Mzee Sumaye ameponzwa na Kubenea

Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
9,274
9,911
"SUMAYE AMEPONZWA NA KUBENEA"

WENGI wamejadili kwa mtazamo tofauti hili suala la Fredrick Sumaye kushindwa kutetea nafasi yake ya mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, wengine wanasema ni demokrasia na wengine wanasema ni kwa sababu za ndani, kuonewa!

Sumaye sio pekee aliyeshindwa, wapo wengine pia walioshindwa kutetea nafasi zao, John Heche (kanda ya Serengeti), Cecil David Mwambe (kanda ya kusini) na Mbasa (kanda ya kati). Lakini Kwanini mjadala mkubwa umebaki kanda ya Pwani?

Kanda ya Pwani, Chadema. Hii ni kanda muhimu kwa Chadema, ni kanda ambayo inabeba makao makuu ya chama hicho, ni kanda ambayo ina wanachama wengi wa Chadema na pia ni kanda inayobeba taswira ya kibiashara ya nchi hii, Dar es

Pia, Fredrick Sumaye ni kati ya mawaziri wakuu (prime Ministers) wachache wa Tanzania waliohudumu kwa miaka mingi katika nafasi hiyo bila kufukuzwa au kung'atuka. Fredrick Sumaye amehudumu kwa miaka 10 katika wadhifa huo chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa.

Itambulike, Chadema sasa ni taasisi ya kisiasa. Chadema wamevuka hatua ya kuwa chama Cha siasa pekee, ndio maana tunaweza kuona chaguzi zao za ndani za chama zinavuta hisia na shauku kutoka nje na ndani ya chama hicho.

Vyombo vya habari nchini Tanzania vinajadili chaguzi za Kanda za Chadema. Tena kurasa za mbele. Wananchi Mtaani, kazini na kwenye vyombo vya usafiri, wanajadili chaguzi na michakato ya uchaguzi ndani ya Chadema. Hii ni tafsiri, Chadema sasa ni "taasisi"

Kukua kwa demokrasia ndani ya Chadema ni pamoja na kujitokeza wagombea wengi katika nafasi ya uenyekiti. BAVICHA sasa kuna wagombea wengi, BAWACHA na hata BAZECHA, pia uongozi wa ngazi ya Taifa. Chadema ni taswira ya upinzani nchini. Ni taasisi imara ya kisiasa.

Kuna mpango madhubuti sana wa kuimega Chadema katika makundi mawili makubwa na dhima ya kuimega ni kuondoa nguvu ya Chadema dhidi ya chama dola. Kundi ambalo linaegemea upande wa Mwenyekiti (Freeman Mbowe) na kundi ambalo linaegemea upande wa katibu Mkuu (Vicente Mashinji)

Katibu mkuu, Vicente Mashinji anaelezwa kwamba ni mtu ambaye anaongozwa na hisia. Anatambua kwamba wanachama, na wafuasi wa Chadema hawaridhiki na utendaji wake, anaamini awamu hii, hawezi kuipata nafasi hii. Anajua utendaji wake upo chini ya viwango.

Hivyo, imepangwa safu ambayo Sumaye amehusishwa bila kufahamu dhima yake. Au anafahamu lakini ameamua kutumika kwa 'ugeni' wake. Sumaye awe Mwenyekiti au Mwambe na Kubenea Makamu Mwenyekiti na watamteua Mashinji kuwa katibu Mkuu wa chama kwa awamu yao.

Kimsingi, wapiga kura hawakumkataa Fredrick Sumaye, wapiga kura walimwadhibu kwa sababu ya ushirika wake wa sasa wa wazi na genge bovu lenye mipango dhalimu la akina Kubenea, Komu na wenzao. Kambi aliyochagua Sumaye sio rafiki kwa wanachadema.

Kuna msemo rahisi na maarufu wa kiingereza, "show me your friends, and i will definitely tell you who you are". Kubenea na wenzake wamefanikiwa kujiweka karibu na Sumaye ili watumie haiba ya jina lake kuaminika. Wakamharibia.

Wana-chadema wanajua, kwamba Magufuli shida yake kubwa ni kuona Chadema ni chama MFU. Magufuli anatamani kuona Chadema ikipata kifo katika uongozi wake. Sababu inayoendelea kumzuia ni uwepo wa Freeman Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti wa Chadema.

