Mwigulu awashukia warajisi wanaoomba rushwa

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, amemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, mamlaka za mikoa na wilaya kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria warajisi wasaidizi na maofisa ushirika wanaoomba rushwa katika kutekeleza kazi zao za usimamizi wa vyama vya ushirika.

Pia amevinyooshea vidole vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) akisema vingi vinategemea mitaji kutoka nje kwa asilimia 100 na hivyo kukiuka matakwa na sheria ya ushirika inayovitaka visikope nje zaidi ya asilimia 25 ya mali zake zote.

Alitoa agizo hilo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Florence Turuka, wakati wa ufunguzi wa kongamano la Wanaushirika Tanzania linalofanyika mjini hapa.

Mwigulu alisema kumekuwa na changamoto kubwa ndani ya vyama vya ushirika, hali inayosababisha vyama hivyo kushindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na viongozi na watendaji wa vyama hivyo kushindwa kuwa waaminifu na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Alisema sasa imefika wakati wa kuwachukulia hatua watendaji wote ambao wamekuwa wakiomba rushwa katika kutekeleza kazi zao za usimamizi.

Kuhusu vyama vya ushirika, Mwigulu alisema hali ya kutegemea mitaji kutoka nje kwa asilimia 100 husababishwa na usimamizi mbovu wa maofisa ushirika na tafsiri isiyokuwa sahihi ya utoaji wa hati za ukomo wa madeni.

Alisema kumekuwepo na mafanikio katika tasnia ya ushirika katika maeneo mbalimbali, huku pia mfumo wa stakabadhi ghalani ukisaidia kuboresha bei ya mazao ya chakula na biashara ambapo bei ya kilo moja ya korosho iliongezeka kutoka Sh 600 mwaka 2011/ 2012 hadi Sh 2,900 mwaka 2015/2016.

Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Audax Rutabazibwa, alisema kupitia kongamano hilo watapata fursa kujadili na kupeana taarifa za kazi zilizofanyika mwaka mzima katika kuendeleza ushirika.
 
Back
Top Bottom