Alfu Lela Ulela
JF-Expert Member
- Oct 29, 2010
- 1,255
- 77
MWONGOZO WA SPIKA NI MSUKULE WA CCM
Kwa watu makini na wanaofuatilia siasa za nchi yetu, watakubaliana na mimi kuwa Makinda wa sasa si yule aliyekuwa naibu Spika kwenye bunge la tisa. Tangu achaguliwe kuwa Spika (kwa mizengwe) Makinda anaonekana kuwa na mtizamo hasi sana kwa vyama vya upinzani bungeni hususani Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA). Sina hakika kama mtizamo huu alikuwa nao tangu kale, lakini nina hakika kuwa mtizamo hasi kuhusu upinzani umezidi maradufu baada ya kuwa Spika. Anawapuuza wabunge wa CHADEMA. Anawakebehi.anawadhalilisha.
Yawezekana Makinda anakilinda chama chake cha Mapinduzi (CCM), na amekwishajua kuwa chama pekee cha upinzani chenye nguvu kwa sasa ni CHADEMA ndio maana anatumia kila awezalo kuwazima.
Wabunge wa CHADEMA wanapochangia mijadala au kuuliza maswali utamwona Makinda anakuwa makini zaidi kuliko wabunge wa vyama vingine wakichangia. Yawezekana wengine hawajaiona hali hii, lakini ukifuatilia kwa makini utabaini ukweli wa niyasemayo. Binafsi siioni hali hii kuwa njema wala siamini Spika Makinda anavutiwa sana na hoja za Chadema kiasi cha kuwasikiliza kwa makini sana.
Bali nionavyo anasikiliza hoja hizo kwa makini ili aweze kuzikosoa kabla hazijawasilishwa, akebehi kabla mtoa hoja hajamaliza, na azipuuze kabla hazijajibiwa. Ili zipoteze nguvu, zionekane hoja dhaifu, na awadhalilishe watoa hoja makini wa Chadema waonekane watu wenye hoja mufilisi.
Hiyo ndio sababu ya Makinda kuwa makini wanapozungumza Chadema. Hii ndio kazi aliyotumwa na chama chake. Kuua upinzani. Na ni lazima atekeleze kazi hiyo kwa uaminifu ili kulinda kiti chake.
Hebu tuanze na hili la mwongozo wa Spika. Jumanne ya tarehe 08/02/2010 mhe.Tundu Lissu (mbunge wa Singida mashariki-CHADEMA) alikalishwa chini mara kadhaa, na maongezi yake kukatizwa zaidi ya mara kumi kwa kile kinachodaiwa mwongozo wa spika. Kuna wakati mwongozo ulikuwa unaombwa mara tu baada ya Spika kutoa mwongozo mwingine. Yaani ilikuwa mwongozo juu ya mwongozo. Jinamizi linaloitwa mwongozo wa Spika likatumika kukatiza hoja za msingi za Mhe.Lissu.
Kwa maana hiyo tukasadikishwa kuwa jinamizi mwongozo wa Spika linaweza kukatiza maongezi ya msemaji yeyote bila kujali hadhi yake. Lakina vichekesho vikaanza. Vituko vikatokea. Mipasho ikatawala. Dudu hili mwongozo wa Spika linaonekana ni mali ya CCM, na wapinzani hususani CHADEMA hawaruhusiwi kulitumia. Limeundwa mahsusi kuzima upinzani, na CCM wamepewa mafunzo maalumu ya namna ya kulitumia.
Chadema hawana haki kutumia mwongozo wa spika. Ikiwa sivyo ni kwanini mhe.Godbless Lema mbunge wa Arusha mjini, alipoomba mwongozo wa Spika tarehe 10/02 kikao cha asubuhi, kwanza alipuuzwa, baadae akakejeliwa na Makinda kuwa subiri kwanza niongee mimi. Akiwa na maana kwamba Mhe.Lema haruhusiwi kuingilia maongezi ya spika.
Lakini Mhe.Simbachawene mbunge wa Kibakwe (CCM) aliingilia maongezi ya Spika wakati Makinda akikaribisha maswali kwa wizara ya mambo ya ndani. Simbachawene akamkatisha Makinda kwa kigezo cha mwongozo wa spika. Lakini tofauti na Lema yeye alisikilizwa, akapewa nafasi na akaitumia fursa hiyo kuonesha upeo wake mdogo wa kufikiri.
Simbachawene bila aibu akahoji uhalali wa Mhe.Lema kumtuhumu Waziri mkuu kusema uongo, ilihali Waziri mkuu ni mkubwa kwa Lema kicheo na kiumri. Katika kuonesha alivyo na mawazo chakavu, akatetea eti kumtuhumu (kuwa ni mwongo) mtu aliyekuzidi cheo na umri ni kinyume na Mila na desturi za Kiafrika. Hivyo eti akataka Lema aadhibiwe. Lahaulah!! Aibu gani hii kwa mtu anayejiita mbunge.
