Mwema ametumika kisiasa-Lipumba

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,013
Mwema ametumika kisiasa-Lipumba



Na Rabia Bakari
Majira

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye alisema kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Jenerali Said Mwema ametumika kisiasa katika kuzuia maandamano hayo kwa kuwa sababu alizotoa ni za kisanii na hazina maana yoyote.

Profesa Lipumba alilaani jeshi la polisi kwa kuwapiga na kuwaumiza viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao na pia kukamatwa na kuhojiwa, kisha kushtakiwa kwa baadhi ya wabunge na mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe.

Profesa Lipumba alitoa tamko hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam, alipowaita kulaani vitendo vya polisi vilivyofanywa katika maandamano ya CHADEMA Arusha juzi.

Alisema kuwa ushahidi wa mazingira, unaonesha wazi kuwa IGP Mwema alitumika kisiasa, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa demokrasia nchini na kinatia doa kubwa.

"Nilikuwa namuheshimu sana Bw. Mwema, ni kiongozi aliyekuwa anaheshimika na vyama vya siasa, lakini vitendo hivi vya kushambulia maandamano ya amani ya kidemokrasia, vinazidi kuharibu sifa na uaminifu juu ya Mwema. Ni muhimu sana kwa taifa letu kwa IGP kulinda heshima yake na asikubali kutumika kisiasa kukandamiza demokrasia ndani ya nchi," alisema Profesa Lipumba.

Aliongeza kuwa amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na IGP saa chache kabla hayajafanyika ilitokana na shinikizo la kisiasa na hoja iliyotolewa kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonesha uvunjifu wa amani ili kuzuia maandamano ni usanii mtupu.

"Kama kweli polisi wana taarifa za kiintelijensia, kuwa kuna watu watavunja amani, basi wazitumie taarifa hizo kuwadhibiti watu hao, lakini kuyasitisha maandamano ni kuwanyima wananchi uhuru wa kisheria wa kufanya maandamano.

"Hivi sasa jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuzuia kila aina ya madai yanayotolewa na vyama ili mwisho wa siku lifanye kazi yake kuu ya kulinda CCM na utawala wao wa kijeuri na kisanii," alidai Profesa Lipumba.

Aliongeza kuwa CUF inaamini kuwa polisi na serikali ya CCM wanataka kutumia kitisho cha ugaidi kilichozikumba Kenya na Uganda kama sababu ya kupinga mikusanyiko mikubwa ya kisiasa kwa lengo la kuitetea serikali.

"Lazima tujiulize hivi magaidi wakitaka kulipua Tanzania mbona kuna sehemu nyingi sana mbazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya CHADEMA au CUF au vyama vingine?"Hivi tujiulize kama kweli pana tishio la ugaidi, iweje mechi za mpira ziendelee bila kuzuiwa na polisi? Mikusanyiko yote inafanyika isipokuwa maandamano ya vyama vya siasa tu?


Hawa magaidi walio tishio kwa jeshi la polisi wanaotaka kulipua maandamano peke yake wametoka wapi? Kwanini nchi hii iendeshwe kisanii na kiujanja ujanja namna hii? Kwa nini serikali inaogopa maandamano?" alihoji Profesa Lipumba.

Alifananisha ukatili huo uliofanywa na jeshi la polisi na ule waliofanyiwa wafuasi wa CUF Desemba 28, mwaka jana wakati wakifanya maandamano ya amani yaliyokuwa yaongozwe na Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Bw. Julius Mtatiro ya kupeleka rasimu ya katiba kwa Wizara ya Katiba na Sheria.

Alisema kuwa maandamano hayo yalipigwa marufuku ghafla na kisha mamia ya polisi wakasheheni na silaha za kila aina wakaanza kuwapiga na kuwakamata wafuasi wa CUF na wananchi wengine walioshiriki katika maandamano hayo.

