Mzee wa Kanisa auawa kinyama

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,557
21,515

Zanny (45), ambaye kwa waumini wenzake alikuwa akijulikana kama ‘Mzee Zanny’ au Uncle Sam kama walivyokuwa wakimwita marafiki zake, aliuawa juzi kwa kupigwa risasi mguuni na mgongoni nje ya ofisi yake, mtaa wa Ruhinde, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kukumbwa na mauti, Zanny ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya Cel Solutuions, muda mfupi kabla ya kukumbwa na mauti, alikuwa ameshuka kutoka kwenye gari lake akitokea benki ya Stanbic kuchukua fedha.

Kaka wa marehemu, Charles Zanny, akizungumza na Nipashe jana nyumbani kwa marehemu, mtaa wa Mkwawa, Kisukuru jijini Dar es Salaam, alisema alipata taarifa za kifo cha mdogo wake akiwa mkutanoni.

Alisema ilikuwa yapata saa 5:00 asubuhi akiwa mkutanoni, alipigiwa simu na mtu wa karibu wa marehemu akimtaka afike katika Hospitali ya Taifa ya Muhumbili lakini akiwa njiani kwenda huko, alipigiwa tena simu kuwa aende Kituo cha Polisi Oysterbay.

"Simu ile kwa kuwa nilipigiwa na mtu wa karibu wa marehemu ilinishtua nikampigia marehemu (Zanny) haikupokewa, kurudia kupiga kwa rafiki yake hakupokea.

"Nilipopigiwa simu nilikuwa mkutanoni sikuipokea nilituma sms tu, lakini nikapiga ile simu baada ya muda akaniambia niende kituoni, nilipofika kituoni nilikuta baadhi ya watu ambao niliwafahamu hata marafiki wa marehemu, nikaambiwa mdogo wangu kafariki (dunia) kwa kupigwa risasi," alisema Charles.

Kaka wa marehemu alisema mmoja wa walinzi wa kampuni binafsi wanaolinda kwenye ofisi ya mdogo wake, alikaririwa akisema walifika watu wawili na bodaboda wakiwa na silaha na kudai pesa, huku mmoja wao akitambuliwa sura na mlinzi.

Alisema wakati Zanny akishuka kutoka kwenye gari lake akiendelea kuzungumza na simu, ghafla watu hao walifika na kumpiga risasi moja mguuni.

"Mlinzi na baadhi ya watu walio katika ofisi zilipo jirani na ofisi ya marehemu walisikia mlio wa risasi, kwa kuwa jirani kuna biashara ya matairi wakafikiri tairi limepasuka lakini walipotoka nje waliwakuta watu hao," alieleza.

“Mmoja wa walinzi alimuuliza mmoja wa watu hao kwamba 'hata wewe' na kisha kuendelea kummiminia risasi za mgongoni marehemu na kuanguka chini. Baada ya mauaji, watu hao walichukua pesa ambazo marehemu alitoka nazo benki na kutokomea nazo,” alisema.

Alisema baada ya tukio na harakati za kumpeleka haraka Zanny Muhimbili zilianza na wakiwa katika harakati hizo, walifika askari wa kituo cha jirani Oysterbay, kwa milio ya risasi ilisikika hadi kituoni.

Licha ya juhudi hizo, alisema hawakumuwahisha kufika Muhumbili kwa kuwa alikuwa ameshafariki dunia.

MCHUNGAJI AMLILIA
Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Segerea, Noah Kipingu, alisema kanisa limepokea kwa mshtuko taarifa za msiba wa muumini wake ambaye alikuwa Mzee wa Kanisa wa Usharika huo kipindi kilichipita hadi mwaka 2014.

Alisema Zanny licha ya kwamba alikuwa amestaafu nafasi ya Uzee wa Kanisa, alikuwa bado akitumika kwa nafasi mbalimbali kwenye kamati za Usharika. Pia alikuwa mshauri na mlezi wa vijana katika Usharika huo.

Mchungaji Kipingu alisema Jumapili iliyopita wakati wa ibada, alimwita madhabahuni ili ahamasishe Tamasha la Twende Zetu kwa Yesu, linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Tamasha hilo limeandaliwa na kampuni ya vyombo vya habari ya Upendo Media Group ya KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

"Kwa kweli tumepokea kwa mshtuko na kanisa limempoteza mtu muhimu. Samson (Zanny) alikuwa msharika wetu kwa zaidi ya miaka 10, mimi nimemkuta, juhudi zote za kuhamasisha ujenzi wa kanisa hili, harambee ya awali iliyofanyika Diamond Jubilee alikuwa mwenyekiti. Kanisa nimepata pigo," alisema.

"Kwa hiyo kitendo cha kuzungumza na Kanisa Jumapili iliyopita ni kama kutuaga. Kazi ya Mungu haina makosa. Tushukuru kwa kila jambo," alisema Mchungaji.

Alisema Zanny alikuwa mjasiriamali ambaye atakumbukwa na vijana wa Usharika wa Segerea kwa kuwa alitumia semina na warsha mbalimbali kuwaelimisha vijana namna ya kujiongezea kipato na kujiajiri.

"Alijitoa sana kwa kanisa lakini neno la Mungu kitabu cha Mhubiri 8:8 kinaelekeza vizuri kwamba hakuna binadamu mwenye uwezo wa kuizuia roho iwapo siku zake za kuishi zimeisha," alisisitiza Mchungaji Kipingu.

MAZISHI
Kuhusu mazishi, kaka wa marehemu alisema maandalizi kwa ajili ya mazishi yameanza na kwamba mdogo wake atazikwa keshokutwa (Jumatatu) katika makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Alisema wakati mipango ya mazishi ikiendelea, wanasubiri kuwasili kwa mama yao kutoka mkoani Mbeya. Zanny ameacha mjane na watoto wawili.

POLISI YATHIBITISHA
Nipashe ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Susan Kaganda, alisema alikuwa safarini hivyo msaidizi wake atakuwa na taarifa zaidi.

Msaidizi wake alithibitisha tukio hilo kutokea na kusema juzi majira ya saa 4:30 asubuhi, walipokea taarifa ya mfanyabiashara mkazi wa Tabata, aliyetajwa kwa jina la Samson Zanny, kuuawa. Alisema tukio hilo lilitokea Kinondoni block 41.

"Ni kweli tukio limetokea jana (juzi) Juni Mosi kwamba mtu mwenye umri wa miaka 45, kauawa na watu wasiofahamika, ilikuwa saa 4:30 asubuhi," alisema.


Chanzo: Nipashe
 
Nilidhani atakayepigwa risasi za mgongoni ni mlinzi kwa kumtambua jambazi.
Unashauriwa kutomwonesha jambazi kwamba umemfahamu hata kama ni ndugu yako kwani kutakuweka katika hatari zaidi.
Mmoja wa Walinzi alimuuliza mmoja wa watu hao kuwa "hata wewe???"
Hii imekaaje mazee
 
Nilidhani atakayepigwa risasi za mgongoni ni mlinzi kwa kumtambua jambazi.
Unashauriwa kutomwonesha jambazi kwamba umemfahamu hata kama ni ndugu yako kwani kutakuweka katika hatari zaidi.


Na mimi nimeshangaa kuona huyo mlinzi kabaki salama.... Hata siamini.
 
Back
Top Bottom