Zipo taarifa za kuaminika kwamba Vicente Mashinji amekuwa akipigiwa simu za mara kwa mara kutoka ikulu, akishawishiwa kuhamia CCM. ameendelea kuwagomea, lakini bado taarifa zinatueleza, mawasiliano yake na Mwenyekiti wa CCM sio 'haba' na yameendelea kukolea nyakati hizi.

Katika kundi hili, wamefanikiwa kumnasa Profesa Safari Abdallah ambaye amekuwa ni mtu mwenye misimamo ya kati. Sio mtu radical hata dhidi ya dola. Hii ni kuonesha kwamba "makamu Mwenyekiti hawaelewani na Mwenyekiti wake" kutengeneza taharuki kwenye chama.

Tazama, Abdallah Safari anakwenda kuzungumza na vyombo vya habari vya Kubenea (Mwanahalisi online) na pia CCM (Mzalendo TV) na hii inatuonesha ni kwa kiwango gani wapanga mipango wao ni watu wasiofikiri vyema. Ni mkakati. Umeratibiwa.

Kwa akili za DOLA na wafuasi wao ndani ya Chadema ni kwamba, wakifanikiwa kuigawanya Chadema katika mawili watafanikiwa kuleta mtafuruku na kuacha mpasuko usiotibika. Zimeendelea kuwepo juhudi za kutoka kwenye DOLA dhidi ya Mbowe (binafsi)

Ni kwa bahati mbaya tu kwamba bado Freeman Mbowe ameendelea kukosa mpinzani 'mzito' katika nafasi ya uenyekiti wa Chadema Taifa. Wagombea ambao wamechukua fomu sasa wanaonekana ni 'wagombea rojo-rojo' na wataangushwa mapema kwa kura nyingi.

Tangu kuanzishwa Chadema takribani miaka 27 iliyopita, haijawahi kutokea Chadema kukumbana na 'zogo' kunyang'anyana madaraka kwa kiwango kilichopo sasa. Hofu ya CCM na DOLA ni kubwa sana. Wanaona ukubwa wa Chadema na 'commitment ya wanachama, wafuasi wake' na wanapata kihoro.

Kinacholeta mwanga mkubwa katika hili, juu ya nia mbaya ya Dola na CCM kwa kushirikiana na wafuasi wao ndani ya Chadema, ni kwamba, wanachama wa Chadema wanajua nini wanataka na wapi wanataka Kwenda na nani awaongoze katika njia hiyo.

Nafasi ya mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania (Chadema) haigombewi hivi-hivi tu, kwa kuviziana, bila kwanza kufanya mashauriano ndani ya Vikao vya juu na kuangalia mwelekeo na mustakabali wa chama kwa ujumla". Kubenea na wenzake hili wanalifahamu.

Upande wa Kubenea, Komu, Lwakatare, Mwambe, Sumaye na katibu Mkuu unatambua vyema kabisa hawajafanya maandalizi ya KUTOSHA na hawana mgombea aliyekamilika kuwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa. Na hawana 'system' wezeshi kushinda chaguzi.

Kubenea ameamua kumpigania Komu ambaye aliondolewa makao makuu (pamoja na Lwakatare, Waitara waliopata ubunge) na wakahamisha hasira zao wakisema "Mbowe ndie katuondoa" ikazaliwa rasmi kampeni Ya "Mbowe Must Go" ikiongozwa na Waitara, KOMU, Lwakatare na Kubenea. Ni visasi. Sasa wameongezeka wengine.

Kumbuka. Saeed Kubenea na KOMU wameoa nyumba Moja. Hawa kwa pamoja ni wamiliki wa gazeti la Mwanahalisi. Ni marafiki tangu wakiwa NCCR - MAGEUZI. Mapambano yao dhidi ya Freeman Mbowe ni 'mapambano ya kuswahiba'. Furaha yao ni kuangusha Chadema na Mbowe kwa gharama yoyote.

Saeed Kubenea amechukua fomu ya kugombea nafasi ya makamu Mwenyekiti, GHAFLA amesikia Tundu Lissu kachukua fomu ya kugombea nafasi hiyo. Ni pigo kubwa Kwake, anajua kabisa wajumbe (wapiga kura) hawawezi kumchagua kamwe mbele ya Tundu Lissu

Sasa wamefanya namna, wamefanikiwa kumpata makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari kwenye kundi lao. Pamoja na elimu ya kidato cha pili ya Saeed Kubenea, lakini ni wazi ana akili na nguvu katika kumshawishi mtu ajiunge nae katika 'mitkasi' yake. Amewavuta hao niliowataja.