"CUF kinaamini kuwa ustawi wa demokrasia, utawala bora, usawa, maendeleo ya nchi yetu na amani ya nchi havitaletwa kwa mtutu wa bunduki wala mabomu wala kila aina ya nguvu, hata kama CCM wataendelea na mbinu zao za kuwadhibiti wapinzani, hatatokaa kimya na wala hatutoacha kutumia fursa za kikatiba kutoa maoni yetu kwa njia ya amani," alisisitiza.

Profesa Lipumba alisema wanaamini walichokuwa wakipigania CHADEMA jijini Arusha ni kitu cha msingi sana, walikuwa wakipinga kitendo cha kukiuka demokrasia katika uchaguzi wa meya, na hawakuwa na budi kutumia njia za kidemokrasia kuonesha kutokukubali na kutotambua utaratibu huo wa kinyemela ulioendeshwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa manufaa ya CCM.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi na serikali ndio wanaostahili kulaumiwa kwa uvunjifu wa amani uliotokea Arusha, na kudai kuwa CUF kinaamini CHADEMA kama chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali ndani ya nchi kilikuwa na haki ya kikatiba na kisheria na kimazingira kufanya maandamano ya amani.

"CUF inalaani ukatili huu waliofanyiwa wakazi wa Arusha katika maandamano hayo na kuwa hauvumiliki na unahatarisha amani na utulivu wa kweli wa nchi yetu."CUF inawapa pole wote waliopigwa na kuumizwa na mabomu, risasi, maji ya kuwasha nakadhalika katika tukio hilo la kihistoria la kudai haki ya wanyonge, tuko pamoja nao katika kuendelea kupigania haki," alisema Profesa Lipumba.

Pia mwenyekiti huyo alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutumia busara za hali ya juu katika kuendesha nchi katika kipindi hiki ambacho anamalizia miaka yake mitano ya mwisho.
 
Hongera sana Lipumba kwa maneno yako mazito.
 
afadhari na wewe mweshimiwa umeona na umekuwa jasiri kukisema.... Mwema aache kutumiwa na mafisadi
 
Hao CCM na polisi wao wana kiu ya damu za watu. Jitihada zifanyike ili wawe wateja wa Ocampo.
 
Hivi ndivyo vyama vya Upinzani vinatakiwa vioneshe ukomavu wa kisiasa. Upinzani ni lazima uelewe kuwa kuna haja ya wao kushikamana na sio kuhujumiana au kurushiana maneno yasiyo na maana, kukebehiana na kuitana majina. Hongera Lipumba kwa kuonesha njia na muendelee kuwa hivyo.

Chama Chochote cha Upinzani pekee Tanzania kitachezea nyundo na jembe la CCM bila huruma. Upinzani Mupeane "tough"!
Jinsi CCM na serikali yake wanavyojaribu kuuparaganya upinzani ni wazi kuwa kuna haja ya vyama vya upinzani kushirikiana pale inapowezekana. Hiyo ni kwa faida ya upinzani na faida kwa jamii.
 
Nina imani Said MWEMA anatunza kumbukumbu hizo AMRI anazopewa.

Kama haweki, basi ITAKULA kwake siku moja kama hawajui WANA SIASA.
 
Ahjsante
Lipumba, umeonyesha ukomavu wako wa Kisiasa, Wote ni nduguzako unahaki ya nKuwatetea ni faraja kwa Mbowe, Slaa, Ndesa Mburo na Wanachadema wote Kufajirika kwa kauli yako ALUTA CONTINUWAAAAA
 
Lipumba amenena. Mtazamo wangu ni huo huo kutokana na uonevu na mabavu waliyoyafanya polisi dhidi ya CUF na CHADEMA. Lakini historia itawahukumu na yote yana mwisho. Kuna siku hawa waliopewa dhamana watakuja kujutia mabaya yote waliyoyafanya. Ndiyo hata maandiko matakatifu yako wazi kwamba waovu watahukumiwa kwa uovu wao
 
Nchi hii kila mtu ni mwanasiasa. Hata wanajeshi wa JWTZ nao ni wanasiasa. Kwa hiyo, Said Mwema kutumika kisiasa sishangai kabisa. Lakini mwisho wa yote haya waja na unabisha hodi mlangoni.
 
Back
Top Bottom