Yaani Simbachawene anataka kutusadikisha kuwa mtu aliyekuzidi umri na cheo, anaruhusiwa kudanganya, kupotosha na kusema uongo anavyojisikia, bila kuhojiwa popote wala kukosolewa, maana tukimkosoa tutakuwa tumekiuka mila na desturi za kiafrika. Mi naomba Simbachawene asiwasingizie waafrika wote. Aseme tu labda ni mila na desturi za Kibakwe. Lakini hivi bunge letu linaongozwa na Kanuni, au mila na desturi?? Katika hili Simbachawene amepotoka.
Lakini hapo awali kidogo nilisema jinamizi liitwalo mwongozo wa Spika ni mali ya CCM, na upinzani hususani Chadema hawana haki ya kulitumia. Katika kikao cha jioni ya tar.10/02/2011 mbunge wa Kawe mhe.Halima Mdee aliomba mwongozo wa Spika muda mchache kabla Spika hajatangaza wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge. Tofauti na Simbachawene, Mdee hakuingilia maongezi ya Spika. Lakini Spika akamjibu kwa kejeli mwongozo sasa hapana, maana ninyi mnadhani kila saa ni wakati wa mwongozo, sasa ni wakati wa kazi
Lakini chuki za Makinda kuhusu Chadema hazikuishia hapo. Ijumaa ya tarehe 11/02/2010 kwenye kikao cha asubuhi, akaibuka mwendawazimu mmoja akajitambulisha kuwa mbunge wa Nkasi kaskazini. Bila kuheshimu bunge, na bila kujali anatazamwa na Watanzania akaanza kutukana Chadema. Akavua hadhi yake ya ubunge kwa muda na kuuvaa upuuzi, na upuuzi nao ukamvaa kwelikweli tangu utosini hadi unyayoni. Akapumbaa. Pamoja na matusi mengine, akahitimisha kwa kusema ..ningejiona wa hovyo sana kama ningechaguliwa kwa tiketi ya Chadema. Akimaanisha wabunge wote wa Chadema ni wa hovyo.
Mwanzoni wabunge wa Chadema walimvumilia kwa kuwa ni wastaarabu. Waliamua kukaa kimya maana maandiko yanasema usimjibu mpumbavu kwa upumbavu wake usije ukafanana nae. Lakini alipozidisha matusi mbunge wa Kawe Halima Mdee akaamua kuvunja ukimya. Maana maandiko kwa upande mwingine yanasema mjibu mpumbavu kutokana na upumbavu wake, asije akajipatia kibali machoni pako
Kwa hekima Mdee akaomba mwongozo wa Spika, maana chama chake kilidhalilishwa, kiliudhiwa na kauli ya aliyejiita mbunge wa Nkasi Kaskazini. Hivyo akatumia kanuni ya 61 inayomtaka mbunge huyo wa Nkasi kufuta kauli yake ama kuomba radhi maana ni ya kuudhi. Ama sivyo bunge lielezwe kuwa ni ruksa kutumia kauli za hovyohovyo bungeni.
Lakini cha ajabu badala ya kutoa mwongozo, Makinda akaendekeza hisia. Akatamka kwa hasira (kama alivyoelekezwa na chama chake) mwenye mamlaka ya kuruhusu kauli za hovyo bungeni ni mimi kisha akamruhusu yule mbunge wa Nkasi aliyekosa adab aendelee kutukana. Jamani hata kama ni kukibeba Chama chake hapa sasa imezidi.
Lakini turejee kidogo katika hoja ya Lema. Je ni kweli Lema alimtuhumu Waziri mkuu kuwa kasema uongo?? Hasha!! Lema hakumtuhumu Waziri mkuu. Wote waliofuatilia kwa makini mjadala ule watakubaliana na mimi. Lema alihoji ikiwa mtu mzito kama waziri mkuu, akidhibitika amesema uongo bungeni, je ni hatua gani mbunge anaweza kuchukua?
Kwa lugha nyepesi ni sawa na kusema Lema alihoji ikiwa kiogozi mkubwa wa serikali (kwa mfano waziri mkuu) akitoa kauli bungeni, na ikadhibitika kuwa kauli hiyo si ya kweli, je bunge linaweza kuchukua hatua gani?
Hivyo Spika alipaswa kutoa mwongozo kuwa iwapo itadhibitika kiongozi mkubwa kama Waziri mkuu, ametoa taarifa ambazo si za kweli, ama anaweza kuchukuliwa hatua au vinginevyo. Na kama zipo hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi yake basi Spika aziweke bayana kwa mujibu wa Kanuni za bunge.
Lakini cha ajabu hoja ikageuzwa. Ikapinduliwa. Ikabadilishwa. Badala ya Spika kutoa mwongozo, akamtaka Lema kudhibitisha. Adhibitishe nini? Lema aliomba mwongozo. Sasa adhibitishe mwongozo au..? Katika hili Spika alionesha fikra kurupushi. Eti adhibitishe tuhuma. Tuhuma zipi? Kumbe CCM wakiomba mwongozo si nongwa, lakini Chadema wakiomba mwongozo wanaambiwa wametoa tuhuma. Wadhibitishe. Ebo!! Ama kweli maskini haokoti,akiokota kaiba.