Kubenea na Komu wamewahi kumtembelea Tundu Lissu akiwa kitandani akiuguza majeraha ya risasi, amefanyiwa upasuaji akiwa kwenye maumivu wakimuomba ajiunge kwenye vuguvugu lao la kumuondoa Mbowe madarakani ambalo wamelipa jina la "Mbowe Must Go". Tundu Lissu aliwakatalia.

Fikiria uwezo wa akili katika kufikiri kwa watu hawa. Tundu Lissu ambaye ana majeraha ya kushambuliwa kwa Risasi zaidi ya 16 mwilini, ana 'oparesheni' 22 mwilini, bado Kubenea na Komu wanamuomba aungane nao kumuondoa Mbowe kwa kujiunga nao kwenye "Mbowe Must Go"

Komu na Lwakatare wana visasi, chukina vinyongo vyao binafsi kwa kuondolewa makao makuu na wanamtuhumu Mbowe kwa hilo. Walianzisha kampeni ya "Mbowe Must Go" wakiwa na Mwita Waitara, wote wakiwa wahanga wa kubadilishiwa majukumu HQ baada ya reshuffle! Chuki binafsi dhidi ya Mbowe!

Cecil David Mwambe ambaye anapinga Katiba ya Chadema akisema ni marufuku kuchanga kwa ajili ya Chama (Katiba ikimtaka kama mbunge wa kuchaguliwa kuchangia 5% ya posho yake), ndie upande wa Kubenea unamtaka awe mgombea wa uenyekiti wa chama Taifa.

Kuna mengi yanafanyika ndani ya chama ambayo yanakiumiza chama Kweli kweli. Wengi hawajui. Yanajeruhi chama. Moja kati ya Mambo hayo ni pamoja na baadhi ya wanachama wa Chadema wameamua kwa sababu za hovyo kutaka kutumika na DOLA ya CCM.. Lazima tuseme.

Saeed Kubenea ni kati ya watu hatari sana kwa ustawi wa jumuiya ya kisiasa ya Chadema. Anajua kabisa kwamba 2020 hawezi kugombea kupitia Chadema (haaminiki tena) na hivyo anajiandaa kugombea ubunge kwa ama CUF au ACT-wazalendo jimbo la MAFIA. Ndio nyumbani kwao.

Kubenea ana historia 'hasi' katika harakati za mageuzi nchi hii. Mwaka 1999, NCCR - Mageuzi ikiwa haina wajumbe wa kutosha Zanzibar, ikatumia wajumbe wa CUF kutoka Pemba kupiga kura nyingi dhidi ya Mzee Marando. James Mbatia akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa NCCR - MAGEUZI.

Kubenea alikuwa ni mwanachama wa NCCR - MAGEUZI pamoja na rafiki yake bwana Komu, ambao wote sasa ni wabunge wa Chadema. Kutoka Ubungo na Moshi vijijini. Wakati wa kumshughulilkia Marando, Kubenea ndie alikuwa anagawa fedha kwa wajumbe.

Baada ya serikali ya Magufuli kufungia magazeti ya Kubenea (Mawio na Mwanahalisi) sasa ameamua kuwa adui wa Freeman Mbowe kumfurahisha Magufuli ambaye kimsingi anamchukia Mbowe na anamuona kama adui wake kisiasa na hatari kwa CCM.

KUBENEA yupo kwenye vita ya kuomba magazeti yake yafunguliwe. Mwanahalisi limeshinda kesi yake lakini hadi leo limepigwa marufuku kuchapishwa. Magufuli alimueleza Kubenea achague moja, kuwa mwandishi wa habari au mwanasiasa. Hivyo anawajibika kumtumikia.

Kubenea na Komu na Cecil Mwambe wamefikisha malalamiko yao ya kukatwa posho kwa maandishi kwenye ofisi ya spika wa bunge. Watu hawa wamemuomba msajili aingilie kati jambo hilo na hata ku' regulate uchaguzi ndani ya chama. Kudhibiti chama. Watu hawa ndio wamemponza mzee Sumaye.

Siku kadhaa kabla ya uchaguzi wa kanda ya Pwani, walimtembelea Sumaye nyumbani Kwake. Wakampa ahadi ya kushirikiana nae kumuondoa Mbowe kwenye madaraka hayo. Mzee Sumaye alikubali kuunda "alliance" na watu hawa.

