Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,318
- 33,125
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, ameainisha sababu kadhaa za kumpigia kampeni Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya, ili wamchague katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Profesa Mwandosya, alikuwa miongoni mwa wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliofuzu kuingia `tatu bora' ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais mwaka 2005.
Wengine walikuwa ni Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Jakaya Kikwete aliyeibuka kuwa mshindi.
Profesa Mwandosya ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo la Rungwe mkoani hapa, alitoa sababu hizo jana katika viwanja vya kata ya Nzovwe mjini hapa, wakati akizindua kampeni za CCM katika jimbo la Mbeya Mjini.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni mafanikio yake (Kikwete) katika kuleta na kusimamia umoja, amani na utulivu, kupunguza utegemezi wa Taifa kwa wahisani kutoka asilimia 49 hadi 28 kwa kipindi cha kati ya 2005 na 2010.
Alifafanua kuwa suala la kupunguza utegemezi, limeiwezesha nchi kuendesha miradi mikubwa kama wa maji kutoka ziwa Victoria hadi Kahama mkoani Shinyanga kwa kutumia fedha za ndani.
Manufaa mengine kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 70 ambapo kati ya hizo, Sh bilioni 15 zinatoka kwa wahisani.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni heshima aliyoijengea Tanzania nje ya nchi, kuleta mustakabali wa kisiasa Zanzibar na kudhibiti ujambazi.
Profesa Mwandosya alisema zipo sababu nyingine ambazo Rais Kikwete hawezi kuzisema mwenyewe, isipokuwa yeye kwa vile anamfahamu vizuri baada ya kufanya naye kazi kwa miaka zaidi ya 20, aliamua kumsemea.
Alizitaja sababu nyingine kuwa ni upole wake (Kikwete), mchangamfu na mwenye tabasamu na anayependa makundi ya rika zote bila ubaguzi.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa pili Rais Kikwete ni mkali wakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mambo aliyowaahidi wananchi.
Ukali huu wa Rais Kikwete ninausema hadharani, kwa sababu mimi nauona kama ni sifa, kwa kweli anapofuatilia mambo aliyowaahidi wananchi anakuwa mkali sana, hapendi masihara, alisema .
CHANZO: NIPASHE