hizi zikatatuliwa wakati tunajiandaa na mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya. Ushiriki na nafasi ya Zanzibar katika mchakato huu mzima uangaliwe upya; ujulikane na ueleweke ili kuondoa manung'uniko na lawama kutoka kwa Watanzania wenzetu. Wahenga walinena; Usipoziba ufa utajenga ukuta.

Tutatue "Kero za Muungano" ili tuuenzi muungano wetu, lakini la muhimu zaidi, kila pande ya muungano ifurahie Muungano huu. Tuepukane na "Tumechokwa Kuburuzwa". Tafakari!
Maisory Chacha ni Mshauri Mwelekezi katika Idara ya Uchambuzi na Utetezi wa Sera-HakiElimu. Anapatikana kupitia; paa@hakielimu.org This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it View attachment 29803
pencil.png
 
Back
Top Bottom