Ukimsikiliza Sumaye wakati akijibu maswali ya wapiga kura ndani ya ukumbi wa mikutano, Kibaha utaelewa dhamira ya Sumaye haikuwa ya dhati kugombea huo "uenyekiti" ambao anasema ameadhibiwa kwa sababu hiyo. Sumaye amejiadhibu mwenyewe. Kambi aliyochagua.

Sumaye anasema mbele ya wapiga kura kwamba "nimechukua fomu kuonesha umma kwamba demokrasia ipo ndani ya Chadema na yanayosemwa kwamba nafasi ya mwenyekiti haiguswi labda sio maneno ya Kweli". Haya ni maneno ya Sumaye akiwa Kibaha kwenye Uchaguzi wa kanda.

Sumaye anaendelea kusema "nafahamu, hakuna mtu mwenye uwezo wa kumshinda Mbowe, nagombea kwa sababu za kidemokrasia tu". Sumaye anawapa sababu wapiga kura wamkatae. Wanapata mashaka na dhamira yake. Wanamuona sio mtu sahihi.

Sumaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, ameshindwa kabisa kusoma Alama za nyakati na kutambua kwamba wanachama wa Chadema wanataka mgombea wa aina gani sasa? Ameamua kujidhalilisha kwa kukubali kuungwana na kambi ya Kubenea ambayo inakihujumu chama?

Sumaye ameponzwa na ugeni wake au ni kutokuwa na UFAHAMU wa siasa za ushindani? Sumaye ameamua kujihusisha na watu wenye tuhuma hadi za jinai ndani ya chama? Wamewahi kupanga Mauaji hawa akina Kubenea na Komu.

Kubenea na Komu wamewahi kupanga njia za kumdhuru Freeman Mbowe, wakisema ni muhimu Boniface Jacob (ambaye ni Meya wa Ubungo kwa sasa) auwawe ili kumfikia Mbowe, Sumaye hakujua athari hii kwa wapiga kura?

Wamewahi kuomba radhi mbele ya kamati kuu ya Chadema, wakaomba radhi hadharani kwa utovu wa nidhamu, na walikiri kukosea na wakasema wamepotoka. Sumaye na uzoefu wake, hakuona Mambo haya? Au amevaa miwani ya mbao??

Kubenea na Komu hawajali tena kufukuzwa Chadema. Wanaomba hata kesho wafukuzwe. Ili wapate sababu za kumnanga Freeman Mbowe. Bahati nzuri wameshtukiwa, wameachiwa waendelee kujiumbua wenyewe.

Kulikuwa na sababu nyingi za kuwafukuza Saeed Kubenea na Komu ndani ya Chadema. Sababu zaidi ya tano. Lakini Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ana busara sana. Hawa hawakupaswa kuwa wanachama hadi sasa.

Wanachochea mipasuko, makundi, migawanyiko ndani ya Chadema. Sasa wamefanikiwa kuwagawa kabisa hadi watumishi wa makao makuu wenye uchu na tamaa ya madaraka na vyeo. Wanaelekea kuwagawa wanachama. Wanapandikiza chuki ya wazi kwa wasiowapenda.

Kubenea sasa anapata ushirikiano mkubwa kutoka CCM na Dola kupitia Mwita Waitara ambaye nae ana ugomvi binafsi na Freeman Mbowe kuhusu kuondolewa Kwake Makao makuu wakati akiwa mbunge kupitia Chadema. Sasa ni rafiki wa Kubenea.

Kubenea na Komu wa najua kabisa hawatarejea Bungeni kupitia Chadema tena wakati mwingine. Sasa wanaandaa mikakati ya aidha wabaki Chadema wakiwa na madaraka au waondoke Chadema ikiwa marehemu kama walivyoiacha NCCR - MAGEUZI.

Upinzani haswaa Chadema wanapita kwenye wakati mgumu kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote, utawala wa mkono wa chuma na wanapambana na dola, lakini mbaya zaidi, Kubenea na wenzake sasa wamekuwa maadui wa ndani wa Chadema na sio CCM tena.

Sumaye hajui? Kwamba Kubenea na Komu hawajawahi kukanyaga kabisa Segerea wakati Freeman Mbowe na Esther Matiko wakitunzwa huko kwa siku 104 (sawa na hukumu ya miezi minne). Sumaye haya alishindwa kufahamu kabla ya kumchagua Kubenea?

Kubenea na Komu hawajawahi kufika hata mara moja mahakama ya hakimu mkazi, Kisutu kusikiliza mwenendo wa kesi dhidi ya uongozi wote wa Chadema na wabunge wenzao. Kwa sababu kesi hii ya kusingiziwa haiwahusu ndio maana hawafki mahakamani? Sumaye hajui haya? Kweli?

Yeyote ambaye ana ukaribu na Freeman Mbowe ndani ya Chadema ni adui wa Saaed Kubenea na Komu. Wawili hawa wanamiliki gazeti la Mwanahalisi ambalo lilimshughulikia ipasavyo Ben Rabiu Focas Saanane akiwa kwenye mikono ya watu wasiojulikana.

Kubenea aliandika makala kupitia gazeti lake la Mwanahalisi kuonesha kwamba Ben Saanane hajatekwa au kupotezwa isipokuwa amejificha Dar es saalam na anaonekana kwenye Vijiwe vya Kahawa jioni. Hivyo anaichafua serikali. Sumaye hakujua haya?

Kubenea haelewani kabisa na Viongozi wenzake ndani ya chama Halima Mdee, John Mnyika, Boniface Jacob, Godbless Lema, SUGU Na wengine wote ambao wamekataa kabisa kuwa kwenye kampeni yake ya "Mbowe Must Go". Wanachama tunajua haya, Sumaye hajui?

Kwa Leo tuishie hapa, Frederick Sumaye akubali kushindwa na asiwatupie lawama wapiga kura kwamba walimuadhibu, isipokuwa atazame sana kambi ambayo ameamua kujiunga nayo, Mwisho ataona anaonewa na atatangaza kuelekea kwingineko na kusema Chadema hakuna demokrasia.

Wanachama wa Chadema wa najua nani anapaswa kuwa nani kwa sababu gani ndani ya chama Chao. Wanachama wa Chadema walimkatalia Sumaye hadharani kwa sababu ya NIA yake kuonekana sio kuongoza mabadiliko Bali kushirikiana na "KKs" Yaani Kubenea na Komu. Akakataliwa.

#MMM, Martin Maranja Masese
 
Hutaweza kupandikiza migogoro kwenye chama cha CHADEMA, mambo hayo huwa mnayafanyaga huko kwenu. Kama huko kwenu CCM mna demokrasia na wewe ni mwanaume kweli chukua fomu ya kogombea Urais uone utakavyotomaswa tomaswa.
 
Mtajijua na chama la wachaga


State agent
FB_IMG_1575388253897.jpeg
 
Kama unataka maisha yako ya kisiasa ndani ya CHADEMA yawe mabaya basi gusa nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA!

Maelezo marefu lakini yote ni katika kuhakikisha nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA ina mwenyewe wa maisha!
Katumia nguvu kubwa sasa kumtetea sultan halafu utasikia wanasema kachukue buku saba.

Huyu mleta mada sijui kachukua buku ngapi!.
 
Mtajijua na chama la wachaga


State agentView attachment 1280591
Mchora katuni wa gazeti la HABARILEO kumbe hata taaluma ya uchoraji hana. Haki ya Mungu muwe mnaleta vitu kama hivi tujionee maana haya magazeti ya UHURU na HABARILEO sijawahi kuyasoma katika maisha yangu...Natamani kumfahamu na mchora katuni wa UHURU..Mimi nawajua Said Michael na Masoud Kipanya
 
Ufafanuzi mzuri kutoka kwa mleta mada. Tunashukuru maana umeyaweka wazi hata yaliyokuwa yamefichika.
 
Au Sumaye amekuwa kama wale vibibi wa Shinyanga wanaoambiwa ni wachawi halafu wanamalizwa kisa wana macho mekundu!
Nadhani tangu Lowassa arudi home, Sumaye naye anaonekana mchawi tu na wengi hapo Ufipa.
Mzee atambue kustaafu sio mwisho wa maisha, afanye maamuzi tu.
 
Kama unataka maisha yako ya kisiasa ndani ya CHADEMA yawe mabaya basi gusa nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA!

Maelezo marefu lakini yote ni katika kuhakikisha nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA ina mwenyewe wa maisha!
Eti chama cha demokrasia!
 
 
Back
Top Bottom